Home Uchambuzi Haki za binadamu zipo kwa wakubwa tu?

Haki za binadamu zipo kwa wakubwa tu?

3366
0
SHARE

Mwalimu Julius Nyerere Rais Magufuli 1KILIO cha Watanzania kwa miaka mingi sasa ni kukithiri kwa ufisadi hususan katika serikali na washirika wake.

Niliandika wiki jana katika safu hii kwamba waliotufikisha hapa tulipokwamia ni makuwadi wa soko huria. Walishiriki kwa kila njia kuhakikisha kwamba tunaingia katika mtego wao wa kuabudu na kusujudia soko huria kwamba ndiyo muarobaini wa kila tatizo letu.

Hili linajidhihirisha hata katika zama hizi tulizokuwa nazo za kinachoitwa utumbuaji majipu.

Tanzania ilijikuta  katika matatizo ya kiuchumi yaliyochangiwa na mambo mengi yakiwemo kutokufuatwa kwa sera za ujamaa na kujitegemea, udhaifu wa kiutendaji uliooneshwa na waliokabidhiwa madaraka ya kusimamia uchumi, kukosekana kwa utaratibu wa kuwahamasisha wananchi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kujipatia kipato na wakati huo huo kusaidia kuinua kipato cha taifa.

Yote hayo yakichangiwa pia na matatizo ya uchumi ya dunia yaliyotokana na kupanda maradufu kwa bei za mafuta na kushuka kwa bei za mali ghafi zilizokuwa zikiuzwa kwa mataifa ya magharibi ni baadhi tu ya sababu nyingi zilizofanya uchumi wa nchi changa kama Tanzania kuyumba sana.

Huku kuyumba kwa uchumi wa Tanzania ambao ulikuwa ukiendeshwa kwa msingi wa siasa ya ujamaa na kujitegemea si jambo la ajabu. Ni katika kipindi hicho cha myumbo wa uchumi ndipo wale ambao walikuwa wakitumika ndani ya serikali lakini bila ya kukubaliana na siasa ya ujamaa na kujitegemea walipopata fursa ya kupenyeza sera zao za kudalalia soko huria.

Tanzania ikaaminishwa kwamba muarobaini wa matatizo ya uchumi yamo kwenye kukumbatia soko huria. Hata hivyo, hakukufanyika jitihada zozote za kuwaandaa wananchi kulielewa soko huria ni nini wala kutaka kuwaelekeza kwamba wakitaka kulijua soko hilo wafanya nini. Kwa hakika kilichofanyika ni kuwadanganya kwamba soko huria ni sawa sawa na soko holela lisilokuwa na sheria, kanuni wala taratibu zake.

Katika kipindi hicho cha sintofahamu hiyo ndipo waliokuwa kwenye madaraka wakiimba ujamaa na kujitegemea kwa wananchi lakini kwao wao akili zote zipo kwenye hicho kiitwacho soko huria. Wananchi wakaaminishwa kwamba kila kinachofanyika ni sahihi na hakuna kosa lolote lile.

Walichokuwa wamesahau watu hao ni kwamba wananchi si mabwege. Wanaweza kuwa hawana hiyo elimu ya darasani kutambua yaliyoandikwa kwenye mabuku makubwa makubwa kama ambayo waliyasoma wao, lakini walikuwa na ujanja na werevu wa mtaani wa kutambua ni wakati gani wanahadaiwa na kurushiwa changa la macho na wakati gani wanaambiwa ukweli.

Katika hili la kuhalalisha kila jambo kwa kisingizio cha soko huria na baadae neno mageuzi na utandawazi wananchi wakagundua kwamba kuna tatizo terna kubwa sana.

Ilianza kwa kukosa huduma muhimu huku waliokuwa ndani ya serikali wakifaidika na kila aina ya huduma. Waliambiwa kwamba wanaweza kufuga lakini wakajikuta kwamba hawawezi kufuga kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokuwa na eneo, mifugo, mitaji na kadhalika.

Wananchi wakaambiwa kwamba wanaweza kulima lakini wakajikuta hawana mashamba ya kulima, maji ya kumwagilia hakuna, mbegu shida kupata na kila aina ya tatizo.

Lakini upande wa pili wananchi hao hao wanawaona wale wanaowahimiza kufuga wakiwa na maeneo ya kufugia tena makubwa kupindukia yakiwa na hati miliki, wana kila aina ya mifugo hadi kware na kanga, wanacho chakula ambacho kinapelekwa shambani na gari la serikali na dereva anayelipwa na serikali.

Aidha, wananchi hao hao kwa sababu si mabwege wakagundua kwamba gari la serikali linaweza kutumwa kwenda shamba kuchukua trei mbili au tatu za mayai kwa ajili ya chakula cha mfugaji-mserikali. Gharama zote zinatumbukizwa katika bajeti ya serikali inayolipiwa na huyu mwananchi.

Ujasiriamali na ubunifu ukaelekezwa katika kupunguza fedha za huduma za mahospitali, mashule, magereza na kwingineko na kutumika kwa ajili ya kujenga gesti na baa kila kona huku vinywaji vikipatikana kwa njia mbalimbali nyingi zikiwa si za halali.

Tukafikia hatua kwamba kufanya kazi ndani ya serikali au shirika la umma kukapimwa ni kwa kiasi gani mtu anafaidika yeye na familia yake.

Hadi majuzi hapa ilikuwa mtu akipata kazi serikalini swali linalofuata ni kwamba je, nafasi yake ni njema? Hiyo ina maana je, anayo nafasi ya kula kwa ulaini? Hiyo ikimaanisha je, hapo anaweza kufisidi?

Ukisikia jibu ni kwamba yupo vizuri inamaanisha kwamba nafasi aliyoipata inamuwezesha kuiba! Hiyo ndiyo Tanzania tuliyoijenga baada ya ile Tanzania ya Mwalimu Julius Nyerere. Yaani mtu anapimwa kwa nafasi aliyokuwa nayo katika ulaji wa haramu!

Tanzania ambayo tumemrithisha Rais wa Awamu ya Tano John Magufuli ni ile ya kusifiana kwa ulaji wa haramu. Ni nchi ambayo wanaopishwa viti ni waliopata utajiri wao kwa njia za haramu ambazo wananchi wanazijua.

Taifa ambalo sifa kuu ya mtu kupishwa kiti ni ukwasi aliokuwa nao na wala sio uadilifu wake. Uadilifu ukachukuliwa kama ni matusi. Mstaafu ambaye hakufisidi japokuwa alikuwa akishika mabilioni ya serikali alionekana bwege na mpumbavu ambaye amechagua kufa masikini.

Japo moja la kutia faraja ni kwamba umma wa Tanzania ulikuwa ukitambua hilo. Kwamba haiwezekani umaarufu ukajengwa kwa ufisadi. Ndiyo sababu wananchi waliokuwa wakigumia kwa ndani walipopata fursa ya kueleza msimamo wao hadharani walifanya hivyo. Waliamua kwa sauti moja kumpata mtu ambaye ataamua kuchukua hatamu za uongozi na sio utawala. Mtu ambaye atasimama nao katika kuhakikisha kwamba walau wnarudishiwa nusu ya utu wao kama si utu wote.

Wananchi ambao wanakwenda hospitalini wanakosa dawa kwa sababu kuna mtu kaamua kutumia fedha za dawa kujenga gesti na kutumbua maraha. Wananchi ambao wanakunywa majitaka badala ya maji safi kwa sababu kuna mtu kafisidi fedha za mradi wa maji. Mwananchi ambaye watoto wake wanapinda migongo kwenye mawe darasani kwa sababu kuna mtu kaamuwa kujiongezea pensheni ya maisha kwa kula fedha za madawati. Orodha yao ni ndefu.

Hawa ni wananchi ambao huwezi kuanza kuwaambia kwamba kurejesha heshima yao ni lazima sheria, kanuni na taratibu zifuatwe na hususan haki za binadamu.

Wanakufa kwa maradhi ambayo dawa zake zimeliwa na bwana mkubwa mmoja ndani ya serikali akishirikiana na mtandao wake wa walanguzi na wafanyabiashara wasiokuwa na maadili halafu unawaambia kwamba ili kurejeshewa walau nusu ya utu wao ni lazima sheria, kanuni na taratibu zifuatwe.

Watoto wao wanazikimbia shule kutokana na kupinda migongo kwenye mawe kwa sababu kuna mtu ameamua kuzitapanya fedha za madawati halafu wanapolazimishwa kuzirejesha tunaambiwa kwamba hiyo ifanyike kwa kufuata sheria, kanuni taratibu na haki za binadamu.

Kwa nini wale wote ambao wananchi wanawatuhumu kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma wasiambiwe kufuata sheria, kanuni, taratibu na hasa hasa haki za binadamu na kuzirejesha mara moja?

Pengine wanaolalamika kwamba haki za binadamu hazifuatwi katika kipindi hiki cha utawala wa Awamu ya Tano wangerudi nyuma kidogo na kuuambia umma wa Tanzania hususan walalahoi je, nani atawafidia gharama za madhila yote yaliyotokana na vitendo vya kifisadi vya hao ambao hivi sasa mawakili wa haki za binadamu wanawatetea? Au mkuki kwa nguruwe?

Tukifanya kile kinachoitwa uhakiki wa mtindo wa maisha (lifestyle audit) ni wazi kwamba wachache sana wanaweza kuhalalisha ukwasi waliokuwa nao. Ufisadi ulikuwa ni mtindo wa maisha kiasi kwamba kila upande ulikwisha kukata tamaa ya kurejea katika uadilifu.

Mafisadi walifikia mahali wakajiaminisha kwamba ni mbele kwa mbele na hakuna kitakachoweza kubadilisha mfumo haramu ambao walijaribu kuujenga kwa kutumia njia zisizo halali kujilimbikizia mali. Upande mwingine wananchi nao walifikia hatua wakaona kwamba hakuna la kufanya isipokuwa kukubaliana na hali hiyo.

Ndiyo sababu katika uchaguzi wa 2015 wananchi walifikia hatua ya kusema potelea mbali liwalo na liwe lazima tupate mabadiliko. Ni wananchi ndio waliolazimisha ajenda ya mabadiliko ambayo hivi sasa inatekelezwa na Rais Magufuli. Wananchi walitaka mabadiliko wakiamini kwamba yatawasaidia kuwaondoa katika dhiki ambayo wamekuwa nayo tangu kutupipiliwa mbali kwa ujamaa na kujitegemea.

Watanzania hawajawahi kupitishwa katika tuisheni ya kujua uchumi wa soko huria ni nini. Wanahitaji tuisheni tena ya nguvu ya kuwafanya waelewe uchumi wa soko huria unahusiana vipi na hapa ni kazi tu.

Wakitambua kwamba hata yote anayoyafanya Rais Magufuli hayatakuwa na maana bila ya kuchapa kazi kwa bidii basi mabadiliko ya kweli katika jamii yetu yatawezekana. Ni lazima kuondokana na fikra kwamba wanaweza kutajirika bila ya kufanya kazi kweli kweli.

Jitihada zinazofanywa bivi sasa ni za kusafisha nyumba na hili lazima litakuwa na maumivu. Lakini kujaribu kusema kwamba kinachoendelea hivi sasa ni kuvunja haki za binadamu ni propaganda isiyokuwa na mashiko.

Tunashuhudia hivi sasa baadhi ya watawala ambao waliwahi kulalamikia hadi bungeni wakiwajibishwa kutokana na makosa ambayo wamekuwa wakiyafanya kama utaratibu wao wa maisha.

Wanawajibishwa kwa haki kabisa tena kwa kusimamishwa kazi tu halafu mtu anadiriki kujitokeza hadharani na kumtetea kwamba kaonewa. Sasa nani aliyekuwa akimuonea mwenzake ni mtawala ambaye alikuwa akifisidi mali za umma kila alikopelekwa kikazi au ni mwananchi ndiye sasa anaonea kwa klumsimamisha kazi huyo mtuhumiwa?

Bila shaka umefika wakati wa kujiuliza ni aina gani ya jamii tunayotaka kuijenga. Tanzania bila ufisadi inawezekana. Kila aliyejilimbikizia mali kwa njia azijuazo yeye kwamba si halali pengine wangekuja na ujasiri wa kujisalimisha kwa umma ili waombe radhi na kurejesha mali za wizi badala ya kupitia katika migongo ya wanaharakati.

Haiwezekani anapodhalilishwa mwananchi isiwe tatizo isipokuwa mdhalilishaji anapoguswa basi haki za binadamu zinakuwa zimekiukwa. Au ubinadamu unapimwa kwa wingi wa fedha na vyeo?