Home Uchambuzi MAKONDA NA VIKARATASI VYA WAUZA “UNGA” KAMA KIKARATASI CHA BEN SAANANE

MAKONDA NA VIKARATASI VYA WAUZA “UNGA” KAMA KIKARATASI CHA BEN SAANANE

3350
0
SHARE

EWE Mkuu wangu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Naamini uliona ule waraka wangu mfupi. Nimesikiliza clip yako ukihamasisha vijana wathubutu bila woga na kwamba wewe umethubutu na huogopi (nadhani pia ni katika hivi vita vya kupambana na wanaojihusisha na dawa haramu za kulevya).

Kuthubutu ni jambo zuri na hayo maneno mimi nimeyatumia sana nilipokuwa naibu waziri wa kazi na ajira. Kila nikikutana na vijana nilikuwa nawataka wathubutu katika maisha na majukumu yao.

Kauli yako hii ya kuthubutu, ingawa ni nzuri, yaonekana wazi umeitoa ukiwaelekezea wanaokusakama kwenye vita hivi hadi unawaita mbwa mwitu wasiostahili kuogopwa. Unaona hawa watu wanauonea wivu uthubutu wako au hawajakuelewa. Unaamini wewe uko sahihi kabisa kwa namna ulivyoshughulikia jambo hili.

Lakini pia wako watu wengine ama kwa hisia za kisiasa tu au mihemuko wamekuwa wakidai kwamba wanaokushambulia kuhusu vita unavyoendeleza dhidi ya madawa ya kulevya, kwamba wanafanya hivyo kwa woga wao, chuki ama kutetea wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya. HAPANA! Walio wengi wako na wewe katika vita hivi isipokuwa wanakupinga kwa utaratibu unaotumia. Wanakupinga kwa hatua yako ya “kuokota” vikaratasi “mlangoni” na moja kwa moja kuitisha vyombo vya habari na kutangaza walioandikwa kwenye vikaratasi hivyo, kuwahusisha na madawa ya kulevya na kuwaita wakutane na wewe Polisi kwa mahojiano.

Sina haja ya kurudia masomo yaliyotolewa Jumapili na Askofu Gwajima na Mwanasheria Tundu Lissu namna ulivyoboronga na kukosea kwenye suala hili.

Watu wangetegemea kwamba baada ya “kuokota” vikaratasi hivyo ungevikabidhi kwa wataalam wa upelelezi wa madawa haya ili wayafanyie kazi, kwanza kimya kimya. Na baada ya kubaini nani mtuhumiwa wa kweli ndio hatua ichukuliwe kwa hao, na siyo wote kwa kuwa tu wameandikwa kwenye hivyo vikaratasi “vilivyookotwa”.

Na ukitaka kujua kwamba hivi vikaratasi vya “kuokotwa” (kama kile cha Ben Saanane kilichookotwa pale mlangoni Ofisi za Mwanahalisi) havikufanyiwa kazi angalia vilivyoandikwa nusu nusu na kwa makosa ya ajabu. Hivi unapotaja tu Hasadi wa Mbezi, au Kiboko wa Tegeta, au Kiiza wa Mwananyamala, au Misanga wa Tabata, hivi unajua Mbezi kuna Hasadi wangapi? Tegeta kuna Kiboko wangapi? Mwananyamala kuna Kiiza wangapi? Au Tabata kuna Misanga wangapi?

Vikaratasi hivi vingefanyiwa kazi “watuhumiwa” hawa wangejulikana majina yao kamili, mitaa na hata nyumba wanazoishi. Na baada ya hapo orodha iliyo kamilifu ingeandaliwa, na hivi vikaratasi vya “kuokotwa” visingewafikia hata waandishi wa habari.

Hivi unapochukua kikaratasi kilichoandikwa Philemoni Mbowe bila kujiuliza huyu aliyeandikwa hapa ndiye Freeman Mbowe ama aliyetupa karatasi “mlangoni kwako” alikuwa na maana ya mtu tofauti, halafu unasema jina lilikosewa, kweli? Kwa nini tusikubaliane na Freeman Mbowe kwamba hivi ni vikaratasi vya kufungia vitumbua na siyo vya upelelezi wa madawa ya kulevya?

Au unaandikiwa jina la Iddi Azan Zungu bila kulifanyia uchunguzi, huku ukijua kwamba kuna watu wawili tofauti, mmoja ni Iddi Azan na mwingine Azan Zungu. Nani hapo alilengwa? Unatoaje majina hayo hadharani kabla ya uhakiki?

Unapoletewa vikaratasi vimeandikwa mmiliki wa Slip Ways, au mmiliki wa Yacht Club, una hakika kuna mmiliki mmoja tu wa hoteli ya Slip Ways au Club ya Yacht? Majina kamili mbona hayakuandikwa? Unatoaje orodha hiyo kwa waandishi wa habari kabla ya kufanyia kazi na kupata majina yao kamili na kujiridhisha na uhusika wao kwenye madawa ya kulevya?

Lakini kubwa, watu wanaoleta vikaratasi hivyo, una hakika gani hawana nia mbaya na baadhi ya watu kwenye hiyo orodha kutokana tu na chuki, siasa, wivu au visasi? Kwanini usifanyie kazi kwanza kujihakikishia kwamba kweli hao wanaweza kuwa na kesi ya kujibu? Au na wewe kama walivyo hao walioleta vikaratasi hivyo, una chuki, visasi na wivu kwa baadhi ya watu humo kwenye orodha? Hivi kijana mwenzako, RC mwenzako, Gambo wa Arusha umemsikia alichosema kuhusu namna na utaratibu wa kuwataja wahusika wa dawa za kulevya mkoani kwake? Au unadhani wewe ndiye unajua kuthubutu kuliko Gambo na wengine?

Au kwa kuwataja watu na kuwapa muda wa kuja kuonana na wewe kituo cha Polisi ulitaka kuwastua wahusika halisi wapate muda wa kuficha ushahidi kwanza ili wasiwe na kesi Mahakamani?

Maswali ni mengi sana, lakini nimalizie kwa kusema: nia na dhamira yako RC Paul Makonda inaweza kuwa nzuri kuhusu vita hivi, lakini namna ulivyoshughulikia “watuhumiwa” uliowataja siyo sahihi. Haikufuata sheria. Ni ya kukurupuka. Ni ya kisiasa. Ni ya uonevu. Ni ya udhalilishaji. Ni ya visasi. Ni ya kitoto.

Ndio maana nawaunga mkono watu kama Freeman Mbowe, Yussuf Manji na Mchungaji Gwajima walioamua kukushughulikia kwa kutumia nguvu ya sheria na nguvu ya Roho Mtakatifu. Ngoja ushughulikiwe ili wakati mwingine ujifunze namna bora ya kuthubutu na kujiamini, mambo ambayo unayapenda lakini hujui namna ya kuyafikia.