Home Makala ANAYOLALAMIKIA MAGUFULI YATAKWISHA  AKITUPATIA KATIBA MPYA

ANAYOLALAMIKIA MAGUFULI YATAKWISHA  AKITUPATIA KATIBA MPYA

1354
0
SHARE
Rais wa Awamu ya nne jakaya Kikwete na rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein wakishika nakala za Katiba Pendekezwa katika hafla maalum ya kukabidhiwa.

NA HILAL K SUED


Katika hotuba zake kadhaa kwa wananchi tangu achaguliwe kuingia Ikulu Rais John Magufuli amekua analalamika kuhusu “mambo ya hovyo hovyo” yaliyokuwapo katika utawala uliopita na ambayo ameyakuta na hata kusema kazi ya urais ni ngumu sana.

Alifafanua mambo hayo ya hovyo hovyo ni pamoja na kushamiri kwa ufisadi katika ngazi zote za utawala, kukosekana uwajibikaji na ambayo yalizaa wafanyakazi hewa wa serikali, maafisa wenye vyeti feki na uchotwaji holela au tuseme wizi wa fedha za umma.

Hivyo kila mara amekuwa akiwaambia Watanzania kuwa yeye amechaguliwa na wananchi basi atawatumikia wananchi kwa uwezo na nguvu zake zote ili kuirudisha nchi katika hali ya uwajibikaji na yuko tayari kuhukumiwa kwa hilo.

Na kweli katika kipindi cha takriban miezi 18 tangu aingie madarakani amefanya makubwa, mengine yasingeweza kutarajiwa kutokea katika hali ya kawaida ya tawala zilizopita za Chama cha Mapinduzi (CCM).

Haya ni pamoja na vita dhidi ya ufisadi ambayo tumeshuhudia watu wazito katika jamii pamoja na watendaji wa ngazi za juu serikalini kufikishwa mahakamani.

Lakini haya anayoyafanya ni hatua za muda mfupi tu – pengine katika kipindi atakachokuwapo madarakani – kwani hazitaondoa kiini cha matatizo yenyewe.

Nasema hivi kwa sababu hayo anayoyaita “mambo ya hovyo hovyo” yametokana na mfumo uliopo wa utawala kutokana na ombwe kubwa lililopo katika katiba na sheria mbali mbali za nchi kuhakikisha hayo hayafanyiki.

Na dawa ya yote haya ni Katiba mpya – suala ambalo Magufuli amekuwa halizungumzii. Sote twakumbuka mkwamo uliotokea kuhusu mchakato wa kuandika Katiba mpya ambayo rasimu yake ilikuwa tayari tangu 2014 na kilichobakia ni kura ya maoni tu. Mchakato wote huo ulitumia nguvu nyingi na mabilioni ya fedha bila tija yoyote – gharama ambazo pengine anaona ni moja kati ya yale “mambo ya hovyo” ya utawala uliopita.

Ingawa rasimu ile ya “Katiba pendekezwa” ilikuwa na mapungufu yake katika mfumo wa utawala lakini angalau ulikuwa umeweka misingi madhubuti ya uwajibikaji kwa watendaji wakuu wa utawala.

Hivyo Rais Magufuli, badala ya kuendelea kulalamika tu uhovyo wa mambo yalivyokuwa, ni vyema sasa akaanza kuangalia kuanzisha kwa mchakato wa katiba mpya – iwapo ni kufufua ule ule mchakato uliokwama, au kuanzisha wa kwake mpya kabisa.

Ni njia hiyo pekee ndiyo itahakikisha ile Tanzania anayotaka ya uwajibikaji itaibuka kwa vizazi vijazo kwa kuwa mambo ya hovyo hovyo hayawezi kutokea kutokana na kubanwa katika katiba mpya.

Kwa mfano Katiba hiyo mpya kamwe isitoe mwanya kwa watawala kuchota hovyo fedha za umma bila ya mamlaka husika za usimamizi na uwajibishaji kustuka, achilia mbali kuchukua hatua stahiki tena za haraka dhidi ya wahusika.

Sababu moja kubwa kwa ufisadi kuenea katika ngazi zote za utawala hadi zile za chini ni kwamba iwapo wale wa ngazi za juu hawachukuliwi hatua, basi nao hao wengine hawaoni sababu ya kufanya kazi kwa kufuata sheria. Umuhimu hapa ni kwamba mfano unatakiwa uonyeshwe kuanzia juu.

Lakini pia mfumo wa uteuzi wa wakuu wa mamlaka za usimamzi na uajibishaji ufanyiwe marekebisho makubwa katika katiba hiyo mpya. Chini ya Katiba ya sasa ni rais pekee ndiyo anateua wakuu vyombo, taasisi na mamlaka mbali mbali zikiwemo hizo nilizotaja.

Kwa mfano wakuu waliowahi kuongoza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) wanaoteuliwa na rais wamekuwa hawana uhuru kamili pamoja na madai yao kuwa wana uhuru.

Inapotokea mkuu mmoja katika utawala amehusika na ufisadi mkubwa, mkuu huyo wa TAKUKURU hawezi mara moja kumchukulia hatua za kisheria bila ya kwanza kuiangalia mamlaka iliyomteua kwa maelekezo na ushauri. Inabidi kwanza “alinde mkate wake” kama msemo maarufu ulivyo.

Angekuwa ameteuliwa kwa mfumo mwingine (kama vile uliopo Kenya) asingekuwa na hofu yoyote ya kuchukua hatua tena za mara moja kwani anakuwa hana hofu ya “kutumbuliwa” na mkuu aliyemteua.

Kwa ujumla sasa hivi hapa nchini, tukiacha ngazi ya kitaifa, watu waliopewa nyadhifa za kuteuliwa bado wana nguvu sana kimaamuzi kuliko wale waliochaguliwa na wananchi. Hii ni kinyume na ilivyo Kenya sasa hivi.

Hapa kwetu Wakuu wa Wilaya na wale wa mikoa huteuliwa na Rais na mara nyingine uteuzi huo hauzingatii uwezo, bali uswahiba tu na baadae kuleana. Lakini wateule hawa wana mamlaka makubwa katika maeneo yao kuliko hata Wabunge. Kenya wakuu wa mikoa – yaani Magavana wa Counties – huchaguliwa na wananchi katika chaguzi.

Mawaziri wa Kenya hawakuchaguliwa kiswahiba kwani Katiba mpya ya nchi hiyo imeweka utaratibu wa kuwapata – lazima wapitie katika Kamati ya Mchujo ya Bunge yenye Wajumbe 28 (Parliamentary Committee on Appointments) waliochaguliwa na Bunge ki-uwiano wa vyama.

Wengi wetu tuliona kupitia runinga baada ya uchaguzi wa 2013 jinsi waliopendekezwa kuwania nyadhifa za uwaziri walivyokuwa wakihenyeshwa kwa maswali mbele ya hiyo Kamati ya Mchujo.

Hapa kwetu itachukuwa muda mrefu sana kuanza kupata kitu kama hiki kwani mfumo wa utawala iliopo unaendeshwa kwa kuleana (patronage), — yaani wananchi (kupitia Bunge lao) hawana sauti kabisa katika utoaji wa vyeo na nyadhifa katika serikali, na pia katika kuwaondoa wale wanaoshindwa kazi.

Bado tutaendelea kupata mawaziri ambao wana sifa feki kutokana na kuwa na vyeti vya elimu vilivyoghushiwa na hakuna katika utawala anayeguswa na hilo isipokuwa wananchi.

Kwa mfano ingekuwa ni Kenya ya sasa, iwapo kuna waziri mwenye cheti cha elimu kilichoghushiwa bila shaka angekataa uteuzi wa uwaziri kwani angeaibika tu mbele ya kamati ya Bunge ya Mchujo inayoendeshwa kwa uwazi, na ambayo pia wananchi hukaribishwa kupeleka malalamiko yao dhidi ya mteule yeyote.

Hali kadhalika utaratibu ni wa aina hiyo hiyo katika uteuzi wa nyadhifa nyingine kuu za nchi kama vile Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi n.k. Kuna Tume (commissions) zilizoteuliwa na kuidhinishwa na Bunge ambazo ndizo hufanya michujo. Ni vigumu kwa Rais kumpachika swahiba wake kiurahisi.

Kwa mfano kulitokea jaribio kwa Rais Uhuru Kenyatta kutaka kumpa u-Jaji Mkuu mtu anaemtaka yeye kumrithi Willy Mutunga aliyekuwa anastaafu. Jaji mmoja wa Mahakama Kuu nchini humo Isaaac Lenaola alizuia Tume ya Utumishi wa Mahakama (Judicial Service Commission) kuanza mchakato (mchujo) wa kumpata atakaekuwa “mrithi” wa Mutunga hadi hapo shauri lililofunguliwa na vyama vya wanasheria nchini humo kupinga marekebisho ya Sheria iliyiounda Tume hiyo isikilizwe kwanza na kutolewa maamuzi.

Marekebisho ya sheria hiyo yalilenga kwamba baada ya mchujo wa mteule wa Ujaji Mkuu Tume ipeleke kwa Rais majina matatu halafu yeye Rais ndiyo achague jina la mmoja tu ili lipelekwe Bungeni kuthibitishwa na baadaye Rais alitangaze. Wanasheria waliona utaratibu huo ungempa mwanya Rais kumpachika ‘mtu wake.’

Swali langu: Hivi kuna wananchi wangapi hapa nchini ambao hawatapenda utaratibu kama huu uwepo hapa nchini?