Home Makala EAC NA HATIMA YA WATANZANIA KIUCHUMI

EAC NA HATIMA YA WATANZANIA KIUCHUMI

1290
0
SHARE
Balozi Augustino Mahiga

NA MOSES NTANDU


JUMUIYA ya Afrika Mashariki imesheheni fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaendelea kutumiwa vyema na mataifa mengine ya jumuiya hiyo, huku idadi kubwa ya Watanzania ikiwa haizitumii fursa hizo ipasavyo.

Pamoja na juhudi kadhaa zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, bado jitihada hizo hazitoshi kujenga uelewa kwa Watanzania kutumia fursa hizo.

Hii si tu kwa wananchi bali hata pia kwa mashirika binafsi na asasi zisizo za kiserikali, nazo bado ziko nyuma katika kutumia fursa hizo ambazo kwa kiwango kikubwa zimekuwa zikitumiwa na mataifa mengine wanachama wa jumuiya hii.

Mwishoni mwa wiki Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustino Mahiga, alikutana na asasi mbalimbali za kiraia katika mkutano ambao ulilenga kujenga uelewa na juhudi za kutumia fursa zilizopo katika jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuimarisha uelewa kwa uma hasa asasi za kiraia za Kitanzania, pia katika kuzitumia fursa hizo za maendeleo ya Taifa.

Kama Taifa tunapaswa kwenda mbali zaidi katika kutazama fursa hizi na kuzitumia ipasavyo kwani licha ya kuwa Tanzania, si tu ndio nchi pekee katika ukanda huu yenye idadi kubwa ya wakazi, bali pia ni nchi pekee inayochukua sehemu kubwa ya ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Pamoja na wingi wa wakazi katika nchi yetu na kuwa na ukubwa wa eneo katika jumuiya hii, lakini bado wakazi wengi nchini hawana uelewa wa kutosha juu ya masuala ya jumuiya hii ya Afrika Mashariki.

Katika tafiti mbalimbali zilizofanywa juu ya uelewa wa umma kwa masuala yahusuyo Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo katika tafiti zilizofanywa na mashirika kadhaa ya kijamii ikiwemo Mfuko wa Asasi za Kirai (Foundation for Civil Society) na lile la Trade Mark East Africa, zimebainisha kuwa asilimia 59 ya Watanzania hawafahamu chochote wala kushiriki chochote katika jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia inaelezwa kuwa hata kwa wale wanaofahamu na kuhusu jumuiya hiyo, bado wanafahamu kuwa ni masuala ya undugu na mahusiano kwa wananchi wa jumuiya hiyo kwa masuala ya kijamii na kiutamaduni pekee.

Nchi nyingine zinaendelea kutumia fursa hii kwa kasi kubwa sana kwa sasa kwa nchi zote za ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kenya ndiyo inayoongoza kutumia fursa hizi hasa kwa masuala ya kiuchumi na maendeleo.

Ni suala la kuamka sasa na kuanza kutoa elimu ya kutosha kwanza kuhusu uelewa kwa jamii zetu kuhusu malengo ya jumuiya hii na mustakabali wake kiuchumi, elimu hii inapaswa kutolewa kwa rika zote kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu na wananchi wote kwa ujumla kupitia asasi za kiraia na jumuiya mbalimbali binafsi na zile za kiserikali.

Katika moja ya kosa kubwa sana jamii ya Kitanzania inalolifanya, ni kusubiri fursa zije kwetu badala ya kuamka na kuzifuata, hulka hii imekita mizizi sana kwani kila jambo wananchi hupenda kusubiri kutangaziwa, huku jamii hiyo hiyo ikisubiri kutoa lawama pale mambo yatakapoonekana kwenda ndivyo sivyo.

Katika agenda kuu ya Taifa toka uhuru kwa Taifa letu, ilikuwa ni ‘Ujamaa na Kujitemea’, hapa bila shaka lengo kuu la kusema kujitegemea haikuwa tu kujitegema kiuchumi bali ililenga kujitegemea kwa kila nyanja, kiuchumi, kifikra, kimtazamo na hata kiubunifu katika kuimarisha uchumi wetu lakini leo je, tunaweza kujitegemea katika nyanja hizo.

Bila shaka kuna mahali tuliteleza na kujisahau na kuacha dira yetu ya kujitemea na kuelekea mahali ambako haikuwa mwelekeo wetu, ndio maana leo jamii yetu kwa kiwango kikubwa imepoteza mwelekeo wa kujitegemea kifikra hasa pale linapokuja suala la kuangalia fursa za kiuchumi.

Si kweli kuwa Watanzania hawana uwezo wa kufanya kazi kama ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya watu la hasha, uwezo kwa kufanya kazi kwa ni wa mkubwa sana na rasilimali zote tunazo, jambo kubwa hapa ni jukumu tu la kujiandaa kiufanisi kuingia katika ushindani huo.

Hakuna asiyefahamu kuwa Kiswahili ndio lugha yetu kuu ya Taifa na kwa nchi zinazoongea Kiswahili bora duniani Tanzania ni ya kwanza, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba fursa nyingi za kufundisha Kiswahili hata katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki zinatumiwa na mataifa mengine licha ya nafasi nyingi za kufundisha lugha hiyo kwa mataifa ya ukanda huu na hata majirani zake.

Ukiachilia mbali suala la lugha ama elimu, pia kuna fursa mbalimbali katika Jumuiya hii ya Afrika Mashariki, mfano katika sekta mbalimbali za uhandisi, kilimo, madini, utalii, biashara na ujasiriamali lakini bado mwamko kwa ushiriki kwa Watanzania ni mdogo sana.

Waandishi wa kitabu cha njia 101 ya kutengeneza pesa barani Afrika (101 Ways to make Money in Africa), Dk. Harnet Bokrezion na John-Paul Ihuoha, mwaka 2015 walichapisha katika kitabu chao sababu kuu nane zinazovutia kufanya biashara katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika kichwa cha habari kisemacho ‘8 Benefits of doing Business in East African Community (EAC)’, walieleza umuhimu wa kufanya biashara katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Katika sababu ya kwanza walioitaja, wanasema kwamba, utaweza kukutana na idadi ya watu takribani milioni 140 na kufanya nao biashara, hapa maana yake ni nini katika idadi hiyo, ikumbukwe kuwa takribani watu milioni 50 ni Watanzania kwa maana ya idadi kubwa hapo ni Watanzania. Pamoja na hayo walitia msisitizo kuwa ukanda huu bado una ushawishi mkubwa sana kwa mataifa ya Ethiopia, Sudan na Sudan Kusini wakieleza kuwa wakati wowote mataifa hayo yanaweza kuomba kujiunga na ukanda huu, tayari tumeshuhudia Sudan Kusini wameomba kujiunga na tayari wamekubaliwa.

Maana yake nini wakati wowote tunaweza kuona Sudan na Ethiopia wakiomba kujiunga na jumuiya hii, je, Watanzania tumejipanga kutokuwa nyuma katika idadi kubwa ya wanachama wa jumuiya hii wakiendelea kuongezeka? Ni swali ambalo tunapaswa kulijibu haraka iwezekanavyo.

Katika sababu nyingine zilizotajwa kuwa kivutio cha kufanya biashara katika jumuiya hii ya Afrika Mashariki ni ushuru kwa kuvuka mipaka kuwa rahisi, Jumuiya hii inatoa fursa za ushuru wa aina moja, jambo ambalo kwa jumuiya nyingine bado ni changamoto kubwa. Mfano Tanzania ilizindua mfumo wa kielektroniki wa uchukuzi wa mizigo kwa nchi wanachama wa jumuiya hii, mfumo ambao unapunguza idadi ya vizuizi vya mizani njiani wakati wa usafirishaji mizigo, huku ukiwa na ushuru wa aina moja, pia nchi nyingine wanachama nazo zikiwa na mifumo ya urahisishaji wa mfumo wa uchukuzi mizigo, jambo hili linaonesha kuwa ni la kipekee kwa jumuiya mbalimbali barani Afrika.

Vivutio vingine ni kuwa na hati moja ya kuingia katika nchi zote wanachama wa jumuiya hii (Single Visa Issuing). Pia  imeelezwa kuwa hakuna vizuizi vingi vya kibiashara na hata usafirishaji katika jumuiya hii ya Afrika Mashariki, hali kadhalika kuna kituo cha kibiashara cha ukanda huu ambacho kipo nchini Rwanda.

Pamoja na sifa zote hizi lakini bado Watanzania hatujaamka na kuzitumia fursa hizi ipasavyo, ni jukumu la kila mmoja wetu kuamka na kuanza sasa kutafuta fursa hizi pasi na kungoja kutangaziwa, badala yake ni vyema tujitume na kuwa na uwezo wa kujitegemea kama ilivyokuwa ajenda yetu kuu toka uhuru.

Tuzingatie ule usemi usemao: “linalowezekana leo lisingoje kesho,” maana kesho huenda ikawa na ushindani mkubwa zaidi kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia mataifa mbalimbali yakijaribu kukimbilia fursa hii ikiwemo Umoja wa Ulaya ambao wamekuwa wakishawishi wanajumuiya hii kuingia mkataba wa kibiashara nao maarufu kama EPA. Fursa zipo kwa ajili yetu sote wanajumuiya hii tuamke na kuzitumia sasa.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa baruapepe mosesjohn08@yahoo.com au namba ya Simu 0714 840656