Home Habari Kifo cha Nkurunziza kitabadili siasa EAC

Kifo cha Nkurunziza kitabadili siasa EAC

1206
0
SHARE

Mwandishi Wetu -Dar es salaam

NI dhahiri sasa sisasa za ukanda wa Afrika Mashariki zinakwenda kubadilika kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza (55), kwani alikuwa ni miongoni mwa wanaotajwa kuwa katikati ya mvutano na uhasama uliodumu kwa takribani miaka mitano sasa kati ya taifa lake na jirani ndugu la Rwanda.

Nkurunziza amekuwa kwenye mgogoro wa kidilpomasia na nchi ya Rwanda inayoongozwa na Rais Paul Kagame hatua hiyo kufikia viongozi hao kukwepana kwa kutoonana kwenye vikao mbalimbali vilivyowakutanisha wakuu wa nchi za Afrika Mashariki.

Mgogoro wa Nkurunziza na Kagame unaweza kufananishwa na ule wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere dhidi ya Rais wa zamani wa Uganda, Dikteta Idi Amin. Mwalimu akikataa kukaa meza moja na Idi Amin kutokana na vitendo vyake vya mauji ya raia wa Uganda. Hali hiyo ilikwamisha vikao vya Jumuiya ya kwanza ya Afika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 labla ya kuundwa tena miaka ya 1990.

Rais Nkurunziza Burundi, alifariki Jumanne wiki hii kwa mshtuko wa moyo taarifa iliyothibitishwa na Msemaji wa Serikali, Balozi Willy Nyamitwe.

Kifo cha Nkurunziza kinatokea ikiwa ni wiki mbili badaa ya kutolewa kwa taarifa kuwa mkewe, Denise alikutwa na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, huku taarifa nyingine zikieleza kuwa rais huyo pia alibainika kuwa na maambukizi hayo.

Kutokana na kifo hicho, Serikali ya Burundi imetangaza siku saba za maombolezo na ametuma salamu za ramirambi kwa familia.

Aidha, Serikali ya Burundi ilieleza kuwa kabla ya kifo chake, Nkurunziza alilazwa hospitalini Jumamosi iliyopita baada ya kueleza kujisikia vibaya na akapata mshtuko wa moyo mapema juzi asubuhi.

Wiki tatu zilizopita nchi hiyo ilifanya uchaguzi wake mkuu huku mikutano ya kisiasa ikishuhudia maelfu ya watu wakijitokeza bila kuzingatia maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kujikinga.

Awali, marehemu Rais Nkurunziza alidai kuwa nchi yake haina haja ya kuchukua hatua zozote za kuzuia mikusanyiko au kuchukua tahadhari kwa kuwa inalindwa na Mungu, akitupilia mbali madai ya hatari ya virusi vya corona.

Mwezi Aprili, pia Serikali ya Burundi ilitangaza kuwafukuza nchini mwake wataalamu sita wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) kwa kile kinachodaiwa kuwa utawala wa Bujumbura haukupenda tathmini zilizofanywa na wataalamu hao kuhusu nchi hiyo kujiandaa kukabili janga la corona.

Nkurunziza anafariki dunia wiki mbili baada ya uchaguzi ambao ulikuwa ukimaliza madaraka yake ya urais, lakini ukitoa nafasi ya yeye kupewa nafasi ya “Kiongozi Mkuu” wa Burundi atakapoondoka madarakani.

Bunge la Burundi lilipigia kura muswada wa sheria wa kumpatia Nkurunziza cheo hicho na kumpatia mabilioni ya faranga za Burundi ($530,000) wakati atakapoondoka madarakani.

Hatua hiyo ilikosolewa na wapinzani wake wa kisiasa na hata kutajwa kumwita kama kiongozi mlafi aliyetaka kujilimbikizia mali hata pale alipotaka kuondoka madarakani huku fumbo likibaki kama sheria hiyo itatekelezwa ama laa.

Muswada huo wa sheria pia ulikuwa umwezeshe kulipwa mshahara katika kipindi chote cha maisha yake, kupata marupurupu yote anayopewa makamu wa rais aliyeko mamlakani na kupewa nyumba ya kifahari, anayopewa kila rais wa Burundi aliyechaguliwa kidemokrasia.

MKEWE NA MATIBABU

Kwa karibu wiki mbili zilizopita, Mei 29, 2020 taarifa zilidai kuwa mke za Rais Nkurunziza, Denise alithibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona na kukimbizwa kwa matibabu nchini Kenya.

Hata hivyo, taarifa za vyanzo vya ndani ya Serikali ya Burundi vilikanusha kuwa anasumbuliwa na maradhi ya corona.

Mei 30, 2020 Serikali ilithibitisha kuwa Denise yuko nchini Kenya, akiendelea kupatiwa matibabu huku vyanzo nchini Kenya vikithibitisha kuwa ni ugonjwa wa Covid-19.

Shirika la habari la Ufaransa, AFP, lilimnukuu ofisa mmoja kwenye uwanja wa Melchior nchini Burundi, akithibitisha kuwa Denise alisafirishwa kwenda nchini Kenya na ndege ya shirika la kiafya Amref.

Vyanzo katika Wizara ya Afya nchini Kenya, ambavyo havikutaka majina yao kutajwa vimethibitiha kuwa mke wa Rais Nkurunziza, yuko nchini humo akisumbuliwa na maradhi ya kupumua ambayo yanahusishwa moja kwa moja na ugonjwa wa Covid-19.

Kuumwa kwa mke wa Nkurunziza kunathibitisha hatari ya virusi hivyo nchini Burundi, taifa ambalo ni miongoni mwa nchi ambazo haijazingatia maelekezo ya WHO na wataalam wengine wa afya juu ya hatua za kuzingatia kujiepusha na maambukizi ya corona.

UHUSIANO NA RWANDA

Juni 8, mwaka huu ikiwa ni siku moja baada ya Serikali ya Rwanda kutuma risala ya pongezi kwa Rais Mteule wa Burundi, Meja Jenerali Everiste Ndayishimiye mjadala umeibuka ikiwa nchi hiyo ina nia ya kukomesha mzozo kati yake na Burundi.

Hiyo ni baada ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Rwanda, kutumia fursa hiyo kusema kwamba nchi hiyo iko tayari kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo ndugu ambazo zinakaliwa na makabila mawili makubwa ya Wahutu na Watutsi.

Ingawa nchi hizo zinafanana kwa kiwango hicho, zikiwa na utamaduni na lugha moja, lakini uhusiano wao ulikuwa mbaya tangu mwaka 2015 kufuatia uchaguzi wenye utata wa rais Pierre Nkurunziza anayeondoka madarakani alipobadili katiba na kujipa muhula wa tatu wa kuwania urais.

Tangu wakati huo nchi hizo mbili zimekuwa zikishutumiana kuunga mkono makundi ya waasi kutoka kila upande.

Risala ya pongezi ya Rwanda kwa Rais Mteule Jenerali Ndayishimiye, iliyozua hisia mbali mbali kwenye mitandao ya kijamii, raia wa Burundi na raia wa Rwanda wakichangia maoni huku baadhi yao wakipongeza hatua hiyo.

Kuna waliohoji kwa nini siyo Rais wa Rwanda Paul Kagame aliyempongeza rais mteule wa Burundi kama ilivyotokea kwa marais wengine wa mataifa ya Kenya, Tanzania na Uganda na badala yake risala hiyo kuandikwa na wizara ya mambo ya nchi za nje.

Kulingana na risala hiyo,Wizara ya Mambo ya nchi za nje ya Rwanda imesema inatumia fursa hiyo kuikaribisha Burundi kusema kwamba Rwanda iko tayari kurejesha mahusiano yaliyotajwa kuwa ya kihistoria baina yao.

Rwanda na Burundi zilikuwa nchi moja iliyofahamika kama Rwanda-Urundi, mji mkuu ukiwa Usumbura, Bujumbura ya sasa, chini ya ukoloni wa Ubelgiji, zikiwa na kabila zinazofanana,utamaduni na lugha moja.

Mzozo wa Rwanda na Burundi uliolipuka mwaka 2015 umesababisha maisha magumu kwa raia wake, lakini pia ukiathiri shughuli za Jumuiya ya AfrikaMashariki kutokana na wakuu wa nchi hizo kugeuka kuwa uadui wa kama paka na mbwa.

Tangu wakati huo nchi hizozimekuwa zikishutumiana kuwa kila mmoja anaunga mkono makundi ya waasi. Burundi iliihusisha Rwanda na jaribio lililofeli la kutaka kumpindua Rais Pierre Nkurunziza mara tu baada ya uchaguzi huo ambapo Nkurunziza aliitangaza Rwanda kuwa adui mkubwa wa Burundi.

Rwanda kwa upande wake imekuwa ikiishutumu Burundi kuunga mkono makundi ya waasi iliyodai kufanya mashambulizi yaliyotikisa maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Burundi miaka miwili iliyopita.

MARAIS WAMLILIA

Kutokana na kifo hicho marais wa nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, walituma salamu za pole kwa Serikali ya Burundi, akiwamo Rais Paul Kigame wa Rwanda, John Magufuli wa Tanzania, Yoweri Museven wa Uganda ambapo kila mmoja alimueleza kiongozi huyo kwa namna yake alivyomfahamu.

HISTORIA YAKE

Nkurunziza aliyezaliwa mwaka 1964 mjini Bujumbura katika familia ya kabila la Wahutu aliwahi kuwa mwalimu wa Chuo Kikuu cha Burundi wakati vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyoanza baada ya kuuawa kwa rais wa kwanza aliyechaguliwa kutoka jamii ya Wahutu, Melchior Ndadaye mwaka 1993.

Baada ya shambulio la jeshi dhidi ya Wahutu kwenye chuo kikuu, alijiunga na kundi la CNDD-FDD mwaka 1995 akawa askari na kupanda ngazi hadi kuwa makamu wa mwenyekiti wa CNDD-FDD mnamo mwaka 1998, halafu mwenyekiti mwaka 2001.

Baada ya mapatano ya amani ya mwaka 2003 aliendelea kuwa waziri wa utawala katika Serikali ya mpito ya Rais Domitien Ndayizeye.

Baada ya ushindi wa CNDD-FDD katika uchaguzi wa 2005 alichaguliwa na bunge kuwa rais. Alichaguliwa tena kwa kura ya wananchi wote mwaka 2010.

Mwaka 2015 alitangaza nia ya kugombea urais tena. Hiyo ilisababisha ghasia kwa sababu wapinzani walidai kufuatana na katiba ya nchi anastahili kuongoza vipindi viwili tu.

Mwenyewe pamoja na chama chake alidai kwamba mara ya kwanza alichaguliwa na Bunge tu na kikatiba anastahili kuchaguliwa mara mbili na wananchi wote.

Zaidi ya miezi miwili kulitokea maandamano ya kumpinga Nkurunziza ambayo yaliandamana na ghasia na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 100.

Mei 13, 2015 jaribio la mapinduzi dhidi ya Nkurunziza lilitokea akiwa nje ya nchi hiyo.

Mkuu wa mapinduzi hayo, Jenerali Godefroid Niyombare alidai kwamba amemng’oa madarakani Nkurunziza, lakini wanajeshi watiifu kwa Nkurunziza walikanusha madai hayo.

Julai 24, 2015 Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Nkurunziza mshindi wa uchaguzi kwa asilimia 69.41 ya kura. Agathon Rwasa alishika nafasi ya pili kwa asilimia 18.99 ingawa alikuwa amehimiza wananchi wasipige kura.

MTAWALA WA KIIMLA

Yeye na mke wake Denise waliwahi kuripotiwa kuwaosha miguu watu waliokuwepo kwenye mkusanyiko.

Siyo tu watu ambao Nkurunziza alikua na imani kuwa wanamuamini. Bali uongozi wake pia aliamini ni kutoka kwa Mungu.

“Anaamini kuwa ni kiongozi kwa matakwa ya Mungu, na hivyo anashughulika na serikali yake katika matakwa hayo,” alisema msemaji wake Willy Nyamitwe.

Wakosoaji wake ikiwamo wapinzani kutoka vyama karibu 40 na watetezi wa haki za binadamu, wana mtazamo tofauti dhidi yake.

Wanamtuhumu kuwa dikteta na ambaye hataki kuachia madaraka kutokana na kuongoza kwake kwa mihula mitatu.

Mbali na kudiwa kuawa kwa watu zaidi ya 100 katika maandamano ya kumpinga kugombea muhula wa tatu. Wengine zaidi ya 100,000 walikimbia makazi yao kwenda nchi jirani kuhofia usalama wao kuwa nchi hiyo ingetumbukia kwenye mzozo kwa mara nyingine

MAPINDUZI

Mkuu wa zamani wa majeshi Godefroid Niyombare aliongoza mpango huo wa kutaka kumuondoa madarakani mwaka 2015. Baada ya kushindwa kwa mpango huo wapinzani wakadai kuwa uchaguzi wa mwaka huo haukua wa uhuru wala haki.

Mkuu wa kitengo cha Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa, Zeid Raad al-Hussein, alitoa wasiwasi wake kuhusu kundi moja la vijana la Imbonerakure washirika wa Nkurunziza.