Home Latest News Dk. Ben Carsson: Ni Kenya au Tanzania

Dk. Ben Carsson: Ni Kenya au Tanzania

2876
0
SHARE

Dr. Benjamin Carson, director of Pediatric Neurosurgery at Johns Hopkins School of Medicine, speaks to the Conservative Political Action Conference (CPAC) in National Harbor, Maryland, March 16, 2013. REUTERS/Jonathan Ernst (UNITED STATES - Tags: POLITICS HEALTH) - RTR3F2WE

NEW YORK, MAREKANI

KAMPENI za kuwania kuteuliwa ndani ya vyama vya siasa nchini Marekani imepamba moto. Vyama viwili vya Democratic na Republican vina wanasiasa wanaochuana kuwania uteuzi wa ndani ili kuwakilisha vyama vyao kwenye kinyang’anyiro cha urais kitakachofanyika mwaka 2016.

Miongoni mwa wanaowania nafasi hiyo ni Dk. Ben Carson ambaye ni mwanachama wa chama cha Republican.  Mwanaisasa huyo ameibuka kuwa mpinzani mwenye nguvu dhidi ya bilionea Donald Trump ambaye anafahamika kwa matamshi ya kibaguzi dhidi ya waafrika na Waislamu kote duniani.

Dokta Carson amefanya jitihada kubwa katika fani yake ambako alijizolea umaarufu mkubwa mno. Yeye ni tabibu ambaye amefanikiwa kuwatibu watu mbalimbali ikiwemo kutenganisha watoto waliozaliwa wakiwa wameungana.

Hata hivyo katika uwanja wa siasa Dk. Carson anapambana ndani ya chama ambacho kinasifika kwa ubabe na matumizi makubwa ya nguvu katika sera za nje pamoja na vita.

Aidha, jambo linalozunguka katika maisha ya Mmarekani huyo mweusi ni kuhusu asili ya wazazi wake. Ili kufahamu hilo Dk. Carson ameanza harakati za kutafuta asili ya wazazi wake ambao wanasadikiwa kutokea nchi za Kenya na Tanzania.

Carson anatafuta mizizi ya familia yao hasa pale walipotokea mababu zake, ambapo ziara yake itaanzia nchini Kenya na kuingia Tanzania.

Dk. Carson anatarajiwa kuanza ziara hiyo mapema Desemba 27 mwaka huu barani Afrika, ambapo atakuwa nchini Kenya, Nigeria, na Zambia kwa siku kadhaa.

Ziara hiyo inakumbusha wakati Rais Barrack Obama alipofanya ziara yake ya kwanza nchini Kenya miaka 1980 akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Harvard. Kisha mwaka 2006 alitembelea nchini Kenya na kukutana na ndugu zake kwenye kijiji cha Kogelo kilichopo katika jimbo la Siaya nchini humo.

Obama alifanya ziara hiyo wakati akiwa Seneta wa jimbo la Illinois, ambapo alifanikiwa kutoa hotuba katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kuelezea madhara ya rushwa na maambukizi ya ukimwi kwa jamii.

Wakati baba yake Obama alijulikana kuwa ni raia wa Kenya, Hussein Onyango Obama, hali imekuwa tofauti kwa Dk. Carson, ambaye hakufahamu aanzie wapi kujua asili yake. Hata hivyo Carson anaamini kuwa mababu zake walitoka Kenya licha ya matatizo makubwa ya kinasababu yanayomkabili kuthibitisha hilo.

“Mababu zangu walitoka maeneo ya Kenya na Tanzania, ni watu wa kabila la Turkana. Nimekuwa nikitafiti kuona mizizi hiyo,” alisema Carson alipozungumza na mwandishi Hugh Hewitt wa Marekani.

Watu wa kabila la Turkana wanaishi kaskazini mwa Kenya umbali wa kilometa 1,000 kutoka mpaka wa Tanzania. Kabila la Turkana halijawahi kuishi Tanzania, ingawa wana nasaba na watu wengine wa kabila hilo wanaoishi nchi za Uganda, Ethiopia na Sudan Kusini.

Dk. Carson ana asili ya afrika, ambapo waafrika waliingia nchini Marekani kupitia biashara ya utumwa. Waafrika wengi waliopelekwa utumwani walitoka Afrika magharibi.

Biashara ya utumwa afrika mashariki iliendeshwa zaidi na Waarabu ambao waliwauza watumwa bara la Asia. Dk. Carson ana nafasi finyu mno kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani, ambapo hadi sasa ameshuka katika kura za maoni kutoka asilimia 22 mwezi Oktoba mwaka huu hadi asilimia 14 wiki iliyopita.

Kura za maoni zinaonesha kuwa ni miongoni mwa wanasiasa 13 ambao wanausaka urais wa Marekani ifikapo mwaka 2016. Miongoni mwa wanasiasa hao, ni bilionea Donald Trump mwenye asiimia 36 za kukubalika, huku Ted Cruz akiambulia asilimia 16.

Carson analaumiwa kwa uwezo mdogo wa kufahamu masuala ya sera za nje. Hilo limekuwa tatizo linalotumiwa na wapinzani wake kumshambulia katika mikutano ya kampeni.

Carson amewahi kuchanganya uanachana wa NATO ambapo anataka nchi za Baltic zijiunge katika jeshi hilo. Aidha, alikosea aliposema China imeungana na Russia kupambana na magaidi wa ISIL nchini Syria.

Jambo jingine linalochukuliwa kama udhaifu ni kushindwa kwake kuitaja Palestina wakati wa mkutano wake kwa kundi la Wayahudi wa Marekani. Hata hivyo nchi za Baltic (ulaya mashariki) zimekuwa mwanachama wa NATO. Pia China haikupeleka majeshi yake nchini Syria kupambana na ISIL.

Carson ametumia sehemu kubwa ya maisha yake kujihusisha na utabibu huku akifanya operesheni mbalimbali kwa magonjwa ya binadamu. Amepanga kuitumia ziara yake barani Afrika kama njia ya kutaka kujua ni mahali gani hasa walipotokea mababu zake.

Aidha amesema atatembelea Zambia kama sehemu ya kuangalia historia ya mababu zake. Jambo hilo linazidisha ugumu kwamba Dk. Carson hafahamu mizizi ya familia yake ilitoka nchini, licha ya kuwa na imani ni kati ya Kenya na Tanzania.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema uamuzi wa Dk. Carson pia umelenga kuwateka wananchi ambao wanaona atakuwa kama Barrack Obama mwenye asili ya Kenya.

Aidha, wanasema Carson anajaribu kuwavutia wamarekani kuhusu masuala ya nje ya nchi yao licha ya kushindwa kuyafafanua kinaga ubaga. Changamoto iliyopo ni ugunduzi wa waalikotoka wazazi wake, kati ya Kenya au Tanzania.