Home Latest News China, Marekani ziko tayari kurejea kwenye mgogoro?

China, Marekani ziko tayari kurejea kwenye mgogoro?

942
0
SHARE

Na LEONARD MANG’OHA

JANUARI 15 mwaka huu ni tarehe ya kihistoria kati ya mahasimu wa kiuchumi duniani yaani China na Marekani baada ya kutiliana saini makubaliano ya kibiashara yanayotamatisha mzozo wa muda mrefu kati ya mataifa hayo.

Majibizano makali na majadiliano ya muda mrefu ya miaka miwili bila kuzaa matunda hatimaye yanaleta muafaka na kufungua ukurasa mpya wa kibiashara kati ya mataifa hayo.

Kupungua kwa biashara kati ya pande hizo ndiko kulikotoa msukumo mkubwa wa kuangalia namna ya kuimarisha uhusiano huo kwa masilahi ya uchumi wa pande zote mbili na dunia kwa ujumla wake.

Wakati wa mgogoro huo kiwango cha biashara kati ya pande hizo kinaelezwa kupungua kwa kiwango kikubwa baada ya pande zote kuwekeana vikwazo katika bidhaa zinazozalishwa na taifa mojawapo.

Inaelezwa kuwa kwa upande wake Rais Donald Trump wa Marekani, alitumia kushuka huko kwa nakisi ya biashara kati ya mataifa hayo kutathimini mafanikio na kubaini kuwa kuendeleza mzozo huo kungeweza kupunguza zaidi biashara kati yao.

Ni wazi kuwa biashara ya bidhaa ya Marekani ilipungua kwa kiasi kikubwa tangu kuanza kwa mzozo huo wa kibiashara kati yake na China kwani katika kipindi cha miezi 12 hadi kufikia Novemba mwaka jana kiasi hicho kilipungua kwa Dola bilioni 60 na kufikia Dola bilioni 360 ikilinganishwa na mwaka mmoja kabla.

Pia inaelezwa kuwa biashara kati ya China na Marekani ilipungua kwa zaidi ya Dola bilioni 100. Marekani ilishuhudia mauzo ya mazao kutoka nchini humo yakipungua kwa kiasi kikubwa baada ya China kuamua kuongeza kodi katika bidhaa za Marekani zinazouzwa China na kusababisha athari kubwa kwa wakulima wa Marekani wanaotajwa kuathirika zaidi wakati wa mgogoro huo.

Mauzo ya mazao ya kilimo ya Marekani ya kila mwaka kwenda China yakapungua kutoka Dola bilioni 25 hadi bilioni saba, kikitajwa kuwa kiwango cha chini zaidi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni.

Kutokana na hatua hiyo ya Marekani, watu wanaojihusisha na kilimo ni karibu asilimia moja ililazimika kutoa kiwango cha juu cha ruzuku ili kukabiliana na athari zilizojitokeza.

Pia China ilishuhudia uwekezaji wake nchini Marekani ukishika zaidi wakati wa mzozo huo wa kibiashara, ambapo jopo la washauri la American Enterprise Institute la Washington Marekani linaeleza kuwa katika kipindi hicho uwekezaji wa China ulipungua kutoka Dola bilioni 54 mwaka 2016 hadi bilioni 9.7 mwaka 2018.

Na inaelezwa kuwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019, kampuni za China ziliwekeza kiasi cha Dola bilioni 2.5 pekee nchini Marekani.

Kampuni za taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani zilisuasua kuwekeza nchini Marekani kutokana na wasiwasi wa mzozo wa kibiashara pamoja na masharti makali ya uwekezaji nchini Marekani na uthibiti wa mtaji nchini China.

Licha ya kuendelea kwa uwekezaji, kampuni za Marekani zilizokuwa zikiendesha shughuli zake nchini China zilisema kuwa mzozo wa kibiashara kati ya nchi hizo ni miongoni mwa mambo yanayowapa wasiwasi.

Taarifa za Baraza la Biashara la Marekani na China mwaka 2019, inaeleza kuwa asilimia 81 ya kampuni za Marekani zilizokuwa zinaendesha shughuli zake China, zilisema kuwa mzozo huo wa kibiashara ulikuwa na athari hasi katika biashara zao. Itakumbukwa kuwa mwaka 2017 ni asilimia 45 pekee ya kampuni za Marekani zilizokuwa na wasiwasi wa suala hilo.

Kutokana na mzozo huo, Marekani ilitarajiwa kutofikia matarajio yake ya kiuchumi kwa asilimia tatu. Hata hivyo wachambuzi mbalimbali walieleza kuwa inaweza kuchukua miaka kadhaa kushuhudia athari kamili ya mvutano wa kikodi kati ya mataifa hayo.

Mzozo huo ulishika kasi katika kipindi ambacho uchumi wa China ulikuwa ukitajwa kukua kwa kasi ndogo, ambapo Benki ya Dunia (WB) ilikadiria kuwa uchumi wa taifa hilo uko chini ya asilimia 6 mwaka huu, ukuaji ambao unatajwa kuwa utakuwa wa chini zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Athari za mgogoro huo zinatajwa kuathiri pia mwenendo wa uchumi wa dunia ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Kristalina Georgieva alipata kunukuliwa akisema kuwa mgogoro huo humwathiri kila mmoja.

IMF lilipunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2019 hadi asimilia tatu kutokana na mgogoro huo yakiwa ndiyo makadirio ya chini zaidi tangu wakati wa mgogoro wa kifedha.

WASIWASI WA KUIBUKA MGOGORO MPYA

Muda fupi tu baada ya kutatuliwa kwa mgogoro huo mataifa hayo ni kama yanaingia katika mgogoro mwingine kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona ulioanza mwishoni mwa mwaka jana.

Mlipuko huo ni kama unatonesha kidonda kinachoelekea kupona baada ya Marekani kupitia kwa Rais wake, Donald Trump kuviita virusi hivyo kuwa ni vya China na vilitengenezwa katika maabara zake katika mji wa Wuhan ambao ndiyo kitovu cha ugonjwa huo.

Suala muhimu la kujiuliza ni je mataifa haya yako tayari kurejea yalikotoka ikiwa bado hata makubaliano yaliyofikiwa mapema Januari hayajaanza kutekelezwa?

Licha ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuonya kuhusisha kwa virusi hivyo na eneo au kundi fulani kunaweza kusababisha unyanyapaa maofisa wa serikali ya Marekani akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo akivitaja kama virusi vya Wuhan.

Mgogoro baina ya mataifa hayo, unaonekana kurejea kiaina kutokana na kauli ya Trump kuwa hawezi kuzungumza kwa sasa na Rais mwenzake wa China, Xi Jinping wa China, kuhusu virusi hivyo huku akisisitiza kuwa anaweza hata kukatisha uhusiano baina ya nchi hizo.

Matamshi hayo ya Trump yalikuwa yakielezea masikitiko yake kuhusu kile alichodai kuwa China ilivyoshindwa kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 na kwamba janga hilo limeweka wingu katika makubaliano ya biashara ya mwezi Januari baina ya mataifa hayo yenye nguvu zaidi kiuchumi duniani.

Kauli nyingine inayoweza kuzorotesha uhusiano wa mataifa hayo ni madai kuwa virusi vya Corona vilitengenezwa katika maabara nchini China baada ya kudai kuwa ameona ushahidi kuwa virusi vya Corona vilitengenezwa katika maabara mjini Wuhan nchini China.

Licha ya kukumbana na ukosoaji kuanzia ndani ya nchi yake kuhusu jinsi anavyokabiliana na mlipuko huo nchini mwake, bado aliishutumu WHO kwa madai kuwa inategemea upande wa China kwamba shirika hilo lilishirikiana na China kuficha ukweli kuhusu virusi hivyo na kufikia ufadhili wa Dola milioni 400 uliokuwa ukitolewa na Marekani kwa WHO.

Chokochoko  za Trump dhidi ya China ziliendelea pale alipodai kuwa huenda nchi hiyo ikaitaka China kuilipa fidia kwa madai kuwa nchi hiyo ilishindwa kuzuia maambukizi ya Corona.

Pia ofisa mmoja wa China akituhumiwa kueneza dhana za uwongo kwamba virusi hivyo viliingizwa nchini China na jeshi la Marekani.

Katika hatua inayoweza kutafsirika kama kujibu mapigo Serikali ya China kupitia kwa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, aliionya Marekani kwa kuitaka ifuatilie mambo yanayoihusu badala ya kuonyesha unyanyapaa dhidi ya China.

Maofisa wa China walikuwa na vyombo mbalimbali wakidai kuwa kauli za Trump ni za kibaguzi huku wakisisitiza kuwa kutowajibika kwa wanasiasa ndiko kunakozua hofu kuhusu virusi vya Corona.