Home Makala Mambo ya Nje ndiyo roho ya uchumi wa viwanda

Mambo ya Nje ndiyo roho ya uchumi wa viwanda

2203
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa si sehemu ya kupumzika kwa kusafiri huku na kule na kunywa mvinyo kama baadhi ya watu wanavyodhani.

Mchambuzi wa masuala ya Kimataifa, Abbas Mwalimu anauelezea ugumu na umuhimu wa wizara hii kwa Waziri,Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Wakurugenzi na hasa mabalozi hasa kwenye diplomasia ya uchumi.

Mwalimu anaweka wazi kuwa wizara ya Mambo ya Nje si sehemu ya kupumzika kwani inabeba roho ya nchi, inahitaji watu makini na ndio maana hata Hayati Mwalimu Julisu Nyerere aliiweka wizara hiyo chini yake kama ilivyo kwa Marekani ambao wanaiita Idara ya Ikulu (Department of State).

Akizungumzia kilichotokea hivi karibuni kwenye wizara hiyo kwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu kuondolewa, alisema zipo sababu za msingi zilizosababisha uamuzi huo na kwamba kilichofanywa na Rais Dk. John Magufuli ni sahihi kwa mustakabali wa nchi kwani wizara hiyo ndio lango kuu la kufanikisha uchumi wa viwanda nchini.

Aliweka wazi ili kuhakikisha mambo yanakwenda kwa weledi wizara hiyo inahitaji watu wenye weledi kwenye masuala ya diplomasia ama waliowahi kupita kwenye majeshi yetu ya ulinzi na usalama.

Alisema wanahitajika wataalamu wengi kwenye eneo la ushauri wa uchumi na watunga sera wazuri hasa za nje, lakini pia wanahitajika watekelezaji wabobezi wa sera hizo waliopikwa katika eneo husika kama kinavyopaswa kufanya chuo cha Diplomasia.

Mbali na hilo alifafanua kuwa ili tuweze kushindana kikamilifu nje ipo haja ya kuwa na balozi nyingi kama ilivyo kwa Kenya ambao wanazo balozi zaidi ya 150 na kuepukana na mfumo wa balozi mmoja kuhudumu kwenye nchi zaidi ya mbili jambo linalompa mzigo wa kufanya vizuri.

UTEUZI WA MABALOZI, NI JAMBO RAHISI?

Watu wengi tumekuwa tukisikia kuhusu mabalozi, lakini je tunawafahamu hawa mabalozi? Mabalozi ninaowalenga hapa si wale ambao tunasikia labda mwanamuziki fulani ameteuliwa kuwa balozi wa kinywaji fulani au bidhaa fulani la hasha.

Mabalozi tunaowalenga hapa ni wale ambao wanateuliwa na Marais au Wakuu wa Serikali au Wakuu wa Taasisi za Kimataifa.

Hivyo kwa tafsiri balozi ni;

“Mwakilishi anaetumwa na Mkuu wa nchi, Serikali ama taasisi ya kimataifa kwenda kumuwakilisha Rais, mkuu wa serikali au taasisi au nchi inayomtuma katika nchi inayompokea.”

Katika muktadha wa uteuzi wa mabalozi huwa kuna mabalozi wa aina mbili.

(1) Wanaoteuliwa kutokana na utashi wa kisiasa

(2) Wanaoteuliwa kutokana na weledi wao.

Hawa wanaoteuliwa kutokana na utashi wa kisiasa huwa ni pendekezo la Mheshimiwa Rais moja kwa moja.

Hawa wanaotokana na weledi ni wale ambao wametokea wizara ya mambo ya nje ambao huwa wanapatikana kutokana na career growth.

Kwa mfano katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania afisa huanzia ngazi ya:

Third Secretary

Hupanda kuwa Second Secretary

Baadae First Secretary

Baadae Minister

Na mwisho Minister Plenipotential.

Hii ni ngazi ya mwisho ya utumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ambapo baada ya hapo inatarajiwa mtumishi huyo kuweza kuteuliwa kuwa Balozi.

Hawa uteuzi wao hutokana zaidi na mapendekezo ya Wizara ya Mambo ya Nje.

NINI HUFANYIKA?

Kwanza mawasiliano ya siri hufanyika baina ya wakuu wa nchi ama serikali hizo mbili juu ya nia ya kumteua fulani kuwa balozi.

Ibara ya pili (Article 2) ya Mkataba wa Vienna unaohusu Mahusiano ya Kidiplomasia wa mwaka 1961 (Vienna Convention on Diplomatic Relations of 1961) imeeleza:

“The establishment of relations between States, and of permanent diplomatic missions, takes place by mutual consent.”

Kama ni mtarajiwa ametokana na kundi la kwanza la wale wanaotokana na utashi wa kisiasa kwa maana ya Mheshimiwa Rais kuona huenda mtu huyo atamfaa na baada ya kushauriana na timu yake ya ushauri, jina lake hupelekwa kwa kitengo ya uchunguzi ili kumfanyia vetting mtajwa huyo.

Wakati huo huo jina hilo huwa limefika katika idara za upelelezi za nchi hiyo pia kwa ajili ya wao pia kufanya vetting.

Hapo sasa kama mtu huyo alikuwa akiwaelezea vibaya nchi hiyo inayomchunguza nao lazima wamfanyie reciprocity.

Endapo watu wa uchunguzi watajiridhisha kwamba fulani anafaa kuwa Balozi watarudisha jina kwa Mheshimiwa Rais tayari kwa hatua zinazofuata.

Lakini kwa upande wa nchi ambayo jina hilo limepelekwa nao watakapokuwa wameridhika na mtajwa huyo baada ya kufanya uchunguzi wao wa kina wataridhia.

Kitendo hiki huitwa agremo/a

Hii imeelezwa kwenye ibara ya nne (Article 4) ya Vienna Convention on Diplomatic Relations:

  1. “The sending State must make certain that the agrément of the receiving State has been given for the person it proposes to accredit as head of the mission to that State.”

Endapo nchi inayotarajiwa kumpokea Balozi mtarajiwa itaona mtajwa huyo hawafai watafanya mawili kati ya yafuatayo:

(1) Nchi hiyo itatoa taarifa juu ya kutomkubali mtajwa huyo kuwa Balozi katika nchi yao.

(2) Nchi hiyo itakaa kimya bila ya kutoa taarifa yoyote.

Hii ya kutoa taarifa huwa haifanyiki sana badala yake nchi huamua kukaa kimya kama wanafalsafa wanavyosema, “Silence is an answer.”

Nini hufuata baada ya nchi ambayo Balozi anatakiwa kutumwa ikiamua kukaa kimya?

Nchi ambayo itakuwa imepanga kumtuma balozi huyo katika nchi hiyo itajua kabisa kuwa mtajwa huyu amekataliwa

Hii kwa lugha ya kidiplomasia tunaita persona non grata

Dola hilo linalotarajiwa kumpokea balozi halipaswi kueleza sababu za kumkataa Balozi huyo mtarajiwa.

Hii hubaki kuwa kazi ya dola ambalo limempendekeza Balozi huyo ama kutafutia nchi nyingine ama kumbakiza nchini mwao.

Ifahamike kuwa wakati huo huwa hakuna anayejua zaidi ya vyombo vya usalama, ofisi ya Rais na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje.

Maana yake hata huyo mtajwa anakuwa hajui kuwa yeye amependekezwa na anafanyiwa scrutiny.

Ingawa hutokea kuna baadhi huwa wanajua na kuanza kumdhihaki mwenzao kuwa fulani kakutana na persona non grata, lakini pia hali huwa mbaya pale muhusika aliyekuwa akijua kuwa alikuwa under scrutiny anapotajwa kuwa ni persona non grata

Kufahamu zaidi kuhusu hili tunaona kuwa limeelezwa pia katika ibara hiyo hiyo ya nne (Article 4):

  1. “The receiving State is not obliged to give reasons to the sending State for a refusal of agrément.”

Nchi hujuaje kama mtajwa amekataliwa?

Kuna kipindi ambacho dola likiona kimya kimetawala hujua kabisa mtajwa amekataliwa.

Inaelezea kuwa ikipita zaidi ya miezi mitatu na nchi mnayotarajia atumwe Balozi haijasema kitu mnajua kabisa kuwa wamemkataa,mnajipanga upya.

Inapotokea nchi hizo kwa pamoja zimeridhishwa na Balozi huyo mtarajiwa hatua nyingine hufuata.

Hapa ndipo jina la mteule huyo hutajwa kwa tangazo toka Ofisi ya Rais.

Kwa upande wa wale ambao hutokana na weledi yaani watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje au waliosomea Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia utaratibu wao ni kwamba majina hupendekezwa na Wizara na baadae kupelekwa kwa Rais kwa ajili ya utaratibu nilizoelezea hapo juu.