Home Latest News Kuna demokrasia ya kimataifa?

Kuna demokrasia ya kimataifa?

1231
0
SHARE

Na Gaspar A. Hiza

NENO ‘demokrasia’ ni neno linalotumika sana, hasa katika ulimwengu wa siasa. Tunalitumia neno hili kama vile tunaelewa na kukubaliana maana yake. Tumefika mahali ambapo wapo watu hutumwa na mataifa yao, au mashirika Fulani, kutembelea nchi zinazoingia kwenye michakato ya uchaguzi na baadaye hutoa maoni hasi au chanya, kuhusu demokrasia katika chaguzi hizo. 

Maoni hayo hutolewa kana kwamba dunia imekubaliana kwamba, ili uchaguzi ukubalike kwamba ni wa kidemokrasia, kuna mambo lazima yatekelezwe. Swali ni kwamba – ukubalike kwa nani? Hivyo vigezo kaweka nani? Je, ana haki ya kuweka vigezo hivyo? Makala moja haitoshi kujadili demokrasia, lakini tusiitupe fursa hii.

Demokrasia ni neno lenye asili ya Kigiriki, nalo ni muungano wa maneno mawili. “Demos” ni watu na “crates” ni utawala. Demokrasia maana yake ni utawala wa watu. Hao watu ni akina nani? Hilo sio swali rahisi kwa sababu hata wakoloni walikuwa watu. Je, utawala wa kikoloni ulikuwa wa watu? Hata kidogo. 

Wakati Wagiriki wakitumia neno hili huko kwao, tena hapo zamani, dola zao zilikuwa miji na sio nchi kubwa kama zetu. Ilikuwa lazima kwao vile vile waamue juu ya “mtu ni nani”, yaani yule atakayeshiriki katika utawala wao. Hapa ndipo utaona kwamba tangu zamani demokrasia ina mipaka yake kila mahali itakapotumika. 

Kwa Wagiriki wale hasa wa miji ya Sparta na Athens, washiriki (watu) ni lazima wawe Wagiriki, wanaume, wawe huru yaani sio watumwa, wawe watu wazima (sio watoto au vijana). Kwa wakati ule kutoshiriki wanawake katika maamuzi muhimu, ilieleweka na kukubalika. Leo je, tunaweza kuongea juu ya demokrasia wakati tunakubali kubagua wanawake? Hao wanawake watakubali? Hivi unaweza kuongea juu ya demokrasia katika nchi yenye watumwa?

Hao Wagiriki waliodai demokrasia kwao walikuwa ni watu HURU. Swala la uhuru ni suala la msingi na ndio maana demokrasia haiwezekani katika ukoloni. Lakini unaweza kuwa huru bila kuwa na demokrasia. Hiyo hali haupendezi, lakini inawezekana.

Somo jingine tunalolipata kutoka kwa Wagiriki ni kwamba katika chaguzi zao, hawakutaka kuchagua viongozi masikini. Walitambua tangu awali kwamba watu wakiwa madarakani hulinda maslahi yao ya kiuchumi. Wenye mitaji wanalindana kama tabaka, na wavuja jasho wanalindana kama tabaka. 

Matabaka haya yana ugomvi wa kudumu hadi leo popote duniani. Kama tunakubali kwamba demokrasia ni utawala wa wengi, je, kuna nchi duniani ambako waajiri ni wengi zaidi ya waajiriwa, ili kuhalalisha utawala wa mabepari dhidi ya wafanyakazi? Kama hakuna, ni nchi gani ya kibepari ambayo inastahili kujiita ya kidemokrasia?

Kuna jambo limejificha hapa. Nchi nyingi za kibepari haziongei jina ya utawala wa kitabaka. Hilo wanalitambua lakini kutokana na uchache wao hupenda kuongea juu ya utawala wa liberali. Huu ni utawala ambao kiongozi hupatikana kwa kigezo cha kukubalika kwa wapiga kura. 

Wakishapata mgombea wamtakaye, watamgharamikia kwa matumaini kwamba ama ni mwenzao, au yupo tayari kulinda maslahi yao ndani na nje ya nchi. Hapa ni vizuri kutambua jinsi neno “wengi” au “majority” linavyotumika kukidhi mahitaji ya wachumi na uchumi. 

Katika mfumo huu, wavuja jasho hugeuzwa kama mashabiki wa demokrasia kwa kupiga kura, lakini “kazi ina wenyewe” – ni wale wenye mali.

Hapa ingefaa kuzungumzia suala la vyama vingi vya siasa na dhana ya demokrasia. Tumekishaona kwamba siasa hizi ndani yake ni uchumi tu. Ukiongea uchumi huwezi kukwepa mgongano wa wanyonyaji dhidi ya wanyonywaji. Hayo hujitokeza katika utumwa, ukabaila, ubepari na ubeberu. Kwa ujumla wake, utumwa umepitwa na wakati. Ukabaila upo, lakini ubepari ndio umetamalaki duniani. 

Zipo nchi chache ambazo zimejaribu siasa ya ujamaa kwa viwango mbalimbali vya ufanisi. Naamini sikosei nikisema mpaka zama hizi ubepari umekolea zaidi duniani kuliko ujamaa. 

Tuendako je?

Tukizingatia uchumi na demokrasia, hata hii ya kiliberali, tungetegemea vyama vya siasa vikijengwa kwa misingi ya ubepari au ujamaa kama itikadi zao. Hapa Tanzania tunavyo vyama vya siasa zaidi ya kumi. Hivi ukitakiwa kuandika makala juu ya tofauti ya vyama hivi, utaandika kurasa ngapi? 

Kuna tofauti ya majina ya vyama na majina ya viongozi. Na itikadi je? Kipo chama kimoja kinachojinasibu ni cha wakulima na wafanyakazi—yaani wanyonge wa nchi hii. 

Siku hizi hakiongei sana juu ya siasa ya ujamaa, japo kinaitekeleza kweli kweli. Mabeberu sio wajinga hata kidogo. Wanafahamu kwamba maslahi yao, yanagongana na maslahi yetu. Katika mazingira hayo, hawapendi nchi zetu ziwe na amani na mshikamano kwani mazingira hayo yanatupa nguvu za kupambana nao kulinda kilicho chetu. 

Wanazo mbinu nyingi za kuendeleza mapambano dhidi yetu. Moja ni kuleta sera za kipumbavu kama ile ya “Utandawazi”. Ule ni “Utandawizi” tu. Eti dunia ni kama kijiji kile cha Sparta au Athens. Kasema nani? Wamesema wao ili wajipe haki ya kudai kauli juu ya maliasili zetu kama madini. Kumbuka hadithi ya makinikia na tanzanite. Zile ni ishara tu za madini yote tuliyo nayo. Eti nao ni yao! Eti vya kwao vyao na vyetu vyao!

Vyama vingi vilevile ni utekelezaji wa sera ya wagawanye ili uwatawale. Wamefanikiwa kutuaminisha kupitia elimu ya darasani, kwamba bila upinzani hakuna demokrasia. Mimi nimefundishwa hayo na mapadre Wakatoliki katika shule za sekondari. Ukiwauliza vipi demokrasia katika Kanisa letu? Wanasema ni Roma locuta causa finite—yaani  Roma imesema na mjadala umefungwa. 

Huku kwenye vyama vingi mgongano huletwa kati ya chama tawala na wapinzani. Wakati ninyi mnaendelea kugombana, wao wanaendelea na unyonyaji, huku wakiendelea kusifu vyama vingi na kulaumu utekelezaji kama vile ukandamizaji na maneno mengine kama hayo. 

Lengo lao ni kuwawekea vigezo ambavyo mnapojaribu kuvitekeleza wao wanaendelea kuwahukumu, lakini unyonyaji wao unaendelea. Hivyo vigezo wamevitoa wapi? Sisi ni taifa huru na tunahaki ya kuweka vigezo vyetu na kuvisimamia. Nani kasema? Wanahoji!

Zipo njia nyingi za kutupotezea malengo. Nyingine ni hii ya kuwapangia ratiba ya kazi viongozi wenu wakuu. Rais wenu anaweza kujiteua kila siku anatekeleza mialiko ya kufanya ziara nchi za nje. Mtu kama huyo hana muda wa kupambana na hali halisi ya umaskini wa taifa lake. 

Huko anakokwenda kufanya ziara huishia kupewa shahada za Uzamivu (PhD) ya utawala bora. “Utawala bora”? Hivi hili ahukumiwa na wapiga kura wake au taasisi za kibeberu? Anaweza kuwa mtawala bora kwa mabeberu na wanyonywaji ambao ndio raia anaoongoza, je? Kwa hili nampongeza sana Rais wetu kwa kukataa kufuata ratiba za kutengenezewa. Ndiyo maana tunaye na maendeleo tunayaona. 

Katika makala haya, nitataja njia nyingine ya kuendeleza ubeberu kinyume na maslahi ya wanyonge ni elimu. Mpaka leo mabeberu wanashiriki katika kutoa elimu kwa vijana wetu, ukiwakataza watakulaumu kwa vigezo vya demokrasia. 

Kuna demokrasia gani katika kuandaa watu wetu wawe na msimamo wako na sio wetu? Hilo wataendelea nalo vyuo vikuu na hata kwenye mafunzo ya maeneo nyeti kama yale ya maafisa na majeshi ya ulinzi na hata polisi. 

Hao hao ndio watakaokuwa wamewafunza demokrasia kwa mitizamo yao na kuiita ya kimataifa. Ndani ya taifa mnaweza kuhitilafiana juu ya uelewa wa demokrasia, kumbe mnarejea tu hoja mlizofunzwa na mabepari. 

Wamewafanya wanafunzi wa kudumu na watu wa aina hiyo wanahitaji ushauri milele na hilo ndio lengo lao. Ubepari watauita mfumo huru wa uchumi. Ujamaa watauita mfumo kandamizi. Wewe kazi yako ni kusema “Ndiyo au Ndiyo Afande.”

Inawezekana kwamba mpaka sasa umetambua kwamba ‘demokrasia’ ni sawa na blanketi safi ambalo hutumika kufunika uchumi wa aina yoyote. Kwa kuwa sera za uchumi hazifanani hata kwa nchi jirani, ukweli unabaki kwamba hakuna demokrasia ya dunia. Zitakuwepo chaguzi za mara kwa mara, kura za siri. Tume huru za uchaguzi na mambo kama hayo. 

Ukiwauliza washiriki wa chaguzi hizi kama kwao jambo la msingi ni kura au kula, wale wa ukweli watasema kula. Hii maana yake ni uchumi bora kwa wengi ambao ndio hao wapiga kura. Vile vile wale waliopo madarakani watambue kwamba japo kwa nia njema wanapenda kuwajibika kwetu, mabeberu hawatawaacha huru. Hata kwao la maana sio demokrasia yetu, bali uchumi wao. 

Hapa Afrika marais waliopindua serikali za kidemokrasia, waliungwa mkono na mabeberu ili mradi tu hawakugusa maslahi yao. Kuna mtaalamu mmoja alisema kuwa: “Politics is the highest concentration of economics”—siasa nia mkusanyiko wa nguvu za uchumi. Nakubaliana naye. Ndio maana wakulima na wafanyakazi wanaojitambua, hujiunga na chama kinachotetea maslahi yao.