Home Makala JEAN PING; Shemeji, msiri  wa rais na familia anayepigwa mabomu

JEAN PING; Shemeji, msiri  wa rais na familia anayepigwa mabomu

1496
0
SHARE

LIBREVILLE, GABON

UCHAGUZI mkuu uliomalizika nchini Gabon umezua tafrani kubwa miongoni mwa wafuasi na mashabiki wa mgombea urais kwa tiketi cha chama cha upinzani, Jean Ping. Kwenye uchaguzi huo Jean Ping alikuwa anapambana na shemeji yake Ali Bongo, ambaye ushindi wake umezusha rabsha na mapambano baina ya vyombo vya dola dhidi ya waandamanaji wanaopinga ushindi wake.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa mapema Jumanne ya wiki iliyopita yanaonyesha Ali Bongo ametetea kiti cha urais kupatia ushindi wa asilimia 49.80 dhidi ya asilimia 48.23 alizopata Jean Ping.

Ushindi wa Ali Bongo unapingwa kila kona ya nchi hiyo, huku akitajwa kupata ushindi wa tofauti ya kura 5,594 na kusababisha mashaka makubwa juu ya ushindi huo huku wa watu 627, 805 ndiyo waliandikishwa kupiga kura.

Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na taswira nyingi hasi na chanya. Katika muktadha huo uchaguzi  huo uliwakutanisha watu wanaofahamiana vizuri familia zao, wagombea wanaotunziana siri zao za kifamilia na kupeana vyeo kwa minajili ya kutunzana hapo baadaye.

Ali Bongo ni mtoto wa Rais wa zamani wa Gabon, Omar Bongo ambaye ametaliwa na utata juu ya mahali alipozaliwa, ambapo wapinzani wake na baadhi ya taarifa zinaonyesha aliasiliwa na Omar Bongo kutoka kambi ya kulea watoto yatima.

Kambi mbili za utafiti zinaeleza mambo tofauti, wengine wanasema alizaliwa nchini Nigeria, huku wengine wakisema alizaliwa nchini Cameron. Kwa ajili hiyo kuna shaka juu ya kuzaliwa kwake katika familia ya Rais mstaafu Omar Bongo.

Mbali ya hilo, Ali Bongo anaye dada yake aitwaye Pascaline Bongo ambaye alikuwa mke wa Jean Ping. Kwa mantiki hiyo uchaguzi mkuu wa Gabon uliwakutanisha ‘mtu na shemeji’ yake. Tungeweza kusema pia kuwa uchaguzi huu umewakutanisha ‘wanafamilia’ ambao wanafahamiana vema kabisa.

Kwanza, familia ya Omar Bongo ilikuwa ikimtunuku vyeo Jean Ping kama mvua za masika. Taarifa rasmi za serikali ya Gabon zinaonyesha kuwa Jean Pinga alipata vyeo vya uwaziri na kubadilishwa wizara mbalimbali kabla ya ‘kukorofishana’ na familia ya Bongo mwaka 2014.

Tangu utawala wa Rais Omar Bongo wananchi wa Gabon walishuhudia Jean Ping akipanda ngazi kwa kasi na kufanikiwa kutumikia vyeo vya hali ya juu.

Jean Ping alianza kuwa waziri wa habari, mawasiliano  na utalii, baadaye akabadilishwa wizara akawa waziri wa nishati na madini, kabla ya kuwa waziri wa mambo ya fedha na waziri wa sera, mipango, mazingira na utalii.

Ping alitumikia nafasi nyingine kubwa ya waziri wa mambo ya ndani ambayo ilikuwa mwendelezo wa familia ya Rais Omar Bongo kusimika utawala na mtandao wake wa kimadaraka kutoka katika familia hiyo ili kuwa kuitawala Gabon.

Aidha, Jean Ping alikuwa mmoja watu muhimu na wasiri wakubwa wa familia ya Rais Bongo. Miongoni mwa sifa anazomwagiwa Jean ping ni kufanikisha ziara ya Rais wa taifa la China Hu Jintao, kipindi ambacho alikuwa waziri wa mambo ya nje.

Inaelezwa ni ziara hiyo ya nchini Gabon ndiyo ilibeba tangazo rasmi la serikali ya China katika sera zake za mambo ya nje. Kwenye ziara hiyo Rais mstaafu Hu Jintao alibainisha kwamba serikali ya China haitakuwa na nafasi yoyote ya kuingilia masuala ya kisiasa kwenye nchi yoyote barani Afrika badala yake itajikita kwenye ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia bila kuathiri misimamo ya mataifa husika.

Mwanadiplomasia huyo alipanda ngazi zaidi baada ya kupendekezwa na Alpha Oumar Konare kuwa mrithi wake katika nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika mwaka 2008.

Wakati wa mchakato wa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, ilishuhudiwa Libya ikimzuia mgombea wake Ali Triki asiwania nafasi hiyo ili kumwachia Jean Ping. Kwa makusudi Ali Triki alichelewesha fomu za kugombea hivyo kukosa sifa za kuingizwa kwenye kinyang’anyiro.

Hata hivyo Jean Ping mwaka 2012 hakuchaguliwa tena baada ya kushindwa mbele ya mgombea mwenzake Dk. Dlamini-Nkosozana Zuma raia wa Afrika Kusini. Tangu alipoondoka kwenye uongozi Umoja wa Afrika, Jean Pinga lijikita kwenye masuala binafsi, ambapo alianzisha Taasisi ya Ping &Ping Consulting kwa kushirikiana na mwanaye.

VITA YA MASHEMEJI

Kama tulivyoeleza huko juu kwamba uchaguzi wa Gabon uliwahusisha watu wawili wanaofahamiana vizuri. Kama wasemavyo vijana wa mjini kuwa walifahamiana ‘nje ndani’, kwa sababu ya ndoa ya Jean Ping na binti wa rais, Pascline Bongo.

Vilevile, tumeeleza huko juu kuwa kukabidhiwa vyeo vyote kulikuwa na nia ya kumweka karibu na familia ili aendeleze mamlaka yao. Na bila shaka ingetarajiwa baada ya raia wa sasa wa Gabon, Ali Bongo angekuja mtawala mpya yaani Jean Ping shemeji yake kupitia chama tawala.

Jean Ping na Pascaline Bongo wamefanikiwa kupata watoto wawili. Kwa miaka mingi Jean Ping alitajwa kama mtu muhimu na msiri wa familia ya rais. Alitajwa kuwa mwanasiasa ambaye hakuweza kufurukuta mbele ya familia ya Bongo kutokana na ndoa yake. Ushemeji huo ulichangia kupiga hatua kubwa kwa Jean Ping na kushika madaraka ya juu zaidi Afrika.

Mara baada ya kuachana na Pascaline Bongo ndipo mambo yalipomgeukia na sasa amekuwa akipigwa mabomu na vyombo vya dola vilivyopo chini ya shemeji yake Ali Bongo na mtoto wa Rais Omar Bongo.

Makao makuu ya Chama chake yamedaiwa kushambuliwa na na vyombo vya dola pamoja na kumwagia maji ya kuwasha, mabomu ya macho na gesi wafuasi wake. Jean Ping anaamini kuwa Ali Bongo amedanganya kujipatia ushindi wa kiti cha urais.

Ping aliiambia Al Jazeera kuwa anatambua kuwa yeye ni mshindi halali wa kiti cha urais mwaka huu nchini Gabon, hivyo Ali Bongo ameiba kura kujipatia ushindi.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanajiuliza, ni wapi ambapo Jean Ping atasimamia? Kifamilia tayari kunazua malumbano na ghasia katika akili zao kufuatia uhasama wa kisiasa ambazo utatawala kwenye familia hizo mbili ambazo zilishikamana kwa miaka mingi ytangu baba yake Cheng Zhiping.

Aidha, Ping na Pascaline wamezaa watoto wawili; ambao wanashuhudia uhasama mkali kutoka kwa watu waliokuwa familia moja, na sasa wamegeuka kuwa maadui.

KIPENZI CHA AFRIKA MASHARIKI

Jean Ping anakubalika pia katika mataifa mbalimbali barani Afrika kutokana na uwezo wake wa uongozi. Kwenye uchaguzi wa kuwania nafasi ya Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2008, nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ziliamua kwa kauli moja kumuunga mkono Jean Ping.

Nchi hizo ni Rwanda, Burundi, Kenya, Tanzania, na Uganda kabla ya Sudan Kusini, zote hazikutoa mgombea kutoka nchi zao ili kumpata mmoja na wala hawakupendekeza nani awakilishe ukanda wa Afrika mashariki.

Ilitafsiriwa kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika mashariki zilikubaliana na sifa za Jean Ping, ingawaje mshirika wao wa masuala ya kisiasa ndani ya Umoja wa Afrika, yaani Afrika kusini walimpinga mgombea huyo kutoka Gabon, Jean Ping.

‘MTOTO WA MUUZA KUNI NA MIKATE’

Kwa asili Jean Ping alizaliwa kwa baba yake Cheng Zhiping mzaliwa wa mji wa Wenzhou nchini China. Baba yake Jean Ping alihamia Gabon miaka 1930. Alianza kupata utajiri wake kwa kuuza mikate, samaki, na kuni. Kutokana na kuwepo uhusiano mzuri baina ya Cheng Zhiping na wenyeji walipendekeza na baadaye kumchagua kuwa mjumbe wa baraza la madiwani wa Wenzhou.