Home Uchambuzi Kuchagua, kuchaguliwa ni haki ya binadamu

Kuchagua, kuchaguliwa ni haki ya binadamu

2521
0
SHARE
Wananchi wakiwa katika foleni ya kupiga kura


Na ANNA HENGA


MWAKA huu na mwaka ujao Tanzania itakuwa katika chaguzi. Uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za Mitaa, ilhali uchaguzi wa mwaka 2020 ni Uchaguzi Mkuu.

Mtu anaweza kujiuliza tofauti ya chaguzi hizi mbili ni nini, na kwanini zifanyike miaka miwili tofauti?

Mpiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni mtu yeyote ambaye ni raia wa Tanzania aliyefikisha umri wa miaka 18 na kuendelea, anaweza kuwa mkazi anayeishi katika kaya au taasisi iliyopo katika eneo la mtaa kwa upande wa mijini au anaishi kwenye eneo la kijiji au kitongoji na ambaye ama ana kaya au anaishi katika kaya au taasisi iliyopo katika eneo la kijiji au kitongoji.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni wa kuwachagua watu wafuatao; Mwenyekiti na wajumbe sita wa Serikali ya Mtaa ambapo nafasi ipo kwa ajili ya viti maalumu vya wanawake.

Katika vijiji, nafasi zitakazogombewa ni ya Mwenyekiti wa kijiji, wenyeviti wa vitongoji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na wajumbe wa viti maalumu wanawake.

Kati ya wajumbe watakaochaguliwa, idadi ya wanawake itakuwa nusu au zaidi ya wajumbe wote na wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji hawatapungua 15 na hawatazidi 25.

Maelezo hapo juu ni kwa mujibu wa kanuni zilizotumika katika uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa mwaka 2014. Hivi karibuni wizara ya TAMISEMI ilitangaza kuwa inazipitia upya kanuni hizo kwa ajili ya maboresho Zaidi.

Uchaguzi Mkuu ni wa kumchagua Rais, wabunge na madiwani. Kwa Tanzania Zanzibar sheria iko tofauti kidogo na Tanzania bara.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

Haki hii iko kwenye Hati ya Haki za Binadamu, kwa hiyo ni haki inayoweza kudaiwa mahakamani endapo itakiukwa.

Haki hii haibagui, jinsi, hali wala kipato cha mtu yeyote. Swali linalokuja ni je kwa nini sio wananchi wote hujitokeza kuchagua viongozi wao? Na kwa nini wakati mwingine wananchi hawajitokezi kugombea ili wachaguliwe?

Tumeshuhudia wakati mwingi mgombea akipita bila kupingwa, Je kunakuwa hakuna kabisa mtu wa kugombea? Je, wananchi hawaoni sababu ya kugombea ili wachaguliwe?

Suala la chaguzi ni suala la hiyari na kidemokrasia. Demokrasia kwa tafsiri nyepesi ni utawala wa watu kwa ajili ya watu na unaotokana na watu. Inapotokea watu hawa hawajitokezi kuchagua ama kuchaguliwa, inatia shaka kama kweli dhana hii ya demokrasia inachukuliwa kama inavyostahili kuchukuliwa.

Dhana ya demokrasia miaka ya zamani ilikuwa ni uwakilishi wa moja kwa moja. Kila mtu anajiwakilisha mwenyewe. Hii ilikuwa ikifanyika huko Athene, Ugiriki.

Lakini baadae dhana hii ilionekana haifai kwa sababu ya wingi wa watu na pia mtawanyiko wa kijiografia. Kwa mfano Watanzania hatuwezi wote tukaenda bungeni Dodoma kujiwakilisha, ni lazima tuteue wachache wetu watuwakilishe.

Hatuwezi wote tukawa viongozi wa kijiji na kujiwakilisha katika mikutano ya mabaraza ya vijiji au mitaa, bali tunawakilishwa na wachache wetu.

Tunapokuwa hatujashiriki ama kuchagua ama kugombea kuchaguliwa, tunakuwa tumekiuka haki yetu wenyewe ya kidemokrasia na haki ya binadamu ya uwakilishi.

Tanzania tunazo sheria nyingi zinazohusiana na haki hii ukiacha Katiba. Kuna sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa, sheria ya uchaguzi, sheria ya gharama za vyama vya siasa, sheria ya vyama vya siasa na kadhalika.

Zote hizi ni kwa ajili ya kutuwezesha kuchagua na kuchaguliwa. Lakini pia zinawezesha taasisi zinazosimamia chaguzi kuwekewa utaratibu mzuri wa namna ya kusimamia haki hii ya kuchagua na kuchaguliwa.

Pamoja na Katiba, sheria na sera zote hizo, Je kwa nini ni hatujitoi kuchagua? Shime tujitoe kwani haki hii ni haki kama ilivyo haki ya kuishi, haki ya kufanya kazi na haki ya kuheshimiwa utu wa mtu binafsi.

Haki hii pia kwenye makundi maalum kama kundi la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inahitaji kuwekewa mkazo wa kutosha.

Nikiwa kama mwezeshaji wa makundi haya nimeshuhudia katika chaguzi nyingi yakibaki nyuma sana katika kufaidi haki hii. Nimekuta mara nyingi wanawake wakiwa ndio waimbaji kwenye kampeni lakini hawaendi kupiga wala hawapo kwenye wanaopigiwa kura.

Wakati mwingine kwa kuzuiwa na mfumo dume ambapo unakuta mume au baba anazuia mkewe au bintiye asiende kupiga kura; wakati mwingine kutohimizwa na kufahamu umuhimu wa haki hii.

Hali hii pia ipo kwa vijana na watu wenye ulemavu ambao pia makundi haya ni muhimu mno katika jamii yetu hususani Tanzania.

Sababu zimekuwa zikitolewa kuwa makundi haya yanakumbana na changamoto nyingi sana ikiwamo kuwa nyuma kiuchumi kutokana na mila na desturi zilizokuwa zimewanyima fursa miaka mingi.

Hata hivyo bado ni makundi muhimu sana kushiriki katika haki hii ya kuchagua na kuchaguliwa.

Mkataba wa Maendeleo na Jinsia wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Ibara ya 12, unasisitiza kuwapo kwa asilimia hamsini kwa hamsini katika ngazi za maamuzi.

Hii inaonesha jinsi ilivyo muhimu sana hata kikanda na kimataifa.

Shime Watanzania wenzangu tutakapotangaziwa kuanza kwa michakato yote ya chaguzi tujitoe kuchagua na kuchaguliwa, maana ni HAKI YA MSINGI sana.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)