Home Makala JPM AMEFANYA UAMUZI SAHIHI KWA WAKATI MUAFAKA

JPM AMEFANYA UAMUZI SAHIHI KWA WAKATI MUAFAKA

1300
0
SHARE

NA FRANCIS GODWIN, IRINGA


SERIKALI  ya awamu ya tano ya  Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais Dk. John Magufuli  ni  serikali iliyoonyesha  historia kubwa na ya aina yake  ndani ya chama na serikali kwa  kufanya magumu mengi kwa masilahi ya watanzania na wanachama wa chama  hicho japo wachache wameumia kwa faida ya  wengi .

Ni  wazi  utendaji  kazi  wa Rais na mwenyekiti wa CCM Taifa Dk.  Magufuli  umekuwa  wa aina yake  na  wenye  kurejesha heshima kubwa kwa  watumishi  wa umma na  viongozi wa CCM na  wanachama  wake kuona  chama  ni mali yao  na  sio mali ya  wenye  pesa na viongozi  wachache  kama   ilivyokuwa  awali  kwa wenye pesa  kuwa na sauti  kuliko wenye chama  chao.

Wapo mawaziri na viongozi  waliokuwa  wakiogopwa ndani ya  chama na  serikali kwa  kusema chochote wakiamini  kuwa wataendelea kudumu  kwenye  nafasi hizo  daima na  hata  baadhi yao kuona   wao ni  bora  zaidi ya wengine  ila  leo hii chini ya  uongozi wa Rais na mwenyekiti wa CCM, Dk. Magufuli mwenye ndoto ya  kuona Tanzania  inakuwa ya watanzania na chama cha  wanachama mwelekeo wa safari umeanza kuonekana na  tunaweza sasa kukadilia masaa ya  kumaliza  safari yetu ndefu iliyoanzishwa na baba  wa Taifa  hayati  Mwalimu Julius Nyerere .

Wengi wetu  tumejikita katika maswali  magumu kuliko majibu ama  kuwa na majibu mepesi  zaidi  kuliko maswali  kwa  kuhoji safari yetu  hii kuwa kutumbuliwa kwa viongozi mbali mbali CCM na  serikali pia  wenye  vyeti  feki na watumishi  hewa  kuna kwamisha uchaguzi ndani ya CCM ama kutafanikisha safari  ya  watanzania  kuelekea  Tanzania ya uchumi wa  viwanda kwa  kila mmoja kufaidi kipande  cha mkate  katika  Taifa na sio  kila mwenye pesa kula mkate mzima wa Taifa?

Maswali  haya  na mengine  yanatokana na hali  iliyokuwepo kabla ya  Rais Magufuli  kuingia Ikulu tulishuhudia hayo kwa matajiri  kujaribu  kuiyumbisha  seriali na hata  kujimilikisha  chama huku wanyonge wakiwa watanzamaji na wapiga  debe kwa  wenye  pesa  zao  kiasi  hata  mchakato wa kumpata  mgombea Urais ndani ya  CCM ulionekana  kuwang’arisha  wenye  pesa na  wasio na pesa  walibaki kuvunjika mioyo katika  safari  hiyo baada ya kila wanapo pita  kusaka  wadhamini  walijikuta  wakikosa  ushirikiano kwa  viongozi wa CCM ama kuulizwa  wanakiasi gani  cha pesa kwa  ajili ya  kukutanishwa na wana CCM  wa kuwadhamini kwa mkoa  wa Iringa Rais Magufuli yeye hakuumiza kichwa baada ya kuona dalili  hizo  aliomba kupelekwa kata ya Magulilwa jimbo la Kalenga  kutafuta  udhamini wa wana CCM tofauti na  wenye pesa  walioandaliwa mjini Iringa .\

Ni  wazi  siku  zote  atakaye  kusaidia huwezi  kumtambua ila pindi  utakaposaidiwa wakati wa  uhitaji wako hapo  ndipo huanza mapenzi ya  kweli hakuna  haja  ya  kutafuta  majibu  kwa maswali mepesi lakini  ukweli kila mmoja anao ni nani aliyetegemea kuona watanzania tunaimba wimbo  mmoja kama  leo kwa  kuwa wamoja na kwenye mambo ya  kitaifa kama  ilivyo leo baada ya mawaziri kutumbuliwa ?

James Mgego  ni katibu  wa umoja   wa vijana wa  chama  cha mapinduzi (UVCCM)  mkoa  wa Iringa  katika tamko la vijana juu ya utendaji kazi wa Rais  Magufuli kwa kutengua  uteuzi  wa aliyekuwa  waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter   Muhongo  baada ya  ripoti ya uchunguzi wa mchanga  wa makinikia ya dhahabu anasema  kuwa uamuzi ni sahihi  na kataka  mawaziri  zaidi  watakaohusishwa na  ufisadi   kutumbuliwa.

Mgego anasema vijana  mkoani  hapa  wamepokea kwa  mikono  miwili uamuzi  huo wa  Rais wa  kumuondoa waziri Prof  Muhongo  na  kutaka  mawaziri na viongozi  wengine wa  umma kuwajibika kwa faida ya umma na si vinginevyo.

“ Umoja  wa vijana mkoa wa Iringa unaungana na kaimu katibu mkuu wa  UVCCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka  kupongeza hatua  iliyochukuliwa na Rais John Magufuli  kwa hatua  alizozichukua  za kizalendo  kwa maslahi ya watanzania  kwa  kutengua  uteuzi wa waziri wa Nishati na madini ….Rais amefanya  jambo zuri  ambalo  linapongezwa na kila mtanzania kwa faida  ya  vizazi  vilivyopo na vijavyo “

Anasema kuwa Rais Magufuli  amechukua uamuzi sahihi  wakati  sahihi  kwani nchi  ilikuwa  ikipoteza raslimali  nyingi kwa  ajili ya kuwanufaisha  wachache  kwa maslahi  yao  wenyewe na sio jamii ya kitanzania .

Hivyo alisema kuwa  umoja wa  vijana  wa CCM mkoa wa Iringa  umeona ni  vema kujitokeza  mbele ya  vyombo  vya habari  kupinga vikali  vitendo vya rushwa na ufisadi ,dhuruma na  wizi  vinavyofanywa na baadhi ya  viongozi  wasio  wazalendo na Taifa.

Mgego  anasema UVCCM mkoa wa Iringa haitasita kuwafichua  wale  wote  ambao  wanaikwamisha  serikali kwa  kufanya vitendo vya ufisadi ama  dhuruma  dhidi ya  watanzania  kwa  kutumia nafasi  zao  za  uongozi walizo  pewa .

Aidha,  alisema  kwa kuwa  ripoti ya  pili  ya kiuchunguzi  dhidi ya mchanga huo wa madini inakuja ni  vizuri  wale  wote  waliohusika kwa namna moja ama nyingine  kujitafakari na  kuchukua hatua ya  kujiuzulu nafasi  walizopewa kabla ya  kutumbuliwa na Rais.

Pia katibu  huyo  aliwataka vijana  kuendelea kujitokeza  kuchukua  fomu  za kuwania nafasi mbali mbali ndani ya chama  hicho na  kutowasikiliza  mafisadi  ambao  wapo  kuona  CCM inakwama katika  uchaguzi  huo wa ndani ya  chama.

Katibu  wa UVCCM wilaya ya Iringa mjini Alphonce Muyinga  anasema kuwa wanazo taarifa  za  wote  wanaohujumu  uchaguzi wa CCM mkoani Iringa na kuwa dawa yao inachemka  kwani  hawataona  haya  kuwashugulikia watu hao  wanaotaka kukwamisha uchaguzi  huo wa CCM.

Anasema  baadhi ya   viongozi  ambao  wametumbuliwa ndani ya chama katika wilaya ya  Iringa mjini  wamekuwa na kampeni  kubwa ya  kukwamisha zoezi la uchaguzi ndani ya  chama kwa ngazi ya mashina na matawi kwa maeneo mengine kuwanunua  wagombea  wazuri  ili wasigombee nafasi hizo  japo baada ya  kupata  taarifa   hizo vijana  wamejipanga   kuona  uchaguzi huo  unafanikiwa.

Anasema  kuwa  uchaguzi  huo umepangwa  kuanza  kati ya Tarehe 4 -10 ya mwezi huu wa sita kwa kuanza  kutoa fomu  kwa  wagombea wa kata hivyo  wanaamini vijana  wengi  wenye sifa  watajitokeza kuchukua  fomu hizo.

Mkuu wa  mkoa wa Iringa  Masenza ambae  alialikwa katika  zoezi hilo la utoaji wa tamko alipongeza  hatua  ya  vijana  hao kutambua kazi  kubwa inayofanywa na Rais Magufuli na hata  kutoa tamko  hilo la pongezi .

Masenza  anasema kuwa kumekuwepo na maombi kutoka kwa wananchi wa kawaida maeneo mbali mbali ya mkoa wa Iringa  kuomba kufanya maandamano makubwa ya  kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na maamuzi mbali mbali yenye lengo la  kuwakomboa  watanzania  na kuwa hakuna kiongozi anaye zuia  wao  kukutana kutoa pongezi  zao  kwa Rais ila si kwa  kuandamana mitaani.

“Mimi kama mkuu wa mkoa wa Iringa nawapongeza  pia wananchi wangu ambao wametambua kazi nzuri inayofanywa na Rais   wetu katika Taifa ….nawaomba sana wananchi wenye  pongezi kwa rais ruksa  kuzitoa ila utaratibu  ambao wanapaswa  kuutumia ni  kukutana katika  vikao  vya ndani kama  walivyofanya  vijana wa CCM na sio  kufanya maandamano mitaani”

Katibu  wa CCM mkoa wa Iringa,  Christopher Magala anasema uchaguzi  unaendelea  pamoja na kuwepo  kwa  changamoto mbalimbali kwa  baadhi ya   watu  kutaka kuvuruga  uchaguzi huo kwa  watu  ambao wanataka  kuvuruga  uchaguzi huo.

“Kama  inavyojulikana  kuwa  hivi karibuni  kuna  baadhi ya  viongozi na  wachama  wa  CCM walivuliwa  uongozi, kufukuzwa na baadhi yao  kusimamishwa  uongozi  na zipo  taarifa  kuwa  watu hao  wanataka  kuona  uchaguzi huo  haufanikiwi  ila  chama  kimejipanga kuwabaini  ili  kama  ni  viongozi wa CCM kuchukuliwa hatua  “

Magala  anasema  baadhi yao  wameshindwa  kukata  rufaa kueleza jinsi  wasivyo  kubaliana na adhabu  walizopewa na  badala  yake  wao wanazunguka kwa  wanachama  kutaka  kuvuruga  uchaguzi  wa Chama jambo  ambalo  halikubaliki  hata kidogo katika  mkoa wa Iringa.

Katibu  huyo  anasema kuwa  hali  ya uchukuaji wa  fomu  ndani ya  chama  linaonyesha  kuyumba zaidi  katika Wilaya ya Iringa mjini baada ya  baadhi ya maeneo  kuwa na mgombea  mmoja pekee jambo  ambalo si kawaida kutokea  kwani  miaka  mingine  wana CCM huwa  wanajitokeza kwa  wingi katika nafasi moja  ila kwa  sasa si  hivyo ila  wanaendelea  kuhamasisha  wana CCM zaidi  kujitokeza  kugombea nafasi  mbali mbali na chama  kinapenda  kuona upana wa  Demokrasia  zaidi kwa  nafasi moja  inagombewa na  wanachama  zaidi  ya  watano .

“Tunahisi  kuna hujuma  inafanywa na  hao  watu  waliotumbuliwa kutaka  kuvuruga uchaguzi wetu kwani  haiwezekani  kasi ya wanachama  kugombea nafasi  kuwa  hivi kama  ilivyo “

Akizungumzia utendaji kazi wa Rais Magufuli  alisema kuwa anafanya kazi nzuri na anatekeleza  vema  majukumu yake kwa kufanya  wananchi  wanyonge  kuona  wanadhaminiwa hivyo  hapaswi  kuyumbishwa na hao  wanaotumbuliwa na badala yake  kusonga  mbele zaidi  kuwatumikia  watanzania .

Magala  anawataka  mawaziri  na  wote  waliopewa  dhamana ya uongozi  kuacha  kufanya kazi kwa mazoea na  wale  waliotumbuliwa akiwemo Waziri Prof Muhongo  kutulia na kufanya kazi ndani ya chama na kuwatumikia  wananchi kwa nafasi  yake ya  ubunge .

“Hawa  wanautumbuliwa  wanapaswa kutulia na  kuchapa  kazi wasigeuke  kuwa maadui  wa serikali  ila  wanapaswa  kutambua  kuwa  CCM ni  chama   cha  Kidemokrasia   hivyo  suala la  kukosoana  na kusahishana ni  jambo la kawaida ndani ya  chama ……..Rais  wetu  anatekeleza ilani ya  CCM hivyo  lolote analo lifanya  chama  kipo  nyuma yake asiyumbishwe  na kelele za waliotumbuliwa “