Home Habari MAENDELEO HAYANA ITIKADI ZA CHAMA

MAENDELEO HAYANA ITIKADI ZA CHAMA

1457
0
SHARE

Mwenyekiti- Kilombero0-1

 

NA VICTOR MAKINDA

TOFAUTI za kiitikadi baina ya madiwani katika halmashauri nyingi  nchini, zimekuwa ni kikwazo kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye tija kubwa kwa wananchi.

Tofauti hizo zimekuwa chanzo kikubwa katika utekelezaji wa miradi inayobuniwa na halmashauri husika, au inayoletwa na Serikali Kuu na wafadhili. Mitazamo ya kisiasa, tofauti ya uwakilishi wa vyama na ubinafsi, ndio sababu kuu.

Mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia migogoro na minyukano baina ya madiwani katika baadhi ya halmashauri. Migogoro hiyo hutokana na ama kujipendelea miradi fulani katika kata Fulani, au kutoa upendeleo wa waziwazi katika baadhi ya kata ambazo zinaongozwa na chama fulani.

Zipo halmashauri ambazo madiwani wake wamegawanyika na kupoteza umoja, mshikamano na uwajibikaji wa pamoja katika masuala ya maendeleo.

Ifahamike kuwa moja kati ya kazi kubwa ya Baraza la Madiwani, ni kusimamia mapato ya Serikali kwa ngazi ya halmashauri sambamba na kuhakikisha miradi ya maendeleo katika kata zao inatekelezwa kwa kiwango kinachokubaliwa. Ikiwa pakatokea hali yoyote ya sintofahamu ya kiitikadi inayotokana na vyama wanavyotoka madiwani, jukumu hili kubwa la Baraza la Madiwani hulegalega na kukosa ufanisi katika utekelezaji wake.

Ukweli ulivyo ni kwamba, katika Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, lenye  jumla ya madiwani 35, ambapo kati yao 17 ni kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), 18 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), na wawili kutoka Chama cha Wananchi (CUF), lina umoja wa kuwa mfano wa kuigwa na mabaraza mengine katika nchi yetu.

Halmshauri ya Wilaya ya Kilombero ina majimbo mawili ya uchaguzi. Majimbo  hayo ni Mlimba ambayo linaongozwa na Suzani Kiwanga (Chadema) na Kilombero, ambalo Mbunge wake ni Peter Lijualikali pia wa Chadema.

Kwa uwakilishi huo, ilitarajiwa kuwa patakuwapo na sintofahamu kubwa katika kusimamia miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Kilombero. Kinyume chake, Baraza la Madiwani, Halmashauri ya Kilombero, linatoa fursa sawa ya mgao wa miradi ya maendeleo katika kata zote ndani ya halmashauri hiyo.

Hivi karibuni safu hii ya ‘Ukweli Ulivyo’ ilitembelea Wilaya ya Kilombero na kuzungumza na Mwenyekiti wa Halimshauri hiyo, Daud Ligazio (CCM), wenyeviti wa kamati pamoja na madiwani wengine. Mazungumzo hayo yalijikita katika kuangazia miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Halmashauri Kilombero  kwa fedha za ndani ya halmashauri hiyo, fedha za wafadhili na fedha kutoka Serikali Kuu.

Ligazio alianza kwa kujitapa jinsi ambavyo ameweza kusimamia nidhamu katika baraza hilo analoliongoza.  Anasema kiini kikubwa kinachoweza kufanikisha mipango ya maendeleo ni nidhamu binafsi ya madiwani na nidhamu ya kusimamia fedha za maendeleo zitolewazo.

Ligazio anasema kuwa mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, alihakikisha kwanza anajenga mazingira ya madiwani kuwa na nidhamu ya hali ya juu, umoja, mshikamano na masikilizano.  Kauli inayoungwa mkono na Brasius Makao, Diwani wa Kata ya Uchindile (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili.

“Unajua hizi halmashauri zenye uwakilishi unaokaribiana idadi sawa kati ya chama tawala na upinzani, zina changamoto kubwa mno. Changamoto ya kwanza ni nidhamu ya madiwani.  Changamoto nyingine ni madiwani wa upinzani kuona kama vile wanaonewa katika kila jambo na mwisho ni ubinafsi na kujipendelea katika masuala anuai. Haya yote kwa ujumla wake hayapo hapa kwetu Kilombero.

“Nilianza na nidhamu.  Kwa kushirikiana na kamati ya maadili nimefanikisha hilo. Mpaka kufikia sasa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero ni wenye nidhamu mno. Pia nimefanikiwa kuwaunganisha na kuwa kitu kimoja licha ya tofauti kubwa za kiitikadi zilizo baina yetu. Na zaidi nimewafanya madiwani kupendana, kusikilizana na kusaidiana. Hili limeondoa dhana ya ubinafsi na baadhi kujiona kuwa ni wanyonge. Huwa pia sina mzaha na huwa mkali sana pale diwani yeyote wa chama chochote, au mtumishi yeyote wa ngazi yoyote, anapoonesha kukengeuka na kwenda kinyume na sheria, kanuni na taratibu. Kwa kufanya hivi miradi mingi ya maendeleo inakwenda vizuri na fedha za Serikali zinapita katika mkondo salama. Hayo yanadhihirishwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Tumepata hati safi,” anasema.

Miradi ya maendeleo

Ligazio anaelezea kuwa Halmashauri yake kwa kushirikiana kikamilifu na viongozi wa Serikali kwa ngazi mbalimbali, wamefanikisha kutekeleza miradi mingi ya kijamii katika kipindi kifupi walichokaa madarakani.

Akielezea miradi hiyo ya huduma za jamii, alisema wamefanikiwa kujenga  vyumba vya madarasa katika shule zilizokuwa zikikabiliwa na upungufu wa vyumba vya madasasa na kukamilisha idadi ya madawati iliyokuwa ikihitajika katika shule zote wilayani Kilombero.

Jumla ya Sh milioni 208 fedha za ndani zimetumika kukamilisha ujenzi huo sambamba na ununuzi wa madawati. Ligazio anasema kwa sasa hakuna upungufu wa madawati katika shule za Halmashauri ya Wailaya ya Kilombero na kwa kushirikiana na wazazi wamefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa kero ya upungufu wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.

Ligazio anaeleza changamoto wanayoipata katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo, kuwa ni baadhi ya wazazi kukataa kuchangia kwa kuwa wameaminishwa kuwa elimu bure. Hata hivyo, anasema kuwa madiwani katika kata zao wamekuwa wakiwaelimisha wazazi ili wafahamu kuwa pamoja na uwepo wa sera ya Elimu Bure bado wazazi wanatakiwa kuchangia iwe ni fedha au nguvu kazi katika kutekeleza miradi ya maendeleo shuleni.

Anaelezea changamoto ya upungufu wa walimu ambao anataja kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero katika shule zake za msingi na sekondari ina upungufu wa jumla ya walimu 788. Hivyo anaiomba Serikali kuifikiria halmshauri hiyo kwa hatua ya dharura kuwaletea walimu watakaokidhi idadi na mahitaji husika. Hata hivyo, anasema walimu waliopo licha ya uchache wao, wamejawa na ari kubwa ya kufanya kazi na wamekuwa wakitoa matokeo mazuri.

 Miradi ya barabara

Halmashauri kupitia Wakala wa Barabara Vijijini, Tarura na wahisani wa DIDF, inatekeleza miradi mingi ya barabara zinazounganisha kata na kata.  Ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na barabara zinazopitika wakati wote katika kata zote za Kilombero.

Ligazio anasema kuwa madiwani wapo makini mno kuhakikisha barabra katika kata zao zinajengwa na ziwe na uwezo wa kupitika katika misimu yote ya mwaka.

Huduma za afya na maji

Kuhusu huduma za afya, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo anasema, wana mipango madhubuti ambayo mingine ipo katika hatua za utekelezaji kuhakikisha huduma za afya katika Wilaya ya Kilombero inatolewa kwa kiwango kinachokidhi haja na mahitaji ya wanananchi. Akitolea mfano anasema kuwa tayari ujenzi wa vyumba vya upasuaji mdogo katika vituo vya afya, Mang’ula, Nyandeo na Mngeta unaendelea.  Kiasi cha shilingi milioni 500 zimetengwa ili kuweza kupanua huduma katika Kituo cha Afya cha Mlimba ambacho kinahudumia maelfu ya wakazi wilayani Kilombero.

Huduma za mama na mtoto zinatolewa katika zahanati zote kwa kiwango ambacho wananchi wanakifurahia. Madiwani katika kata zao wamekuwa ni chachu kubwa kusimamia huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma hizo.

Pia anaeleza kuwa kuwa vijiji 14 vimepatiwa maji safi, na mipango kabambe ya kusambaza huduma hiyo katika vijiji vichache visivyo na huduma hiyo iko mbioni na hivi karibuni, wananchi wa Kilombero watasahau adha ya upatikanaji wa maji kwani ni vijiji vichache mno vimesalia kupata huduma ya maji safi na salama.

“Dira yetu ni maendeleo, maendeleo hayana chama. Wote tunahitaji maendeleo ili kuepukana na adha za upatikanaji wa mahitaji ya lazima. Hivyo sisi kama madiwani, wawakilishi wa wananchi katika kata zetu, tunapigana kufa au kupona kwa pamoja kuhakikisha Kilombero inapiga hatua za maendeleo kwa kasi. Tunamuunga mkono rais katika kupambana na umaskini wa kipato na kusimamia rasilimali za nchi ziwanufaishe wananchi.

“Tunawahamasisha wananchi kuzalisha mazao ya kilimo na biashara na kufuga kitaalamu. Wataalamu wetu wa kilimo na mifugo wanatenda kazi zao kwa bidii. Tunajitahidi kuhakikisha kuwa pembejeo za kilimo zinawafikia kwa wakati.

Tunaamini kwa kufanya hivyo, Kilombero itazidi kupiga hatua kubwa za maendeleo. Madiwani Kilombero, ajenda yetu ni maendeleo tu,” anasema Ligazio.