Home kitaifa CCM wamejitekenya na kucheka wenyewe Zanzibar

CCM wamejitekenya na kucheka wenyewe Zanzibar

3469
0
SHARE

RAI-KATUNIHATIMAYE uchaguzi wa marudio uliokuwa umepangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu umemalizika na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein amefanikiwa kutetea nafasi yake ya urais kwa asilimia 91.

Kwangu sina tatizo na ushindi wa Dk. Shein kwa sababu naamini hakuna Mtanzania aliyetarajia matokeo kuwa tofauti na hayo  kutokana na chama hicho kuingia kwenye uchaguzi bila ya kuwepo kwa mahasimu wao wa kisiasa CUF.

Uchaguzi huo ungekuwa mgumu kubashiri hasa nani angeibuka kuwa rais wa visiwa hivyo kama CUF chini ya Maalim Seif Sharif Hamad kingeingia kwenye uchaguzi huo wa marudio.

Uwepo wa mgombea wa urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif umeonekana kuwa mwiba kwa CCM, jambo ambalo linafanya hata baada ya kutangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo ilikuwa ni ahueni kwao.

Upepo ulioonyeshwa na CUF kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ulikuwa ni salamu tosha kwa CCM wa kujipima na kuona kwamba walikuwa na kazi kubwa katika kuangusha ngome ya chama hicho.

Pamoja na Dk. Shein kutangazwa kuwa mshindi kwa kupitia uchaguzi ambao kimsingi wapenda demokrasia wengi ndani na nje ya nchi hatukufurahishwa nao kutokana na kutoshiriki kwa chama kikuu cha upinzani visiwani humo cha CUF.

Kutoshiriki kwa CUF katika uchaguzi huo imekuwa ni doa kwa sababu ikumbukwe kwamba kina wapenzi na wanachama wengi hivyo ilitakiwa ifanyike jambo lolote litakalowezesha kuhakikisha amani inasalia visiwani humo kwa kushirikisha chama hicho.

Wapo watakaosema kwamba uchaguzi huu ni wa kidemokrasia kwa sababu imeshirikisha vyama vingi vya siasa vya visiwani humo.

Kwangu ushiriki huo wa vyama vingi vya upinzani nimekuwa nikiutilia shaka kama ambavyo inatiliwa shaka na kuwahi kuzungumzwa na wapenzi, viongozi na wadau wa siasa nchini.

Sababu kubwa ya wengi kutilia shaka akiwemo mimi mwenyewe ni ukigeugeu waliouonyesha vyama hivyo vilivyoshiriki kwenye uchaguzi huo ambako hapo awali walitangaza kutoshiriki kwenye uchaguzi huo wa marudio lakini siku chache kuelekea uchaguzi huo wakabadili msimamo na kukubali kushiriki.

Jambo hilo kwa mtu mwenye kufikiri sawasawa lazima ujiulize kwa nini kwa muda mrefu tangu kufutwa kwa uchaguzi huo mwaka jana wamekuwa wakishikiria msimamo wa kutoshiriki, je ni kwanini siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio wakubali kuingia?

Naamini kwa mtu mwenye akili anayetafakari atakuwa amejua mambo yanayoweza kuwakengeusha wanasiasa wengi pindi wanapokuwa wanaonyesha kuwa na msimamo mkali.

Wapo baadhi ambao hushawishiwa kwa kupewa rushwa za fedha na wengine hupewa ahadi ya  rushwa ya vyeo kama serikali husika pindi itakapofanikiwa kuingia madarakani.

Ili kuepusha Zanzibar kuingia kwenye vurugu ambazo siombei zitokee ni lazima waachane na kukalia kushabikia ushindi huu ambao ulikuwa haukuwa na mshindani na badala yake watafute namna ya kuwaondolea kinyongo CUF.

CCM wakumbuke kwamba wao wakati wanafurahia ushindi huo, wajue CUF wamebaki na kinyongo ambacho wanaamini kwamba walipokonywa ushindi wao katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.

Hadi sasa hakuna anayejua hasa wanachama, viongozi wa chama hicho wanafikiria nini baada ya Shein kuingia Ikulu katika njia ambayo kwao wanaichukulia kama kuwapokonya haki yao.

Sababu hiyo ndiyo iliwafanya hata wao kuona tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha la kutangaza uchaguzi wa marudio ni muendelezo wa tamko batili la kufuta uchaguzi alilolitoa Oktoba 28, 2015.

Hadi kesho bado CUF wanaamini Oktoba 25, 2015 ndipo uchaguzi ulipomalizika na kuwapata Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani ambapo washindi wakapewa shahada za kuwathibitisha na kuwatambua.

Kazi aliyobakisha Shein na serikali yake kuieleza CUF ni kwa vipi uchaguzi ule ulifutwa wakati matokeo yote ya vituo 54 yalikuwa yameshabandikwa nje ya vituo ili waweze kuamini kweli uchaguzi ule ulikuwa na tatizo.

Kazi nyingine wanatakiwa kuifanya ni kuwaonyesha kifungu cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar inachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio jambo ambalo wanaamini halipo.

Kama watawaacha na kuendelea kuwa na imani hiyo maana yake ni kwamba hawatakuwa wakimtambua rais Shein kama rais wa nchi hiyo jambo ambalo litakuwa hatari kwa mustakabali wa nchi hiyo.

Jambo jingine wanalotakiwa kufanya ni kuwarejeshea imani yao kwa Rais John Magufuli kwamba yuko pamoja nao na hata kitendo chake cha kujitoa kwenye utafutaji wa suluhu wa jambo hilo haikuwa kukwepa dhamana na wajibu wake kama Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu.

CCM hawatakiwi kwa sasa kujitekenya na kucheka wenyewe bali wakumbuke kwamba kazi iliyo mbele ya  Rais Shein ya kuwakusanya na kuwafanya Wazanzibar kuwa wamoja ni kubwa kuliko ushindi mnono na wa kilaini walioupata kwa kuvishinda vyama dhaifu.