Home Makala Kimataifa Machafuko kuvuruga uchaguzi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Machafuko kuvuruga uchaguzi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

2125
0
SHARE

KINSHASA, DRC

HALI ya usalama wa raia na mali zao katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imezidi kuwa mbaya, na kusababisha idadi ya raia kuyakimbia makazi yao. Sababu kubwa ya kuyakimbia makazi yao ni kushamiri wimbi la machafuko yanayotokana na maandamano pamoja na mapambano kati ya vyama vya upinzani na wafuasi wao dhidi ya serikali ya Rais Joseph Kabila.

Kuongezeka mivutano ya kisiasa na maandamano ya wapinzani wa serikali, ghasia na machafuko kumesababisha watu wasiopungua 50 kuuawa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Kinshasa.

Wakati hayo yakijiri, jumatatu wiki hii serikali nchini humo kupitia wizara ya mambo ya nje imetangaza kuwa ni watu 17 pekee ndiyo waliopoteza maisha na siyo 50 kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari.

Taarifa hiyo ilitolewa na  Waziri wa Mambo ya Ndani, Evariste Boshab ambaye alibainisha kuwa kati ya watu hao  17 waliopoteza maisha ni pamoja na askari polisi watatu waliokuwa wkaikabiliana na waandamanaji.

Alieleza kuwa watu hao walipoteza maisha wakati wa maandamano  yaliyofanyika Jumatatu wiki hii katika miji mbalimbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lambert Mende, askari polisi walichomwa moto wakiwa hai na raia waliouwawa walikuwa miongoni mwa waandamanaji. Watu kadhaa wamekamatwa.

Miongoni mwa waliokamatwa katika mapambano kati ya askari na waandamanaji ni wabunge wawili wa kambi ya upinzani, akiwemo Martin Fayulu.

Muungano wa upinzani nchini humo ulifanya maandamano katika miji kadhaa nchini kote Jumatatu wiki wakidai uchaguzi wa urais ufanyike mwezi Novemba, kama inavyotakiwa na Katiba, na kutomruhusu Rais wa sasa Joseph Kabila kuwania tena kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaoiunga mkono serikali ya nchi hiyo wamebainisha kuwa uchaguzi wa urais hauwezi kufanyika kabla ya mwisho wa mwaka.

Kufuatia hali hiyo, Katibu Mkuu wa Moja wa Mataifa, Ban Ki-moon alilazimika kutoa taarifa Jumatatu wiki hii mara baada ya mapambano kati ya waandamanaji na askari. Katika taarifa yake Katibu huyo alitoa tahadhari kwa pande zote husika nchini humo kuhusiana na hatari ya kuongezeka mivutano hiyo ya kisiasa.

Amelaani vikali vitendo vya pande zote mbili zinazohasimiana kwa kusababisha idadi ya Polisi na raia wa kawaida kupoteza maisha katika mivutano hiyo ya kisiasa. Malalamiko na ghasia zimekuwa zikiendelea kwa muda sasa,  ambapo zimeongezeka na kufikia kilele katika siku za hivi karibuni kufuatia uamuzi wa kuahirishwa uchaguzi mkuu wa rais.

Hivi karibuni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) nchini humo iliwasilisha rasmi ombi lake la kutaka kuahirishwa uchaguzi huo kwa Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo. Mkuu wa tume hiyo, Corneille Nangaa alitaka kuahirishwa uchaguzi huo hadi mwakani.

Kwa mujibu wa katiba, Tume ya Uchaguzi inapaswa kuwasilisha na kutangaza hadharani majina ya wagombea na daftari la wapiga kura miezi mitatu kabla ya kumalizika kipindi cha rais  Kabila. Tume hiyo inadai haina uwezo wa kutekeleza masharti hayo katika muda uliobaki na kwamba serikali haina bajeti ya kuandaa uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa Katibaya nchi hiyo, Kabila ambaye anamaliza kipindi chake cha pili na cha mwisho cha urais wake tangu aingie madarakani mwaka 2001, haruhusiwi kugombea tena urais wa nchi hiyo baada ya kumalizika muhula wake ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

Kwa msingi huo wapinzani wanasema kuwa visingizio vyote vinavyotolewa na Tume ya Uchaguzi vimelenga kumbakisha madarakani Rais Kabila hadi wakati wa kufanyika uchaguzi mkuu ujao.

Wanasema kama walivyofanya viongozi wengine wakongwe wa Afrika, Rais Kabila ana nia ya kubadilisha katiba ya nchi hiyo ili aendelee kuongoza nchi kwa kipindi cha tatu mfululizo, na kwamba kuahirishwa uchaguzi kunalenga kutayarisha fikra za waliowengi nchini zikubaliane na suala hilo.

Aidha, wapinzani wa Kabila wanamkosoa kwa kushindwa kuimarisha hali ya usalama wa nchi hiyo na uchumi wake. Wanasema kwamba ameshindwa kabisa kuboresha uchaumi wa nchi na hivyo kuongeza kiwango cha ukosefu wa ajira na ughali wa maisha.

Pia wanasema machafuko na mapigano katika mpaka wa nchi hiyo na nchi jirani yamewasababishia matatizo makubwa wakazi wa maeneo hayo na hasa ya mashariki mwa nchi. Siku chache zilizopita mji wa Kinshasa ulishuhudia maandamano makubwa ya wapinzani wa serikali waliokuwa wakilalamikia utendaji mbovu wa askari usalama katika kupambana na wanamgambo wanaovuruga usalama wa nchi.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini humo wanasema wimbi la malalamiko katika nchi hiyo inaonekana wazi kwamba mnyukano mkali kati ya serikali na wapinzani umedhihirika na huenda ukawa uadui mkubwa kuliko inavyodhaniwa sasa, na baadaye kuzua maafa nchini humo.

Kwa msingi huo wanasisitiza juu ya udharura wa kufanyika haraka mazungumzo ya kitaifa ambayo yatazihusisha pande zote kwa upataishi wa upande usiopendelea upande wowote yani serikali na vyama vyote vya kisiasa na kiraia kwa ajili ya kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro huo kwa msingi wa sheria za nchi na kulindwa haki za wananchi.