Home Makala Kimataifa Mapambano dhidi ya ufisadi Angola, Familia ya Rais wa zamani dos Santos...

Mapambano dhidi ya ufisadi Angola, Familia ya Rais wa zamani dos Santos itasalimika?

1928
0
SHARE

OTHMAN MIRAJI UJERUMANI

HAPO zamani Rafael Marques de Morais alipachikwa jina la “Haini“. Alisingiziwa kulifanyia kazi Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, alilaumiwa kwamba si mzalendo, ni mwendawazimu na mtu aliyechanganyikiwa.

Aliwahi kusimamishwa kazi huko kwao Angola, akapelekwa mahakamani mara kadhaa na hata kutupwa gerezani. Waliomfanyia yote hayo ni genge lililokuwa linamuunga mkono Rais wa zamani, Jose Eduardo dos Santos, aliyeitawala na kuipora Angola kwa miaka 38.

Angola ingekuwa nchi inayonawiri kwa neema. Ukiitoa Afrika Kusini hakuna nchi nyingine katika Afrika chini ya Jangwa la Sahara inayochuma fedha nyingi kama Angola- dola bilioni 40 kwa mwaka.

Ni miongoni mwa nchi 60 zilizo tajiri kabisa duniani. Hata hivyo, theluthi mbili ya wakaazi wa nchi hiyo kila mmoja wao anaishi kwa chini ya dola moja ya Kimarekani tu kwa siku.

Rafael de Morais, kama mwandishi wa habari na mwanaharakati, mara kadhaa aliandika juu ya namna mabilioni ya fedha za serikali zilivyotoweka, fedha zilizotokana na kuuzwa mafuta na gesi ya ardhi ya nchi hiyo.

Yeye anakadiria dola bilioni 640 zimepotea tangu mwaka 2002. Morais amefichua visa vingi vya ufisadi na rushwa, jambo ambalo lilipelekea akasirikiwe na genge lililowazunguka wakuu ndani ya serikali ya dos Santos. Tangu miaka miwili sasa Angola inatawaliwa na Rais mpya, Joao Manuel Lourenco, aliyetangaza kupambana dhidi ya rushwa na ufisadi nchini humo.

Mwisho wa mwaka jana rais mpya alimwalika mwandishi wa habari Morais kufanya naye mazungumzo. Walibadilishana mawazo kwa saa nne. Mwishoni Rais huyo alimtia moyo Morais atoe taarifa kwake baadaye atakapogundua kisa cha ufisadi serikalini.

Tangu wakati huo Morais, aliyepagazwa na wala rushwa wa zamani jina la “Adui wa Rais“ amebadilika na watu sasa wanamtania na wamempa jina la “Rafiki wa Rais“. Amegeuka na sasa anaangaliwa kuwa ni alama ya hali mpya ya mambo ambayo hadi hivi karibuni hakuna mtu aliyetarajia kwamba itaweza kuchomoza Angola.

Rais Lourenco tangu alipokamata usukani wa nchi amewaondosha kutoka nyadhifa zao serikalini na kutoka mashirika ya umma watu wa familia ya mtangulizi wake. Miongoni mwao ni Isabel dos Santos, binti wa aliyekuwa Rais dos Santos, aliyeiongoza kampuni kubwa ya mafuta ya serikali, Sinangol. Anajulikana kwamba ni mwanamke tajiri kabisa barani Afrika na katika miaka iliyopita amejitahidi kujionesha hadharani na mbele ya majukwaa ya kimataifa kwamba ni mfanyabiashara aliyefanikiwa kutokana na akili, uwerevu na ujasiri wake.

Amekuwa akialikwa katika vyuo vikuu vya Kimarekani kuwahutubia wanafunzi na kuwapa “mikoba“ juu ya namna ya kufanikiwa kibiashara na hasa namna ya kuendesha biashara ya mafuta.

Lakini katika mji mkuu wa Angola, Luanda, wanaharakati huvunjika mbavu kwa kucheka na wakati mwingine kumbeza Isabela kutokana na mihadhara yake hiyo anayoitoa ng’ambo. Wanashangaa! Kwani kila siku wanashuhudia vipi mali za Angola zinavyonyonywa na kuporwa, makampuni ya kimataifa yakishiriki katika wizi huo. Karibu watoto wote wa dos Santos wamekimbilia ng’ambo wakihofia kutiwa mbaroni na kushtakiwa nchini mwao kwa tuhuma za ufisadi.

Ushawishi wa Isabel mwenye umri wa miaka 44 ni mkubwa bado katika Angola. Mwenyewe bado anajigamba kwamba ni kijana na amezaliwa katika nafasi nzuri. Mali inayodaiwa anamiliki inathaminiwa kufikia dola bilioni tatu. Mara nyingi anawabishia watu wanaomlaumu, akidai kwamba licha ya yote yeye ni mchapa kazi kwelikweli na utajiri wake haujaja hivihivi tu au kwa urahisi.

Isabel alipofukuzwa na Rais Lourenco kazi ya kuwa mkuu wa Kampuni la Taifa la Mafuta, Sonangol, kuna watu ndani ya kampuni hiyo waliosheherekea wakidai kwamba binti huyo wa aliyekuwa rais alikuwa fisadi ndani ya mojawapo ya nchi zilizofurutu ada kwa ufisadi hapa duniani.

Isabel anamiliki hisa nyingi katika makampuni ya nishati na mawasiliano, za simu ndani na nje ya Angola, mabenki na vyombo vya habari pamoja na uzalishaji wa bidhaa, simu za mikononi na pia maduka makubwa ya Candamo.

Lakini propaganda za dola huko Angola zilimsifu Isabela kuwa ni mfanyabiashara wa kike anayeunda nafasi nyingi za ajira. Kuna watu wengine wanalaumu kwamba ukiritimba wake umezuwiwa kuundwa nafasi za ajira katika makampuni mingine.

Ukosefu wa kazi nchini Angola umefikia asilimia 25. Theluthi mbili ya wakaazi wa nchi hiyo hawajui kama jioni watakuwa na mlo wa kutia tumboni. Nchi hiyo inadaiwa kope si zake, licha ya kwamba ni mtoaji mkubwa wa mafuta na almasi.

Wakati wa Vita Baridi, pale baba yake- dos Santos- akiwa mpiganaji wa chini kwa chini akipambana na wakoloni wa Kireno, Isabela aliishi na mama yake- Tatiana Kukanova wa kutokea Azerbaijan- mjini London. Ndoa ya wazee wake ilivunjika. Isabela alirejea nyumbani Angola mwishoni mwa vita virefu vya ukombozi. Yeye ameolewa na Mkongomani Sindika Dokolo, wakiishi  Luanda, London, Lisbon  na mara nyingine Johannesburg.

Bado kuna watu wa kutosha wa genge la zamani lililokuwa madarakani ambao hawajali. Bado wanaendelea na shughuli za ufisadi. Wengi wao wanajiuliza: Mapambano haya ya Rais wa sasa dhidi ya ufisadi yatafikia umbali gani; na je kweli haya ni mabadiliko au ni kupapasapapasa tu? Kuna Waangola wanaoamini kwamba Rais Lourenco anakusudia kweli kufanya kile anachokisema. Lakini Morais anasema Rais huyo hawezi peke yake kuubadilisha mfumo mzima wa mafisadi na waharibifu unaomzunguka. Mafisadi hao ni wengi zaidi kuliko watu wanaomtakia heri Rais.

Tangu Angola ilipopata uhuru mwaka 1975 kutoka ukoloni wa Ureno, Chama cha MPLA (People‘s Movement for the Liberation of Angola) kimekuwa madarakani. Mwanzoni kilikuwa ni chama kilichofuata nadharia ya Karl Marx, kikisaidiwa na Urussi wakati wa Vita Baridi. Lakini hivi sasa hakuna ujamaa uliobaki ndani ya chama hicho. Sababu inaeleweka.

Dunia imebadilika na Angola nayo imebidi ibadilike. Inafuata upepo mkali wa ushindi wa mfumo wa masoko huru dhidi ya mfumo wa wa uchumi unaopangwa na serikali. Katika miaka iliyopita serikali imewekeza mabilioni ya fedha katika “maeneo maalumu ya kiuchumi na kibiashara“- mfano wa yale yanayoonekana huko China.

Wazo ni kwamba uchumi wa nchi hiyo, ambao asilimia 95 unategemea mauzo ya mafuta yake nchi za nje, ujitanue na kujiingiza katika sekta nyingine. Ni wazo zuri, lakini ubaya ni kwamba utekelezaji wake umekuwa ovyo.

Viwanda katika maeneo hayo mpya ya kiuchumi vimebakia havifanyi kazi kwa ufanisi au vinatoa bidhaa zisizokuwa bora na za bei ya juu. Mwandishi Morais anasema: “Wanahitajika washauri walio bora kwa ajili ya marekebisho ya uchumi ambao bado uko mikononi mwa makada wa zamani.“ Hivi sasa Rais anapanga angalau kuyabinafsisha makampuni mengi ya umma ambayo yaliwafaidisha tu mafisadi wakubwa serikalini.

Pia Kampuni kubwa ya mafuta ya serikali, Sonangol, litagawanywa. Hapo kabla lilikuwa linafanya kila kitu-kupanga bei ya mafuta, kutoa haki ya kutafuta mafuta, kutoa vibali vya kuchimba na yenyewe kuchimba na kuuza mafuta.

Kwa miaka mingi Isabel dos Santos alikuwa anaiongoza Sonangol na matokeo yake yanaonekana na nchi hiyo hivi sasa. Kutokana na kuendeshwa ovyo uchumi na wakuu kushughulikia tu kujitajirisha wenyewe, kulisahauliwa kuyaendeleza maeneo mapya yalikogunduliwa mafuta.

Nchi hiyo iliyokuwa hapo kabla tajiri wa kutoa mafuta sasa imerejea nyuma. Inatoa tu milioni 1.4 kwa siku badala ya milioni 1.9 ilivyokuwa kabla. Mwaka 2027 Angola inatarajiwa itatoa mapipa 0.8 tu kwa siku. Karibuni serikali inatarajiwa kuzipiga mnada haki mpya za kuchimba mafuta.

Kwa muda mrefu uchumi wa Angola ulikuwa ukipanda kwa haraka sana pale bei ya mafuta katika masoko ya dunia ilipopanda hadi kufikia dola 100 kwa pipa. Sasa imeshuka chini ya dola 70, hivyo uchumi wa Angola imepigwa kabari. Nchi hiyo inabidi ikope ng’ambo. Peke yake China inaidai Angola dola bilioni 50.

Rais mpya amezungukwa na hali ngumu. Kama ataweza kuishinda mikiki ya “vikaka“ wa zamani ambao bado wamo ndani ya serikali yake na wanaomuona Morais bado ni “adui wa Taifa“ ni jambo ambalo mtu hawezi kulitilia dau. Angola si nchi masikini tu kiuchumi, lakini si masikini pia wa viongozi wake kupikiana majungu na kutiliana fitina. Uhondo wa kuongoza ni mkubwa sana katika nchi hiyo na kila mtu anaurandia.