Home Afrika Mashariki CCM inastahili kupumzishwa

CCM inastahili kupumzishwa

3927
0
SHARE

TANZANIA ina ukubwa wa eneo la ardhi mita za mraba milioni 364,915. Kenya ina ukubwa wa mita za mraba milioni 224,962, Uganda mita za mraba milioni 91,136, Rwanda mita za mraba milioni 10,169 na Burundi mita za mraba 10,745.

Tanzania pekee ndiyo nchi kubwa kuliko nchi zote za Afrika Mashariki. Nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zikijikusanya kwa pamoja zinakuwa na jumla ya eneo la mita za mraba milioni 337,012. Kwa hiyo ukiigawa Tanzania utapata nchi nne zenye ukubwa sawa na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi na litabaki eneo lenye ukubwa wa mita za mraba milioni 27,903 eneo ambalo linaweza kutengeneza nchi nyingine yenye ukubwa sawa na Togo. Hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Tanzania ni sawa na nchi tano.

Yaani Tanzania ni nchi moja yenye nchi tano ndani yake. Hivyo basi rais anayeweza kuongoza taifa hili na kuleta maendeleo lazima awe rais mmoja lakini mwenye akili za marais watano. Yaani awazidi akili mara tano akina Uhuru Kenyatta, Yoweri Museveni, Pierre Nkurunziza na Paul Kagame.

Marais wote wa Afrika Mashariki wanapokuja Tanzania wanapaswa kujiona ni kama wakuu wa mikoa. Na ili wajione hivyo lazima kuwe na hatua kubwa za kimaendeleo kuliko kwao. Kagame akija hapa akikuta treni za umeme (kwake hana), akikuta Hospitali za kisasa watu wanatoka Asia kuja kutibiwa hapa (kwake hakuna), akikuta Barabara za juu katika miji mikubwa (fly over’s), akikuta maslahi mazuri kwa watumishi, akikuta umeme wa uhakika na tunalipa TZS 3000 kwa mwezi, akikuta elimu ni bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, lazima ajione nafasi aliyonayo nchini mwake ni sawa na nafasi ya ukuu wa mkoa nchini mwetu.

Kama Kagame nchini kwake ana fly over’s (sisi hatuna), wanafunzi wa Rwanda wana loptop kuanzia shule ya msingi (sisi hatuna), Elimu ya sekondari bure (sisi tumeshindwa), halafu akituangalia tuna bandari, madini, gesi, mlima Kilimanjaro na mbuga za wanyama lazima amuone rais wetu kama “diwani”.

Licha ya Tanzania kuwa ni nchi yenye rasilimali lukuki lakini ndiyo inayoongoza kwa kukata kodi kubwa kwa watumishi wake kuliko nchi zote za Afrika Mashariki. Serikali kila mwisho wa mwezi inajikusanyia asilimia 18 ya mishahara ya watumishi kana kwamba haina chanzo kingine cha mapato zaidi ya kunyonya watumishi. Rwanda isiyo na rasilimali nyingi kama nchi yetu, watumishi wanalipa asilimia sita kama kodi kwenye mishahara yao.

Yaani mtumishi anayelipwa Sh. 700,000 kwa mwezi nchini anakatwa Sh.108,000 kama kodi. Wakati mtumishi anayelipwa mshahara kama huo nchini Rwanda anakatwa Sh. 36,000 tu kama kodi. Rwanda ambayo haina gesi, haina bandari, haina madini inawajali watumishi wake. Tanzania yenye gesi, mlima, madini, bandari haitaki kutoza kodi huko kote badala yake inamnyonya mtumishi kama vile serikali haina chanzo kingine cha mapato zaidi ya kodi za watumishi.

Hivi mantiki ya kumtoza mtumishi asilimia 18 ya kodi ni ipi wakati kuna vyanzo vingi vya mapato nchini? Unatoa msamaha wa kodi kwa wawekezaji wa madini na wachimbaji wa gesi, halafu unakazana kumnyonya mtumishi. Hii ni kukosa akili. Mwaka huu Tanzania imepoteza Sh. Trilioni 4.7 kutokana na misamaha ya kodi, hii ina maana kwamba ni karibu robo ya bajeti.

Makadirio ya gharama za kusomesha watoto wetu kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu kwa mwaka ni Sh. Trilioni 1.6 (kwa mujibu wa Mbatia). Maana yake ni kwamba tukipunguza misamaha ya kodi kwa mwaka mmoja tu, tunapata fedha za kutosha kusomesha wanafunzi wote wa shule za msingi hadi chuo kikuu kwa miaka miwili.

Lakini serikali ya CCM haiwezi kuliona hili kwa sababu ya ufinyu wa uelewa. Mtumishi yoyote anayeiunga mkono CCM yafaa akapimwe uwezo wake wa kufikiri. Fikiria mwalimu unalipwa Sh. 700,000 kwa mwezi kodi tu ni Sh.108,000, Pensheni Sh.70,000 sawa na asilimia10, UWT Sh. 21,000 sawa na asilimia 03 mwisho wa siku anapokea Sh. 498,000. Kwa mtazamo hapo utaona jinsi serikali ya CCM inavyomnyonya mwalimu bila huruma. Pamoja na madhila yote hayo bado baadhi ya watumishi wanaimba wimbo wa “ CCM ni ile ile” au “CCM mbele kwa mbele”.

Ikimbukwe kwamba makato yote hayo bado mtumishi huyo anapaswa kulipa kodi ya nyumba, maji, umeme, ada ya watoto, nauli, chakula na mavazi. Hali kama hiyo kwanini usiwe maskini? Kwanini usikope kabla ya tarehe 05? Hivi unadhani waalimu wanapenda kuwa na “vidaftari” vya mkopo kwenye maduka ya kina mangi? Serikali ya CCM ndiyo inawalazimisha kudhalilika Sasa mwaka huu iwe mwisho. Uwezo wa kufanya mabadiliko uko mikononi mwako Mtanzani, suluhisho la matatizo hayo ni kumchagua Lowassa kuwa rais ili maisha ya Watanzania yaweze kulingana na ukubwa wa taifa hili na rasilimali zilizopo. Miaka 50 ya utawala wa CCM imetosha.

Let them rest in peace. Magufuli hana uwezo wowote wa kufanya mabadiliko yoyote ndani ya CCM. Haiwezekani CCM hii iliyowatesa Watanzania zaidi ya miaka 50 leo ilete neema kwa sababu ya Magufuli. Hakuna nadharia yoyote ya kisayansi duniani inayoweza kuthibitisha kuwa gari bovu lililoshindwa kutembea kwa miaka 50, linaweza kukimbia spidi 120 likipata dereva mpya.

Tanzania inahitaji rais mwenye akili za marais watano, ili marais wengine wa Afrika Mashariki wakimuona wamuogope na wamheshimu kwa kasi ya maendeleo atakayotuletea. Hakuna ubishi kwamba Lowassa ndiye anayeweza kuivusha nchi hii na kufikia nchi ya kupigiwa mfano katika maendeleo ya kiuchumi.