Home Makala KENYA WANA DEMOKRASIA PANA KULIKO TANZANIA

KENYA WANA DEMOKRASIA PANA KULIKO TANZANIA

1294
0
SHARE

NA BALINAGWE MWAMBUNGU


TANZANIA ilikuwa iweke historia mwaka 2015 kama Katiba pendekezwa ingelikuwa imepita bila kuondoa mapendekezo muhimu kutoka kwa wananchi ya kupanua demokrasia kama ilivyoorodheshwa na Tume ya Jaji Warioba.

Lakini wajumbe wa Bunge la Katiba, wengi wao wakitokea Chama cha Mapinduzi (CCM), walihofia kuingiza kifungu kinachotamka:

‘Bila kuathiri masharti ya Ibara 88 na Ibara 140, mtu atakuwa na haki ya kuwa mgombea huru katika uchaguzi unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi.’
Wajumbe wa CCM ambao walikuwa wengi, wakakubaliana kuifuta Ibara hii, licha ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu kumpa ushindi Christopher Mtikila (r.i.p) aliyekata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
Mtikila alishitaki Serikali ya Tanzania mara tatu kuhusu suala la mgombea binafsi, na mara tatu Serikali ya Tanzania ilishindwa, pia imeshindwa kubadili vifungu vya Katiba ambavyo vinalalamikiwa kuwa ni kinyume kinyume cha Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki za Binadamu ambao Tanzania ilikwisha ridhia.
Mara ya mwisho jambo hili lilipokuwa mbele ya Mahakama ya Rufaa, jopo la majaji chini Jaji Mkuu, Augostino Ramadhan (wakati huo), ikakwepa kutoa tamko la wazi kwamba inaouwezo wa kuvifuta vifungu kinzani, badala yake ikatamka kuwa suala hilo lilikuwa ni la kisiasa.

Ni kwa mtizamo huo kwamba hapa Tanzania kuweka vifungu katika Katiba ambavyo vinakinzana na suala la haki za binadamu, na wakati huo huo Serikali ikiwa imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu, ni kiini macho kama vile kuendesha uchaguzi kwa gaharama kubwa halafu watawala wanayakataa matokeo yake!
Sasa wenzetu wa Kenya wametutangulia. Tungelikuwa na Katiba mpya yenye kutambua haki za raia wake kugombea nafasi yoyote bila kulazimisha kupitia chama cha siasa, tungekuwa mbela na nchi nyingine zingetuona kama kioo na mfano wa uchaguzi wa kidemokrasia.
Kenya wanaingia kwenye Uchaguzi Mkuu, Agosti 8, mwaka huu, akiwa na wagombea huru zaidi ya 1,500—wengi wao ni wale walioshinda kwenye kura za maoni, lakini vyama vyao vikawatema. Kwa jinsi ilivyokuwa mwaka 2015—jinsi CCM kilivyowatema wagombea wa nafasi ya urais bila hata kuwapa nafasi ya kujieleza—kama Katiba yetu ingelikuwa na kipengele cha mgombea huru, chama hiki kingelikuwa kimepukutika.
Kwa kuwangalia wagombea wote au mmoja mmoja, walikuwa wanamkubali Edward Lowassa ambaye alikuwa namba moja kwenye kura za maoni. Kama kungekuwapo nafasi ya mgombea binafsi, wengi wangeungana naye na wangepata ushindi mnono.

Hii ndio sababu CCM hawataki mgombe binafsi—endapo Serikali itaruhusu, mfumo wa vyama vingi utaleta maana, tofauti na ilivyo hivi sasa.
Kitu kinacho tia shaka ni kwamba mtu mmoja kusimama kwenye uchaguzi ni lazima awe na rasilimali fedha na watu. Lowassa alikuwa na rasilimali watu na alikuwa amejianda vizuri na kwa muda mrefu. Alikuwa na wafuasi Tanzania nzima wa rika zote na na angeweza kupata watu wa kusimamia kura wa kujitolea kama ilivyokuwa kwa Ross Perot wa Marekani.
Changamoto nyingine kwa wagombea binafsi ni kwamba kama mgombea hana mvuto wa kisiasa, alikuwa mwanachama wa chama cha siasa—kwa hiyo wanachama ambao anakwenda kuwaomba kura watamwona kama mslaliti.

Kwa hiyo, watamtenga na kumpiga madongo. Lakini kwa watu matajiri kama Ross Perot, ambaye hakuwa mwanachama wa chama cha siasa.

Alikuwa miongoni mwa Wamarekani waliokuwa wamechoshwa na mfumo wa kuendesha siasa. Mwanzoni mwa Februari, 1992, Perot alitangaza kwamba atagombea nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huo.

Watu wengi katika miji mbalimbali, waliokuwa wameuchoka mfumo wa kisiasa wa Marekani, waliunda mashina katika majimbo yote 50 ilia kumpa sapoti Perot.
Perot aliwagusa wananchi wengi wa kawaida kwa sera zake—kwamba angeutuliza uchumi wa Marekani ambao ulikuwa umeyumba, angebalansi bajeti ya taifa (federal budget), angetilia mkazo uchumi wa kitaifa (economic nationalism), angeongeza nguvu kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya, angejenga kumbi za elektroniki (electronic halls) katika kila jiji na kuanzisha utaratibu wa maisha ya Wamerikani wa kuamua na kuendesha mambo yao (direct demokrasy), bila kuhusisha vyama vya siasa.

Kwenye matokeo, alishika nafasi ya tatu—Mgombea wa Democratic Party, Bill Clinton alishinda uchaguzi huo.
Jaribio la Kenya la kuruhusu wagombea binafsi sio jambo dogo na ni nadra katika nchi za Kiafrika.

Hapa kwetu katika uchaguzi wa mwaka 1958, alijitokeza Herman Sarawatt (r.i.p) kule Mbulu, alisimama kama mgombea huru na akashinda. Baada ya uhuru, Tanganyika ikawa nchi ya chama kimoja—hii ilitokana na chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kupata ushindi wa kishindo (asilimia 98.15 (waliojiandikisha kupiga kura 1.8m) katika Uchaguzi Mkuu wa 1962 dhidi ya chama cha African National Congress.
Mfumo wa vyama vingi umepanua wigo wa demokrasia, lakini utakuwa bora zaidi endapo watu wasiounga mkono chama chochote, kuwa huru kugombea nafasi mbalimbali katika jamii bila kuwekewa vizuizi.
Kwa maoni ya wasomi, nafasi ya mgombea binafsi itakuwa chachu kwa vyama vya siasa ambavyo vinaatamia madaraka. Kuna watu wanaokubalika katika jamii, lakini wanaenguliwa katika siasa kwa mizengwe na hila.

CCM wana uchaguzi wa ndani mwaka huu na wanatamba kwamba wanachama ambao hawakuwaunga mkono (wasaliti), katika Uchaguzi Mkuu uliopita, wasipewe nafasi ya uongozi.

Hii ni kinyume cha haki—lakini kama ikatokea kipengele cha mgombea huru kitaingizwa katika Katiba—nina uhakika kutakuwa na kasheshe na sekeseke ya kisiasa kwa CCM nchi nzima—CCM hawatakubali kipengere hicho kiingizwe kwenye Katiba.

Faida ya mgombea binafsi italiwezesha Taifa kupata viongozi waaminifu kwa wapiga kura na wenye uwezo wa kufanya maamuzi yasiyo na shinikizo la kisiasa kama tunavyoona kwenye Bunge letu. Kukiwa na suala gumu, wanaitana kwenye ‘party caucus’ kuwekana sawa.

Mgombea huru kwa upande mwingine, mgombea huru ataua mambo ya kutafuta uongozi kwa njia ya mtandao. Wanamtandao hutegemea sana fedha na fadhila za kisiasa baada ya uchaguzi, hivyo wanakuwa wamevuruga mpangilio wa watu kutumuia uhuru wao wa kumchagua mtu wanayemtaka, wanamtandao huwanunua wapiga kura.

Nawasilisha.