Home Makala Kimataifa Hii ndiyo Sudan baada ya al-Bashir

Hii ndiyo Sudan baada ya al-Bashir

1665
0
SHARE
Mwanamke Alla Salah aliyepata umaarufu katika maandamano ya kumuondoa dikteta Omar al-Bashir nchini Sudan.

MWANDISHI WETU Na MASHIRIKA

KUONDOLEWA madarakani kwa aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar al-Bashir mwaka mmoja uliopita kulipokelewa kwa matumaini makubwa ya mabadiliko ya kiutawala na kimfumo nchini Sudan.

Al-Bashir ambaye alitawala nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika kwa miongo mitatu aliondolewa rasmi madarakani Aprili 11 mwaka 2019 baada ya maandamano ya umma nchini mwake.

Kuondolewa kwa al-Bashir ambaye hata hivyo aliweza kudumu madarakani akiwa miongoni mwa watu waliokuwa wametangaziwa hati ya kukamatwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kulitokana na mambo mengi, utawala wa muda mrefu lakini zaidi wananchi kuchoshwa na kuminywa kwa demokrasia na hata vita ya ndani katika eneo la Darfur. 

Katika mwaka wa kwanza tangu kuondolewa kwake madarakani, hakuna cha kusherehekea, hali ya demokrasia bado ni kitendawili, uchumi bado uko dhaifu, hali ya kisiasa bado ni tete, huku mlipuko wa ungonjwa wa Covid-19 ukizusha mtafaruku mwingine.

Maandamano ya wananchi mwaka mmoja uliopita, ambao kwa umoja wao waliamua kukusanyika kwa maelfu kwa wiki nzima mbele ya makao makuu ya jeshi kwenye Mji Mkuu wa nchi hiyo, Khartoum yalionesha mafanikio.

Kinachokumbukwa zaidi na kuibuka kwa nyota mpya, ambapo mwanafunzi kijana mwanamke, Alla Salah alionyesha ujasiri wa aina yake, ambao hakuna aliyeutarajia.

Alla Salah kwa mara ya kwanza alionekana akiwa amesimama juu ya paa la gari akiimba nyimbo za kuhamasisha, zenye kauli mbiu za kisiasa, kisha baadaye alikuja kuwa ishara ya  vuguvugu la maandamano katika jamii ambayo kwa kiasi kikubwa inadhibitiwa na wanaume zaidi.

Kila mmoja aliingia mitaani, ikiwa ni pamoja na maprofesa,walimu na madaktari. Wasanii waliandika ujumbe na kuchora picha za uhuru katika kuta mjini Khartoum.

Kwa miezi kadhaa, nchi hiyo ilikumbwa na sintofahamu hadi hatimaye kile ambacho hakikufikirika kikatokea, kupinduliwa kwa al Bashir baada ya karibu miongo mitatu madarakani, ambaye sasa jeshi liliamua kumpumzisha.

Yalikuwa mapinduzi yaliyoelezwa na wengi kuwa ni vuguvugu la mapinduzi ya mataifa ya Kiarabu namba mbili. Raia walijisikia furaha kubwa.

Lakini mwaka mmoja baadaye, katika kusherehekea mwaka mmoja wa siku hii kubwa, hali mjini Khartoum imenyong’onyea. Kwa sababu ya janga la virusi vya corona, shule na vyuo vikuu vimefungwa. 

Sherehe za maadhimisho, kupeperusha bendera na kuimba wimbo wa Taifa ama nyimbo za mapinduzi,vimefanyika nyumbani ama katika mitandao ya kijamii.

Lakini kuna sababu nyingine ya hali hiyo ya kunyong’onyea: Baada ya miezi 12 ya uhuru wa kisiasa, Sudan haijapiga hatua ambayo ilitarajiwa baada ya kufanyika mapinduzi yaliyomwondoa al-Bashir ambaye pamoja na kupewa sifa karibu zote za udikteta, alilindwa na Umoja wa Afrika (AU) na hata viongozi wa nchi jirani walimuunga mkono.

Nchi hiyo iko imara kisiasa lakini tete. Uchumi wake umeporomoka na janga la virusi vya corona linatishia kuharibu mafanikio madogo yaliyopatikana katika miezi 12 iliyopita katika kufufua biashara na uchumi.

Sudan ni mshirika mdau muhimu katika eneo la kanda hiyo. Ni nchi ya tatu kwa ukubwa katika Bara la Afrika, pamoja na watu wake milioni 42 inaonekana kuwa ni daraja kati ya Afrika na ulimwengu wa Kiarabu. 

Vijana wa Sudan waliojiunga na maandamano ya kumuondoa Omar al-Bashir

Sudan pia ni moja kati ya nchi muhimu za kupitia watu wanaokwenda kusaka uhamiaji  kutoka Bara la Afrika.

Iwapo hali ya kisiasa na kiuchumi itakuwa bora, Sudan inaweza kutoa fursa ya uwekezaji  kutoka nje, kwa mfano katika sekta ya mafuta na kilimo.

Philipp Jahn, mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Wakfu wa Friedrich Ebert nchini Sudan anakaririwa akisema kuwa kwa hivi sasa, Sudan imelala na kutishia kuleta madhara kutokana na hali hiyo kwa eneo la kanda hiyo.

HAKUNA MABADILIKO KWA WANAWAKE

Kuibuka kwa mwanafunzi kijana mwanamke, Alla Salah kulikoongeza chachu ya maandamano yaliyomuondoa al-Bashir madarakani kuliibua hisia mpya, baada ya wanawake wengi kujitokeza katika maandamano hayo.

Lakini, kwa mwaka mmoja sasa, makundi ya wanaharakati wanawake nchini Sudan ambayo yalishirikiana na Alla Salah walitoa mchango mkubwa katika kufanikisha vuguvugu lililomuondoa madarakani Rais al-Bashir, hadi sasa wanalalamika, kwamba kwa upande wao hakuna kikubwa kilichofanyika kuwashirikisha katika uongozi wa nchi. 

Mwanaharakati aliyehusika kuanzia mwanzo wa vuguvuvu la maandamano yaliyohitimisha utawala wa miongo mitatu wa al-Bashir, Zeineb Badreddine, anakaririwa akisema hakuna kilichofanyika kutekeleza madai ya wanawake.

Karibu miaka 30, Badreddine alifukuzwa kazi chini ya al-Bashir kutokana na “dhana zake za mageuzi na haki za kiraia”, hivi sasa amerejea kwenye ufundishaji. 

Lakini licha ya kupinduliwa kwa utawala wa al-Bashir, anasema serikali mpya inakosa uwakilishi wa wanawake.

Baada ya Waziri Mkuu, Abdalla Hamdok kuunda serikali yake Septemba mwaka 2019, aliahidi kuboresha hali ya wanawake licha ya ugumu wa kiuchumi na kijamii nchini humo. Alitoa nafasi 17 za mawaziri kwa wanawake, ikiwemo wizara nyeti ya mambo ya kigeni. Mwanamke pia aliteuliwa kuongoza idara ya mahakama.

Lakini mamlaka ya juu kabisa ya nchi, Baraza la uongozi linaloundwa kwa pamoja kati ya raia na jeshi likiwa na mamlaka ya kusimamia kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia, lina wawakilishi wawili tu wa kike katika ya jumla ya wajumbe 11. 

“Iwapo wanawake wangekuwa na uwakilishi mzuri, wangekuwa na sauti zaidi za kuwatetea,” anasema Badreddine.

Chini ya utawala wa al-Bashir, sheria ya “utulivu wa kijamii” ilitumika kuwaadhibu wanawake hadharani au kuwafunga gerezani kwa uvaaji usiyo wa heshima au kunywa ulevi, vitendo vilivyotazamwa kama ukosefu wa heshima na maadili.

Serikali ya Hamdok iliondoa sheria hiyo mwaka jana, lakini sheria nyingine nyingi za kibaguzi zinaendelea kutumika. 

Badreddine analalamikia sheria ya jinai kuhusu unyanyasaji wa kingono. Majaji nchini Sudan wana mamlaka ya kuamua iwapo mwanamke amebakwa au la, jambo ambalo wakati mwingine linapelekea waathirika kushtakiwa kwa uzinzi.

Wakili na mwanaharakati wa wanawake, Inaam Atiq anakosoa sheria ya hadhi binafsi ya mwaka 1991, ambayo anasema “inasababisha mateso kwa maelfu ya wanawake kote Sudan.” Anasema sheria hiyo inaruhusu watoto wa kike wenye umri wa miaka 10 kuozeshwa kinyume na matakwa yao.

“Maandishi haya yanapaswa kurekebishwa haraka na hili linaweza kufanyika vila kugusa  kanuni za Sharia (Sheria ya Kiislamu),” anasema. 

Sheria nyingine inawapiga marufuku wanawake kusafiri nje ya nchi hadi wapate ruksa kutoka kwa msimamizi wa kiume, hatua iliyofutwa hata na Saudi Arabia. 

“Msimamizi wangu anaweza kuwa mdogo wangu wa kiume niliemlea, au hata mwanangu,” anasema Atiq.

Na hata mahakama zinazoshughulikia masuala ya hadhi binafsi hayazingatii matokeo ya vipimo vya vinasaba (DNA), yanayoruhu wanaume kushiriki katika malezi ya watoto, suala ambalo linazidisha masaibu ya wanawake, anasema.

Mwanaharakati Manal Abdelhalim anaeleza kushangazwa na sauti, zikiwemo za wanawake, wanaosema kwamba suala la (haki za wanawake) siyo la kipaumbele na kwamba linaweza kusubiri.

“Tunahitaji hatua za mara moja, na nadhani wizara ya sheria and serikali zinaelewa hali. Nina matumaini kuhusu uwezekano wa kuchukuwa hatua katika mwelekeo sahihi,” anasema.

USTAWI BADO KITENDAWILI

Katika mwaka mmoja tangu kuondoka al-Bashir, Sudan bado inatafuta ustawi, huku serikali ya mpito ikijaribu kuboresha uchumi wa taifa hilo ulioporomoka.    

Mmoja wa viongozi wa Serikali ya mpito alielezea Februari mwaka huu kwamba Serikali inataka kumaliza tofauti nyingi za mwaka 2019 baina ya jeshi na viongozi wa waandamanaji, Baraza la Kitaifa la Mpito lililoundwa baina ya raia na wanajeshi ili kufuatilia Serikali ya Mpito kwa ajili ya uchaguzi utakaorejesha madaraka ya kiraia.

Hata hivyo, Mtafiti katika Taasisi ya Rift Valley, Magdi al-Gizouli, anakaririwa akisema kuwa changamoto za kipindi hicho cha mpito cha miaka mitatu ni sawa na zile zilizochangia kuanguka kwa serikali ya al-Bashir.

Anataja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni mageuzi ya kisiasa, mzozo wa kiuchumi na kuboreshwa kwa hali ya maisha ya wananchi. 

Mzozo sugu wa kiuchumi umedhihirika nchini Sudan, ambao umesababisha nchi hiyo kutopiga hatua kwenda mbele kufuatia miongo mitatu ya uongozi wa kimabavu.

Katika nchi hiyo ambayo kuapanda kwa bei ya mkate kulisababisha maandamano yaliyoipinduwa serikali ya al-Bashir, matatizo ya kiuchumi yameuweka hatarini ustawi wa kisiasa. 

Agosti mwaka 2019, Sudan iliunda Serikali ya wasomi kufuatia makubaliano ya ugavi wa madaraka baina ya jeshi na viongozi wakuu wa upinzani.

Mtaalamu wa zamani wa kiuchumi katika umoja wa mataifa, Abdallah Hamdok aliteuliwa kuwa waziri mkuu. 

Miongoni mwa changamoto anazokumbana nazo ni kuporomoka kwa thamani ya faranga ya Sudan kwa asilimia 70, deni kubwa la taifa hilo na mazungumzo ya amani na waasi wa Darfur, magharibi mwa nchi.

Mzozo huo uliozuka mwaka 2003 baina ya jeshi na makundi ya waasi ya kikabila ulisababisha zaidi ya watu 300,000 kuuliwa na wengine milioni mbili na laki tano kuyahama makaazi yao, kwa mujibu wa umoja wa mataifa.

Mwaka 2011, Sudan ambayo ilikuwa katika hali ngumu ya kiuchumi kutokana na vikwazo vya Marekani, ilijikuta pia imegawanyika kutokana na kujitenga kwa Sudan Kusini, yenye utajiri wa mafuta na iliyojitangazia uhuru wake.

Marekani iliondoa vikwazo vyake vya kiuchumi dhidi ya Sudan mwaka 2017 baada ya miaka 20, hali hiyo iliwapa matumaini viongozi wa nchi hiyo kwa ajili ya kuweko na uwekezaji kutoka nje.

Miezi ya hivi karibuni serikali ya mpito ilikumbana pia na changamoto hasa za kiusalama kufuatia jaribio la mauwaji ya waziri mkuu mwezi uliopita.

Huko Darfur bado makabiliano ya umwagaji damu yanaendelea baina ya makundi ya kikabila licha ya serikali kuanzisha mazungumzo na makundi ya waasi ya Kordofan Kusini na Blue Nile.

KUNA LILILOFANIKIWA?

Kupinduliwa al-Bashir ndio ulikuwa mwanzo wa kipindi cha mpito kuelekea demokrasia nchini Sudan. Lakini mzozo wa kiuchumi na wadau kadhaa wa kijeshi wanatishia kuyapindua mapinduzi.

Hata hivyo makubaliano yaliyofikiwa kwaajili ya kipindi cha mpito kuelekea mfumo imara wa kidemokrasi bado ni dhaifu.

Vuguvugu la maandamano ambalo kwa sehemu kubwa lilikuwa la amani lilikuwa kilele cha muundo wa taasisi za akiraia na upinzani chini ya utawala wa al-Bashir.

Tangu alipong’olewa madarakani, hatua za kutia moyo zimechomoza.

Jonas Horner, Mtaalam wa mauala ya Sudan wa shirika la kimataifa linalochunguza mizozo, anakaririwa akisema:  “Si kitu chengine isipokuwa mageuzi ya kina katika utambulisho wa wasaudan, taasisi na jamii,” anasema.

Licha ya mauwaji yaliyofanywa na wanamgambo wa vikosi vya kuingilia kati haraka waliowaauwa watu 100 mwezi Juni mwaka jana, upande wa upinzani-muungano wa makundi yanayopigania uhuru na mageuzi yalifanikiwa kuunda baraza la raia na wanajeshi miezi miwili baadae ili kusimamia kipindi cha mpito cha miaka mitatu kabla ya uchaguzi kuitishwa.

Kuteuliwa Waziri Mkuu, Abdallah Hamdok mwezi wa Agosti, ambaye ni mtaalamu wa kiuchumi anayeheshimika pamoja pia na baraza la mawaziri wa serikali ya mpito mwezi wa Septemba 2019 ilikuwa hatua muhimu iliyoleta mataumaini hatua zaidi zitachukuliwa kuinua haali ya kiuchumi ambayo ndio chanzo cha maandamano ya mwaka jana.

Kuibadilisha sura ambaya ya Sudan kama dola lililotengwa na jamii ni jambo la maana pia katika kuipatia sudan misaada ya kiuchumi. 

Na ziara aliyoifanya Waziri Mkuu Hamdok mapema mwezi wa Desemba 2019 mjini Washingon ikapelekea kuteuliwa balozi wa Marekani mjini Khartoum kwa mara ya kwanza baada ya miaka 23.

Serikali ya Hamdok imeangaza hivi karibuni orodha ya hatua 10 muhimu ikiwa ni pamaoja na zile za kuupatia ufumbuzi mzozo wa kiuchumi, mapambano dhidi ya rudhwa na kumaliza mizizozo ya muda mrefu inayoizonga nchi hiyo. 

Wadadisi wanaona kuna matumaini ya kufikiwa amani pamoja na makaundi ya waasi.