Home Uchambuzi HERI KUFIA WENYE KUONEWA NA KUNYANYASWA…

HERI KUFIA WENYE KUONEWA NA KUNYANYASWA…

3232
0
SHARE

NA JOSEPH MIHANGWA

s“Serikali za wanyama, na ndege au  wadudu/Ndani zina taadhima, kama kwa maabudu; Na watu wenye hekima, siku hizi hawamudu/Madaraka  na heshima, heri mnyama na  dudu; Na heshima imehama, baki taka na mashudu/Na madhara na dhuluma, miungu ya kuabudu”. [Shaaban Robert:  Kielelezo cha Fasili uk. 37]. Endelea..

Tafsiri ya neno “Mafia” kwa mujibu wa Kamusi ya TUKI [2006], ya Kiingereza – Kiswahili, ni Chama cha siri [katika Sisilia, Italia na Marekani] kinachojishughulisha na ujangili na ujambazi wa kiuchumi na kisiasa”.  Mara nyingi lengo lake ni kuitesa na kuitifua Serikali madarakani.

Kwa kifupi “Mafia” ni genge la wahalifu dhidi ya Serikali.  Linaweza kuwa la ndani ya nchi; au linaweza kuwa la kimataifa likiendesha shughuli nchini kutoka nje ya nchi kwa kushirikisha mawakala wa nchini kama vile Wafanyabiashara wakubwa na Wawekezaji, Ma-Afisa wa Umma, Wanasiasa na wengineo.  Genge hili limejidhihirisha siku za karibuni katika kashfa za IPTL/TANESCO/Richmond/Dowans; EPA/BOT, Meremeta, Tangold; kashfa ya rada na ununuzi wa ndege ya Rais [BAe Systems] na katika uporaji na utoroshaji rasilimali za Taifa, wakiwamo wanyama hai kama Twiga, kwa kutaja matukio machache tu.  ni kundi lenye kupinga au kupiga vita miradi sahihi ya maendeleo kuhakikisha nchi haiendelei wala kujitegemea, bali kugeuzwa “shamba la Bibi”.

Katika nchi kama vile Italia, Columbia, Marekani na hata nchini Urusi, genge hili lina nguvu kubwa [kama ambavyo tu linajaribu kujiimarisha hapa nchini] na Serikali yoyote ikitaka kupambana nalo, yapashwa ijizatiti kikamilifu.

Genge la “Mafia” huendesha Serikali yake isiyo rasmi [parallel government] lakini yenye nguvu kuliko hata Serikali halali madarakani.  Angalia jinsi Maazimio mengi ya Chama tawala, Miswada na Maazimio ya Bunge yenye kujenga nchi na yenye kujali wanyonge, yanavyoweza kuyeyuka bila kutekelezwa, kwa nguvu ya genge hili!. Genge hili limejidhihirisha pia katika chaguzi za kisiasa na katika kupinga sera bora za Chama na Serikali.

Kwa mfano, Kikao kimoja cha Halmashauri Kuu [NEC] ya CCM kilichofanyika huko Butiama miaka ya karibuni, kilijadili  Maazimio makubwa mawili yaliyopitishwa huko Dodoma kabla ya hapo. Moja lilikuwa kwamba, Wafanyabiashara wanaopenda kuwania uongozi wachague moja, kati ya siasa na biashara; kwamba iwe mwiko kutumikia vyote viwili kwa wakati mmoja kwa mtu mmoja.

Azimio la pili lilikuwa kwamba, Viongozi wote wa Chama wanaoguswa na tuhuma za ufisadi wajiengue madarakani wenyewe chini ya dhana ya “kujivua gamba”, vinginevyo Chama kitawang’atua kwa aibu.  Walipewa miezi minne au sita hivi kufanya hivyo.

Si Azimio kuchagua biashara na siasa wala “kujivua gamba” lililotekelezwa.  Ilipofika kugombea, Wafanyabiashara walichangamkia nafasi za uongozi, tena kwa nguvu ya fedha kana kwamba hapakuwa na Azimio hilo lenye masharti kwao; wakapeta na hakuna anayehoji.

Vivyo hivyo, pamoja na kufahamika kwa umma na kwa Serikali pia baadhi ya Viongozi hao waliotakiwa “kujivua gamba”, mtandao wa ufisadi ulipojipanga kwa mapambano, kila kitu kikalegea; Azimio la Chama la kuwang’atua kwa nguvu wanaotuhumiwa likabadilishwa kisanii kwa kutoa ruhusa “wajipime wenyewe”, kisha wajivue gamba. Ikawa kimya; wakaendelea kudunda, tena kwa kejeli, maringo na dharau kwa Chama na Serikali madarakani, na baadhi yao kusikika wakikejeli kwamba, wamejaribu kulivua gamba, lakini limekatalia kiunoni, halitoki; na zaidi kwamba, “Mwenye kutaka litoke ashike shoka aje kujaribu kulitoa na tuone”.

Hilo lilikuwa ni sehemu tu ya genge la “Mafia” ndani ya nchi, lina mkono katika utoroshaji wa matrilioni ya fedha na kuzihifadhi kwenye Mabenki nje ya nchi; lilikuwa na mkono pia katika chaguzi chafu za CCM kwa matumizi makubwa ya fedha na kuibuka kwa makundi ndani ya Chama hicho.  Linajihusisha na biashara ya dawa za kulevya hapa, magendo na biashara ya utakatishaji fedha [money laundering]. Angalia jinsi ilivyo vigumu kupambana na dawa za kulevya. Angalia namna lile Azimio la Bunge wakati huo, la Serikali kufuatilia tuhuma za “vigogo” kuweka fedha nje ya nchi, lilivyojifia kwa nguvu za genge hili. Hata leo, hakuna kinachoendelea juu ya hilo licha ya Serikali kujua mengi.  Kwa nini?. Hofu au ushirikishwaji?.

Genge la Mafia lina vikosi vya mauaji na kudhuru watu wanaoonekana kupingana nalo.  Laweza kumuondoa ki-uhai au ki-madaraka kwa staili mbali mbali, yeyote anayeonekana kulikwaza.  Halichagui hadhi ya mtu, awe Rais wa nchi, Waziri Mkuu, Jaji, Mkuu wa Polisi hata Wakili nguli anayeweza kutumia Sheria za nchi kuliumbua. Hupenyeza watu wake katika taasisi nyeti za utawala wa nchi, ikiwamo Utumishi wa Umma kuhakikisha kwamba Serikali inatumikia uharamia zaidi kuliko kutumikia wananchi; na pia kuhakikisha kwamba mipango ya nchi inanufaisha maharamia wa Kimataifa na mawakala wao wa nchini badala ya kuneemesha nchi na wananchi na kwa Katiba ya nchi kubezwa..

Angalia jinsi ibara ya 9 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inavyobezwa, kupuuzwa na kudhalilishwa, na sisi kusalimu amri kwa nguvu ya genge hili, kwa kuwasaliti wananchi bila hofu ya kuwajibishwa.  Ibara hiyo 9 (C) inaitaka Serikali kuhakikisha: “Kwamba …. utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na kumzuia mtu kumnyonya mtu mwingine”, na 9 (i), “Kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi, na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umaskini, ujinga na maradhi”; na 9 (j), “Kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi”.

Haya nimeyaelezea vizuri hapo mwanzo kwa kutoa tahadhari kwa uongozi kwamba, kuongoza ni kujitoa mhanga ili unaowaongoza wasalimike na kustawi; bora kufa ukiwa upande wa wanyonge, maana utaacha jina zuri, kuliko kufa swahiba wa mafisadi, maana utalaaniwa pamoja na vizazi vyako.  Je, kwa kubeza yote haya, ni kweli tumesalimu amri kwa uharamia huu?.

Nchi inataka Viongozi shupavu, mithili ya Mfalme Julius Caezar wa Rumi ya kale, ambaye hakutawala na hofu; mwenye kuthubutu kusimama kichwa juu kuokoa kudidimia kwa Taifa aseme, kwa maneno ya Caezar:  “Waoga hufa mara nyingi kabla ya vifo vyao, mashujaa hawaonji kifo ila mara moja …. kwani kifo, kwa sababu ni hatima ya lazima, kitakuja siku itakapotimia; Caezar hawezi, yeye [mimi] ni hatari kali kuzidi hatari”  [Julius Caezar, Kitendo cha II Onesho la II]. Yataka uongozi bora, shupavu na “hatari” kuweza kuogopwa na maharamia wa ndani na nje; na wale wanaokejeli kwamba “gamba limekomea kiunoni, halitoki” wajue hivyo.

Genge hili hatari laweza kujipenyeza pia ndani ya vyombo vya Usalama – hususani Jeshi la Polisi, ili kuhakikisha kwamba uhalifu haushughulikiwi na kutoa mwanya lifanye shughuli zake bila kufuatiliwa. Linaweza kujipenyeza pia kwenye taasisi za dini ili kuzua mitafaruku ya kidini Taifa lipoteze dira ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake na nchi isitawalike, iwe “vita vya panzi, furaha kwa Kunguru”.

Bunge la nchi lenye kutekwa na genge la Mafia huwa na sura mbili zifuatazo:  Kwanza ni Bunge lenye Wabunge ambao wengi huingia kwa ushindi wa mizengwe na wenye kutawaliwa na fedha chafu.  Wabunge hao wako Bungeni kutafuta maslahi binafsi badala ya kuwakilisha wananchi. Hawasimamii hoja za wananchi, bali kazi yao ni kushawishi kupitishwa kwa miswada isiyowakilisha maslahi ya jamii pana.

Pili, ni Bunge lisilowakilisha matakwa ya walio wengi – Wakulima na Wafanyakazi; bali ni Bunge la Wafanyabiashara, Wasomi na Wanataaluma walioziasi taaluma zao kufukuzia “malisho mapya”. Ili kuhakikisha Bunge halihoji na kuchukua hatua dhidi ya uharamia huo, baadhi ya Wabunge watapewa Ukurugenzi wa Bodi katika Makampuni ya kifisadi na ya Umma yaliyo na ubia na Wawekezaji, ili kuwaziba midomo wasihoji Bungeni. Genge hili la Mafia linaundwa na kina nani?  Na kwa nini hupata nguvu siku hadi siku?

Kwa maudhui yake, genge hili huhusisha baadhi ya Wanasiasa Waandamizi, Vigogo wa Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Wafanyabiashara wakubwa na Watendaji Waandamizi Serikalini.  Ndiyo maana mtandao huu huweza kuhujumu nchi bila wahusika kuhofia kukamatwa wala kuwajibishwa.

Tumeambiwa mara nyingi na Viongozi wetu kwamba, “Mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe”; sasa tunagundua kwa kuchelewa kwamba, kumbe “mtaji” na nguvu za baadhi ya Viongozi ni matokeo ya kutumia madaraka yao vibaya kwa kushirikiana na genge la maharamia waporao jasho la wadunda kazi wa nchi. Kwa sababu hii, ilivyo sasa ni kwamba, nguvu sawazishi [countervailing power]  kwa maovu yanayoisibu nchi ilitoweka, Viongozi wakaweka mbele maslahi binafsi badala ya maslahi ya nchi na watu wake  bila hofu ya kuwajibishwa; siasa ikabinafsishwa na kikundi kidogo chenye nguvu ya fedha; asasi za kiraia zikabanwa; Chama ambacho hapo mwanzo kilikuwa kimbilio la wanyonge kikabakia kwa jina tu na kwa ajili ya chaguzi, kikageuzwa taasisi ya kitabaka kuwanufaisha wachache kiuchumi badala ya kuwa chombo cha kuwasemea watu na kutetea haki zao.

Wakati haya yakiendelea wananchi wako kimya, na kwa ukimya huo wakiangalia na kujihoji: “udhalimu huu utaendelea hadi lini bila kukoma?”. Ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anayetoa jibu kwa kutahadhalisha katika kitabu: “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania”  kwamba, “Kimya kina mshindo mkuu, Kimya msidhani ni ishara ya amani”.

Mwalimu anaendelea kwa kumnukuu Bwana Muyaka bin Haji, anasema: “Kimya msikidharau, nami sikidharawile;/Kimya kina mambo mbele; tahadharini na kimya”.

Tumesema, “turuhusu fikra mia moja tofauti kumea; mawazo kinzani mia moja kumenyana” ili kupata ukweli na mawazo mapya chanya.  Ukimya wa kulazimishwa ni hatari; hujenga chuki na milipuko isiyoleta afya wala kuneemesha jamii.