Home Latest News KWANINI XI JINPING KAPEWA HADHI YA MAO ZEDONG?

KWANINI XI JINPING KAPEWA HADHI YA MAO ZEDONG?

2537
0
SHARE

Na Abbas Abdul Mwalimu

Hivi karibuni Chama Tawala cha Kikomunisti Communist Party of China (CPC) kinachoongoza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kilifanya Mkutano wake Mkuu wa 19 wa Mwaka ambapo kiliweza kujadili mambo mengi ikiwemo uchumi, biashara, ulinzi, usalama sambamba mahusiano ya kimataifa baina ya China na mataifa mengine duniani.

Katika Mkutano huo mkubwa chama cha CPC ambacho kilianzishwa mwaka 1921 kilimpa hadhi aliyokuwa nayo Rais wa kwanza wa nchi hiyo na Baba wa Taifa hilo Hayati Mao Zedong Rais wa sasa Bwana Xi Jinping sambamba na kuyaingiza mawazo yake ndani ya Katiba ya CPC kama ambavyo ilifanywa kwa Mao mwenyewe pale ambapo “Mawazo ya Mwenyekiti Mao” yaliingizwa kwenye Katiba ya CPC pamoja na mawazo ya Mwanamapinduzi wa uchumi wa kisasa ambao China inautembelea Bwana Deng Xiaoping anbaye alifariki mwaka 1997.

Makala hii inakudadavulia sababu zilizopelekea Rais Xi Jinping kupewa hadhi aliyopewa Mao Zedong.

Lakini kabla ya kufafanua sababu hizo ni vema kwanza tukamtazama Mao Zedong alivyokuwa ili tuweze kutambua sifa linganifu walizotumia chama cha CPC.

MAO ZEDONG NI NANI?

Mao Zedong alikuwa mwanamapinduzi, mzalendo, mshairi, mwanafalsafa na muumini mzuri wa nadharia ya kiuchumi ya Marx (Marxist Theory) ambayo ililenga kuondoa matabaka ya kiuchumi kati ya walionacho na wasionacho.

Mao Zedong alizaliwa mwaka 1893 na kuishi mpaka 1976 ambapo alifariki. Kama Mao angekuwa hai mpaka sasa basi tarehe 26 mwezi Desemba mwaka huu angetimiza miaka 124.

Mao Zedong anaelezwa kuwa alianzisha Mapinduzi ya Kiutamaduni (Cultural Revolution) mnamo miaka ya 1960 mpaka 1976 alipofariki. Inaelezwa kuwa mapinduzi hayo ya kiutamadunj ndiyo yaliyopelekea China tunayoiona leo hii.

Katika mapinduzi haya China iliweza kufanikiwa kurusha satelaiti yake ya kwanza katika anga la mbali na kufanikiwa kuanzisha na kuingia katika mahusiano ya kidiplomasia na mataifa 60 duniani, mahusiano ambayo yameongezeka maradufu na kuimarika kiasi cha kuitisha Marekani.

Mwezi Oktoba mwaka 1950 Mao alianzisha vita dhidi ya uvamizi wa Marekani katika nchi ya Korea Kaskazini na kufanikiwa kuzima mpango wa Marekani wa kutaka kuweka utawala utakaokuwa na maslahi na wao. China imeendelea kuilinda Korea Kaskazini kwa kupitia nguvu yake ya kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mpaka leo hii, ingawa jambo hili haliwezi kuelezwa wazi.

Tukumbuke kuwa ndani ya kipindi hicho pia China iliweza kupambana na iliyokuwa Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti ambayo iliivamia China kwa lengo la kulazimisha mfumo wake wa uongozi wa kiuchumi kutumika China. Ikumbukwe kuwa Mao alikuwa muumini mzuri wa nadharia ya Marx (Marxist theory) lakini yeye Mao aliitohoa ili iendane na mazingira ya China ya kipindi kile.

Mwaka 1953 China ilifanya mapinduzi ya viwanda ya kijamaa ambayo yalilenga kuondoa umiliki wa viwanda kutoka kumilikiwa na umma kwenda mikononi mwa wananchi.

Hapa inaelezwa kuwa chini ya utawala wake katika kipindi hiki China iliendelea kufanya mapinduzi ya kidemokrasia.

Changamoto kubwa ya utawala wake inaelezwa kutokea mnamo mwaka 1958 kipindi ambacho Mao alianzisha kampeni ya kuhamishia wananchi vijijini iliyojulikana kama Great Leap Forward kwa lengo la kuanzisha vijiji vya ujamaa. Wapinzani wengi wa dhana ya mapinduzi ya Mao wanakosoa utawala wake kwa kuangalia kampeni hii ambapo inaelezwa kuwa Mao aliua watu wengi mamia kwa mamilioni, wakiwemo ndugu, jamaa, marafiki na hata washirika wake wa karibu. Sambamba na hilo inaelezwa kuwa hata shule na viwanda vingi vilifungwa kitendo ambacho kiliathiri vijana na jamii kwa ujumla. Chama cha CPC kimekuwa kikipinga ukosoaji huu kwa kuekeza kuwa umekuwa ukipotosha jamii badala ya kuelezea mazingira halisi yaliyokuwepo kipindi kile na hasa kwa kuangalia dhana ya wale waliokuwa wakipinga dhana ya kimapinduzi ya Mao iliyojulikana kwa kingereza kama “Anti-Right Campaign” mwaka 1957 kampeni iliyokuwa na lengo la kuendeleza matabaka ya walionacho na wasionacho ambayo Mao aliyapinga kwa nguvu zote.

Katika kipindi chake Mao aliweza kuanzisha mapambano dhidi ya maadui watatu ambayo walikuwa Kupokea Rushwa, Uchafu na Urasimu. Mbali na hilo Mao pia alianzisha vita dhidi ya maadui wengine watano ambao ni Kutoa Rushwa, Ukwepaji Kodi, Wizi wa Mali za Umma, Uongo kwenye Mikataba ya Serikali pamoja na Kuiba Taarifa za Kiuchumi.

Mao alifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mikakati yake aliyoipanga kwa lengo la kuinua uchumi wa China, kujenga nidhamu ya uwajibikaji, uzalendo,utu sambamba na umoja na mshikamano wa kitaifa ambao tunauona kwa wachina leo hii popote wanapokuwepo duniani.

KWA NINI XI JINPING NA SI HU JINTAO?

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza, kwa nini hadhi hii na heshima apewe Xi Jinping na wala si mtangulizi wake Hu Jintao?

Tukumbuke kuwa mtu pekee ambaye mawazo yake yaliweza kuingizwa moja kwa moja kwenye Katiba ya CPC akiwa hai tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1921 alikuwa Rais wa kwanza wa China Bwana Mao Zedong. Mwanamabadiliko wa kiuchumi Deng Xiaoping mawazo yake yaliingizwa katika Katiba ya CPC mara baada ya kufariki mwaka 1997. Deng alifahamika zaidi kwa dhana yake ya kiuchumi inayojulikana kama Deng Xiaoping Theory.

Kwa mantiki hiyo kitendo cha kumpa hadhi na heshima hii ya kipekee Rais Xi akiwa hai ni cha pili baada ya kile kilichofanywa kwa Mao katika uhai wake.

Chama cha CPC kiliangalia mambo yafuatayo katika kumpa hadhi hiyo Rais Xi Jinping:

(1) Uchumi, Biashara na Uwekezaji

Tangu Rais Xi alipoingia madarakani uchumi wa China sambamba na biashara baina yake na mataifa ya nje vimekua maradufu.

Mnamo mwezi Desemba mwaka 2015 Rais Xi Jinping aliingiza China kwenye muelekeo mpya wa kimahusiano akiuita “Real Win-Win Cooperation” kati ya China na nchi za Afrika (Sino-Africa trade).

Mkakati mkubwa ni kutengeneza mahusiano yenye manufaa kwa pande zote mbili yaani China na Afrika, na katika hili China imeingiza kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 60 kwenye miradi mikubwa ya Afrika (Capital Investment Projects) yenye lengo la kuimarisha uchumi wa Afrika.

Rais Xi alipokuwa katika Mkutano nchini Afrika ya Kusini (Summit) mnamo mwaka 2015 aliahidj mambo yafuatayo;

(a) Ukuaji endelevu wa uchumi

(b) Viwanda

(c) Kufanya kilimo kuwa cha kisasa Afrika

(e) Kuboresha na kuimarisha miundombinu Afrika

(f) Huduma za kifedha

(g) Maendeleo ya kijani

(h) Uwezeshaji katika biashara na uwekezaji

(I) Kuondoa umasikini na kuboresha ustawi wa jamii

(j) Afya kwa Umma

(k) Mbadilishano wa mtu na mtu na

(l) Amani na Usalama

Ingawa ukuaji wa uchumi wa China kwa mwaka 2016 ulishuka kufikia asilimia 6.7 lakini China imebaki kuwa mbia Mkuu wa Biashara Afrika toka ilipoiondoa Marekani (USA) katika nafasi hiyo mwaka 2009.

China ni fikio (destination) la asilimia 15 hadi 16 ya usafirishaji (exports) wa bidhaa toka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (Sub-Saharan Africa Exports) na asilimia 14 hadi 20 ya chanzo cha ununuzi (imports) wa bidhaa zinazotumiwa katika bara la Afrika.

Mwaka 2015 nchi ya Afrika Kusini iliongoza kusafirisha bidhaa nchini China ikifuatiwa na Angola na Sudan.

Mwaka huo huo Afrika ya Kusini iliongoza kwa kununua bidhaa toka China ikifuatiwa na Nigeria na Misri.

Biashara kati ya China na Afrika (Sino-Afrika Trade) inaelezwa kuwa imeongezeka katika kipindi cha miaka 15 iliyopita tokea ulipoisha mdororo mkubwa wa kiuchumi (economic slowdown) duniani mwaka 2007 mpaka mwaka 2009.

Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha John Hopkins cha Marekani kinachofanya utafiti unaojulikana kama “China-Africa Research Initiative” kimeeleza kuwa kuanzia mwaka 1992 mpaka mwaka 2015 China imeingiza zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 732.99 kwa kusafirisha bidhaa kwenda nchi za Afrika. Ingawa wachambuzi wengi wanadai takwimu hizi zilizochukuliwa kutoka kwenye chanzo cha Umoja wa Mataifa “UNComtrade” zinaweza zisiwe na uhalisia hasa ikidaiwa kuwa China haipendelei kuweka wazi takwimu za biashara yake na Afrika.

Bara la Afrika linakadiriwa kuwa na watu wapatao bilioni 1.216 idadi ambayo inalifanya bara hili kuwa la pili kwa idadi ya watu duniani kwa mujibu wa mtandao wa worldometers.info. Tafsiri iliyopo hapa ni kuwa Xi Jinping amelenga kulikamata soko la bara zima la Afrika duniani.

Hili linajionesha wazi kwa namna ambavyo China imejiingiza kwenye miradi mikubwa yenye kuhamasisha ukuaji wa uchumi barani Afrika kama vile umeme, barabara na miundombinu mingine katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Tanzania na Angola.

(2) Nguvu za Kijeshi (Military Power)

Bajeti ya Jeshi la China kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni Dola za Marekani Bilioni 215.7. Kiwango hiki ni ongezeko la asilimia 7 ya matumizi ya kijeshi na kinaifanya China kuwa ya pili Duniani kwa Bajeti kubwa ya Jeshi nyuma ya Marekani. Tukumbuke hivi karibuni Rais Donald Trump nae alitangaza kuongeza bajeti ya jeshi kwa asilimia 10 mwaka ujao wa 2018, hii inatoa picha kwamba matumizi ya kijeshi ya nchi ya China yanaitisha Marekani na wachambuzi wengi wa masuala ya kiusalama wanaeleza kuwa huenda China imeficha kiwango halisi cha matumizi ya kijeshi kwa kuwa masuala ya ulinzi na usalama yamekuwa hayawekwi wazi na nchi nyingi duniani.

China pia imeweza kuweka base yake ya kijeshi katika nchi ya Djibouti hali inayoashiria kuwa China inataka kuhakikisha maslahi yake yaliyopo Afrika yanalindwa ipasavyo. Haitashangaza kuona China ikiendelea kujipanua kijeshi katika nchi nyingine za kiafrika.

Mbali na base hiyo China imeweka base nyingine katika eneo la bahari nyekundu ya China ya Kusini hii nayo inatoa picha ya jinsi gani China inajipanua kijeshi.

(3) Ushawishi (Influence) wa China Duniani.

Katika hotuba yake Rais Xi Jinping aliionesha dunia kuwa China hii ya sasa si China iliyokuwa kipindi cha mtangulizi wake. Xi mara kadhaa katika hotuba ile aliita China kama nchi yenye nguvu yaani “Great Power” hii inaonesha wazi dhamira ya China katika kuchukua ukuu wa dunia.

Ushawishi wa China Duniani umezidi kuongezeka. Tukumbuke jinsi Rais Donald Trump alivyomuomba Rais Xi kumsaidia kutatua mgogoro wa uzalishaji wa silaha baina ya Marekani na Korea Kaskazini, ni ishara tosha ya kuimarika kwa Ushawishi wa China Duniani.

China pia imekuwa na ushawishi mkubwa katika Mataifa yanayounda Umoja wa nchi za BRICS yaani Brazil, Russia, India, China yenyewe na nchi ya Afrika ya Kusini kiasi cha kupeleka umoja huu sasa kuwa na Benki yake inayoelezwa kuwa na makao makuu yake nchini China.

China pia ni nchi mwanzilishi wa Umoja unaojulikana kama Shanghai Cooperation Organization kwa kifupi SCO unaojumuisha nchi za India ,Iran, Uzbekistan na nyinginezo. Umoja huu ulianza kujikita kwenye masuala ya kiuchumi lakini sasa unajielekeza pia kwenye masuala ya kiulinzi na kiusalama hivyo kukua kwake kunaweza kuwa na athari kwa Umoja wa Kujihami wa nchi za Magharibi yaani NATO.

(4) Ustaarabu wa Kichina (Chinese Civilization.

Ustaarabu wa kichina umeenea sana duniani leo hii kama Samuel Huntington alivyoeleza katika Clash of Civilization.

Ustaarabu ninaoeleza hapa ni dhana nzima ya utamaduni ambayo imejikita katika lugha, vyakula na hata mavazi.

Katika utawala huu wa Rais Xi Jinping ustaarabu wa kichina unaonekana kuoenea kwa kasi zaidi kama ambavyo Mao Zedong alitamani.

Nchi kama Tanzania lugha ya kichina imekuwa ikifundishwa katika vyuo vya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Chuo cha Diplomasia Kurasini na Chuo Cha Sayansi Mbeya. Mbali na kufundisha vyuoni serikali ya China inawezesha wachina kufundisha kichina katika shule za msingi Bagamoyo, Mtwara na Mbeya. Waswahili husema ukitaka kumjua mtu fahamu lugha yake, ni wazi kuwa wachina wanatufundisha lugha yao ili waweze kurahisisha mahusiano ya nchi yao na nchi za kiafrika hasa kwa vijana kama nchi  Tanzania ambapo kwa mpango huu wa Xi wameonesha kufanikiwa na watafanikiwa zaidi.

Watafiti wanaeleza kuwa kufikia mwaka 2050 asilimia 25 ya idadi ya watu  bilioni 9 watakaokuwa duniani kote itatoka bara la Afrika na wengi wao watakuwa vijana wa umri chini ya miaka 30. Kwa picha hii tunaweza kuona China imejipanga vipi katika kuhakikisha inateka soko la Afrika kiuchumi, kiushawishi na hata kiutamaduni hali ambayo itapelekea China kunufaika zaidi.

Katika kumalizia hotuba yake Rais Xi aligusia suala la Rushwa na ubadhilifu na kusema serikali yake safari hii itakuwa inakata kama kiwembe, jambo ambalo Mao alilipigania kwa moyo wake wote. Baada ya kumaliza hotuba ile mtu wa kwanza kuonesha kuguswa na kumpa mkono Rais Xi alikuwa Rais Mstaafu Bwana Jiang Zemin mwenye miaka 91. Kitendo cha Zemin kusimama kilionesha ni jinsi gani Xi aligusa pale CPC inapotaka.

Sasa kwa nini wasimpe Xi heshima na hadhi ya Mao?

Makala hii imeandikwa na Abbas Abdul Mwalimu Mchambuzi wa Masuala ya Kimataifa na Kidiplomasia kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Anapatikana Facebook kwa anwani ya Abbas Abdul Mwalimu

Simu 0719 258484