Home Uchambuzi Fursa za kibiashara DRC zisisubiri mbiu ya JPM

Fursa za kibiashara DRC zisisubiri mbiu ya JPM

2707
0
SHARE

Na Mwandishi Wetu-MAELEZO

WIKI iliyopita Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi, alifanya ziara ya siku mbili nchini Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine aliomba Rais John Magufuli ampigie debe ili aweze kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki – EAC.

Katika ziara hiyo, Rais Tshisekedi alitembelea pia mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, pamoja na bandari ya Dar es Salaam ambayo ndio lango kuu la kupitishaia bidhaa za DR Congo ambazo zinatoka katika mataifa mbalimbali duniani.

Ziara hiyo ambayo kwa ujumla ilikua ya kujitambulisha baada ya kuchaguliwa kuongoza taifa hilo kubwa na lenye utajiri wa madini barani Afrika, ilikuwa pia na lengo la kusisimua ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Kongo ulioasisiwa tangu enzi za Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, Patrice Lumumba pamoja na Mobutu Sesseseko.

Katika salamu zake aliwataka wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa zilizopo DR Congo kwani zinaweza kuinufaisha  nchi yetu kiuchumi lakini pia, Watanzania wanaweza kunufaika na fursa za miundombinu wezeshi tuliyonayo katika kukuza uchumi wetu kupitia biashara na DR Congo.

Hivi karibuni Rais Magufuli, alikutana na wafanyabiashara na wadau wa biashara na uwekezaji Ikulu, Dar es Salaam, ambapo aliwataka wafanyabiashara kutoogopa kufungua milango ya biashara hata nje ya nchi ilimradi walipe kodi stahiki na wazingatie sharia kanuni na taratibu zinazosimamia biashara husika.

Mkutano huo wa aina yake ambao pia ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya biashara na uwekezaji, pamoja na mamlaka za serikali zinazosimamia kwa karibu masuala hayo, ulikua ni changamoto kwa wafanyabiashara hao kujitathmini kama kweli wana nia ya dhati ya kujitajirisha kupitia fursa zilizopo.

Rais Magufuli kwa upande wake aliwaambia wafanyabiashara kuwa kuwa lengo lake ni kuona wakati anaondoka madarakani anaacha mabilionea zaidi ya miamoja hapa nchini, hii inamaanisha kwamba anataka wafanyabiashara ambao wanafanya biashara zenye tija kwa taifa na hata kwa wao wenyewe, ndiyo maana akasisitiza kuwa serikali yake iko pamoja nao ili kuona vikwazo vyote vinavyosasabisha wasisonge mbele vinaondolewa.

Ujio wa Rais Tshisekedi, ni fursa nyingine kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuweza kutumia utajiri wa nchi hiyo katika kukuza biashara na uwekezaji, mfano hakuna uwekezaji mkubwa wa wakongo hapa nchini, kadhalika uwekezaji wa Tanzania nchini DR Congo ni kwa kiasi kidogo sana.

Kwa kutumia bandari ya Dar es Salaam  wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza kuchangamkia masoko ya DR Congo kwa kuagiza na kuuza bidhaa mbalimbali, aidha kwa kutumia reli ya kati wanaweza kujinufaisha kiuchumi kwani bidhaa nyingi hasa zinazozalishwa hapa nchini zinahitajika sana DR Congo, mfano bidhaa za Unga wa mahindi, unga wa muhogo ,maharage na jamii zote za kunde , lakini pia mazao ya mifugo kama nyama na wanyama hai, pamoja na bidhaa za mafuta ya kupikia mabazo zinapatikana kwa wingi hapa nchini.

Fursa nyingine zinazopatikana hapa nchini ni za masoko ya madini, kwakua wakongo nao ni wazalishaji wakubwa wa madini ya aina mbalimbali, nivyema wafanyabiashara wa Tanzania wakalifanyia kazi soko la DR Congo kwa ajili ya kununua madini na kuyaongezea thamani na hatimaye kuyauza katika masoko ya kimataifa.

Mkakati wa DR Congo kujiimarisha kibiashara haukuishia tu kwa Rais Tshisekedi kuja kuwaomba wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza nchini kwake, umejikita pia katika kuhakikisha wanapata nafasi katika jumuiya ya Afrika Mashariki ili kujiimarisha zaidi kiuchumi.

Wakati umefika sasa kwa wafanyabiashara wa Tanzania wakatumia fursa zilizotokana na ziara ya Rais Tshisekedi, ili kujiimarisha kiuchumi hii itaiwezesha nchi yetu ambayo uwepo wa bandari la reli unatosha kusaidia kusisimua biashara kati yetu na DR Congo.

Waswahili wanasema chelewa chelewa utakuta mwana si wako, wenzetu watakaporuhusiwa kuingia kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki, huku tukiwa bado tumelala bila kutumia fursa za uwepo wao tutashtukia wajanja kutoka mataifa mengine wameshakamata masoko yote ya DR Congo.

Aidha ni vyema jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania wakajipanga kuhakikisha wanalitumia soko kubwa la DR Congo kwa ajili ya kujineemesha kibiashara, itakuwa ni jambo la ajabu sana kwa watanzania kushindwa kutumia vyema neema za banadari na reli kwaajili ya kujinufaisha, pia itakua jambo la ajabu zaidi kama wafanyabiashara watasubiri hadi Rais Magufuli aje awaamshe tena na kuanza kuwaomba watumie fursa zilizopo kwaajili ya kujiletea maendeleo.

Soko la DR Cong likitumiwa vizuri Tanzania inaweza ikapaa kiuchumi kwakuwa wana mahitaji makubwa sana hasa ya bidhaa za vyakula ambazo zinalimwa kwa wingi hapa nchi na wakati mwingine zinaharibika kutokana na kukosekana kwa masoko ya uhakika.