Home Habari HESLB ilivyorejesha faraja kwa walioomba mikopo mwaka 2020

HESLB ilivyorejesha faraja kwa walioomba mikopo mwaka 2020

3822
0
SHARE
Afisa Mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Goodluck Goda akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya wateja waliofika katika Banda la HESLB wakati wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 5 mwaka huu.

NA ISMAIL NGAYONGA, HESLB

SERIKALI kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), hivi karibuni ilitangaza kuongeza siku 10 za kupokea maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo na taasisi za elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2020/2021.

Uamuzi huo ulitokana na maombi na maoni ya wadau mbalimbali wakiwemo waombaji mikopo, wazazi na walezi baada ya kumalizika kwa muda wa awali wa siku 40 uliotolewa na HESLB kuomba na kukamilisha maombi ya mikopo kwa mujibu wa mwongozo na mwingiliano wa mifumo ya kimamlaka ya utambuzi wa taarifa  za waombaji.

Julai 21 mwaka huu, HESLB ilitoa mwongozo wa uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ulioainisha sifa, vigezo na taratibu mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa na waombaji mikopo, ili kuhakikisha kuwa maombi hayo yanawasilishwa kwa ukamilifu ikiwemo kuwa na nyaraka na viambatisho sahihi vilivyosainiwa na kupata uthibitisho kutoka mamlaka zinazohusika.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, HESLB ilitoa muda wa siku 40 kwa kufungua dirisha la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kuanzia Julai 21 hadi 31 Agosti mwaka huu kwa wanafunzi wahitaji kujaza fomu za maombi ya mikopo kwa usahihi kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa kwa kuambatisha nyaraka mbalimbali ili kuthibitisha sifa na vigezo vya uhitaji wa mikopo hiyo.

Hivi karibuni, HESLB ilikuwa ni miongoni mwa taasisi 60 zinazohusika na elimu ya juu zilizoshiriki maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 5 mwaka huu, ambapo ilitumia maonesho hayo kutoa ufafanuzi wa majukumu mbalimbali ya taasisi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maonesho hayo kuhusu hali ya uombaji mikopo kwa mwaka 2020/2021, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema kufuatia maoni ya wadau mbalimbali, HESLB imeamua kuongeza muda wa maombi ya mikopo kwa siku 10 kuanzia Septemba Mosi hadi 10 mwaka huu ili kutoa fursa kwa wanafunzi wahitaji wengi zaidi kukamilisha na kuwasilisha maombi yao.

Badru anasema kufikia Agosti 31 mwaka huu, HESLB ilikuwa imepokea jumla ya maombi 85,921, ambapo kati ya hayo maombi 71,888 (asilimia 84) yamewasilishwa kwa ukamilifu yakiwa na viambatisho pamoja na kusaiwa sehemu zinazohitajika (mwombaji, mdamini, serikali za mitaa/kijiji, wakili n.k) na maombi mengine 14,033 yapo katika hatua mbalimbali na yanahitaji kukamilishwa na waombaji.

Anaongeza kuwa kundi la waombaji wasiokamilisha maombi yao ni pamoja na wanafunzi wahitaji waliowasilisha nyaraka muhimu za uombaji mikopo ikiwemo vyeti vya kuzaliwa au vifo bila kudhibitishwa na Mamlaka ya Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa waombaji wa Tanzania Bara na Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA) kwa waombaji wa Zanzibar.

Akifafanua zaidi Badru anasema tathimini iliyofanywa na HESLB wakati wa programu ya uendeshaji mafunzo ujazaji wa fomu za maombi ya mikopo kwa vijana waliopo katika Kambi 18 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ilibainika upo umuhimu wa kuongezwa muda wa kukamilisha maombi yao kutokana na mafunzo ya JKT kuingiliana na dirisha la maombi ya mikopo.

“Baadhi ya vijana waliopo katika kambi za JKT walipendekeza kuwa ipo haja ya kuongeza muda wa ziada ili kukamilisha maombi yao, kwa kuwa wapo waliomaliza kukamilisha na wengine bado ambao ni kati ya hao 14,033 na kwa kuwa malengo ya HESLB ni kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia za kaya masikini, hivyo tumeona ni bora tukaongeza muda wa kukamilisha maombi hayo’.

‘’Mwaka jana 2019/2020 tulipokea jumla ya maombi 87,636 na kati ya hayo 82,043 yalikuwa kamilifu, tumeamua kushirikiana na wadau wetu muhimu ikiwemo Shirika la Posta Tanzania (TPC) na RITA ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na nguvu ya pamoja katika kufikia malengo tuliyojiwekea kuwa yanakamilika ndani ya muda uliotolewa,”alisema Badru.

Kwa mujibu wa Badru, baadhi ya changamoto zilizojitokeza wakati wa uwasilishaji wa maombi hayo HESLB ni pamoja na waombaji mikopo kutoambatisha nyaraka muhimu ikiwemo vyeti vya kuzaliwa au vya vifo vya wazazi vilivyothibitishwa na RITA au Wakala wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA), hivyo kuhitaji kukamilishwa na waombaji.

Badru anasema HESLB inaendelea na program za elimu ya uombaji mikopo kwa usahihi, ambapo tayari program hizo zimeendeshwa katika mikoa 14 ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kambi 18 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambazo zina vijana wengi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu

Naye Meneja Masoko wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Josephat Kimaro anasema ofisi yake imeendelea kushirikiana na HESLB katika kusaidia wanafunzi wahitaji kukamilisha kwa wakati fomu za maombi ya mikopo ikiwa ni pamoja na kufanya uhakiki kwa wakati wa vyeti vya kuzaliwa au vyeti vya vifo kwa waombaji waliopoteza wazazi/walezi.

Kimaro anasema hadi kufikia Agosti 30 mwaka huu, RITA ilikuwa imepokea maombi ya uhakiki wa vyeti vya vizazi 97,736, ambapo tayari imekamilisha uhakiki wa vyeti vya vizazi 83,088 na kurudisha kwa waombaji kwa ajili ya kukamilisha taratibu za ujazaji wa fomu za maombi ya mikopo kama ilivyoelekezwa katika mwongozo wa uombaji mikopo kwa mwaka 2020/2021 uliotolewa na HESLB.

‘’Bado tuma maombi 13,038 ambayo yanafanyiwa kazi, ambapo kwa karibu asilimia 70 tuliyapokea zamani na pia yana mapungufu ikiwemo kusahaulika au kutonakiliwa kwa usahihi kwa namba ya ingizo la cheti. Tayari tumewasiliana na wahusika na kuwataka kurekebisha kasoro zilizojitokeza na wao wametuma taarifa sahihi na RITA imeanza kuzirekebisha,”anasema Kimaro.

Aidha Kimaro alitaja changamoto iliyokuwa ikikabili zoezi hilo la uhakiki wa vyeti, kuwa ni pamoja na watoa huduma za mtandao kuchanganya taarifa za waombaji kutokana na kuzidiwa na idadi kubwa ya waombaji na kujikuta wakichanganya akaunti za majina ya waombaji na hivyo kuibua changamoto kwa RITA wakati wa kuchakata maombi hayo.

Kwa upande wake Valeriana Pius, mhitimu wa Kidato cha Sita (2020) katika Shule ya Wasichana Jangwani alipongeza uamuzi wa HESLB wa kuongeza muda wa kuwasilisha maombi ya mikopo kwa kuwa utatoa fursa kwa wanafunzi wengi wahitaji kukamilisha maombi yao kwa wakati kutokana na wengi wao kuchelewa kupata majibu ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa kutoka RITA.

‘’Tulianza kupata taharuki kwani wengi wetu hadi leo hii tulikuwa hatukupata majibu ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa kutoka RITA, tunaipongeza Serikali kwa uamuzi huo ambao tumeupokea kwa furaha nawashauri waombaji wenzangu tutumie vyema muda uliotolewa katika kujaza fomu zetu kwa usahihi,”alisema Valeriana.

Anaongeza kuwa uamuzi huo wa Serikali pia umegusa masilahi ya wadau wote wa elimu wakiwemo wazazi, walezi na wanafunzi hususani waliopo katika familia na kaya masikini kutokana na wengi wao kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za kusomesha watoto wao masomo ya elimu ya juu, hivyo kuwa ni mfano na kielelezo cha Serikali ya Awamu ya Tano jinsi inavyojali na kusikiliza wananchi wa hali ya chini.

Naye Bakari Hussein, mhitimu wa Kidato cha Sita (2019) katika Shule ya Sekondari Minaki mkoani Pwani anasema amepokea kwa furaha uamuzi huo wa HESLB, kwani umelenga kutoa fursa kwa wanafunzi wahitaji wanaotoka katika familia na kaya masikini kujiunga na masomo ya elimu ya juu, ambao wengi wao wameshindwa kutimiza ndoto hizo kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali hasa za kifedha.

“Nilihitimu masomo yangu ya kidato cha sita mwaka jana, hata hivyo nilipoomba mkopo nilishindwa kupata kutokana na fomu zangu kuwa na kasoro, mwaka huu nimesoma mwongozo kwa makini na kujaza fomu yangu kwa usahihi ikiwa imeambatanishwa nyaraka zote muhimu pamoja na saini kutoka mamlaka mbalimbali kama ilivyoelekezwa,’’alisema Hussein.

Kwa upande wake Irene Simon, mhitimu wa Kidato cha Sita (2020) Shule ya Wasichana Korogwe iliyopo mkoani Tanga aliipongeza HESLB kwa kushiriki katika maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyomalizika Septemba 5 mwaka huu kwani yamemwezesha kufahamu wajibu na majukumu ya taasisi hiyo katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wanaotarajia kujiunga na masomo ya elimu ya juu.

Anasema upo mkanganyiko miongoni mwa wanafunzi waombaji kuhusu sifa na vigezo vinavyotumika katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi waliosoma shule binafsi katika masomo ya kidato cha nne hadi sita, jambo ambalo HESLB inapaswa kuendelea kutoa elimu kwa wadau ikiwemo wazazi, walezi na wanafunzi ili kuweza kuondoa hofu iliyojengeka katika jamii.

“Kuna maneno yaliyoenea kuwa wanafunzi walisomeshwa na wazazi wao katika shule binafsi tangu masomo ya awali hadi kidato cha sita, hawana sifa ya kupata mkopo wa elimu ya juu, tunaiomba HESLB iendelee kutoa elimu na kufafanua kwa mapana jambo hili kwani limekuwa likileta mkanganyiko na mgawanyiko usio na msingi,”alisema Irene.

Serikali katika mwaka wa masomo 2020/2021 imetenga kiasi cha Sh bilioni 464 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 145,000 wakiwemo wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza pamoja na wanafunzi 91,000 wanaoendelea na masomo yao katika vyuo na taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini, ambapo kwa mwaka 2019/2020 jumla ya Sh bilioni 450 zilitolewa na Serikali kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi 132,292.