Home Makala Changamoto za elimu ya juu zinahitaji mjadala wa Kitaifa

Changamoto za elimu ya juu zinahitaji mjadala wa Kitaifa

2044
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

MWAKA 2002 kijana ajiitaye D-Knob aliimba wimbo wenye mahadhi ya kufokafoka akauita ‘Elimu ya Mtaani’. Wimbo huo ulipata umaarufu na ulipendwa kusikilizwa na wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Huo ulikuwa ni mwaka ambao Bunge la Jamhuri ya Muungano lilikuwa likijadili Muswada wa kuanzisha Bodi ya Mikopo nchini.

Katika wimbo huo, Msanii huyo alikuwa akionesha namna serikali ilivyoanza kukimbia wajibu wake wa kutoa elimu bure katika Vyuo vya Elimu ya Juu, huku pia kukiwa na shule binafsi nyingi ambazo zilikuwa zikijipangia ada zitakavyo.

Kutokana na hali hiyo D-Knob aliona mazingiora na mwanafunzi atokaye katika familia duni yakiwa hatarini. Alibaini kuwa huo ndio mwisho wa mwanafunzi maskini kuweza kupata elimu na hivyo kujikomboa. Aliweza kuona kuwa elimu imebadilisha njia na sasa inageuka fimbo ya kuwachapa maskini na sio tena kuwapa njia ya kupita.

Unaweza kuchambua Elimu ya Juu nchini Tanzania kwa kuanzia kuangaza mabadiliko yaliyoanzia mwaka 2004, hasa baada ya kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Ni jambo lililo wazi kuwa, kuanzishwa kwa bodi hiyo kuliongeza wigo wa udahili lakini kulileta changamoto katika suala la udhibiti viwango vya ubora wa Elimu ya Juu hapa nchini.

Baada ya kupatika kwa unafuu wa kupata gharama za masomo ya juu, ilifuata pia kuanzishwa kwa vyuo vikuu vingi binafsi. Vyuo hivyo vikaanza kushindana na vyuo vikuu vya umma ambavyo ukitazama kwa umakini kabla ya mwaka huo, vilikuwa na ukiritimba mkubwa hasa katika utoaji wa alama za mitihani kwa wanafunzi. Ukritimba mwingine ulikuwa ni ule wa kutokuwepo muda maalum kwa wanafunzi wa shahada za Uzalimi na Uzamivu kuhitimu shahada zao.

Vilikuwepo vitivo ambavyo vilisifika kwa kile kilichoitwa kufelisha wanafunzi. Vitivo hivi vilianza kupungua makali baada ya vyuo binafsi kuingia. Vyuo binafsi kwa kiasi kikubwa vilileta kile kiitwacho mahusiano baina ya muuzaji na mteja, ambapo mwanafunzi akageuzwa mteja na mwenye chuo akawa muuza bidhaa ya elimu.

Wahadhiri walikuwa na tabia ya ‘kubana’ au kufelisha wanafunzi sasa wakadhibitiwa. Ikawa ni lazima wanafunzi wahitimu. Dai hili li wazi lakini pia linahitaji uchunguzi zaidi.

Pia kulitokea uwepo wa haki za wanafunzi kujadiliana na wahadhiri kuhusu masaibu ya masomo yao jambo ambalo lilikuwa gumu kufanyika kabla ya mwaka huo na hasa kwenye vyuo vya umma. Aina za maksi za ufaulu ambazo zilikuwa hazipatikani katika baadhi ya masomo kwenye vyuo vya umma sasa zikaanza kuonekana kutolewa na wahadhiri hao hao waliokuwa wakifundisha vyuo binafsi.

Kimsingi kipindi hiki kiliibua mabadiliko makubwa hasa yahusuyo haki za wanavyuo na kupungua kwa ukiritimba, ubabe na aina nyingine za manyanyaso mengine ambayo yaliwafanya wanavyuo kujihisi kuwa walikuwa  vyuo vikuu kupata fadhila na kwamba elimu haikuwa haki bali huruma ya wale waliopata nafasi ya kuitoa.

Ukitazama Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 pamoja na masuala mengine inazungumzia umuhimu wa kuwa na taifa lililo na wasomi wazuri na walioelemika vema. Kwa Mujibu wa Profesa Peter Msolla katika andiko lake la “Masuala mbalimbali katika Elimu ya Juu nchini Tanzania,” anafafanua kuwa dira hiyo imeweka mkazo katika suala la kuwa na viwango bora vya elimu huku pia ikijadili uongezaji wa idadi ya wahitimu walio na viwango vya juu katika taaluma zao.

Profesa Msolla anabainisha kuwa serikali peke yake haiwezi kubeba jukumu la kuendesha sekta ya Elimu na hasa Elimu ya Juu na kuifanya iwe fanisi. Anaelezea umuhimu wa wadau wengine kushiriki na hasa wachangiaji wa huduma za jamii kama Benki ya Dunia kwa kuwa eneo hili lina gharama kubwa.

Kwa mujibu wa Profesa Msolla, Elimu ya Juu inakabiliwa na changamoto nyingi ukiacha suala la fedha. Zingine ni suala la utanukaji wa sekta hii pamoja na upatikanaji wa nafasi za masomo. Pia lipo suala la usimamizi wa ubora pamoja na umuhimu wa elimu inayotolewa. Pia yapo masuala ya upatikanaji wa Teknoljia ya Mawasiliano (ICT), ujenzi wa tabaka la wasomi wanaoweza kumudu ushindani katika soko la ajira pamoja na kufanya tafiti.

Madai ya Profesa Msolla yanashabihiana kabisa na Dk. S. Tamilenthi na mwenzake L. Emmie Junior ambao katika andiko lao la “Vikwazo katika Elimu ya Juu Barani Afrika kwa nchi za Zambia na Tanzania” wanafafanua kuwepo sera zinazobadilika mara kwa mara nchini, hali inayofanya elimu ya juu kutoimarika. Jambo hili unaweza kulitazama hasa kwa kuzingatia nafasi za wanasiasa hasa Mawaziri wenye dhamana ya eneo hili ambao mara kwa mara wamekuwa wakija na mipango yao mipya na kuua ya zamani.

Eneo muhimu la kuzingatia hapa ni vigezo vya wanafunzi kupata udahili ambavyo ukitazama mwaka huu vimebadilishwa, na mabadiliko hayo yanafanyika wakati wanafunzi wanaotakwa kudahiliwa wakiwa tayari wamekwisha kuomba nafasi za udahili. Lingine ni lile la vigezo vya utoaji mikopo, vigezo ambavyo hubadilishwa kila mwaka huku mabadiliko hayo yakiwa hayahusishi wadau wote wa sekta hii.

Jambo linguine wanalolizungumzia wataalam hawa ni vikwazo kati ya taasisi zenyewe za elimu ya juu. Hapoa unaweza kutazama ushindani usio na tija kati ya vyuo vya umma dhidi ya vile vya binafsi, huku wanafunzi wanaosoma vyuo vya umma wakilalamika kutotendewa haki ukilinganisha na wale wa vyuo binafsi ambavyo vuinasimia kuhakikisha kile wanachokilipa wanafunzi wanakipata.

Suala linguine nyeti ni kuhusu mbinu za kutahini ili elimu ya juu ilete picha ya usawa. Jambo hili kwa hapa nchini bado lina ukakasi maana kuna program ambazo awali zilikuwa miaka mine zikashushwa na kuwa mitatu na nyingine zilikuwa miaka mitatu zikaongezwa kuwa miaka minne. Mabadiliko haya ambayo huchangiwa na ubutu wa sera ya elimu ya juu ya mwaka 1999, yanafanya jamii kuwa na wahitimu wa taaluma moja ambao wana uelewa tofauti kabisa na hivyo kulifanya taifa klushindwa kufikia lengo lake la kuwa na wasomi wenye uelewa na wenye kuweza kumudu changamoto za kulipatia maendeleo.

Dk. Daniel Mkude mwaka 2003 aliandika kuhusu masuala ya Elimu ya Juu hapa Tanzania na akafafanua kuwa, lipo tatizo la kukosekana umakini katika elimu yetu kuanzia chini. Elimu ya Juu hupokea wanafunzi waliotoka chini na kama huko chini hakuna viwango ni vigumu kuvipata juu.

Ukiichambua elimu ya juu na ukitazama wanafunzi wanakotoka unabaini kuwa lipo hitaji la muhimu la mjadala mpana wa kitaifa katika kubainisha aina ya taifa tunalolitaka na aina ya elimu inayotakiwa kutolewa. Si lazima wanafunzi wote wakae darasani kama Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) ingeweza kutumika vema. Bado eneo hili na lile la Elimu Masafa halijapewa mkazo na hivyo kuweka fursa ya udanganyifu na pia kudharaulika kwa mfumo huo, ambao kimsingi ungeweza kupunguza gharama za ada kwa wanafunzi na hivyo elimu ya juu kuwa rahisi kupatikana katika maeneo yote ya nchi ukizingatia kuwa mkongo wa taifa upo katika maeneo yote ya wilaya za Tanzania.