Home Habari CUF yataja siri mpya za mgogoro wa kisiasa Z’bar

CUF yataja siri mpya za mgogoro wa kisiasa Z’bar

2013
0
SHARE

mnyaaNA GABRIEL MUSHI

MBUNGE wa zamani wa jimbo la Mkanyageni na mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Habib Mnyaa, amesema migogoro ya kisiasa ya muda mrefu Visiwani Zanzibar inachangiwa na uamuzi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano kukataa kuridhia mkataba wa Afrika unaoshughulikia masuala ya utawala bora, uchaguzi na demokrasia.

Mchakato wa kuandaa mkataba huo wa Afrika ulianza 2003 na kuhusisha nchi zote za Afrika mchakato na kufanyiwa marekebisho 2004 ulipitishwa mwaka 2007 kwenye mkutano wa kawaida wa Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika nchini Ethiopia.

Hata hivyo kati ya nchi zote za Afrika zilizoshiriki kuuandaa na kuupitisha mkataba huo ni nchi 10 tu ndio zimeuridhia huku Tanzania inayotambulika kama kisiwa cha amani ikisuasua.

Nchi zilizouridhia ni Burkinafaso, Ethiopia, Ghana, Guinea, Lesotho, Mauritania, Rwanda, Sieraleon, Afrika Kusini na Zambia.

Katika mazungumzo yake na RAI, juzi jijini Dar es Salaam,  Mnyaa alisema licha ya Tanzania kuungana na nchi nyingine za Afrika katika kuandaa mkataba huo mwaka 2003 na baadaye kuupitisha,  bado imejiweka kando katika kutekeleza makubaliano hayo.

Alisema mkataba huo ambao uliandaliwa mwaka 2003 Maputo nchini Msumbiji na kufanyiwa marekebisho mwaka 2004 AddisAbaba nchini Ethiopia ulianza kutumika rasmi mwaka 2007 baada ya kufanyiwa marekebisho ya mwisho.

“Kati ya nchi zote za Afrika ni nchi 10 tu zilizoridhia mkataba huu, huku nchi zilizosalia zikiuweka kando kana kwamba hazikushiriki kuuandaa.

“Hii inaonesha namna gani nchi za Afrika ikiwamo Tanzania zimelenga kuendeleza ukandamizaji katika masuala mbalimbali ya haki za binadamu ikiwamo uchaguzi ambao sasa umezaa migogoro isiyokwisha Zanzibar.

“Suala la Zanzibar limetokana na utawala mbovu, usiofuata demokrasia, mikataba kama hii ingeziwekea vikwazo serikali hizi na kuzilazimisha kufanikisha chaguzi hizi kwa amani na utulivu bila uonevu,” alisema.

Alisema migogoro ya uchaguzi Zanzibar imesababisha watu kufariki dunia na wengine kupata ulemavu.

Kauli ya Mnyaa inaungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu nchini, Hellen Kijo-Bisimba, aambaye alisema Serikali inaogopa kuridhia mikataba ya aina hiyo kwa sababu wanajua hawatapata pa kutokea pindi yanapotokea madhara makubwa yanayosababishwa na ukiukwaji wa demokrasia katika mambo ya kiuchaguzi.

Kwamba hofu ya serikali ya Tanzania ni kuwekewa vikwazo kama ilivyofanyiwa Zimbabwe, lakini pia pamoja na uwapo wa mikataba mingi ambayo Tanzania imeiridhia bado utekelezaji wa matakwa ya mikataba hiyo na kuiheshimu umekuwa hafifu.

“Sasa hivi suala la kuridhia au kutoridhia limeonekana kuwa kama halina faida sana kwani ipo mikataba mingi ambayo imeiridhia,  lakini sasa inaivunja bila hatua kuchukuliwa na wakuu wa nchi zilizopitisha mikataba hii.

“Kuna mkataba mwingine wa Haki za raia na Kisiasa, ingawa Serikali imeuridhia bado haitekelezi wajibu wake, vilevile kuna mikataba mingine ambayo serikali haijairidhia hadi sasa bila sababu za msingi.

“Kwa mfano kuna mkataba wa  mateso ambao unapinga vitendo vyote vya kikatili ambao uliasisiwa mwaka 1984, hadi leo Tanzania haijauridhia ingawa kwenye Katiba yetu hili jambo lipo.

“Mambo kama haya yanatupatia wakati mgumu sisi watetezi wa haki za binadamu kuendeleza utetezi kwa sababu Serikali isiporidhia mikataba hii, hatutakuwa na nguvu ya kisheria kuilazimisha kutekeleza wajibu wake kwa wananchi,” alisema.

Kuanzia uchaguzi wa 1995 ambao ni wa kwanza kufanyika baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hadi wa mwaka 2015 hakujawahi kuwa na uchaguzi uliopita bila kuzalisha mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

Uchaguzi wa mwaka 1995 ambao CCM ilitangazwa kuwa mshindi ulizaa mgogoro baada ya CUF kudai kuwa imeporwa ushindi na kugoma kumtambua rais aliyetangazwa.

Taarifa za waangalizi wengi wa kimataifa zilieleza masikitiko yao kutokana na vitisho dhidi ya raia na udanganyifu katika kuhesabu kura, jambo ambalo waliamini huenda lilipelekea matokeo yaliyotangazwa kuwa sio sahihi.

Baadhi ya nchi wafadhili kama Norway na Sweden zilisimamisha misaada kwa Zanzibar kutokana na kadhia ile ndipo Jumuiya ya Madola ikasimamia mazungumzo ya upatanishi na hatimaye kufikiwa makubaliano yaliyosainiwa Aprili 29, 1999.
Pia, kufuatia uchaguzi wa mwaka 2000, mnamo Januari 27, 2001 wanachama 31 waliuawa, 48, walipata vilema vya maisha na 243 walijeruhiwa, baada ya polisi kutumia nguvu kuzuia maandamano ya kupinga matokeo ya au uchaguzi Unguja na Pemba.

Chanzo cha mgogoro wa uchaguzi wa mwaka 2000 ilikuwa ni kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi na kuamuliwa kurudiwa katika majimbo kadhaa ambapo CUF haikukubaliana na uamuzi huo na kuamua kususia uchaguzi wa marudio.

Mgogoro ukaendelea tena hata katika uchaguzi wa 2005, ambapo kwa mara nyingine tena, CUF waligoma kuitambua serikali ya Rais Amani Abeid Karume. Kutokana na kutoridhika kwa uwepo wa hali hiyo ya migogoro iliyogawanya jamii ya Wazanzibar, baadhi ya wanasiasa kutoka CUF na CCM walifanya jitihada ya kuanzisha mazungumzo ya kutafuta muafaka ambayo ndio yaliyozaa mpango wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010 ambayo ilikubaliwa na Wazanzibar wengi.

Mazungumzo yaliyozaa muafaka na ambayo yalifanywa na Wazanzibar wenyewe yalianza Machi 2009 na kufikia tamati Novemba 2009 kwa mkutano wa Rais Karume na Maalim Seif Sharif Hamad na kukubaliana kufuta tofauti za kisiasa zilizoigawa jamii ya Wazanzibari kwa zaidi ya miaka 15.

Kutokana na muafaka wa kisiasa uliofikiwa uchaguzi wa mwaka 2010 haukuhojiwa sana, ingawa bado kulikuwa na malalamiko ya hapa na pale.

Hata hivyo, mwaka 2015 umekuwa ndio kilele cha migogoro yote baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuamua kufuta matokeo ya uchaguzi wote, ingawa Tume ya Uchaguzi ya Tanzania, (NEC) haikufanya hivyo kwa matokeo ya Zanzibar.

Jambo la kuzingatia ni kuwa kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Zanzibar mwaka huu waangalizi wote wameuita huru na wa haki.