Home Afrika Mashariki Hotuba ndefu majukwaani ndizo zimeifikisha nchi ilipo

Hotuba ndefu majukwaani ndizo zimeifikisha nchi ilipo

3402
0
SHARE

KUNA usemi mmoja katika lugha ya Kiiengerza usemao “Being prolific does not mean one is an accomplished person” – yaani mtu wa harakati nyingi si kwamba amekamilika. Usemi huu unaendana na ule usemao kwamba mtu wa maneno mengi mara nyingi huwa ana hulka ya kuficha mapungufu yake mengine. Na haya yote yamo katika siasa hasa pale mwanasiasa anapokuwa na harakati za kuaminika kwa wapigakura. Lakini je, baada ya kupata anachokitafuta, yaani nafasi anayoigombea, matendo yake huendana na maneno yake? Historia inatuambia kwamba kuanzia karne iliyopita wanasiasa wengi duniani ambao walikuwa wasemaji wakubwa majukwaani na baadaye kufanikiwa kuingia katika uongozi wa nchi zao, ama hushindwa kuwahudumia na kuwapatia maendeleo au huzitumbukiza nchi zao katika mfarakano mkubwa.

Mfano mmoja mkubwa ni Adolf Hitler, aliyekuwa kiongozi wa chama na Nazi cha Ujerumani katika miaka ya 1930. Hotuba zake majukwaani au Bungeni zilikuwa zinachukua masaa kadha – lakini angalia jinsi alivyoitumbukiza nchi hiyo katika vita dhidi ya nchi nyingine barani Ulaya na kuenea sehemu nyingine duniani. Mfano mwingine ni Fidel Castro, mwanamapinduzi wa Cuba katika miaka ya 1950 na aliyechukua uongozi wa nchi hiyo hadi 2008. Hotuba zake majukwaani, hasa zilizokuwa zikikandia ubeberu wa Marekani zilikuwa ndefu sana, na alipoachia madaraka miaka minane iliyopita, Cuba ilikuwa bado nyuma kimaendeleo ingawa sababu kubwa inatajwa ni vikwazo iliyowekewa na Marekani kwa miaka zaidi ya 60.

Hata hivyo wengi wanasema sababu hasa hasa ni kukumbatia kwake kwa itikadi ya Kikomunisti na sera zake za kiuchumi, sera ambazo awali zilididimiza kiuchumi nchi kama Urusi ya Kisovieti, China, Vietnam, na hadi sasa Korea ya Kaskazini. Hotuba ya Castro katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 26 September 1960 ilichukua masaa 4 na nusu, hotuba ambayo haikuisadia chochote Cuba. Na tujikite hapa kwetu yanayojiri katika harakati za kampeni za uchaguzi zinazoendelea nchini. Mgombea wa urais kupitia mwamvuli wa UKAWA, Edward Lowassa anasakamwa na wapinzani wake katika CCM (chama alichokihama baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kutafuta mgombea) kwamba hawezi kuzungumza kwa muda mrefu akiwa jukwaani, hawezi kushika maiki n.k – na yote hii wanasema inasababishwa na hali ya afya yake kuwa si nzuri.

Aidha, kwa mara kwanza baada ya kukacha midahalo katika kampeni za chaguzi mbili (2005 na 2010) safari hii CCM imejitutumua na kudai kuwa mgombea wake Dk. John Magufuli yuko tayari kwa mdahalo na wagombea wengine. Hapa anayelengwa ni Edward Lowassa na dhana ni kwamba eti Lowassa hawezi kuongea au kujibu hoja zitakazokuwa zinatolewa na waendesha mdahalo.

Inashangaza kweli kweli! CCM haikusema kwa nini walikacha midahalo safari zilizopita ingawa wengi walihisi ni kwamba mgombea wao Jakaya Kikwete asingeweza kumudu hoja za wagombea kama vile Professor Ibrahim Lipumba wa CUf na Dk. Willbrod Slaa wa Chadema hasa katika hoja za maendeleo na ufisadi nchini. Kama itakumbukwa CCM waliwakataza hata wagombea wa Ubunge na Udiwani wasishiriki midahalo. Kama safari ile ilikuwa ‘dhambi’ kushiriki midahalo kwa nini sasa iwe ‘halali?’ Au ni kwa sababu tu kwamba wamegundua kile wanachodhani ni udhaifu wa Lowassa katika suala la mdahalo, kama vile walivyodhani kulikuwa udhaifu kwa Kikwete wakati ule? Na kuhusu afya ya mgombea si mara ya kwanza suala hili kuhojiwa kwa mgombea wa urais.

Katika mchakato wa kutafuta mgombea wa urais wa CCM mwaka 2005, John Malecela aliyekuwa anawania kuteuliwa alikuwa anaelezwa na wapinzani wake kwamba alikuwa ana umri mkubwa (miaka 70 wakati ule) hivyo asingeweza kazi ya urais. Sote twakumbuka kauli yake akijibu hoja hiyo: “Kwani urais ni kubeba zege?” Sasa Lowassa azungumze kwa muda mrefu majukwaani ili iweje? Na ‘muda mrefu’ hapa ni wa kiasi gani? Nauliza hivi kwa sababu nimekuwa nazifuatilia sana hotuba zake katika kampeni na kwa muda mfupi huo huo anagusia yote yale muhimu, tena kwa muhtasari tu. Maneno mengi yana tabia ya kupambaza watu na uwezekano wa kuingiza pumba na uongo.

Hebu tazama: Kama maneno mengi katika majukwaa ya kampeni huwa yana tija, basi nchi hii isingefika hapa tulipo ambapo kila mtu anaulalamikia utawala wa CCM, malalamiko ambayo mgombea wao Dk. John Magufuli naye sasa anayatoa.

Sote tunafahamu urefu wa hotuba za Rais Jakaya Kikwete, si kwenye majukwaa ya kampeni au mikutano ya ndani. Turejee kampeni za miaka mitano iliyopita. Sidhani kama kuna mtu anakumbuka katika hotuba hizo ni ahadi ngapi Rais Kikwete alizitoa kwa wananchi wakati akiwa majukwaani.

Lakini kitu gani kimetokea? Miaka miwili iliyopta Kikwete alitumia zaidi ya saa mbili akihutubia katika ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba, hotuba ambayo ndiyo ilikuwa chanzo cha kuitupilia mbali rasimu ya Katiba iliyokuwa imetayarishwa na tume ya Jaji Joseph Warioba. Aidha, wakati anakabidhiwa ‘Katiba Pendekezwa’ katika sherehe mjini Dodoma Oktoba 9 2014 Kikwete alitumia masaa mengine kadha kuisifia ubora wake. Pamoja na masaa mengi aliyotumia katika hotuba hizo, mwisho wa siku hakuna katiba yoyote tuliyopata, na mabilioni yametumika bure katika mchakato huo, fedha za walipakodi.

Ingefaa kabla ya kuachia ngazi baadaye mwaka huu angetafuta siku na kutumia masaa mengine zaidi kwaeleza wananchi kitu gani hasa kiliusibu ‘mradi’ wake wa katiba na hasara iliyosababishia nchi kifedha. Na wakati wa sakata la kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu ilipokuwa inauathiri utawala wake, Rais Kikwete aliita kikao cha wazee (wa CCM) wa Mkoa wa Dar es Salaam ambako pia alitumia zaidi ya saa mbili kujaribu kutetea uchotwaji wa mabilioni hayo kutoka Benki Kuu na kueleza hatua nyingine za kuchukua kwa baadhi tu ya wahusika. Baada ya mkutano huo wananchi wengi hawakuwa wameridhika au kuwa na ufahamu iwapo kulikuwa na dhati yoyote au la katika vita inayosemekana inaendeshwa na utawala wake dhidi ya ufisadi na wizi wa fedha za umma.

Nachotaka kueleza ni kwamba si lazima maneno mengi katika hotuba za wanasiasa yatazaa matunda kwa wananchi. Kuna viongozi katika nchi mbalimbali ambao ni nadra sana kuzungumza lakini wananchi wanaona tu matokeo yake. Mfano ni Mfalme Qaboos Said wa nchi ya Oman, ambaye anaweza kupitisha hata miaka miwili bila ya wananchi kusikia sauti yake.

Lakini nchi hiyo imepiga maendeleo makubwa kiuchumi. Miradi mbalimbali ya miundombinu na kadhalika hutekelezwa kimya kimya na kufuanza kutumika bila hata ya mfalme huyo kuizindua na/au kuifungua. Hata Kanali Gaddafi wa Libya hakuwa mtu wa hotuba ndefu au maneno mengi, alikuwa ni mtu wa maneno machache sana lakini mtekelezaji mkubwa – tena wa kimya kimya – anawawajibisha viongozi wazembe na wala rushwa bila huruma yoyote