Home Uchambuzi Afrika HAKUNA WA KUMZUIA MUSEVENI KUONGOZA MAISHA

HAKUNA WA KUMZUIA MUSEVENI KUONGOZA MAISHA

1322
0
SHARE

KAMPALA, UGANDA

Wiki hii kamati moja ya Bunge la Uganda imeanza kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu ule mradi wa serikali uliopachikwa jina la ‘urais wa maisha.’

Kamati hiyo ya Sheria na Masuala ya Bunge (Legal and Parliamentary Affairs Committee) imewaandikia barua vikundi na watu mbali mbali kufika mbele yake ili kutoa maoni yao kuhusu muswada wa marekebisho wa kuondoa au kutoondoa vipengele katika Katiba ya nchi hiyo vilivyoweka ukomo wa umri kwa wagombea urais.

Wadadisi wa mambo wanasema kuna baadhi ya watu watafika mbele ya kamati hiyo lakini wengine hawatakwenda. Wanasema kwa wale watakaokwenda, baadhi wataunga mkono marekebisho, wengine watapinga na wengine watazungumza lugha ya kutokuwa na upande.

Kwa vyovyote vile kwenda tu kwenye kamati hiyo kutakuwa kumehalalisha mchakato ambao Rais Yoweri Museveni ameuanzisha ili ajipatie urais wa maisha.

Kuondoa kwa ukomo wa umri kutamruhusu Museveni kugombea tena urais mwaka 2021 wakati atakuwa ameshapita umri wa miaka 75 ambao ni kikomo kilichopo katika Katiba.

Kutokana na kuondolewa kwa ukomo wa vipindi vya urais katika Katiba hiyo hiyo, hakuna kihunzi chochote sasa hivi kitakachomzuia rais Museveni kuendelea kukaa tu madarakani hadi labda yeye mwenyewe aamue kuondoka kwa hiari yake, atimuliwe kwa nguvu za wananchi au afariki dunia.

Wadadisi wa mambo wanasema iwapo kikundi au mtu yoyote atakayefika mbele ya kamati hiyo ya Bunge na kupinga mapendekezo ya muswada, hilo halitakuwa na maana yoyote. Wanasema kufika kwenye kamati au kutofika kutachukuliwa kama wameshiriki katika mjadala wa mapendekezo katika kuwezesha urais wa maisha.
Wadadisi wa mambo wanasema kwa kawaida viongozi wanaodhamiria kuwa marais wa maisha hutafuta mchakato wa kukumbatia ili kuwa na uhalali wa mradi wao. Wanasema kama maoni yatakayotolewa yatazingatiwa, kuna kila sababu ya mradi huo kukwama.

Lakini kinachotokea kinakwenda mbali zaidi na mjadala tu unaohusisha raia wa kawaida. Nguvu za ziada zinaonekana ndani na nje ya kamati hiyo ya Bunge.

Rais Museveni anataka mjadala unaoweza kudhibitiwa – hususan mjadala unaoanzia na kuishia na “ndiyo” kuhusu urais wa maisha.

Na iwapo kama ni kweli yanayoandikwa na magazeti kuhusu yaliyojiri katika kikao cha Baraza Kuu la  chama kinachotawala cha NRM (National Resistance Movement), basi hakuna uthibitisho mwingine unaohitajika kuhusu kufanikiwa kwa mradi huo.

Wajumbe wa Baraza hilo walitakiwa kutia saini zao za kuunga mkono taarifa iliyotayarishwa kabla.

Hivyo kwa namna yoyote ile kujifanya eti kuna mjadala wa wazi unaoendelea unaowataka wananchi watoe mawazo yao katika kamati ya Bunge ni kuota ndoto za mchana.

Hata iwapo kamati hiyo itapendekeza kwamba kutokana na maoni ya wengi vipengele vya Katiba husika visirekebishwe, ripoti yake itapinduliwa Bungeni kwa kutumia uwingi wa Wabunge wa Chama tawala – NRM.
Wengi wanaona kwamba Museveni si mtu wa kufukuzia kitu kikubwa kama hiki cha urais wa maisha kwa moyo nusu. Na hii inaelezea kwa nini Wabunge wengi wanaopinga watatembezewa bakora ndani ya majengo ya Bunge, au kwa nini Wabunge hawa na watu wengine wenye mawazo kama yao hawaruhusiwi kujihamasisha kwa uhuru kabisa katika kuchangia mawazo yao hadharani, au kwa nini baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanaandamwa.

Na si vyombo vya usalama pekee vilivyoshirikishwa katika kutetea mradi wa urais wa maisha. Kuna taasisi nyingne kama vile Tume ya Mawasiliano (Uganda Communications Commission –UCC) nayo pia inaunga mkono mradi huo.

Na zipo nyenzo nyingine nyingi zilizotayarishwa dhidi ya wapinzani katika kufanikisha mradi wa urais wa maisha wa Yoweri Museveni. Inadaiwa mamilioni ya fedha zimetengwa kuwalainisha au kuwanunua wapinzani.

Wadadisi wa mambo wanasema wapinzani wa mradi wa urais wa maisha bado wanayo nafasi nzuri ya kuzuia na wanataja sababu kubwa ni kwamba chama tawala NRM sasa hivi kinaonekana kujificha mbele ya wananchi katika kuitetea hadharani hoja yao, bila shaka ni kutokana na kukosa hoja za msingi za kuitetea.

Badala yake wanawatumia zaidi Wabunge wao (wa NRM) ambao ni rahisi kuwadhibiti kwa kutumia mbinu mbali mbali ili wasimame kwenye mstari rasmi wa serikali.

Aidha ghasia zilizoibuka Bungeni hivi karibuni baada ya muswada wa marekebisho ya katiba kuwasilishwa zilizimwa kwa kutumia vikosi vya usalama. Picha za runinga zilionyesha Wabunge wa pande mbili wakirushiana makonde na samani za Bunge kama vile viti nk.

Matukio haya yote ni ishara kwamba mradi huo wa urais wa maisha hauungwi mkono na wananchi wengi nchini Uganda, pamoja ukweli kwamba utapita tu.