Home Makala Nisamehe Kikwete

Nisamehe Kikwete

2261
0
SHARE

Rais wa Awamu ya Nne Jakaya KikweteNa Richard Hizza

KAKA Jakaya Mrisho Kikwete, Shikamoo! Najua siku zote wewe ni mwepesi kusamehe. Nakumbuka siku ile pale Mbagala Juni 2006 uliposema mimi ni ndugu yako lakini nilikuwa nakusema maneno mabaya lakini umenisamehe.

Siku ile niliyojiunga na chama chako kwa mara nyingine tena kaka nakuomba unisamehe kwa kukiacha chama chako ukiwa bado umeshikilia usukani wa chama na ukifanya kila hila kuhakikisha hakifii mikononi mwako.

Leo ninastahili kukuomba msamaha kwa kutopima maneno yako vizuri, hasa lile ulilotuambia Watanzania wote siku moja kwamba tutakusema na kukulaumu sana lakini tutakuja kukukumbuka ukishaondoka.

Leo ndiyo nakumbuka vizuri yale maneno yako na yale uliyoyasema ulipofika bungeni kwa mara ya kwanza ukiwa Rais kuzindua Bunge jipya “I might be wearing a smiling face but very serious on issues”.

Kwa kweli kaka tangu Januari mwaka huu nilikuwa na hisia kwamba hautapita muda mrefu sana kabla hatujaanza kukukumbuka. Januari ndiyo nilianza kuhisi demokrasia yetu changa ipo hatarini.

Nikaandika makala nyingi katika magazeti kutahadharisha, baada ya kuona baadhi ya misingi tuliyojiwekea ikianza kuvunjwa. Mifano chaguzi za umeya Dar es salaam, Tanga, Kilombero, kupigwa kwa wabunge na kutolewa kwa nguvu bungeni, bila kutaja sakata la Zanzibar nisije nikakuchokoza tena maana inasemekana ulihusika husika.

Kaka hali ya demokrasia yetu sasa imekuwa ya shaka kubwa, wabunge waliochaguliwa na wananchi leo wanafukuzwa bungeni na wenzao wa chama walichoshindana nacho katika uchaguzi kupitia kamati inayoongozwa na mjumbe wa NEC kutoka Newala, George Mkuchika.

Wabunge 114 wa upinzani wapo hatarini kutupwa nje ya Bunge kila vikao vinavyoendelea wengi tayari wapo nje. Joseph Mbilinyi Mbunge wa Mbeya anafuata na hadi Bunge litakapoahirishwa hatujui idadi hiyo itafikia wapi.

Hawana tena uhuru wa kuchangia kama zamani, wanapigwa ndani ya Bunge na kutolewa kama majambazi, wakiwa nje nako hawapo salama, wakiitisha mikutano ya hadhara ya vyama vyao wanazuiwa, na kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi nchini hata makongamano na vikao vya ndani ya vyama vya upinzani tunasikia vinatakiwa kuombewa vibali polisi.

Serikali yetu inaviogopa hata vyama vyenye uungwaji mkono wa chini ya asilimia moja kitaifa (0.68%), itafikia sehemu hata hotuba za wanasiasa wa upinzani zitatakiwa zikaandikwe polisi, ili zisiwe tofauti na mawazo ya watawala na kuitwa za uchochezi.

Mifano mingine ni yaliyotokea Zanzibar hivi karibuni ya kusambaratisha vikao vya ndani vya CUF, msafara wa Maalim Seif kuzuiwa njiani asiende kuzungumza na wanachama wake, kuzuia viongozi wa Chadema kuingia katika ofisi yao pale Shinyanga, kukamatwa kwa viongozi wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe huko Mwanza na msukosuko alioupata Zitto Kabwe baada ya kuhutubia wananchi hapa kwetu Mbagala.

Bila kusahau kesi zilizofunguliwa mahakamani dhidi ya wabunge wa Chadema akiwemo Halima Mdee ni mifano michache inayoonyesha hali ya kisiasa si shwari tena hapa nchini.

Hivi sasa kila mwanasiasa wa upinzani hana uhakika kesho kitamkuta nini, imefikia mahali kila kibaya kitakachomtokea mwanasiasa hivi sasa kuweza kuhusishwa na chama chako au serikali jambo ambalo si afya sana kwa usalama wa nchi.

Inashangaza kuona wakati uliopita wa awamu yako wapinzani walizunguka nchi nzima kuelezea mapungufu ya bajeti, mikataba mibovu ya madini, IPTL, Net group solutions, wizi wa EPA na mengine mengi hawakuzuiwa wala kukamatwa na polisi na kuitwa wachochezi.

Chama kiliunda kikosi chake kikiongozwa na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana (usisahau nilikuwemo) kuisaidia serikali katika kile ambacho Mheshimiwa Makamba alikiita kikosi cha kujibu mapigo, serikali kwa upande wake iliteua mawaziri wenye weledi katika kujieleza kama mzee Stephen Wasira kuungana na timu hiyo kutoa ufafanuzi wa kutosha na kuitetea serikali kwa makosa ambayo mengi yalifanywa na awamu ya tatu ikiaminika kwamba zote zilikuwa za CCM.

Sitaki kutaja majina ya mawaziri wote lakini nakumbuka binafsi nilifuatana na waziri mmoja katika mikoa mitatu katika utekelezaji wa mpango huo na mambo yakaisha kwa usalama mwaka 2010 ukashinda tena.

Sasa huu wasiwasi uliopo katika awamu hii ambayo kila siku tunaambiwa ni safi na makini kuliko yako sijui unatokea wapi? Msemaji wa CCM, Ole Sendeka alishatangaza kuwa watajibu mapigo kwa kuzunguka kote watakapopita wapinzani sijui kwanini vyama haviachiwi vitimize wajibu wake!

Hivi hizo wiki mbili za mikutano ya Chadema zinawezaje kusambaratisha nchi wakati mwaka jana walifanya kampeni kubwa ya miezi miwili na hakukutokea tatizo lolote? Naona nisiendelee kutaja mengi lakini ujue nimeshtuka sana na mambo yanavyokwenda ndiyo maana nimeamka usiku huu mkubwa kuandika waraka huu wa kukuomba msamaha ili kwa kimbele mbele changu unachokijua ukisikia nipo ndani usisite kumtuma mtu kuniletea dawa zangu za pumu na chakula.

Ikitokea nimekufa kwa sababu za kisiasa usikose walau kuja kunirushia mchanga wa mwisho maana mimi kama unijuavyo kunyamaza siwezi labda nikose nafasi . Kaka nakuomba sana unisamehe kwa yote niliyokukosea, najua chama chako kimezidiwa nguvu.

Si wewe wala chama kinachoweza kuzuia hali hii isiendelee bali kukuomba unisamehe mimi na Watanzania wenzangu tulioshindwa kuelewa uliposema ukiondoka tutakukumbuka, kwa kweli tunakukumbuka na bado tutakukumbuka zaidi na zaidi.

Mimi nimeamua binafsi kusamehe yale machache ambayo binafsi nilikuwa na kinyongo na wewe, uchaguzi wa Zanzibar ulivyowaacha wapinzani na TCD kwenye mataa katika mchakato wa katiba mpya, sheria ya makosa ya mtandaoni na mwisho kumtosa Edward Lowasa katika uteuzi wa kugombea urais.

Ningekuwa na uwezo ningesema umesamehewa dhambi zako zote, lakini sina ila naamini maombi yangu katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu yatafika na mola wetu atakusamehe, kaka usisikie cha moto tunakiona ni afadhali upandishiwe bei ya sukari lakini usinyimwe haki na uhuru wa kujieleza na kupata habari.

Inauma kweli kweli, leo bunge halitangazwi, wabunge bungeni wamefukuzwa, mikutano marufuku, mkutano ukifanyika unayosema yanaenda kujadiliwa na kuitwa ya uchochezi hata kama hakuna madhara yaliyo jitokeza baada ya mkutano huo,kaka tukasemee wapi?

Ukiandika mtandaoni wasiyoyapenda faini milioni 7 au jela miaka mitatu, safari ni ndefu lakini tutafika tu. Leo ukichukua picha za mikongoto ya polisi kwa wanamageuzi au picha ya mbunge wa kilombero Peter Lijuakali inayonikumbusha sana zile za Patrice Lumumba alipokuwa chini ya ulinzi wa wauaji wake na si rahisi kuzitofautisha na zile za makaburu enzi za ubaguzi wa rangi.

Mwisho nisalimie shemeji na watoto, kaka shikamoo sana, naamini utanisamehe, ni hayo tu kwa leo sina zaidi. Ni mimi nduguyo Richard Tambwe Hiza.