Home Latest News Magavana wagawanyika usawa wa jinsia uongozini

Magavana wagawanyika usawa wa jinsia uongozini

2185
0
SHARE
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Wycliffe Oparanya, akisoma maazimio ya magavana ambayo wanataka yajumuishwe kwenye ripoti ya BBI

NA ISIJI DOMINIC

RIPOTI ya Building Bridges Initiative (BBI) tangu iwekwe hadharani na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga, mawazo mapya yameanza kuibuka.

Baadhi ya wanasiasa wanataka ripoti hiyo ipitishwe kama ilivyo huku Juni mwakani ikitengwa kama mwezi utakaofanyika kura ya maoni itakayopelekea Katiba kufanyiwa marekebisho. Kundi lingine la wanasiasa linataka Wakenya wapewe muda kupitia upya ripoti hiyo na kuifanyia maboresho.

Miongoni mwa kundi hili la pili la wanasiasa ni Naibu Rais, William Ruto ambaye amesisitiza umuhimu wa ripoti hiyo ya BBI kuendelea kuboreshwa zaidi kwa kuhakikisha mawazo ya kila mtu wanapata nafasi.

Wiki iliyopita mjini Naivasha, magavana, manaibu wao na wawakilishi wa mabaraza ya kaunti (MCAs) walikutana kwa siku mbili kuweka mawazo yao pamoja kuhusu ripoti hiyo ya BBI kabla ya kuwasilisha mapendekezo mapya kwa Rais Uhuru na Raila.

Viongozi hawa wawili walitarajiwa kuhudhuria kikao kilichoandaliwa na Baraza la Magavana (CoG), lakini ikashindikana dakika za mwisho jambo ambalo liliwafanya wanakongamano kuondoka huku wakinung’unika.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CoG ambaye pia ni Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya, alisema mapendekezo yao yatawasilishwa kwa viongozi hao wawili ili kujumuishwa kabla ya kufanyika kura ya maoni itakayosimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) nchini Kenya.

“Tumeshaandaa mapendekezo yetu na tutawasilisha Ikulu kwa Rais Uhuru na Raila,”alisema Oparanya huku akidokeza Raila alihudhuria kikao kupitia video na kuwaahidi mapendekezo yao yatafanyiwa kazi kwenye ripoti kabla ya hatua za kura ya maoni kuanza.

Katika mapendekezo ya awali kwenye ripoti ya BBI, suala la usawa wa jinsia limeainishwa ambapo kama kitapita, Wakenya watashuhudia jinsia tofauti katika nafasi ya ugavana na unaibu. Hii ni kumaanisha, endapo mgombea kiti cha ugavana atakuwa mwanamume, basi atahitajika kumteua mwanamke kuwa mgombea mwenza kwenye nafasi ya unaibu gavana.

Mjadala unadaiwa ulikuwa moto sana na ilibidi Mwenyekiti wa CoG, Oparanya, kuingilia kati. Gavana wa Kitui, Charity Ngilu, ambaye ni miongoni mwa magavana wachache wanawake, aliunga mkono mapendekezo ya awali akisema muda sasa umeshafika suala la jinsia kwenye nafasi za uongozi ukatekelezeka.

“Niliwasilisha suala hilo lakini wenzetu wengi wakiume ni wazito kuikubali. Ili sisi tuwe na nchi iliyoendelea, wanawake lazima wawepo kwenye meza ya maamuzi, sehemu ambayo rasilimali inagawanwa kwa sababu wao (wanawake) wanaunda idadi kubwa. Wanadai ni vigumu kumpata mwanamke ng’ang’ari kama mgombea mwenza,”alisema.

Wanaopinga mawazo ya Charity wengi wakiwa wanaume wanasisitiza hatua hiyo inaminya uhuru wa kupata mtu sahihi kwenye nafasi ya naibu gavana. Mfano, Gavana wa Migori, Okoth Obado, alisema hatua hiyo itawapunguzia nafasi ya kidemokrasia wakuu wa kaunti.

“Magavana wanapaswa kuwa na uhuru wa kuchagua naibu gavana. Hata kwenye nchi ambazo zimepiga hatua katika demokrasia kama Marekani, si lazima kisheria kuwa na mwanamke awe mgombea mwenza,”alisema Obado aliyeungwa mkono na magavana Kiraitu Murungi wa Meru na Wycliffe Wangamati wa Bungoma.

Utekelezaji wa usawa wa jinsia ni mtihani kiasi cha Jaji Mkuu David Maraga kumshauri Rais Uhuru kuvunja Bunge ambalo lilishindwa kupitisha sheria ya thuluthi mbili ya jinsia itakayopelekea idadi ya wanawake bungeni kuongezeka.

Wanaounga mkono sheria ya thuluthi mbili wanasisitiza si tu bungeni ambapo usawa wa jinsia unahitajika bali na nafasi zote za uteuzi serikalini. Hivyo basi mbali na kuwa na jinsia mbili tofauti kwenye nafasi ya gavana na naibu gavana, suala hilo limetakiwa pia kumwulikwa kwenye wadhifa wa juu zaidi kwenye uongozi wa nchi.

Ripoti ya BBI iliyozinduliwa mwishoni mwa mwezi uliopita imeainisha endapo gavana atakuwa mwanamume, sharti mgombea mwenza awe mwanamke lakini haijasema chochote kuhusu mgombea wa nafasi ya urais. Hapa pia wanawake na mashirika yanayotetea haki sawa kijinsia, wanataka mgombea urais amchague mwanamke kuwa mgombea mwenza.

Vilevile, wanataka kuona thuluthi mbili ya jinsia ikitekelezeka katika baraza la mawaziri na mahakamani ambazo ni mihimili ya serikali pamoja na bunge.

Mbali ni mjadala wa kuhakikisha kuna kuwa na usawa wa jinsia katika nafasi ya ugavana na unaibu gavana, mapendekezo mengine yaliyoibua mjadala mzito kwenye kikao cha CoG mjini Naivasha ni manaibu gavana kukabidhiwa majukumu ya kiutendaji.

“Ni lazima magavana wawe na uhuru wa kuamua ni majukumu yapi ambayo watawakabidhi manaibu wao,” alisema Gavana wa Bungoma Wangamati.

Ni dhahiri kikao cha Baraza la Magavana linaongeza idadi ya makundi ambayo yanataka ripoti ya BBI ipitiwe upya kuboreshwa zaidi kabla ya kufanyika kura ya maoni. Miongoni mwa mapendekezo ya CoG ambayo wamewasilisha kwa Rais Uhuru na rafiki yake kisiasa, Raila, ni kuruhusiwa kuchagua manaibu wao baada ya uchaguzi mkuu kuliko ilivyosasa ambapo wanahitajika wawe na wagombea wenza kwenye karatasi ya upigaji kura.

Uhuru ambayo magavana watapata katika kuchagua manaibu wao baada ya uchaguzi mkuu, utawafanya kuwa na nguvu ya kuwatimua. Kama hiyo haitoshi, wanataka ufafanuzi kuhusu vigezo vya uteuzi wa waziri mkuu na manaibu wawili kama hatua ya kuhakikisha kila jamii inajumuishwa katika utendaji wa serikali.

Katiba ya sasa ya Kenya, imetoa ukomo wa muhula wa ugavana ambapo kama ilivyo kwa urais anayetakiwa kuhuduma kwa mihula miwili ya miaka 10, ndivyo ilivyo kwa magavana. Hii inamaanisha magavana 22 ambao wanahudumu kwa muhula wao wa pili, wamezuiwa kuwania tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Magavana walikuwa na imani pendekezo la Raila la kubuniwa serikali tatu lingeweka matumaini yao hai ya kubaki kwenye siasa baada ya uchaguzi mkuu 2022. Katiba mpya inampa mamlaka rais kuongoza nchi na magavana kuongoza kaunti ambapo kaunti zipo 47. Hivyo hiyo serikali ya tatu ingehusishwa kubuniwa mikoa 14. Hata hivyo, katika ripoti ya BBI iliyowasilishwa mwishoni mwa mwezi uliopita, hilo pendekezo la serikali tatu lilitupiliwa mbali.

“Tuliweka matumaini yetu kuundwa kwa serikali tatu, lakini kwa bahati mbaya, hilo halikwepo kwenye ripoti ya mwisho ya BBI. Hivyo basi tutachukua fursa hiyo kutafuta hakikisho kutoka kwa wakuu wawili nini hatima yetu baada ya 2022 kama magavana wanaohudumu kwa muhula wa pili,” moja wa magavana anayemaliza muda wake alinukuliwa na chombo cha habari nchini Kenya.

Katiba iliweka wazi ukomo wa ugavana ili kuondokana na ukiritimba wa baadhi yao ambayo wanaweza kuingiwa na tamaa ya kujimilikisha raslimali za kaunti. Tayari Wakenya wameshuhudia baadhi ya magavana wakifikishwa mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi ikiwemo ubadhirifu hivyo kusingekuwa na ukomo magavana wenye nia mbaya watajimilikisha raslimali zote zinazopatikana kwenye kaunti zao.