Home Makala Hoja ya Kangi Lugola mufilisi

Hoja ya Kangi Lugola mufilisi

2012
0
SHARE

 

Kangi LugolaNa Malimbili Mwamlima

KWA kipindi kifupi ndani ya Taifa letu yametokea mambo mengi yanayogusa hisia za wengi. Mengi kati ya hayo yalitarajiwa kutokea kutokana na aina ya mtu ambaye ndiye kiongozi mkuu wa serikali yetu.

Tumeshuhudia shughuli za kiserikali bungeni zikifanyika huku baadhi ya wabunge wakiwa wamesusia kushiriki shughuli hizo kwa madai ya kutomtaka Naibu Spika Tulia Ackson.

Tumeshuhudia wapinzani wakikosoa na kulaani utendaji wa Rais John Magufuli na serikali yake, ikiwa ni pamoja na namna anavyobana matumizi kwa kufuta posho mbalimbali.

Lakini baada ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016 -2017, waliwasilisha mapendekezo yao juu ya bajeti kuu ya serikali na kupendekeza serikali kutoishia tu kufuta misamaha ya kodi kwa wabunge, bali ifute pia posho za vikao.

Ni jambo jema, lakini ikikumbukwe kuwa wamewahi kulaani kitendo cha Rais Magufuli kufuta posho mbalimbali kwa watendaji wa serikali, kwa kile walichodai anawarudisha matajiri kwenye umaskini badala ya kuwapeleka maskini kwenye utajiri.

Yaliyopita si ndwele, tuangalie ya leo. Tukiangalia leo ni dhahiri kuwa mapendekezo ya upinzani hasa kwa upande wa kufuta posho za wabunge ni ya kizalendo. Kwa hiyo wanapaswa kuungwa mkono.

Mbali na hayo ya upinzani, Kangi Lugola mbuge kupitia Chama Cha Mapinduzi –CCM alionyesha kukereka sana na bajeti hiyo. Inaonyesha kilichomkera hasa ni kipengele cha mpango wa kufuta misamaha ya kodi kwa wabunge.

Kipengele hicho alidai kuwa ni ishara ya wazi kwa serikali ya Dk. Magufuli kujaribu kuchezea maslahi ya wabunge.

Akichangia bajeti kuu ya serikali alidai wabunge wana mahitaji mengi, wakati fedha wanayoipata ni kidogo, kitu ambacho kinatafsiri kuwa mpango wa kufuta msamaha wa kodi kwao ambao uliwasilishwa ni kuwafanya wawe ombaomba.

Napingana na hoja ya Kangi Lugola juu ya kufutwa kwa msamaha wa kodi kwa wabunge, kwa kuwa kuna watu nchini wanapokea mishahara midogo na wanafanya kazi ngumu na kubwa ya kulitumikia taifa, lakini wanakatwa kodi na serikali.

Nchi hujengwa na wananchi kupitia michango mbalimbali ikiwemo kodi kwa kila shughuli halali inayofanywa nchini. Na mbuge akiwa mwananchi kama walivyo wananchi wengine anapaswa kuijenga nchi yake kwa kutoa kodi.

Hata hivyo tukirudi kwenye bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016-2017 kwa ujumla wake, ingawa kuna watu wanaipongeza na wengine wanaikosoa ni dhahiri kuwa inaendelea kumtambulisha Rais Magufuli kuwa ni mtu ambaye haogopi kufanya maamuzi anayoamini yanakidhi hitaji la taifa katika kuleta maendeleo.

Sina maana wanaokosoa baadhi ya mambo kwenye bajeti hiyo wanafanya makosa. Kwa kuwa hakuna jambo ambalo mwanadamu anaweza kulifanya likakosa kasoro.

Ninachowaasa Watanzania wasitumie baadhi ya kasoro ndogo ndogo wanazoziona kwenye bajeti iliyopitishwa kuiona bajeti yote ni mbaya. Kikubwa wanapaswa kuangalia ikiwa inakidhi hitaji la taifa kimaendeleo kulingana na wakati tulionao.

Kwa kuangalia hitaji la taifa kwa wakati huu hakuna mtu anayeweza kuichukia bajeti yote kwa kutumia kigezo cha serikali kuongeza kodi kwenye baadhi ya maeneo. Kwa kuwa mahitaji ya mtu au watu huongezeka kadiri siku zinavyozidi kuongezeka.

Na kama ni hivyo ni dhahiri pia mahitaji ya serikali  kiutawala na katika utoaji wa huduma kwa wananchi wake huongezeka kadiri miaka inavyozidi.

Kwa maana hiyo, si jambo la kuilaumu serikali pale inapoonekana kufuta misamaha ya kodi au kuongeza kodi ili kuendena na ongezeko la mahitaji ya kiutawala na katika utoaji wa huduma za kijamii kiufasaha. Mapato ya serikali hutegemea kodi.

Ikihitaji kuwa na kiwango kikubwa cha mapato hakuna namna zaidi kuchukua hatua kali zinazoweza kuziba mianya ya matumizi mabovu ya fedha za serikali, rushwa, kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kuongeza kodi na kutengeneza mazingira yatakayo wawezesha walipakodi kuwa na kipato kikubwa ili waweze kumudu kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yao na pia waweze kumudu gharama za maisha ambazo zina desturi ya kupanda kadiri wakati unavyokwenda.

Mambo yote hayo si rahisi Rais Magufuli ayafanye yote kupitia bajeti ya serikali yake kwa mwaka mmoja tu. Kwa kuwa ni kipindi kifupi mno tangu aingie madarakani, hasa ikizingatiwa na uharibufu mkubwa wa nchi kwenye maeneo mbalimbali ulikuwa umefanywa kwenye awamu zilizopita.

Kinachotakiwa kwenye bajeti hii ni kuonyesha namna gani Serilikali imejipanga kuijenga upya nchi yetu ambayo ilikuwa imeharibika kila kona na rushwa, ufisadi na matumizi mabovu ya fedha za serikali.

Katika hayo kupitia bajeti mwaka huu, imeonesha dhamira ya serikali ya kutaka kubomoa misingi yote mibovu na kujenga misingi mizuri itakayoondoa matumizi mabaya ya fedha za serikali, rushwa na ufisadi.

Mambo hayo ndiyo hasa yalikuwa yanakwamisha maendeleo nchini kwa kufanya fedha nyingi za walipa kodi kuishia kwenye mifuko ya wachache, badala ya kutumika kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na tayari serikali kupitia bajeti hii imeonyesha dhamira ya dhati kuyatokomeza.

Kikubwa kila mmoja wetu atambue katika maisha kuna kipindi cha mateso na kuna kipindi cha furaha. Kuna furaha inayomsababisha mtu kwenye mateso na kuna mateso yanayoweza kumpaleka mtu kwenye kipindi cha furaha.

Hatua ambazo amekuwa akizichukua Rais Magufuli ikiwa ni pamoja na bajeti kuu ya serikali yake, pengeni zinatengeneza utamaduni wa kimaisha tofauti na tuliozoea kipindi cha nyuma.

Kwa kuwa tulizoea kuishi kwa matumizi makubwa ya fedha, tukifanya kazi kivivu na kupata fedha nyingi, lakini sasa inatubidi kuishi kwa kufanya kazi kwa akiri  na bidii, tukiepuka kutumia fedha ovyo ili kuendena na falsafa ya hapa kazi tu na mpango wa serikali wa kubana matumizi ambao unaonekana kuakisi mpaka wananchi wa kawaida.

Tunapaswa kuvumilia kwa ajili ya nchi yetu. Kwa kuwa yanayofanyika inaonyesha yanalenga kuleta mabadiliko yenye tija kwa kizazi cha leo na cha kesho katika taifa letu.

Pia kwa upande wa serikali inapaswa kuhakikisha maisha tuyaoishi sasa kama watanzania yanakuwa ya mpito na si ya kudumu. Isijekubweteka kwa kuona wananchi wanaimani kubwa dhidi ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali.