Home Makala Kimataifa FUAMBAI SIA AHMADU: MWANAMKE ANAYETETEA UKEKETAJI AFRIKA

FUAMBAI SIA AHMADU: MWANAMKE ANAYETETEA UKEKETAJI AFRIKA

1676
0
SHARE

NA KIZITO MPANGALA

FUAMBAI SIA AHMADU alizaliwa mwaka 1969 nchini Sierra Leone katika jamii ya kabila la Kono, Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo. Alifanya kazi na Unicef nchini Gambia. Fuambai Sia Ahmadu, alipata shahada ya uzamili katika chuo cha masuala ya uchumi jijini London, Uingereza akiwa kama mataalamu wa Anthropojia. Baadaye aliendelea na masomo zaidi katika chuo kikuu cha Chicago na kupata shahada ya uzamivu.

Anafahamika zaidi kwa utetezi wake wa ukeketaji hasa akifikiria zaidi kutoka katika jamii ya kabila la Kono ambapo yeye mwenyewe amekeketwa na anafurahia jambo hilo. Anasema masuala mengi kuhusu ukeketaji hayajaeleweka kwa ufasaha miongoni mwa watu wengi duniani.

Katika kitabu cha “AFRICAN STUDIES” chenye masuala mbalimbali kuhusu jamii mbalimbali za Afrika, lipo swali linalouliza hivi ‘je, ukeketaji ukubaliwe na kuendelezwa kama jambo bora la kimila?’ Watu kadhaa walitoa majibu kuhusu swali hilo kulingana na mtazamo wao wanavyoona. Fuambai Ahmadu alikubali katika insha yake maarufu ya “Rites And Wrongs” kwa mujibu wa kitabu cha “Female circumcision africa: culture, controversy and change” kilichoandikwa na Lynne Rainer, 2001.

Kabla ya jibu la Fuambai Ahmadu, mwanadada Liz Creel Et Al alipinga suala la ukeketaji. Jibu la mwanadada huyu ni kwa mujibu wa ripoti ya “Abandoning female genital cutting: prevalence, attitudes and efforts to end the pracitce” iliyoandikwa na taasisi ya Population Reference Bureau, Agosti 2001 Marekani ambapo Liz anasema Serikali za Afrika zipitishe sheria kali inayobana wakeketaji.

Fuambai Ahmadu anatetea ukeketaji na kukosoa baadhi ya waandishi hasa wasio wa Afrika na wa Afrika pia wanaohimiza ukeketaji ukomeshwe na kuwataka wanawake na wasichana wa Afrika wawe na mwonekano wa Kimagharibi.

Fuambai Ahmadu, anasema na anaamini kwamba ukeketaji haupaswi kuzuiliwa kwa kuwa unaambatana na mila nyingine kulingana na jamii husika inayotekeleza zoezi la ukeketaji ambazo zinampa mkeketwaji kuwa mwanamke anayekubalika zaidi na jamii yake katika mapokeo ya kihistoria ya jamii hiyo. Yeye ni mmojawapo kati ya waliokeketwa katika jamii ya kabila la Kono nchini Sierra Leone.

Fuambai Ahmadu, anasema anachukizwa na wale wanaohubiri ubaya wa ukeketaji kwamba hawajaona na hawajui jema lililomo kwenye shughuli hiyo na hivyo hulinganisha na maeneo wanayoishi wao ambayo ukeketaji haufanyiki.

Katika makala yake ndefu ya “Rites and wrongs: excsion and power among kono women of sierra leone” amezungumza mengi kuhusu ukeketaji. Katika makala hayo, anazishauri Serikali za Afrika siruhusu ukeketaji ufanyike na ziboreshe mazingira ya kufanyia ukeketaji yawe ya kitabibu zaidi yaani ukeketaji ufanyike hospitalini badala ya kienyeji. Anasema “the issue of female initiation and circumcision is of significant intellectual and personal interest to me” yaani “suala la uhamasishaji na ukeketaji kwa wanawake ni jambo la muhimu la kiakili na matakwa binafsi kwangu.”

Fuambai Ahmadu anasema yeye kama mtaalamu wa Anthropolojia kama walivyo Wanaanthroplojia wengine anavutiwa sana na masuala ya kijamii, kidini, kiitikadi na kimila katika jamii nyingi na zaidi ni katika maeneo anayoyajua zaidi. Andai zaidi kwamba suala la ukeketaji liboreshwe mazingira yake na hivyo liwe la kitabibu zaidi ili kuondokana na athari ndogondogo.

Fuambai anasema utafiti mwingi kuhusu ukeketaji unafanywa na wale wasioishi Afrika na pengine hawana asili ya Afrika au wale wanaoishi Afrika na wenye asili ya Afrika, lakini hawaishi katika jamii ambazo zinafanya ukeketaji. Anasema wanawake wengi wanaoandika habari kuhusu madhara ya ukeketaji hawajaishi katika jamii zinazoheshimu ukeketaji. Anaongeza kusema kwamba, ukeketaji hauna madhara, kinachotakiwa sasa ni kuboresha mazingira ya kufanyia shughuli hiyo.

Fuambai ansema wanaopinga ukeketaji wameathiriwa na hoja za kizungu na hisia hasi dhidi ya ukeketaji. Anasema wengi wanaokosoa ukeketaji wanajitetea kwa hoja za Kimagharibi dhidi ya miili ya wanawake kwa kigezo cha hoja kwamba sehemu inayoondolewa katika shughuli ya ukeketaji ndiyo msingi mkuu msisimko wa hisia za mwanamke katika  tendo la ndoa. Yeye anapinga vigezo hivyo vyote na kusema kwamba hata sehemu hiyo ikiondolewa mwanamke atabaki na msisimko wake kama kawaida. Na vile vile inasaidia kumfanya mwanamke awe mwaminifu zaidi katika ndoa yake na kuepukana na tamaa ya kunuia kufuata wanaume wengine.

Fuambai Sia Ahmadu kwa sasa ana uraia wa Marekani. Anatoa msisitizo kwamba kutokana na madhara ya muda mfupi baada ya kukeketwa ni vema jambo hilo lifanyike hospitalini ili kuepuka madhara hayo kuwa makubwa.

Msomaji wa makala haya, umepata nyongeza ya maarifa kuhusu ukeketaji na jinsi Fuambai anavyotetea suala hilo kwa nguvu. Huo ndio msimamo wake. Maoni yako ni muhimu sana kuhusiana na suala hili la ukeketaji hasa katika dunia ya leo ya sayansi na teknolojia kama ilivyoasisiwa rasmi mwezi Januari mwaka 2000.

0692 555 874, 0743 369 108