Home Latest News Mapambano dhidi ya ujangili, wanawake wakataa kubaki nyuma

Mapambano dhidi ya ujangili, wanawake wakataa kubaki nyuma

2596
0
SHARE
Watalii na magari wakipitisha miguu yao kwenye maji ya dawa kabla ya kuingia hifadhini, lengo ni kuzuia maambukizi ya magonjwa kwa wanyama.

NA MWANDISHI WETU, ALIYEKUWA THAILAND

KASI ya mwanamke kushiriki katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na ulinzi imeonekana kushika kasi baada ya kuwapo kwa kundi la wanawake walio tayari kushiriki kwenye mapambano dhidi ya ujangili. Thailand ni moja ya nchi zilizowapa nafasi wanawake kushiriki katika mapambano hayo, nchi hiyo imeweka mikakati ya kuzishirikisha jamii kuanzia ngazi ya chini. Lengo kuu la hatua hiyo mbali ya kushiriki kwenye vita dhidi ya ujangili, lakini pia kuhakikisha rasilimali zilizopo zinaboresha maisha ya wananchi, hasa wale waishio kando kando ya Hifadhi za taifa.

Hayo yalidhihirika katika mahojiano yaliyofanywa waandishi wa Habari za Mazingira kutoka Tanzania waliofanya ziara maalum nchini Thailand kwa nia ya kujifunza masuala ya uhifadhi kwa vitendo kupitia programu maalumu iliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la RTI chini ya ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID-Protect).

Sarmon Sansthong ambaye ni mwanachama wa Kui Buri Wildlife Ecotourism Club, anasema kuwa yeye pamoja na wenzake wanafaidika sana na namna wanavyoshirikishwa katika masuala ya Uhifadhi wa wanyamapori kwa ujumla.

Sansthong alieleza kwa kina namna ambavyo wanashirikiana katika kutunza mazingira na kupambana na ujangili wa wanyamapori.

“Sisi hatujaajiriwa moja kwa moja na hifadhi lakini tunashirikiana na hifadhi kwa karibu haswa katika kuwatembeza watalii, lakini pia tunatumia magari ambayo tunagawana na madereva kiasi tunachokipata na kingine tunakiweka kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kikundi.”

Kama wanakikundi wanamiliki magari na watalii wanawalipa wao moja kwa moja. Aliongeza kuwa, “Watalii tunawatoza shilingi 850 za Thailand (ambazo ni sawa na shilingi 64,000 za Tanzania), katika pesa hizo shilingi 500 hupewa dereva, mtembeza mgeni hupata shilingi 170, shilingi 130 hupelekwa kwenye hifadhi lakini pia shilingi 50 hupelekwa kwenye kikundi kwa ajili ya uendeshaji.”

Sansthong alisema kuwa wao wanamiliki mashamba ya mananasi nje ya hifadhi na wanafanya kazi zote za hifadhi bila kubaguliwa kama wanawake na anasisitiza kuwa hali iko hivyo kwasababu na wao wamuonyesha umma kwamba wanaweza. Kama ilivyo katika shughuli nyingine kuwa hazikosi changamoto, wao nao wanaitaja lugha kuwa ni changamoto kubwa kwao kwani huwapatia wakati mgumu kuwasiliana na wageni ambao wanatoka katika mataifa mbalimbali.

Akizitaja changamoto wanazokumbana nazo Sirinton Yai-in ambaye pia ni mwanakijiji kando kando ya hifadhi alisisitiza kuwa bado wanaathiriwa na tembo kwenye mashamba yao ya mananasi.

“Lakini sisi kupitia kikundi chetu tunajitolea kuwalinda na kuwafukuza tembo hao bila kuwadhuru na ikitokea wametushinda nguvu basi huwa tunawaarifu wataalamu kutoka katika Hifadhi kwa msaada zaidi,” alisisitiza Sirinton Lakini pia kwenye kukabiliana na ujangili huwa tunahakikisha tunafanya ulinzi na tuko makini kwa kila kinachotokea katika ndani na nje ya hifadhi hii ya Kui Buri.

Faida kubwa wanayoipta ni kuwatembeza watalii mbugani, huduma za usafiri lakini kuwauzia matunda watalii kama vile madafu na mengineyo.

Anaongeza kuwa kundi lao hilo lenye watu 130 na zaidi ya nusu yao ni wanawake wanaotoka katika vijiji vitatu na ambalo limekuwa likifanya kazi kwa miaka 13 sasa, kama wanachama licha yakujipatia kipato kupitia hifadhi, huwa wana utaratibu wakujitolea kuwapeleka hifadhini wanafunzi wenye umri kuanzia miaka 15 ambao huwafundhisha kwa vitendo masula mazima ya utunzaji mazingira, umuhimu wa kuwajali na kuwatunza wanyama lakini pia kuwaelimisha namna ambavyo wataweza kushiriki katika kuendeleza na kuukuza utalii wa nchi yao.

Pamoja na hilo bado katika nchi ya Thailand biashara ya biadhaa zinazotokana na wanayapori bado ni kubwa na ni ya halali jambo ambalo kwa namna moja ama nyingine linaendelea kuchochea uwapo wa ujangili dhidi ya wanyama hao.

Matumizi ya Pembe za ndovu nchini Thailand Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na USAID Wildlife Asia juu ya matumizi ya pembe za ndovu nchini Thailand, takwimu zinaonesha kuwa kati ya idadi ya watu waliopo, asilimia mbili ya watu hao wanamiliki au wanatumia bidhaa zinazotokana na pembe za ndovu na hawa ndio wanaoifanya biashara hii iendelee kuwepo.

Pia inaonesha kuwa wanunuzi wa biadhaa hizo ni wale wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea na wengi wao wakiwa ni wafanyabiashara huku wateja wao wakubwa wakiwa wanawake.

Na asilimia 90 ya watu wa Thailand hawaoni tatizo la kwanini wasinunue bidhaa hizo lakini pia utafiti unaonyesha kuwa kadri siku zinavyozidi kwenda wanunuzi wanaendela kuongezeka na watafikia hadi asilimia 69 na haswa vijana wale wa miaka 25 hadi 29.

Naye Prof. Ekarin Pungpracha ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Silpakorn, Kitivo cha Kumbukumbu, anasisitiza kuwa sababu kubwa inayowafanya wanunue bidhaaa hizo zinazotokana na wanyamapori ni kutokana na imani kuwa zinaleta bahati, kulinda amani na wengine hutumia bidhaa hizo kama tiba ya asili kama vile kuongeza nguvu za kiume na maradhi mengine.

Anaongeza kuwa pamoja na hilo bado wapo raia ambao hawaelewi kama bidhaa hizo ni halali au la lakini pia hawana hakika kama ndizo zenyewe zinatokana na wanyama kama vile tembo na wengineo ama ni feki kwa maana ya kwamba wanatapeliwa na wauzaji hivyo kuuziwa kama mapambo tu. Hata hivyo, kulingana na sheria inayohusu meno ya tembo nchini Thailand, biashara ya pembe za ndovu nchini humo ni halali isipokuwa ni haramu kwa pembe za ndovu kutoka barani Afrika.

Arnold Sitompul, Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Mfuko wa Dunia wa Kuhifadhi Mazingira (WWF) nchini Thailand anaongeza kuwa kwa Thailand si tu biashara hiyo kuwa ni halali bali hata kummiliki tembo nyumbani kwako pia inaruhusiwa kikubwa tu mtu apate kibali rasmi.

Kwa upande wa Tanzania, jamii zinazoishi kando ya Hifadhi zinashirikishwa kikamilifu kupitia Jumuiya zaUhifadhi za Jamii (WMAs).

Miradi hii ya jumuia za hifadhi za wanayama pori za jamii inahusisha kwa kiwango cha juu ushiriki wa jamii na umiliki wa mradi, kwa lengo la ufumbuzi endelevu wa jamii katika kupunguza changamoto za migongano na wanyamapori .

Jamii hizi zimekuwa zikizuia migogoro baina ya Tembo na binadamu kwa muda mrefu na mpaka sasa zimepata uzoefu mkubwa katika kupunguza uharibifu wa mazao unaosababishwa na wanyamapori hususani Tembo lakini pia kuutokomeza uajangili wa wanyamapori.

Vilevile, kutokana na ukweli kwamba matukio mengi ya ujangili na ukataji wa miti, ambao kwa kiasi kikubwa wahusika ni wakaazi wa maeneo ya jirani kwa kushirikiana na majangili kutoka maeneo ya mbali, kumekuwa na jitihada kadhaa zinazofanywa na mamlaka zinazohusika moja kwa moja na hifadhi, hasa za wanyamapori za kuanzishwa kwa mtandao wa ujirani mwema, ambao unawahusisha wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi.

Kwa mujibu wa Mhifadhi wa Ujirani Mwema wa hifadhi ya Taifa Ruaha, Moronda B. Moronda, Ujirani Mwema ni mpango wa kuwafikia wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi kutoka ngazi ya kijiji hadi wilaya ili kushirikiana nao katika uhifadhi.

“Miradi ya ujirani mwema inalenga kusaidia jitihada za jamii katika kuboresha na kuimarisha maisha salama, kuboresha uhusiano katika maeneo ya wanyamapori na maisha ya wananchi, kukuza na kuendeleza miradi rafiki na mazingira lakini pia kukuza uelewa wa jamii katika athari zitokanazo na mazingira,” alisisitiza Moronda John Chikomo ambaye ni Mkurugenzi wa Chama Cha waandsihiwa Habari za Mazingira Tanzania (JET) anasisitiza kuwa katika kuunga mkono juhudi za utoaji elimu ya masuala ya uhifadhi, JET kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani USAID chini ya mradi wake wa PROTECT kimeiona haja na umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii juu ya masuala ya uhifadhi.

“Tumekuwa tukitoa mafunzo haswa kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo ili wafahamu jinsi ya kuandika masuala yote yanayohusu uihifadhi na hifadhi zenyewe na tumefanikiwa kwa hilo kwa kiasi kikubwa kwani habari za uhifadhi zinaibuliwa kwa wingi na mengi tunayaona yakifanyiwa kazi,” alisema Chikomo Bila kusahau kuanzishwa kwa Asasi ya kiraia kama vile Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) ambao dhumuni lake ni kuwapa wanakijiji haki ya kumiliki ardhi, kuandaa mpango kazi wa kijiji wa matumizi ya ardhi na kuimarisha uwajibikaji wa jamii katika taasisi za kijiji na wanajamii, na kukuza uelewa wa umuhimu juu ya usimamizi mzuri wa misitu na Serekali.

Dhumuni lingine likiwa ni kutambua na kusaidia jamii inayoishi karibu na misitu katika kuimarisha maisha yao kwa kupitia programu mbalimbali, kukuza uelewa kwenye maendeleo endelevu na usimamizi wa misitu ya asili Tanzania Bara kupitia tafiti, mafunzo, semina, uhamasishaji wa kimtandao, na kuwajengea uwezo wa kimaendeleo taasisi zinazo simamia misitu, kama washiriki wa MJUMITA pamoja na washikadau wengine.

Hitimisho Usimamizi kamilifu wa hifadhi za wanyamapori unatokana na maadili ya ausimamizi ambao unazingatia ushirikishwaji wa wahusika wote katika kupanga na kutekeleza mipango ya usimamizi na utumiaji rasilimali na mazingira kwa uwiano na uendelevu.