Home Makala Dk. Bashiru Ally anamuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo

Dk. Bashiru Ally anamuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo

4121
0
SHARE

NA VICTOR MAKINDA

Ni miaka 19 sasa tangu Rais wa kwanza wa Tanganyika huru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atangulie mbele za haki. Mwalimu Nyerere alikuwa mjamaa wa kweli, aliyesimamia misingi ya umoja wa kitaifa, utu na uzalendo uliotukuka.

Sifa za Mwalimu Nyerere ni nyingi na kuziorodhesha inahitaji zaidi ya kurasa. Inatosha tu kusema kuwa Mwalimu Nyerere atabaki kuwa alama ya utii, bidii, utu wema, umoja, mshikamano, muungano na nembo ya shujaa wa Taifa huru, mjamaa kweli kweli aliyeamini katika misingi ya ujamaa na kujitegemea pasipo kutetereka.

Mwalimu Nyerere, mwasisi wa TANU na baadae CCM, chama kinachotawala hata sasa, ameacha warithi  wachache. Warithi hao ni wale waumini wa falsafa yake ya kijamaa sambamba na wasema kweli wanaoamini katika kweli inayoweka huru. Hawa si wengine bali  ni wale ambao wanaziishi kanuni za mwana TANU hususani ile kanuni ya, Nitasema kweli Daima, fitina kwangu ni mwiko. Wapo wachache kama nilivyotangulia kusema kwani wengi wetu tumejawa na unafki wa kuziimba fikra za Mwalimu Nyerere sambamba na falsafa zake huku kiuhalisia hatuziamini na  kwa kuziishi kwa minajiri ya kuzishabihisha na matendo yetu.

Mwalimu Nyerere alikuwa mjamaa kweli kweli. Je ni wajamaa wangapi waliobaki nchini hata sasa? Mwalimu Nyerere alikuwa msema kweli asiyemuonea haya mtu yeyote hata chama chake CCM. Na tujiulize ni wana CCM wangapi leo hii wenye uthubutu  wa kuusema ukweli pasipo chembe ya unafiki na kuoneana haya? Jibu ni kwamba wapo. Ila wapo wachache wenye uthubutu huo. Wengi ni wanafiki wanaoiimba misingi ya Mwalimu Nyerere huku mioyoni mwao wakiwa kinyume na kuiamini na kutenda sivyo ndivyo.

Ukweli Ulivyo kati ya wana CCM wachache waliobaki ambao wanaonesha dalili za kuweza kumudu kutembea juu ya falsafa za Mwalimu Nyerere ni Dr Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyechaguliwa kushika wadhifa huo mapema mwaka huu. Ukweli  Ulivyo huyu  ukimtazama usoni, ukimsikiliza maneno yake, ukivisawili vitendo vyake kwa mbali unaiona taswira ya Mwalimu Nyerere. Bashiru Ally anamuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo.

Ndiyo, Dr Bashiru Ally anajipambanua kuwa ni miongoni mwa wana CCM wachache wanaoweza kufungua vinywa vyao na  na kuusema ukweli pasipo kuhofu juu ya ama wana CCM wenzake watauchukuliaje ukweli huo ama utakuwa na athari gani kwa ustawi wa chama lakini kubwa analolifanya ni kuusema ukweli ulivyo kwa kuwa anamaamini kuwa ni ukweli. Tabia hii ilikuwa ni tabia ya Mwalimu Nyerere ambaye tarehe 14  ya jumapili ya wiki ilyopita tulikuwa tukifanya kumbukizi ya miaka 19 ya kifo chake.

 DR BASHIRU ALLY NI NANI

Mzaliwa huyu wa Mkoa wa Kagera,ambaye kwa muda mrefu alikuwa mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya siasa na utawala, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, pia alijihusisha na utafiti na ni mwandishi wa makala mbalimbali zilizochapishwa kwenye matoleo na machapisho mbalimbali Duniani. Kiitikadi Dr Bashiru Ally amejipambanua kuwa ni mjamaa na mfuasi wa sera za hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Dr Bashiru Ally hakuwa amejinasibu  kuwa ni mwanachama wa CCM mpaka pale alipoteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati maalumu iliyopewa jukumu la kuhakiki mali za Chama cha Mapinduzi, ndipo wafuatiliaji wa masuala ya siasa tulipobaini kuwa Dr Bashiru  ni mwana CCM kindakindaki.

KAULI MATENDO YA DR BASHIRU ALLY

Mwaka 2013 akiwa anashiriki mjadala wa Kigoda cha Mwalimu, Dr Bashiru Ally aliwahi kunukuliwa akisema kuwa aliwahi kumshusha kwenye gari mbunge mmoja wa CCM ambaye ni msemaji sana na anayejiita mzalendo kutokana na kujimilikisha gari kwa njia za wizi. Dr Bashiru alimueleza mbunge huyo kuwa  “Hata kama wewe ni mbunge shukaaa”  Dr Bashiru alisema  kuwa mbunge huyo ukimsikiliza utadhani ni mzalendo sana kumbe ni mwizi.Hiyo ilikuwa ni mwaka 2013.

Dr Bashiru Ally akiwa amepata fursa ya kuiongoza kamati ya kuhakiki mali za CCM Tanzania nzima, anatajwa na wana CCM wenzake kuwa aliifanya kazi hiyo kwa uadilifu na uaminifu mkubwa. Hakuwa tayari kumwonea mtu yoyote wala kumpendelea yoyote katika zoezo hilo linalotajwa kuwa ni gumu ambalo lilikuwa na changamoto nyingi. Ujasiri, ukweli na uadilifu wa Dr Bashiru Ally uliifanya kamati aliyoiongoza kupekua kila kona na kubaini na kuainisha kikamilifu mali zote za chama hata kama zilikuwa mikononi mwa vigogo wakubwa wa chama na serikali.

Wana CCM na waTanzania kwa ujumla ni mashahidi wa namna Dr Bashiru alivyoifanya kazi hii kwa uadilifu mkubwa. Wengi wanasema hata nafasi ya kuiongoza sekretarieti kuu ya chama kwa nafasi ya ukatibu mkuu imetokana na jinsi ambavyo aliifanya kazi  kwa uaminifu mkubwa.

Hivi karibuni Dr Bashiru Ally, alinukuliwa akisema kuwa ndani ya CCM kuna majizi ambayo ukiyataja umma utashituka. Hii ni kauli nyingine iliyotoka kinywani mwa Dr Bashiru ambayo ni agharabu mwana CCM kuthubutu kuitamka. Wafuatiliaji wa masuala ya siasa tumefurahishwa na ujasiri wa Dr Bashiru Ally wa kutamka wazi wazi kuwa ndani ya chama anachokiongoza kuna majizi. Kauli hiyo imewapa tumbo joto majizi yaliyomo ndani ya CCM na ni matumaini ya wengi kuwa Dr Bashiru Ally kwa nafasi yake  ya Ukatibu Mkuu wa chama atayashughulikia majizi hayo haraka.

Mwalimu Nyerere alipata kusema kuwa bila CCM imara nchi yetu itayumba. Ni ukweli usiopingika kuwa uimara wa CCM ndio uimara wa Tanzania. Uimara wa CCM utatokana na viongozi imara wa aina ya Dr Bashiru. Kwa kuwa CCM ndio chama kinachoiongoza Tanzania ni wazi kuwa chama hiki kinahitaji viongozi imara wasio yumba, wakweli na wawazi na wenye uthubutu wa kuisimamia misingi ya chama aliyoiasisi Mwalimu Nyerere.

Kana kwamba haitoshi Dr Bashiru amewahi kunukuliwa akizungumzia juu ya mchakato wa katiba mpya. Dr Bashiru alisema kuwa mchakato wa katiba hautoachwa mpaka ipatikane katiba mpya. Ukweli Ulivyo wana CCM walio wengi hawakuwa wamependezwa na mchakato wa kuipatia Tanzania katiba mpya. Kauli ya Dr Bashiru Ally juu ya kuendelea  na mchakato wa kuidai katiba mpya mpaka ipatikane imeonekana kwenda kinyume na mtazamo wa wana CCM wenzake juu ya mchakato huo wa katiba. Lakini kwa kuwa DR Bashiru amechagua kuuishi Ukweli, amesema ukweli ambao watanzania walio wengi wangeusema. Ukweli ni kwamba watanzania wanaihitaji sana  katiba mpya kulingana na matakwa ya wakati. Ni matamanio ya wengi kuona mchakato wa katiba mpya unaendelezwa toka pale ulipokwamia na hatimae tuipate katiba mpya itayoendana na matarajio, matakwa na uhalisia wa nchi ya kidemokrasia.

Makala hii itaendelea wiki ijayo. Leo tumalizie kwa kuisawili kauli hii ya hivi karibuni ya Dr Bashiru Ally akiwa katika kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA), mjini Morogoro hivi karibuni. Kauli ya Dr Bashiru Ally, imezua gumzo kubwa ndani nan je ya nchi. Dr Bshiru Ally alitamka wazi wazi juu ya rushwa ilotamalaki katika chaguzi zetu nchini.

Dr Bashiru Ally alisema na nina mnukuu. “Mfumo wa uchaguzi nchini umegubikwa na rushwa kiasi kwamba imefika mahali ambapo ukifika uchaguzi wagombea wanauza nyumba. Akishazikusanya fedha anakwenda kuwanunua wale mawakala na mawakala wanajua. Nao wanawanunua wapigaji kura. Msimu wa uchaguzi unakuwa msimu wa rushwa ya uchaguzi.Mnachotakiwa kufanya ni kubomoa na kuharibu soko la kura.”

Kauli hii ya Dr Bashiru ukiisawili kiuhalisia inalenga kutoa hadhari kwa wapiga kurakutochagua wagombea  watoa rushwa. Lakini kwa upande mwingine tunaweza kuijuliza maswali machache, kipi chama kilichoshinda viti vingi kuanzia wenyeviti wa vitongoji, mitaa, madiwani na wabunge.

Jibu ni kwamba CCM ndio iliyoshinda viti vingi katika hivyo. Ni wagombea wa chama gani hutoa rushwa katika chaguzi? Kwa nini hutoa rushwa?  Je kauli hii ya Dr Bashiru imewalenga wagombea wa chama gani? Ni wagombea wa vyama  pinzani au hata wa chama chake? Kauli hii ina athari gani kwa wapiga kura, wagombea na hata kwa chama chake CCM?

Itaendelea Alhamisi ijayo…..