Home Makala Kimataifa KUMBUKIZI MIAKA 26 MAUAJI YA KIMBARI Maendeleo, amani ndio kipaumbele Rwanda

KUMBUKIZI MIAKA 26 MAUAJI YA KIMBARI Maendeleo, amani ndio kipaumbele Rwanda

1233
0
SHARE

Na ALOYCE NDELEIO 

WIKI ya kumbukizi ya mauaji ya kimbari Rwanda ilianza Aprili 7 mwaka huu, yaliyotokea miaka 26 iliyopita mwaka 1994 na ambayo lengo lake yalionesha dhahiri kutaka kuangamiza kabila la Watutsi. 

Licha ya kumbukizi ya mwaka huu kutofanyika kwa maadhimisho katika mikusanyiko kutokana na janga la ugonjwa wa Corona (COVID -19) bado hisia, tafakari, na mitazamo mingi ipo kwamba ni tukio lisilo la kawaida kutokana na madhila yake.

Mauaji hayo ya kimbari yaliyodumu kwa siku 100 yaliishtua na kuishangaza dunia kwani watu 800,000 walipoteza maisha na  kumbukizi la maafa hayo, unaonesha  uwepo wa kovu la jeraha lililoikumba jamii hiyo.   

Dhihirisho lililopo ni kwamba waliouawa wengi walikuwa ni raia wasio na hatia ambao hawakuwa na silaha wala namna ya  kujilinda na wengi walikuwa ni wanawake na watoto, ambao waliteswa, walibakwa na hata kuuawa.  

Wanamgambo wa Kihutu waliwalazimisha Wahutu wenzao kushiriki mauaji ya kuwaangamiza watu ambao katika kampeni zao waliwaita ‘mende’ au ‘nyoka’. 

Vyombo vya habari hususan Radio-Television Libres des Mille Collines (RTLMC) na vilitumika kusambaza habari za tukio  hilo mithili ya kwamba ni jambo la utani. 

Majonzi yaliyotokana na janga hilo si tu  kwamba hayafutiki baliukweli unabaki kuwa hadi siku ya 100 ya tukio hilo la kutisha na  kusikitisha, takriban robo tatu ya wakazi milioni saba ama waliuawa au kukimbilia uhamishoni katika nchi za Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Uganda na Burundi.

Asilimia 15 ya raia wa Rwanda waliuawa, milioni mbili waliyakimbia makazi yao na wengine milioni mbili waliyanusuru maisha kwa kukimbilia nje ya nchi na mandhari ya kutisha yalibakia kuitawala nchi hiyo.  

Rwanda hivi sasa inaelezwa kuwa na mabadiliko au mageuzi makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii na imani imerejea.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha CNN Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame alisema mshikamano uliopo nchini humo unatokana na sera sahihi za upatanishi na maridhiano ambazo zimekuwa  zinaendeshwa nchini humo. 

Mambo mengine yanayoipa Rwanda heshima ni pamoja na kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasia mwaka 2003, uliowezesha kupatikana kwa wabunge na rais ambapo Kagame alishinda na kuwezesha kuwapo kwa uwakilishi wa makundi yote ya jamii kwenye bunge la  nchi hiyo. 

Kwenye sekta ya elimu, serikali ya Kagame imeingia kwenye mkakati wa kupanua elimu ya msingi kwa kufuta karo ya shule za sekondari licha ya kwamba idadi yao ni ndogo kutokana na wengi kukumbwa na mauaji na asilimia 80 ya watoto wenye umri wa kuanza shule wameandikishwa.  

Pamoja na hali hiyo, serikali hiyo imezingatia uwiano wa jinsia katika uandikishaji wa watoto shuleni licha ya kwamba imekuwa ni kawaida wavulana  kuwa wengi wenye elimu ya sekondari lakini hatua kwa hatua uwiano kamili  utakuwepo kwenye elimu ya sekondari. 

Katika dhana ya uwakilishi bungeni uwiano wa jinsia umepewa kipaumbele na bunge la nchi hiyo lina wabunge wanawake 39 kati ya wabunge wote 80, idadi ambayo hakuna nchi yoyote duniani yenye uwiano wa kijinsia bungeni unafikia huu wa Rwanda.

Biashara ya nje nayo imepanuka na kwani zao la kahawa ambalo ni zao kuu la biashara, limeanza kupata mauzo mazuri kwenye soko la dunia, japo bei katika soko hilo ni ya chini ikilinganishwa na miongo kadhaa iliyopita, hususan kabla ya mauaji ya kimbari. 

Katika kubaini hali ya mageuzi yaliyopo, Chama cha Mshikamano wa Wanawake wa Rwanda (ASOFERWA), kimekuwa kinawasaidia wanawake na watoto walioathiriwa na mauaji ya kimbari na kinasisitizia uwepo wa hali ya usalama na walio wengi na hususan wahanga wa mauaji hayo wanaamini kuwa hali kama iliyotokea mwaka 1994 haitatokea tena nchini humo. 

Kutokana na madhila ya janga hilo ililazimu wafungwa 120,000 wanaume kwa wanawake wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari kesi zao zisikilizwe kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya Rwanda (ICTR) jijini Arusha, Tanzania na wapo waliopatikana na hatia na wengine kuachiwa huru. 

Mahitaji ya kifedha na mengine ya kiuchumi yanapata kasi baada ya kukwamishwa na mauaji hayo. Lengo lipo katika kuwasaidia wahanga wa mauaji, yatima, walemavu, familia zinazoongozwa na watoto, wanawake waathirika wa VVU/Ukimwi, gharama za kuendesha mfumo wa sheria na kupatiwa makazi mapya maelfu ya wakimbizi walio nje ya nchi na kuziunganisha jamii au familia zilizopoteana na  hususan inapozingatiwa kuwa sehemu kubwa ya waliokuwa uhamishoni wamesharejea nchini humo.  

MANDHARI KABLA YA MAUAJI 

Awali Rwanda ilikuwa inajulikana kama “Uswisi” ndani ya Afrika ikiwa ni eneo ambalo ni takriban theluthi moja ya Ubeljiji, ambayo iliitawala kuanzia 1919 chini ya udhamini wa Umoja wa Mataifa kutoka kwenye mikono ya Ujerumani hadi ilipopata uhuru wake 1962. 

Kutokana na hali hiyo watalii wamekuwa wanaelezea nchi hiyo kuwa ni nzuri, lakini Mnyarwanda mmoja anasema kuwa baada ya mambo yaliyotokea nchini humo uzuri huo ni kama ulitoweka. 

Kiutamaduni Wahutu ni wakulima na kwa miaka mingi Watutsi wamekuwa ni wafugaji na makundi haya yamekuwa yakishirikiana katika masuala ya kilimo na mambo mengine, achilia mbali lugha, utamaduni na hata utaifa pia wamekuwa wanaoana kwa takriban karne sita.  

Jadi yao na michango kihistoria kwamba ni wakulima na wafugaji, Watutsi walikuwa ndiyo wamiliki wa ardhi na Wahutu kuwa wanaitumia ardhi hiyo kwa kukodi na hivyo mgawanyo wa kazi ulileta kutowiana kwa idadi ya watu wakati idadi ya Wahutu iliongezeka kushinda Watutsi. 

Chimbuko la kukorofishana kati ya makundi haya mawili ni wakati wakoloni walipoingia nchini humo. Ilikuwa ni kawaida kwa tawala za kikoloni kuchagua kabila litakalokuwa linapendelewa na kupatiwa ‘elimu,’ ili kuweka daraja kati ya watawala na watawaliwa. 

Hivyo Wabeljiji waliwachagua Watutsi waliokuwa wanamiliki ardhi, warefu na kwa udhanifu wa wakoloni walionekana ndiyo wenye sifa za kutawala.  

Aidha, kuanzishwa kwa nadharia zisizofikirika, upeo duni wa kugawa watu kwa matabaka, ndiyo uliokuwa mwanzo wa kuiyumbisha jamii ya Rwanda. 

 Watutsi walianza kujiona ndiyo ma-Mwinyi na Wahutu kuchukuliwa kama wakulima tena wasio na ardhi na huu ukawa mwanzo wa kugawanyika kisiasa ndani ya jamii hiyo. 

Tawala za wakoloni pia ziliingiza nchini humo silaha za kisasa na mbinu mpya za kivita, lakini kwa uhalisia zilikuwa ni kuziingiza jamii za Rwanda kwenye migongano na migogoro.  

Wamisionari pia walileta wimbi jipya la kuwayumbisha kisiasa. Kanisa liliwafundisha Wahutu kujiona ni watu wanaokandamizwa na kuwachochea kufanya mapinduzi na hivyo kuwafanya kuingia kwenye mapigano, njia Wahutu waliyoiona ni sahihi katika kujikomboa. 

Katika uasi ulioanza mwaka 1956 takriban Watutsi 100,000 walipoteza maisha na haya ndiyo yaliyokuwa mauaji ya kwanza ya kimbari na 1959 Wahutu waliwanyang’anya madaraka na ardhi. 

Hali hiyo ilisababisha, Watutsi wengi kukimbilia uhamishoni walikounda na kuwafunza askari na kuunda chama cha Rwandan Patriotic Front (RPF). 

Baada ya uhuru na serikali dhaifu ikiwa inaongozwa na Wahutu kuingia madarakani mwaka 1962, Rwanda ilianza kukabiliwa na migogoro ya ndani sanjari na  uhasama uliibuka kati ya jamii na tawala za majimbo. 

Hata hivyo, upinzani uliokuwa unatolewa na Watutsi mara kwa mara ulikuwa unajibiwa kwa kuchukua hatua kandamizi. Mfano, 1973 walibaguliwa kabisa kwenye suala la elimu ya sekondari na chuo kikuu.  

Katika kuponyesha jeraha ambalo ni matokeo ya uadui wa kurithi ni jukumu  linalotakiwa kutoka mioyoni mwa wanajamii wa Rwanda wakiongozwa na serikali yao na kuondokana na dhana ya kuulizana nani ni nani badala yake iwe nani anahitaji nini. 

Bado uchungu mwingi umekuwa unazikabili jamii zilizonusurika na ambazo leo zinaweza kuishi pamoja tena. Hata hivyo, kila hatua inayoonekana kuwa inawezekana kutumika katika kuponya majeraha yaliyotokana mauaji ikiwamo kufanywa uchunguzi upya wa baadhi ya mauaji kama ya Rais Juvenali Habyarimana. 

Lakini historia inasema kuwa hakuna jambo lisilo na mwangwi na tukio hilo limekuwa na athari za kisaikolojia na kuwafanya baadhi ya watu kupatwa na hali  lukuki  kama mfadhaiko, lakini jamii imekuwa inawajibika na kuona kuwa jambo hilo si la mtu binafsi bali ni la jamii yote. 

Kila jua linapochomoza macho ya jamii nyingi na hususan nchi jirani haiyumkiniki kwamba zinaomba amani idumu katika nchi hiyo na Mungu mweza wa  yote aiepushe Rwanda na janga jingine la mauaji ya kimbari.