Home Habari BBI, kura ya maoni kupandisha joto la siasa Kenya

BBI, kura ya maoni kupandisha joto la siasa Kenya

2276
0
SHARE
Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga (kuhoto), akiteta na mwenyekiti wa kamati ya jopo kazi ya BBI ambaye pia ni Seneta wa Garissa, Yusuf Haji.

NA ISIJI DOMINIC


ZIKIWA zimebaki miaka miwili kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Kenya, joto la siasa limeshaanza kupanda huku wanasiasa wakirushiana cheche za maneno.

Ndani ya chama tawala cha Jubilee, hali si shwari kufuatia wanasiasa wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuvamia makao makuu ya chama hicho wakitishia kushinikiza kufanyika uchaguzi kuteua viongozi wapya.

Kitendo hicho kilitafsiriwa kufanya mapinduzi wakati kiongozi wa chama cha Jubilee ambaye pia ni Rais Uhuru Kenyatta akiwa kwenye ziara ya kikazi nchini Ufaransa. Siku moja baada ya tukio hilo, Kamati ya Usimamizi ya Kitaifa ya chama cha Jubilee kilipendekeza Kamati ya Utendaji ya Kitaifa ambacho ndicho chombo kikuu chenye maamuzi kumtimua Naibu Rais Ruto ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Raphael Tuju, alisema Ruto amevuka mipaka na kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakitazama matendo yake ambayo yanavishiria vya kampeni kuelekea 2022 katika wakati ambapo Rais Uhuru amekuwa akisisitiza kuelekeza nguvu kwa miradi ya maendeleo.

“Tumekuwa tukimuona akizunguka nchi na kuzindua vuguvugu la ‘hustler’. Hii yote ni kampeni na dhihirisho la wazi la kumpuuza Rais,” alisema Tuju.

Katika kile ambacho kinaonekana ni dalili mbaya za kuibuka machafuko kuelekea uchaguzi mkuu 2022, watu wawili walipoteza maisha baada ya pande mbili kuanza kushambuliani hivi karibuni, Naibu Rais alipozuru eneo la Kenol katika kaunti ya Murang’a kwa ajili ya ibada ya Jumapili.

Inadaiwa kuna kundi ambalo halikutaka Ruto kwenda Murang’a hivyo kuanza kukabiliana na kundi lililomkaribisha. Polisi wanaendelea kufanya uchunguzi huku viongozi wa dini na watetezi wa haki za binadamu wakiwataka wanasiasa kuacha kufanya kampeni kwa sababu uchaguzi mkuu ni miaka miwili ijayo.

Moja wa wanasiasa ambao wamelaani vikali vurugu za Kenol na kutaka shughuli zozote zinazohusu kampeni kusitishwa ni kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, japo naye anajiandaa na kufanya kampeni pindi ripoti ya Building Bridges Initiative (BBI) itakapozinduliwa.

Raila na wale ambao wanaunga mkono BBI walikuwa wanazunguka nchi nzima kuipigia debe ripoti hiyo inayotajwa kutoa mustakabali wa kura ya maoni kabla ya Serikali kusitisha mikusanyiko ya aina yoyote kufuatia kuzuka kwa janga la virusi vya corona.

Mapema mwezi huu, Serikali ya Kenya ilitangaza kulegeza masharti yaliyowekwa kupambana na covid-19 japo tayari Wakenya walikuwa wameshaanza kushuhudia mikutano ya siasa pasipo kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya.

Raila ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), alidokeza kuwa ripoti ya BBI itazinduliwa hivi karibuni na kuweka mazingira ya kufanyika kura ya maoni.

“Ripoti ya BBI ipo tayari na ni suala la muda tu. Mimi na Uhuru tutaipokea na kuiweka hadharani ili kila mtu aweze kusoma. Hivyo huwa napigwa na butwaa ninaposikia baadhi ya watu wakiiponda. Hivi unawezaji kupinga kitu ambacho hujakiona?” alihoji Raila akiwa katika Kanisa la United Christian Ministries iliyopo Kawangware jijini Nairobi katika eneo bunge la Dagoretti Kaskazini.

Hadi sasa hakuna anayejua nini kilichopo kwenye ripoti hiyo ukizingatia BBI iliundwa baada ya Rais Uhuru na Raila kuzika tofauti zao Machi 9, 2018. Hata hivyo wanaomuunga mkono Ruto wanadai ripoti hiyo inalenga kuongeza nafasi za madaraka.

Wanasiasa waliyoandamana na Raila wakati anadokeza kuzinduliwa ripoti ya BBI hivi karibuni walikuwa wabunge Simba Arati (Dagoretti Kaskazini), Elisha Odhiambo (Gem), George Aladwa (Makadara), Tom Kajwang’ (Ruaraka), Justus Kizito (Shinyalu), Mpuru Aburi (Mbunge wa Afrika Mashariki) na wabunge wakuteuliwa Dennitah Ghati, Maina Kamanda na Gertrude Musuruve.

Kamanda alimuidhinisha Raila kuwania urais mwaka 2022 akisema nchi ipo tayari kwa uongozi wake.

“Haturudi nyuma tena. BBI ndiyo suluhisho ambayo tulikuwa tunaisubiri. Huu sasa ndiyo muda wa BBI,” alisema Kamanda.

Hata hivyo maswali bado yanaulizwa hususan na wanaoipinga ripoti ya BBI wakihoji ni kwanini inachukua muda mrefu kwa ripoti hiyo kupokelewa na Uhuru na Raila.   

Katibu Mkuu Msaidizi wa Jubilee ambaye yupo kwenye mrengo wa Naibu Rais Ruto, Caleb Kositany, alisema watetezi wa BBI wameingiwa na uogo kuiweka wazi ripoti hiyo.

“Hatujui chochote kuhusu ilipo BBI. Tunachofahamu ni Raila anaongea sana kuhusu ripoti hiyo na yeye ndiye anayejua zaidi,” alisema Kositany ambaye pia ni mbunge wa Soy huku makatibu wenza wa kamati ya BBI, Balozi Martin Kimani na Paul Mwangi, wakisisitiza ripoti hiyo iko tayari.

“Tutashauriwa na vinara wawili hatua inayofuata,” alisema Kimani huku Mwangi akiongeza kuwa jukumu lao lililobakia ni kuwasilisha ripoti.

Kucheleweshwa kutoka kwa ripoti hiyo kumehusishwa na kuvuta subira hadi Serikali ijiridhishe na kupungua kwa maambukizi ya covid-19 ukizingatia pindi ripoti hiyo ya BBI itakapotoka itafungua tena ukurasa mpya wa kampeni sawa na ilivyokuwa kuelekea kupitishwa Katiba mpya 2010 ambapo kulikuwa na makundi mawili; yanayopinga na yanayounga mkono, zote zikizunguka nchi nzima kufanya kampeni.

Katika moja ya hotuba zake kwa taifa, Rais Uhuru alisema Katiba ya Kenya ambayo sasa ina miaka 10 tangu ilipopitishwa, imefika muda muafaka kufanyiwa marekabisho.

Raila ameiambia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujiandaa kufanyika kura ya maoni pindi tu yeye na Rais Uhuru watakapokabidhiwa ripoti ya BBI.

Katika kile kinachoonekana kupunguza gharama, baadhi ya wanasiasa kutoka kundi la Tangatanga linalomuunga mkono Naibu Rais Ruto wanataka kura hiyo ifanyike pamoja na uchaguzi mkuu 2022.

“Walisema reggae imesimama. Haijasimama. Bado ni kipindi cha kwanza. Wachezaji wamekuwa wakikandwa na kupata maelekezo kutoka kwa makocha,” alisema Raila wakati wa kuwaapisha maofisa wapya wa bodi ya uchaguzi na kamati ya nidhamu ya chama cha ODM.

Raila alisema fedha ipo na hawawezi kumfundisha Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, namna ya kufanya ila watamuonyesha namna inavyofanywa.

Chebukati mwenyewe alinukuliwa na moja ya chombo ya habari nchini Kenya akisema kura ya maoni inaweza kufanyika muda wowote ilimuradi mchakato unazingatia vipengele vya katiba, sheria ya kura ya maoni na kanuni zingine.

“Tume iko tayari kutekeleza agizo hili la kikatiba baada ya kupokea notisi ya kutosha na mgawo wa bajeti kwa shughuli hizo,” alisema bosi huyo wa IEBC.