Home kitaifa Hedhi salama inapogeuka kikwazo utoaji elimu

Hedhi salama inapogeuka kikwazo utoaji elimu

2842
0
SHARE

LEONARD MANG’OHA

LICHA ya juhudi za kuwezesha kutoa elimu kwa wote watoto wa kike wanaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowakwamisha kupata haki hiyo kama inavyokusudiwa.

Moja ya changamoto hizo ni pamoja na wasichana wengi kushindwa kuhudhuria masomo wakati wa hedhi kukosa taulo za kike na shule nyingi kutokuwa na mazingira salama ya kujihifadhi.

Kupitia kongamano la hedhi salama lililoratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) hivi karibuni baadhi ya wadau wanadai kuwa kushindwa kupatika ufumbuzi kunatokana na wanawake wengi kutokuwa katika nafasi za uongozi za kufanya uamuzi.

Mhandisi Wilhelmina Malima, anasema moja ya mambo muhimu wakati wa hedhi ni pamoja na upatikanaji wa huduma za maji, elimu, afya na usafi wa mazingira kwa mfano shule kuwa na chumba maalumu kitakachotumiwa na watoto wa kike wakati hedhi wawapo shuleni.

Anasema ingawa miongozo ipo, utekelezaji wake ndiyo umekuwa changamoto katika maeneo mengi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ukosefu wa fedha.

“Kwa mfano kuna utafiti wa NIMR wa mwaka jana, unaoendelea hadi mwaka huu ukiangalia upatikanaji wa huduma muhimu, ambapo ni asilimia 17 tu ya shule ndizo zenye hivyo vyumba. Lakini pia tuangalie uendelevu wa mambo hayo yanatekelezwa vipi,”anasema Mhandisi Wilhelmina.

Mshauri wa Kujitegemea wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi, Dk. Lucy Sendi, anasema wamefanya utafiti mdogo wa kuangalia mahitaji ya hedhi salama mashuleni na kubaini kuwa kukosekana kwake kunasababisha wasichana wengi kukosa masomo, kupungua kwa ufanisi mashuleni na kukosa kujiamini. 

Hata hivyo anasema kuwa serikali yenyewe haiwezi kumaliza changamoto hiyo badala yake inaweza kwa kushirikiana na sekta binafsi ikiwa kutakuwa na sera nzuri za serikali.

Anasema kuwa tafiti nyingi zilizofanyika hazijaangazia unyanyapaa kuhusu hedhi na kwamba ni muhimu elimu hiyo itolewe kupitia vyombo vya habari na vyombo vingine ambavyo si kawaida kuzungumzia suala la hedhi.

“Tusiwaache wenzetu wanaume nyuma tuwafanye waone hedhi si suala la wanawake tu ila ni muhimu ambalo kila mwanamke lazima anapitia,”anasema Dk. Lucy.

Mtaalamu wa Afya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Rabia Yusuf, anasema tayari sera iko katika hatua za mwisho na kwamba itakapopitishwa itakuwa moja ya nyenzo muhimu itakayosaidia kufanya utekelezaji wa hedhi salama nchini.

Anasema tayari wamefanya majabio kwa kuingiza masuala hayo katika baadhi ya shule za msingi katika baadhi ya mikoa baada ya kuona ina mwitikio mzuri wamefanya tathimini.

Anasema wanategemea elimu hiyo ifike shule za sekondari, vyuo vya kati na hata vyuo vya elimu ya juu.

Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan lyimo (Chadema), anasema kumekuwa na hali ya kutokuelewana katika hoja nyingi kwa sababu ya mtazamo wa kisiasa, lakini ziko baadhi halmashauri zimefanya vizuri na kwamba suala hilo linahitaji nguvu ya pamoja ili kulifanikisha. 

Anashauri kuwa suala hilo linapaswa kuanzia kwenye sera kisha litungiwe sheria ili kurahisisha utekelezaji wake.

“Ninashukuru sasa baadhi ya wanaume wameanza kulizungumzia suala hili. Serikali inapaswa ije na sera nzuri ambazo zitawawezesha wadau kushiriki vema katika suala hili.

Kuhusu nafasi ya wadau na serikali katika kuwezesha hedhi salama pamoja na utengwaji wa rasilimali kupitia bajeti Ofisa Programu wa TGNP, Deogratius Temba, anasema utetezi wa hedhi salama na usafi wa mazingira kwa wasichana ni matokeo ya chambuzi za bajeti na tafiti ambazo zimekuwa zikiibua mahudhurio hafifu au kukosa masomo kwa wasichana wakati wa hedhi.

Kutokana na kukabiliana na changamoto zinazosababisha wasichana wengi kukosa utulivu na kuzingatia masomo wakati wa hedhi, wasichana wengi wamekuwa watoro na baadhi yao wameacha masomo.

Temba anasema mwaka 2015/16 chambuzi za bajeti ya taifa na zile za halmashauri zilipendekeza kuweka nguvu kwenye halmashauri na serikali kuu ili hedhi salama liwe suala la kisera. 

Anasema kupitia utafiti shirikishi wakawa wanatoa elimu kwa jamii na suala la hedhi salama likawa linaibuka lakini likawa linafanywa kwa kificho.

Anasema kupitia mpango uliohusisha kiasi cha halmashauri 10, mbili kati ya hizi yaani Kishapu na Kisarawe zikatenga sehemu kwenye bajeti zao kutokana na mapato yao ya ndani kuwezesha upatikanaji wa hedhi salama katika maeneo ya shule na kuonesha mafanikio makubwa.

Temba anasema kupitia utaratibu huo wa uchambuzi wa bajeti wamekuwa wakipata matokeo ya haraka ambayo pia yamewezesha kutoa elimu inayowasaidia wananchi kulijadili masuala ya hedhi salama kuanzia ngazi za chini, kwenye vikao vya baraza la madiwani na hatimaye kwenye halmashauri.

Hata hivyo anakiri kuwa licha ya kuwapo mabadiliko ya hapa na pale, bado kuna matatizo ya upatikanaji wa miundombinu ya maji katika shule nyingi nchini na hata baadhi ya shule zenye miundombinu hazina maji.

Ushawishi huo ulianzia kwenye timu iliyokuwa ikipitia mwongozo wa uandaaji wa bajeti na kushauri taasisi za afya, kilimo, maji, elimu, ardhi na Tamisemi kama vinara wa masuala ya jinsia waanze kutenga bajeti yenye mrengo wa kijinsia.

Kwa kushirikiana na wabunge wanawake na kikundi cha wabunge vinara wa jinsia waliendelelea kuibua mijadala bingeni na katika za Kamati za Kudumu za Bunge na kusababisha kuondolewa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

TGNP imejikita katika kufanya tafiti, chambuzi wa sera, sheria, miongozo na bajeti katika mrengo wa kijinsia na mapendekezo ya kazi hizo huwapatia nguvu ya kufanya ushawishi kwa serikali na wadau wengine na kuweka msukumo katika nyanja zote. 

Kutokana na jitihada hizo mwaka 2016/17 Halmashauri ya Kishapu ilikuwa ya kwanza kutenga Sh milioni 6.2 katika bajeti yake kwa ajili ya kununua taulo za kike na kuzisambaza kwa wasichana wa shule za sekondari.

Temba anasema hadi kufikia mwaka huu wa fedha halmashauri za Kishapu, Mbeya, Morogoro, Ilala na Kisarawe zinatenga bajeti kupitia mapato yake ya ndani kutoa taulo hizo kwa wanafunzi wa kike wawapo shuleni. 

“Kwa hiyo mtaona suala lolote linalohitaji mabadiliko chanya ni lazima kushirikisha wadau wengi kadiri muwezavyo. Lengo letu ni kuhakikisha vifaa husika kwa hedhi salama vinapatikana kwa shule zote.

Anasema kuwa mwaka 2016 Serikali ilianza kutekeleza mwongozo wa Taifa wa SWASH unaotoa maelekezo kuhusu hedhi salama kwa wanafunzi linapewa kipaumbele.

Na kuelekeza wajibu wa wadau wote kuanzia wafadhili, wizara husika, halmashauri, kata, kijiji, kamati za shule, wazazi na wanafunzi.

Mwaka 2018, wadau wa utekelezaji wa mwongozo huo likiwamo Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) na Shirika la Afya Duniani (WHO) walifanya tathimini na utafiti mdogo uliofanyika unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 52 ya shule kwa Tanzania mwaka zilikuwa na vyanzo vya maji ya kunywa. 

Hata hivyo utafiti huo ulibainisha kuwa zaidi ya asilimia 16 ya shule hizo zilipata maji kwa wakati tu baadaye yakakoma kupatikana. 

Temba anasema kuwa lengo la TGNP ni kuhakikisha hedhi salama linakuwa suala la kisera na linaingizwa kwenye miongozo ya bajeti na sheria za fedha ili kujenga uendelevu.

Anashauri bajeti ya serikali ioneshe kiasi cha fedha kinachoelekezwa kupitia Wizara ya Elimu, kuboresha mazingira na mahitaji ya hedhi salama, halmashauri ziendelee kutenga bajeti kwa ajili ya kutoa pedi kwa wasichana.

Pia anashauri kuangaliwa kwa bei ya taulo za kike ili kuwasaidia watoto wa kike wanaotoka katika familia masikini hususan wale wa kijijini, mamlaka kama vile TBS kuihakikishia jamii usalama wa bidhaa zilizopo masokoni kama inavyofanyika kwenye vipodozi. 

Anasema utaratibu wa uanzishwaji wa viwanda vya pedi kuwa na mlolongo mrefu kama ilivyo kwa viwanda vya dawa na kinga huenda pia inatatiza uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza bidhaa hiyo.

Serikali kuhamasisha viwanda vya ndani kwa kupunguza uingizwaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi kama inavyofanyika kwenye sukari.