Home Habari ‘Busara zitumike kulimaliza hili la CAG, Spika’

‘Busara zitumike kulimaliza hili la CAG, Spika’

2261
0
SHARE

Jimmy Charles

KWA zaidi ya wiki sasa kumekuwa na mnykano na mvutano wa maneno kati ya Sipika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mussa Assad.

Sababu ya mzozo huu inatajwa kuwa ni hatua ya CAG kutumia lugha iliyotazamwa vibaya na Spika na kutakiwa kujieleza mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili.

CAG, alikwenda mbele ya kamati hiyo na kutoa maelezo yake, ambayo yalionekana kutowaridhisha waliomuita na kuamua kumchukulia hatua ya kumsusa kwa maana Bunge liliazimia kutofanya kazi na kiongozi huyo.

Uamuzi huo uliibua mvutano mkubwa miongoni mwa wanasiasa, wasomi na hata wachambuzi wa mambo, wengi wao wakiamini kuwa kitendo cha Bunge kumsusa CAG ni sawa na kuvunja sheria ambayo inatambua nafasi hiyo kikatiba.

Baada ya mvutano wa muda mrefu hatimae Bunge liliipokea ripoti ya CAG, na kuiwasilisha bungeni, hata hivyo mzozo huop uliondelea na kuonekana kuvaa sura ya mvutano binafsi kati ya Ndugai na Assad.

Kutokana na umuhimu wa watu hao wawili hasa kwa kuzingatia nafasi wanazoziongoza RAI liliiona haja ya kufanya mahojiano na mmoja wa wanasiasa wakongwe nchini, Mudhihir Mudhihir ambaye alishawahi kuwa Mbunge wa Mchinga kupitia Chama Cha Mapinduzi.

Ufuatao ni mtiririko wa maswali na majibu ya mahojiano hayo. Endelea:

RAI: Kumekuwepo hili sakata la vuta nikuvute baina ya Spika wa Bunge la Tanzania na CAG kwa muda sasa. Badala ya mvutano huu kupoa ndiyo kwanza unapamba moto. Wewe ukiwa ni mwanasiasa mkongwe nini maoni yako ya jumla.

Mudhihir:  Huu ni mtihani mkubwa kwetu Watanzania. Unajua linapotokea jambo usikimbilie kulitazama jambo lenyewe bali watazame wahusika katika jambo hilo.Kwa kuzitazama busara na hekima za Mheshimiwa Spika na CAG, na kwa kuzitazama dhamana walizopewa na sisi Watanzania wenzao, sipati jawabu kwamba neno “UDHAIFU” lingeweza kulifikisha Taifa letu hapa walipotufikisha.

RAI; Ungepewa nafasi ya kushauri juu ya namna bora ya kulitatua tatizo hili kiungwana, ungependa nini kifanyike.

Mudhihir; Sisi  Watanzania tunayo mambo makubwa na muhimu tunayotaraji kuyasikia kutoka kwa Spika na CAG. Wanaziongoza Taasisi kubwa zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba na zenye majukumu muhimu ya kuishauri na kuisimamia Serikali. Bunge na NAO ni Taasisi zinazojenga nyumba moja na kwa hivyo hazipaswi kugombea fito tena hadharani. Hivi sasa zinapewa kipaumbele habari za U – Ndugai na U – Assad badala ya habari za maendeleo na huduma za kijamii.

RAI: Unaonekana kukwazika kutokana na habari hizi kupewa umuhimu katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Mudhihir: La! Hasha! Mimi sina ngowa na starehe za watu. Kinachosumbua akili yangu ni kutaka kufahamu iwapo Spika na CAG wanatambua kwamba Taasisi wanazoziongoza ni mamlaka za umma. Hivyo ni kweli kuwa hakuna njia bora ya kuliendea suala hili ila ni kulembeana vimondo mbele ya wanahabari? Wanaamini kuwa kwa kutumia njia hii ndiyo wataifikia suluhu ya mvutano wao?

RAI: Nini maoni yako juu ya Bunge letu kudhaniwa kuwa ni dhaifu.

Mudhihir: (kicheko). Wewe unanitaka nikae upande upi kati ya upande wa Mheshimiwa Spika na ule wa ndugu yangu Profesa Assad. (kicheko). Unajua swali lako ndugu yangu ni muhimu sana na ili jibu la swali lako liwe muhimu pia na lenye manufaa,  linatakiwa lisihusishwe na kuzishobokea pande zinazovutana. Aidha, ni muhimu pia kuzikimbia tafsiri za kikamusi.

RAI: Mheshimiwa sijakufahamu vizuri. Sasa huo udhaifu tutakao uzungumza nje ya pande hizi mbili na nje ya tafsiri ya kamusi, si utakuwa udhaifu mwengine mpya wa kuja kuchochea moto ambao tayari unawaka.

Mudhihir: (kicheko). Unanipa kazi ya kurina asali na papo unanihurumia ati nisije kutafunwa na nyuki (kicheko). Unajua Bunge kwa mujibu wa Katiba yetu linaundwa na Wabunge wanaowakilsha majimbo, viti maalumu na wanaoteuliwa na Rais. Waheshimiwa wote hawa ni wanadamu ambao wao na sisi sote hatuna ukamilifu. Sijui kwa nini neeno UDHAIFU limetufikisha hapa tulipo. 

Wabunge wetu wanayo majukumu ya kutuwakilisha wananchi wenzao Bungeni, kutunga sheria, kuishauri Serikali juu ya mwelekeo wenye maslahi kwa wananchi na Taifa, na kuisimamia Serikali katika kutekeleza majukumu yake. Sitaki kutilia shaka juu ya kuwepo kwa udhaifu kwa mbunge yeyote eti kutokana na sababu za ubinadamu. Sipendi kuwakosea adabu waheshimiwa ambao kabla ya kuanza kiko husoma dua ili kujilinda dhidi ya udhaifu wa kibinadamu.

Pili, upo utamaduni wa Kibunge kuwa na mikutano ya vyama(Party Caucus). Ndani ya mikutano hii agenda kubwa huwa ni kujenga msimamo wa pamoja ili kuunga mkono au kupinga hoja ndani ya Bunge. Mbunge mmoja mmoja anatakiwa kuachana na anachokiamini. Sisemi kuwa utamaduni huu ndani ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola unachangia udhaifu wa Bunge, lakini hapana ubishi pia kuwa hisia na matakwa binafsi hudhoofishwa na athari ya msimamo wa pamoja. 

Tatu, mahitaji ya majimbo na hata ya kikanda hasa wakati wa Bunge la Bajeti huwaparaganya Wabunge wakasahau mambo ya msimamo wa chama na hata msimamo wa utaifa. Wengine hufikia kukamata shilingi kutoka mshahara wa Waziri. Lakini siku yakupitishwa bajeti ni msimamo wa Chama ndiyo utakaomuongoza Mbunge kupiga kura ya sauti ya ndiyo au hapana. Kimuundo tunaona kuwa huu ni udhaifu lakini bila bajeti nchi itaendeshwaje!

Na nne, ni utamaduni wa CCM kumteua Spika anayetokana na chama hicho kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu. Hata kama Spika atakuwa ba msimamo usiyoyumba hawezi kuwa yeye ana nguvu na Chama kikawa dhaifu. Kwa hakika isiyo na shaka udhaifu unaosababishwa na tamaduni za Kibunge duniani kote hauepukiki. Ndiyo maana naendelea kujiuliza iwapo upo ulazima wa kuendelea kutoleana povu juu ya neno “UDHAIFU” kwenye vyombo vya habari. 

RAI: Mheshimiwa umezungumza sana. Ni nini hofu yako juu ya jambo hili kuendelea kuzungumzwa kwenye vyombo vya habari.

Mudhihir: (kicheko). Na wewe una raha gani juu ya jambo hili kuendelea kunogeshwa kila kukicha (kicheko). Tulikotokea tulianza na neno UDHAIFU  kulichafua Bunge nje ya nchi. Ngoma ilipochanganya mashairi yakasema Bunge halina ugomvi na CAG wala NAO bali halimtaki Profesa Assad. Zikafutia nyanga za kumtaka Profesa Mussa Assad ajiuzulu ili asimletee  Mheshimiwa Rais shida. Sasa zinapulizwa zumari za kumshabihisha Profesa Assad na ujasiri wa mbwa kuutafuna mkono wa bwana anayemlisha. Baada ya haya yatakuja mengine yapi? Haya ndiyo yanayonitia hofu.

RAI: Una neno la nyongeza Mheshimiwa. 

Mudhihir: Nchi yetu sasa ipo katika ubora wake na nguvu zetu zote tunazielekeza katika kutuletea ustawi wa kiuchumi na huduma za kijamii. Mataifa mengi barani Afrika na huko Ughaibuni yanatukubali na sisi hatuna budi kuyalinda mafanikio yetu kwa huba na wivu mkubwa. Viongozi wetu  wajiepushe na ujasiri wa mambo ya kuzungumzwa chumbani kuyahamishia varandani. Tunaelekea kwenye kuijenga nchi chonde wasitutoe barabarani.

RAI: Tumalizie mahojiano kwa kuangalia iwapo Rais anao uwezo wa kulimaliza tatizo hili.

Mudhihir: Ndiyo. Mheshimiwa Rais anao uwezo wa kulimaliza suala hili kwa salama na amani. Sizungumzii uwezo wa Rais kikatiba kwa kuwa jambo lenyewe halijafikia upeo wa kukiukwa Katiba. Mheshimiwa Rais amesheheni busara na hekima. Waheshimiwa Wabunge waliyomsusa Profesa Mussa Assad ni wa CCM na Rais ni Mwenyekiti wa CCM Taifa. Na halafu Profesa Assad ameteuliwa na Rais huyo huyo. Lakini Mheshimiwa Spika na CAG ni watu wanaojitambua. Ndiyo, Mheshimiwa Rais anaweza kulimaliza sakata hili.

Pili, upo utamaduni wa Kibunge wa kuwa na mikutano ya vyama (Party Caucus).