Home Makala HISTORIA NA UKUAJI WA SIMU ZA MKONONI TANZANIA

HISTORIA NA UKUAJI WA SIMU ZA MKONONI TANZANIA

5908
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Zaidi ya watu nusu bilioni Barani Afrika kwa sasa wamejiunga na huduma ya simu za mikononi, hatua ambayo si tu inawaunganisha bali pia inatoa fursa kwao kuweza kupata huduma nyingine kama vile huduma za afya, utambuzi wa kidijitali na huduma za kifedha.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ‘Uchumi wa simu za mikononi: Afrika 2016’ iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam Julai mwaka huu, na ambayo iliitaja Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa manane Barani Afrika ambayo yana soko kubwa la simu za mikononi.

Miongoni mwa mataifa haya ni Nigeria, Misri na Ethiopia ambayo jumla yao yanachukua zaidi ya theluthi moja ya soko la aina hiyo ya mawasiliano barani Afrika.

Hivyo hakuna ubishi kwamba tasnia ya simu za mkononi (mobile phones) nchini imekuwa ikikua kwa kasi. Makampuni ya simu kama vile Vodacom, Airtel, Tigo na mengineyo yaliyoingia hivi karibuni yamo katika ushindani mkali sana katika kutafuta wateja.

Hufanya hivyo kwa njia mbali mbali kama vile kuuza simu za bei nafuu na kutoa viwango nafuu pia – mikakati ambayo imekuwa ikiifanya huduma hiyo kuenea kwa wananchi wengi wakiwemo wale wa sehemu za vijijini na wa kipato cha chini.

Kwa ujumla kuongozeka kwa idadi ya watu wanaotumia simu za mkononi Barani Afrika kumeibua matumaini makubwa katika upatikanaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani humu. Kuna baadhi ya watu wanasema simu za mkononi ni zaidi ya vifaa vya mawasiliano, bali pia ni vya kuokoa maisha na kupunguza umasikini wa Bara hili.

Ripoti moja iliyoandaliwa na taasisi ya Centre for Economic Policy Research na kampuni ya kimataifa ya Vodafone ya mwaka 2005, asilimia 97 ya Watanzania waliweza kufikiwa na huduma za simu za mkononi wakati ni asilimia 28 tu ndiyo waliweza kufikiwa na huduma za simu zile za kawaida – yaani landline.

 Hadi mwaka 1993 tasnia ya mawasiliano hapa nchini ilikuwa imekamatwa na shirika moja la umma – Kampuni ya Mawasiliano (Tanzania Telecommunications Company – TTCL). Lakini baada ya kubinafsisha sekta hii na kuenea kwa huduma ya simu za mkononi duniani, kampuni kadha za simu za mknoni zikasajiliwa, hadi sasa hivi kufikia kampuni saba zenye kutoa huduma hiyo kwa viwango na masharti mbali mbali.

Kampuni ya kwanza kabisa ilikuwa ni Mobitel iliyopewa liseni Novemba 1993 na ilikuwa inatumia mfumo wa analojia kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja waliokuwa Dar es Salaam na Zanzibar. Makao makuu na mitambo ya kampuni hiyo ilikuwa pale maeneo ya Gerezani – Mtaa wa Lugoda.

Kampuni hii ilikuwa inamilikiwa na MIC Tanzania Limited na wenye hisa walikuwa ni pamoja na kampuni ya Millicom International Cellular ya Luxembourg, Ultimate Communications Limited ya Tanzania na Tanzania Telecommunications Corporation – yaani TTCL.

Mapema mwaka 2006 kampuni ya Millicom International Cellular ya Luxembourg ilinunua hisa zote za makampuni yake yaliyo Barani Afrika ikiwemo MIC Tanzania na hivyo kubadilisha jina la utanbulisho wa kampuni hiyo maarufu ya simu za mkononi kuwa TIGO.

Hapo mwanzo – kabla ya ujio wa mfumo wa digitali (GSM) ni wachache sana waliweza kuwa na simu za aina hii kwani awali ilikuwa ni kwamba unachajiwa hata pale unapopigiwa simu. Hizo simu awali zilikuwa zinauzwa na kampuni hiyo lakini iwapo mteja atakuwa na simu yake mwenyewe basi huipeleka pale kwa ajili ya kusanidiwa (configured) na pia kulipiwa gharama za kuongea – yaani kuwekewa salio.

Mwaka uliofuata – 1994 – kampuni nyingine – TRITEL ilisajiliwa. Kampuni hii – ambayo ndiyo chimbuko la kampuni ya Airtel ya sasa – ndiyo ilikuwa ya mwanzo kabisa kuwa na mfumo wa dijitali GSM. Baadaye shughuli za kampuni hii zilichukuliwa na Celtel ya Mohamed Ibrahim – bilionea wa Sudan ambaye naye aliuza shughuli zake kwa kampuni ya Kuwait – Zain – mwaka 2007.

Mwaka 2010 kampuni ya Bharti Airtel ya India ilinunua hisa zote za kampouni ya Zain Africa kwa dola za Kimarekani 10.7 bilioni na hivyo jina la kampuni hii ya simu za mkononi hapa Tanzania likavadilishwa na kuwa Airtel.

Mwaka 1999 kampuni ya simu ya Vodacom yenye makao makuu Afrika ya Kusini nayo ilipata usajili hapa Tanzania na ni kampuni ambayo ilikua kwa haraka sana – kwa maana ya kuchota wateja wengi katika muda mfupi. Hi ilitokana na uwezo wake wa kuingia katika maeneo ya ndani ya nchi kutokana na kujengwa minara mingi ya kusambaza mawasiliano (communication towers).

Aidha kampuni hii ilikuwa ya kwanza kuingiza huduma za kutuma pesa katika simu (MPesa) huduma ambayo ilikua kwa haraka sana na kuigwa na makampuni mengine ya simu za mkononi.

Kwa ujumla ukuaji wa kasi wa huduma za simu za mkononi nchini Tanzania kulisaidiwa na kuwepo kwa huduma ndogo na duni sana za huduma za simu za kawaida yaani landlines zilizokuwa zinatolewa na TTCL.

Hii ilichangiwa na unafuu wa huduma za simu za mkononi hasa katika ile huduma ya malipo kabla (prepaid services). Aidha gharama za kuunganisha simu za mkononi (installation charges) ni rahisi sana ikilinganishwa na gharama za kuweka huduma za simu za landline.

Kama ripoti iliyotajwa hapo mbele ilivyosema, watu nusu bilioni barani Afrika au asilimia 46 kwa sasa wamejiunga na huduma ya simu za mikononi huku kukiwa na idadi kubwa ya watumiaji wa aina hiyo ya mawasiliano wanaohamia kwenye huduma ya internet inayopatikana kwenye simu zao.

Aidha ripoti ilitupia macho mchango wa sekta ya mawasiliano ya simu hizo kiuchumi, ikiwemo ajira, ufadhili kwa umma (social responsibility) pamoja na mchango wa mawasilian hayo katika ukuaji wa digitali na ushirikishwaji wa kifedha. Uwekezaji kwenye mtandao (Network) na simu za kisasa (Smartphones) kunachochea uhamiaji zaidi kwenda kwenye matumizi ya internet kupitia simu za mkononi.

Kwa ujumla watumiaji wa simu za mikononi kwa sasa wanahamia kwa kasi kwenda kwenye huduma za internet kutokana na ongezeko la mapinduzi ya internet na ongezeko la upatikanaji huduma nafuu za internet kwa kupitia msimu za kisasa yaan smartphones.

Inakadiriwa Internet ya 3G/4G ilichukua zaidi ya robo ya watumiaji wa simu mwishoni mwa mwaka 2015, na inatarajiwa kuchukua zaidi ya theluthi mbili ifikapo 2020. Hadi kufikia katikati ya mwaka 2016 kulikuwa na mitandao (networks) ya live 4G ipatayo 72 kwenye mataifa 32 kote barani Afrika, nusu yake imezinduliwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Wakati huo huo idadi ya simu za kisasa (smartphones) barani Afrika inakadiriwa kuwa zaidi ya mara tatu ya sasa, na katika miaka mitano ijayo, zinakadiriwa kuongezeka kutoka simu milioni 226 mwaka 2015 hadi kufikia milioni 720 ifikapo mwaka 2020.