Home Uchambuzi MAKONDA HAKUNA KULALA HADI KIELEWEKE

MAKONDA HAKUNA KULALA HADI KIELEWEKE

2690
0
SHARE

KATIKA muda wa zaidi ya wiki mbili sasa, jina ambalo limetawala katika kila kona ya nchi hii ni la Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Si tu kwamba jina hilo linasikika katika kila kona ya nchi, bali limekuwa ni sawa na ushabiki wa Yanga na Simba. Yameibuka makundi ya wanaomuunga mkono na wanaomkandia na hata wengine kupendekeza aondolewe. Ili mradi katika duru za mitandaoni gumzo ni Makonda na mihadarati.

Makonda amekuwa gumzo kwa sababu ya uthubutu wake tu na wala si kwa sababu ya kitu kingine chochote. Kwa miaka kadhaa sasa suala la mihadarati limekuwa likijadiliwa katika duru mbalimbali kote nchini. Na kwa miaka yote hiyo uthubutu umekosekana.

Mihadarati au unga kwa lugha ya mitaani ni janga ambalo lilianza kuinyemelea nchi yetu kuanzia tulipohalalisha soko huria na kuhalalisha kuwa si haramu hata kidogo.

Kitendo cha kuhalalisha watu kujitajirisha kilifungua milango ya kila aina ya ulimbikizaji mitaji, ikiwa ni pamoja na ulimbikizaji wa kutumia njia za haramu kama vile uingizaji, usafirishaji na usambazaji wa unga hapa nchini.

Tatizo la unga lilijichimbia kwa miaka kadhaa na kujijenga hadi kuwa janga la taifa kama ambavyo hivi sasa Makonda na kikosi chake cha waliojitoa muhanga wanavyotutaarifu.

Kwamba Taifa letu limekuwa katika tatizo kubwa la matumizi ya dawa za kulevya, si siri wala uvumbuzi wa akina Makonda. Hili lilikuwa likijulikana kwa muda mrefu na ndiyo sababu katika Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 ya CCM kuna sehemu inayozungumzia suala hilo kwa ahadi na maelekezo kwa Serikali.

Serikali iliyoingia madarakani iliazimia kutimiza ahadi iliyokuwapo katika Ilani ya CCM ya uchaguzi na ndiyo sababu vita hii inapiganwa hivi sasa.

Ni busara kujiuliza swali kwanini katika awamu zilizotangulia suala hili lilionekana kama vile ni kaa la moto ingawa kulikuwa na matamko mbalimbali yaliyoashiria kwamba huenda hatua zingechukuliwa?

Pamoja na kwamba si rahisi kulijibu swali hilo hapo juu, lakini ni vyema ikakumbukwa kwamba suala la dawa la kulevya ni mtambuka sana. Ni suala linalohusisha fedha nyingi sana. Ni biashara kubwa ya kimataifa.

Wanaofanya biashara ya dawa za kulevya si watu wa mchezo kwani wanayo nguvu kubwa kifedha. Tunazungumzia bidhaa ambayo katika soko la rejareja kilo moja inaweza kukupatia hadi zaidi ya dola laki moja kulingana na ubora wa bidhaa yenyewe.

Huko unakozalishwa unga huo (kokeni) huuzwa kama ifuatavyo: El Salvador $24 kwa gramu, Paraguay $20 kwa gramu, Costa Rica $17 kwa gramu, Guatemala $13.30 kwa gramu Brazil $12 kwa gramu, Haiti $10 kwa gramu, Venezuela $9.30 kwa gramu, Honduras $9.20 kwa gramu, Chile $8.80 kwa gramu, Dominican Republic $8 kwa gramu, Argentina $5.90 kwa gramu, Ecuador $5 kwa gramu, Peru $4.50 kwa gramu,  Bolivia $3.50 kwa gramu na Colombia $3.50 kwa gramu. (Takwimu za mwaka 2016 za Havocscope).

Bei za huko kunakozalishwa huo unga anaopambana nao Makonda na wenzake wanaoitakia heri nchi yetu ndiyo hizo. Unga huo unapogusa nchi za ughaibuni kama China na  Australia unapanda bei na kufikia hadi dola 300 kwa gramu, ikimaanisha kilo moja ni dola 300,000 yaani sawa na zaidi ya Sh milioni 660 kwa sasa!

Hizo takwimu ni muhimu ili kuelewa ni aina gani ya watu hao waliojifunga vibwebwe kupambana na mihadarati, wamedhamiria kupambana nao na ni kwa nini isishangaze hata kidogo kuona aina ya muhemuko ulioibuka baada ya suala hili kuwekwa hadharani na wananchi kutakiwa kushiriki kikamilifu.

Vita dhidi ya dawa za kulevya si lelemama. Hili analielewa Rais John Magufuli vizuri sana. Ni wazi kwamba hakuna mshiriki yeyote katika vita hii anayeamini kwamba anapigana vita nyepesi na kama yupo basi huyo hajui anapigana na adui mwenye uwezo mkubwa kiasi gani.

Adui ambaye Makonda amemkurupua huko alipokuwa ni tishio. Anao uwezo wa fedha wa kutisha. Anayo majeshi ya ndani na nje ya nchi. Ni majeshi ambayo yapo tayari kujitoa muhanga kwa sababu ya fedha.

Vita ya kupambana na uingizaji wa mihadarati ndani ya nchi yetu ni kubwa na ngumu kuzidi vita ya uvamizi wa majeshi yoyote yale. Hii ni vita inayozidi ile ya kulinda sehemu ya mpaka wa nchi yetu kwani vita ile ilituunganisha wote tukatupia macho katika kaeneo kadogo huko Kagera. Pamoja na ugumu wake, lakini iliwezekana kutokana na mshikamano uliokuwapo.

Vita ya safari hii ni ngumu zaidi. Adui yu miongoni mwetu. Ni mwenzetu. Adui anayeingiza nchini ni mtoto wetu. Ni mjomba. Anatulisha. Anatuvisha.

Vita hii ni ngumu kwa sababu anayetumia yaani soko pia ni mwenzetu. Tunaye ndani ya familia.

Ugumu unazidi kwa sababu anayefadhili usafirishaji ni mshikaji na msitiri wetu. Ni kiongozi wetu tena tunayemtetea kwa kila jambo kwa sababu ana uwezo wa kutosha wa fedha na kila tutakacho anatupatia na kwa maana hiyo tunaona upande mmoja tu wa shilingi.

Pia ikumbukwe kwamba dawa za kulevya zinazoingizwa nchini zipo katika makundi mawili. Kundi la dawa zinazopita njiani kwenda ughaibuni. Hizo hupitia tu hapa kwenda kule mbali kwenye fedha nyingi. Halafu kuna zile ambazo zinakuja hapa kwa ajili ya matumizi ya hapa nchini.

Wakati Makonda na wenzake wanaumia kuona jinsi familia zinavyosambaratika, baadhi yetu tunahangaika kulalama jinsi hadhi za watu zinavyoshushwa, si kwa kufungwa jela la hasha bali kwa kutajwa kwamba wanatakiwa kuisaidia polisi katika sakata hili la mihadarati! Ni kama vile kutajwa tu kwenda kuisaidia polisi basi kunakushushia hadhi yako kiasi cha kukosa usingizi. Kama hivyo ndivyo, ni busara kujiuliza tu kulikoni hadi ukaombwa kuisaidia polisi katika suala la mihadarati na si suala jingine? Kwanini kelele ziwe nyingi sana? Kelele zinatumika kama njia ya kuwanyamazisha na kuwatisha akina Makonda.

Hadhi ya mtu mmoja ni bora kuliko maisha ya mamia ya familia yanayoteketea kutokana na kuwa na waraibu chungu nzima wanaosababishiwa uraibu huo na hao ambao wanaombwa kuisaidia Serikali kupata suluhu ya tatizo hili kubwa. Inachosha kuona jinsi baadhi ya wasomi wetu wanavyokwepa kuzitazama sheria zote kwa pamoja na badala yake kudonoa hapa na pale ili kujaribu kuhalalisha maoni yao kwamba Makonda anafanya mambo kwa kutokufuata sheria. Tufike mahali tutambue kwamba hili Taifa ni letu wote na tukimwachia huyu mvamizi anayeitwa dawa za kulevya andelee, tujue hakuna familia itakayobaki salama. Tukumbuke tishio la ukimwi.

Hii ni vita ngumu sana kwa sababu wanaozalisha mihadarati huko Marekani ya Kusini, Afghanistan na Pakistan wanataka soko liwepo na kwa mantiki hiyo hii vita ni yao na watashiriki bila kupepesa macho.

Kumbeza Makonda na kumkejeli hakutusaidii sisi kama Taifa. Tatizo lipo, ni kubwa. Hii ni vita. Kutoshiriki ni usaliti. Hakuna lugha nyepesi zaidi ya hiyo.