Home Makala Kimataifa ANC kuendelea kutikiswa na EFF

ANC kuendelea kutikiswa na EFF

1809
0
SHARE

HILAL K SUED NA MITANDAO

Chama cha upinzani nchini Afrika ya Kusini kinachokua kwa kasi ya ajabu – Economic Freedom Fighters (EFF) kimefanya mkutano wake mkuu wiki iliyopita mjini Pretoria uliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi, wengi wao wakiwa vijana na kutoa ilani yao ya uchaguzi tayari kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Mei mwaka huu.

Inaelezwa kwamba chama hicho kinatarajiwa kuwa mwiba kwa chama cha ANC katika uchaguzi huo hasa kutokana na utawala mbovu ulikithiri kwa ufisadi hususan katika kipindi cha utawala wa Rais Jacob Zuma.

Ilani ya chama hicho, kinachoongozwa na kiongozi wake machachari Julius Malema, inasema iwapo chama hicho kitafanikiwa kushinda na kuunda serikali kitaweka sera mpya ya ardhi ambapo ardhi na ajira zitagawanywa upya na hivyo kuwa kipaumbele kwa wananchi wazalendo ambao wako wengi bila ardhi.

Wafuasi waliofurika kwenye uwanja wa Giant Stadium katika kitongoji cha Soshanguve walimsikiliza rais wa chama chao Julius Malema akizindua ahadi zilizomo katika ilani hiyo, na alisema zimetokana na hali halisi ya nchi baada kushindwa kwa chama cha ANC katika kipindi cha robo karne kuwa madarakani.

Ilani hiyo iliyopewa jina la “Ardhi yetu na ajira sasa hivi” (Our land and jobs now), inasema kikiingia madarakani chama kitasitisha utegemezi wa serikali wa kutoa zabuni kwa makampuni na taasisi binafsi kwa ajili ya huduma zake, kitu ambacho, Malema anasema, kilitokana na sera mbovu za serikali katika kipindi cha utawala wa ANC, na hivyo kuunda alichokiita tabaka la ‘ujasirimali-zabuni’ (tenderpreneur class).

Alisema chama chake – EFF ni serikali inayosubiri kuapishwa na wananchi hawako tena kuwa tayari kuendelea kusubiri kupata ajira na ardhi, vitu viwili ambavo serikali ya ANC imeshindwa kabisa kuwapatia tangu 1994.

Alisema takriban asilimia 50 ya vijana hawana ajira na wengi wa wale waliajiriwa walikuwa wananyonywa na mawakala wa ajira, hivyo serikali yake italishughulikia suala hili mara moja.

Alisema rasimu ya ilani hiyo ya kurasa 170 itachapishwa kwa wingi na kusambazwa nyumba hadi nyumba mara tu baada yta mkutano huo wa uzindizi.

Aidha alisema kwamba ule aliouita ‘upuzi’ uliopo wa tofauti kubwa ya ya vipato kati ya wanawake na wanaume katika michezo utakomeshwa mara moja na serikali ya EFF.

Kuhusu Baraza la Mawaziri, Malema alisema litapunguzwa, na nafasi za manaibu mawaziri zitaondolewa na watu mahodari tu ndiyo watateuliwa kuwa mawaziri katika serikali ya EFF.

Katika hatua nyingine Malema alisema majengo na barabara zilizopewa majina ya aliyowaita “wabakaji wa kibaguzi” yatapewa majina mapya ya kizalendo.

Kufuatana na ilani hiyo, EFF ina mipango ya kuanzisha sera za ugawanyaji wa ardhi kwa watu wasiokua na ardhi kwa ajili ya kilimo, sehemu za kuishi na biashara. Aidha EFF itaanzisha sehemu maalum za viwanda kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa, kujenga upya sekta ya uzalishaji viwandani, na kuhakikisha madini yanayochimbwa nchini humo yatasaidia katika kuzalisha bidhaa kwa ajili nchini humo na pia kusafirishwa nje kutengeneza ajira.

Ruzuku kutoka serikalini zitaongezwa mara mbili wakati nyenzo za serikali zitatumika katika kuongeza ajira kwa kuhakikisha serikali inajijengea uwezo wake katika sekta ya ujenzi na nyinginezo, kuliko kuendelea kutoa zabuni kwa wazabuni binafsi kwa ajili ya shughuli hiyo.

Kutokana na hilo, Malema alisema hatimaye serikali yake itapunguza kabisa suala la ufisadi kutokana na kutowatumia washauri (consultants).

Kuhusu suala la utawala, ilani ya EFF inasema itaondokana na tawala za majimbo, na badala yake rasilimali nyingi zitaelekezwa serikali ya kitaifa na zile za mitaa.

Kuhusu suala gumu la ufisadi nchini humo, ilani ya EFF inasema itaanzisha mahakama za kuwashughulikia mafisadi na itaweka adhabu ya chini ya miaka 20 jela kwa kwa wanaotafuna fedha za umma na kuwalazimisha wazilipe.