Home Makala BARUA YA WAZI KWA CHADEMA: Magufuli haijui….. na Mbowe Naye…..

BARUA YA WAZI KWA CHADEMA: Magufuli haijui….. na Mbowe Naye…..

1765
0
SHARE

 

Rais John Magufuli (kulia) akisalimiana na Freeman MboweNa Mwinjilisti Kamara Kusupa

NDUGU zangu viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Nawaandikia barua hii nikijua mnajiandaa kuwaandamanisha Watanzania ifikapo Oktoba Mosi, mwaka huu sipendi siku hiyo iandikwe historia mbaya katika nchi yetu.

Sipendi vizazi vijavyo waje kuikumbuka Oktoba Mosi kwa mabaya kama yanavyokumbukwa mauaji ya Sherparville.

Sipendi Watanzania watakaoishi baada yetu waje kuikumbuka Oktoba Mosi kwa mabaya kama Wanyarwanda wanavyoyakumbuka mauaji ya kimbari.

Sote tunajua mauaji ya halaiki jinsi yanavyoiaibisha Afrika kwa kutuletea simanzi na matukano. Leo watu kama Donald Trump wanatukashifu kwa kusema hadharani, Waafrika tunatakiwa “tukoloniwe” upya kwa sababu tumeshindwa kujitawala.
Kauli ya Trump ni tusi jipya kwa Waafrika wanaothamini utu wao, ingawaje kauli hiyo imetolewa na mtu aliyelewa utajiri na nguvu za dola kuu ya Marekani na asiyeelewa uhalisia wa Afrika, bado kuna ukweli uliojificha nyuma ya kauli yake.

Inatakiwa dunia ifanye kitu kuwanusuru Waafrika “wanaokoloniwa” na Waafrika wenzao, watawala katili wanaoumiza wananchi wasioweza kuziondoa madarakani serikali mbaya. Trump hajui kuwa tayari Afrika inakoloniwa, inahitaji uhuru wa pili yaani ukombozi.

Chadema wengi mnanifahamu nami nawafahamu, wengine mnakumbuka jinsi wanamageuzi tulivyokutana mwaka 1991, tulivyopendekeza majina mengi ya chama kipya likiwemo Chadema, tulivyomwita Mzee Edwin Mtei arudi nchini kutoka Washington Marekani na alivyoamua kulichukua jina hili akaasisi chama kilichodumu hadi leo.
Lengo langu ni kulinda dhana ya upinzani kwa sababu tangu mwanzo tulipoanzisha mageuzi tuliweka wazi upinzani si uadui. Namwona Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe haijui Serikali na Rais wetu John Magufuli haijui siasa.
Mbowe hajawahi kushika madaraka ya kiserikali wala hajafanya kazi serikalini akaujua utendaji wa serikali ulivyo na maana halisi ya utawala. Dk Magufuli kabla hajawa Rais hakujishughulisha na siasa ingawa alikuwa Mbunge baadaye akawa waziri. Ubunge si kazi ya kisiasa na uwaziri haungemfanya awe mwanasiasa, mara zote Dk Magufuli alipogombea ubunge alibebwa na umaarufu wa CCM iliyobebwa na dola. Mazingira hayo yalimfanya Dk Magufuli apande juu kirahisi pasipo kupitia ushindani mkali ambao ungemwezesha kuielewa siasa.
Matokeo ya Rais Magufuli kutoijua siasa yanamfanya awe tayari kutumia nguvu za dola kupita kiasi kushughulikia masuala mepesi ya kisiasa ambayo kama angekuwa mwanasiasa angeyamaliza kwa kutumia mbinu rahisi na ufundi wa kisiasa. Lakini kinyume chake Magufuli anayakabili matatizo ya kisiasa akitumia “ukali wa kiserikali.”

Hili litailetea Tanzania maafa yatakayoitia doa historia ya nchi yetu.
Rais Magufuli sasa akiwa Mwenyekiti wa CCM hawezi kuiepuka siasa wala hawezi kutenganisha shughuli za kisiasa na wadhifa wake kama mkuu wa dola. Hali hiyo inaibua matatizo kwa kuwa Tanzania iliukubali mfumo wa vyama vingi, enzi za mfumo wa chama kimoja kofia mbili hazikuonekana tatizo.
Inabidi viongozi wa CHADEMA, wanachama wa vyama vya upinzani na Watanzania kiujumla, kuelewa kwamba hakuna ufundi utakaomtenganisha Rais na shughuli za kisiasa, hawezi kuuvua Urais wake akabaki Mwenyekiti wa CCM tu ili afanye shughuli za kisiasa akifuata kanuni na taratibu za siasa.

Hapa ndipo Rais Magufuli anajikuta akiingiza “userikali” kwenye siasa na kusababisha matokeo hasi, mambo madogo yanayostahili kumalizwa kisiasa Rais anataka ayamalize kwa nguvu za dola.
Rais Magufuli ameshindwa kuyasoma mazingira ya “siasa na utawala” kwenye nchi anayotawala ili aelewe atakavyozitumia kofia zake mbili ya Urais na Uenyekiti. Tatizo la kiufundi likijumlishwa na marufuku aliyoitoa Rais, litaiathiri hata CCM yenyewe, hatimaye makada wake watajikuta hawafanyi kazi za siasa maana hakuna shughuli za kisiasa zisizohusisha umma.
Mbowe haielewi serikali maana angeielewa serikali katika uhalisia wake na pia angejua ipo siku aidha yeye mwenyewe ama mwanachama mwingine wa CHADEMA anaweza kuongoza serikali, asingefanya haraka kuwahamasisha Watanzania wainuke dhidi ya serikali inayotawala nchi yao.
Nimeusoma waraka wa Kamanda Mbowe, hakuna mwenye uhakika Tanzania itakuwaje baada ya Oktoba Mosi, nayaweka wazi yaliyojificha ili Mbowe akiyaona abadilishe uamuzi, asiwaandamanishe tena Watanzania.

Serikali inaendeleza msimamo wake, Chadema nayo inaendelea na dhamira yake, kwa hiyo ifikapo Oktoba Mosi dunia itashuhudia majeshi mawili yakipambana. Jeshi linaloongozwa na Kamanda Mbowe aliyewahamasisha Watanzania kuungana kuunda ngumi ya chuma anayoiita “people’s power.”

Hiyo nguvu itapambana na jeshi la polisi ikiwezekana hata Jeshi kuu yote yakiwa chini ya Amiri Jeshi Mkuu Rais Magufuli, anayetaka Watanzania waitii marufuku aliyoitoa kama Rais hapo alipoagiza vyama vya siasa visubiri hadi 2020.
Hayo yakitokea yatakuwa mapambano ya Watanzania wenyewe kwa wenyewe, mwisho wake hakuna jeshi litakaloshinda, historia imethibitisha yatokeapo mapambano ya wenyewe kwa wenyewe kila upande hupoteza na kupata hasara.

Tunaoitakia mema Tanzania tunalazimika kusema hapana, hali ya Rais Magufuli na Mwenyekiti Mbowe kukosa uelewa isituingize kwenye gharama kubwa na hasara isiyoweza kufidiwa.
Mbowe na Watanzania wengine waelewe fika serikali ni yetu sote, maana yake halisi “wananchi tumezikusanya nguvu zetu tukazirundika pamoja ili zitulinde pia ziilinde nchi.”

Kwa kuwa tumezikusanya nguvu zetu pamoja tukamrundikia mtu mmoja anayeitwa Rais wa nchi, hakuna uhalali sisi kuanza tena kupambana na nguvu yetu wenyewe hata kama huyo tuliyemrundikia akituonyesha amepotoka.

Hakuna uhalali wa kusigana na Rais “direct confrontation” hata tukimgundua kuwa amepagawa na pepo mchafu sawa na yule Mfalme Sauli anayesimuliwa katika Biblia kwamba alipoacha kumtii Mungu, naye Mungu alimwacha, akaruhusu ashukiwe na “rohochafu” iliyomsumbua mara kwa mara.

Kwa kuwa serikali ni nguvu yetu tuliyoirundika pamoja itumike kwa manufaa yetu, tukiinuka kusigana na huyo tuliyemrundikia nguvu yetu, maana yake tutakuwa tunapambana naye tukitumia nguvu nyingine iliyoundwa pembeni, hiyo itakuwa jinai isiyokubalika mbele ya Mungu na mbele ya wote mwenye akili timamu.

Kwa sababu Watanzania watakuwa wanailazimisha nguvu yao inayoitwa serikali iinuke kufanya kazi ya kuwaletea madhara na hasara isiyoweza kufidiwa kwa namna yoyote. Hapa linaibuka swali je; tufanye nini tuonapo nguvu yetu ikitumika kwa namna tusiyoridhika? zipo hatua mbili kabla ya kuyafikia mapambano.

Itaendelea wiki ijayo……