Home kitaifa Maswali kwa wakuu wa nchi za SADC

Maswali kwa wakuu wa nchi za SADC

1234
0
SHARE

Na DK. HELLEN KIJO BISIMBA

WIKI hii Tanzania ilianza kupokea ugeni mkubwa kutokana na uwepo wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambapo Agosti 5 mwaka huu Rais John Magufuli alizindua mkutano huo utakaohitimishwa Agosti 18 mwaka huu.

Mkutano wa wakuu wa nchi hizo, hufanyika mara moja kila mwaka katika miezi ya Agosti au Septemba. Mkutano huo hutanguliwa na mikutano mingine ya maandalizi kama vile ya kamati mbalimbali zikiwemo za fedha, kamati ya utendaji na hata mkutano wa baraza la mawaziri wa SADC.

Mkutano huu ni mkubwa na kwa mara ya mwisho ulifanyika hapa nchini mwaka 2003 wakati Rais akiwa Benjamin William Mkapa.

Nimeona maandalizi kemkem ya mkutano huo ikiwemo usafi, matangazo ya kuwasaidia watanzania kuuelewa mkutano huu na faida zake wakati ukiendelea kuwemo nchini.

Nimesikia hata Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwatahadharisha wananchi wa mkoa huo kuwa wasafi kiasi kwamba mtu anaweza kuzuiliwa kuingia mjini iwapo ataonekana kuwa mchafu. Haya yote yanaonyesha kiasi ambacho mkutano huo ulivyo muhimu na mkubwa.

Ninajua si watu wengi sana wanaofuatilia mikutano ya aina hii kwa hapa nchini na hata wanaofuatilia wana mrengo wanaouangalia. Matangazo mengi niliyobahatika kuyaona yanaonyesha kuwa zipo fursa za biashara kwa uwepo wa mkutano huu, hivyo watu waangalie wanavyoweza kuziteka fursa hizo. Yapo masuala ya kiusalama ambayo nayo ni muhimu sana kusisitizwa ambapo pia nimeyaona.

Nilipata kufuatilia mikutano ya aina hii iliyopita ambayo wa mwisho ulikuwa ni mkutano wa 38 uliofanyika Windhoek nchini Namibia ambapo mwenyekiti wake alikuwa Rais wa Namibia, Hage Geingob aliyepasiwa kijiti na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Kwenye mkutano huo pamoja na mengi yaliyoendelea itifaki ya SADC kuhusu jinsia na maendeleo ilifanyiwa marekebisho.

Katika marekebisho hayo moja ya mambo muhimu yaliyorekebishwa ni suala la mabadiliko ya tabia nchi na haki za watoto wa kike na hasa suala la ndoa za utotoni.

Katika itifaki hii Ibara ya 8 inaagiza kuwa hakuna mtoto aliye chini ya miaka 18 atakayeolewa. Tanzania ni moja ya nchi zilizotia saini itifaki hii na hadi sasa itifaki hii iliyorekebishwa imeshaanza kutumika kwani nchi zaidi ya robo tatu zimeikubali itifaki hii.

Kabla sijauliza maswali kwa wale wahamasishaji wa mkutano huo na hasa watendaji wa serikali yetu na hata serikali na nchi nyingine za SADC katika suala hili, napenda ifahamike kuwa SADC haifanyi kazi zake ikiwa kisiwa inaongozwa na mifumo ya kikanda na hata kimataifa kama Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063,  Malengo ya Maendeleo Endelevu kufikia mwaka 2030 ya Umoja wa Mataifa na  Mpango wa Beijing na vinginevyo.

Wakati tunaufurahia mkutano huu kuwepo nchini kwetu na kuwa Rais wetu ndiye atachukua uenyekiti tutazame eneo hili la jinsia na kuona kwa kiwango kipi sisi kama nchi tumepiga hatua na tuna uwezo wa kuhoji nchi nyingine zitakazokuwepo katika mkutano huu, pamoja na sisi kama nchi kuonyesha mfano kwa jinsi tulivyo.

Najua mada kuu zimekuwa kwa miaka kadhaa zikihusu masuala ya viwanda kama mada kuu ya mkutano wa 38 iliyokuwa ‘kuzidi kuendeleza viwanda na kuharakisha miundombinu itakayowezesha uwepo wa viwanda na umuhimu wa kushirikisha vijana ambao ndio wengi katika nchi hizi za SADC’.

Pamoja na mada hii, suala la kurekebisha itifaki ya jinsia lilikuwepo kwani ni suala mtambuka na linaweza kuathiri kwa ukubwa ufikiwaji wa malengo hayo ya uwepo wa viwanda kama lisipoangaliwa vizuri.

Mwaka huu pia naona mada kuu inahusu ‘mazingira mazuri yanayowezesha maendeleo endelevu ya viwanda, kukuza ushirikiano wa biashara na kuzalisha nafasi za ajira’.

Hizi mada zote ni bora kabisa lakini hii jumuiya ya SADC inapaswa kuendeleza na kusimamia yale iliyojifunga nayo katika itifaki na mikataba iliyojiwekea.

Ukiangalia hii itifaki iliyorekebishwa ina nia ya kukuza usawa na haki kijinsia, kukuza uwezo wa wanawake, kuondoa ubaguzi na kuendeleza usawa na haki kwa kuhakikisha zipo sera, sheria, mipango na miradi itakayowezesha hayo.

Zipo nchi za SADC ambazo hazikuweza kutia saini mkakati huo kwa vile bado zinakubali ndoa za utotoni katika sheria zake. Tanzania ni nchi iliyosani itifaki hii lakini ina sheria inayoruhusu mtoto wa chini ya umri wa miaka 18 na hasa msichana kuweza kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 kwa ruksa ya mzazi na mtoto wa miaka hadi 14 aweza kuolewa au hata kuoa kwa ruksa ya mahakama.

Hili suala ni kinyume kabisa na itifaki hii na hata lengo la 5 katika yale Malengo Endelevu ya Milenia ambalo hili nalo linahusu kukuza usawa na kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake.

Yote haya yanasisitiza kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kama vile ukatili wa majumbani, ndoa za kulazimishwa, ndoa za utotoni na mila zote hatarishi.

Ndoa za utotoni zimeonekana jinsi zinavyoweza kufifisha maendeleo ya kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi. Na vifo hivyo vinapunguza uwepo wa watu wanaolegwa katika maendeleo hayo endelevu.

Wakati tunajipanga kushiriki mkutano huu mkubwa na kuupokea uenyekiti, hebu tujihoji kama nchi kwanini tuko katika kushikilia uwepo wa ndoa za utotoni kiasi cha kupinga uamuzi mzuri uliotolewa na Mahakama yetu Kuu iliyoirahisishia serikali kuondokana na adha hii ya kuwa na sheria inayokwenda kinyume na ukubali wake katika SADC na hata Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wa kulinda haki za mtoto wa kike.

Iwapo swali hili litatujia kama waandaji wa mkutano huu na nchi ambaye Rais wake atauchukua uenyekiti tuna majibu gani mazuri ya kuieleza dunia fahari tuliyo nayo ya kuona watoto wakiingia kwenye ndoa.

Licha ya hili la ndoa za utotoni, pia tuna maswali katika suala zima la kijinsia hasa masuala ya uzazi wa mpango na kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto majumbani na hata sehemu za umma.

Nimeona kichwa cha habari kwenye moja ya magazeti hapa chini  kilichosema, inaonekana nyumbani si sehemu salama tena kwa wanawake na hata watoto, kutokana na matukio ya waume kuua wake zao, watoto kuuwawa na wazazi n.k.

Haya si mambo madogo ni makubwa ya kuyaangalia kama nchi wakati tukijinafasi kwa fursa zilizopo kwa uwepo wa mkutano huu.

Nina imani patakuwepo mikutano  sambamba ya AZAKI ambayo inaweza kuwa na warsha zitakazoibua masuala mbadala yakiwemo masuala yanayoendana na mada kuu lakini pia yanayohusiana na makubaliano ya jumuiya hii katika maeneo yote yakiwemo ya haki na usawa wa binadamu na zaidi wanawake na watoto ambao wameendelea kuingia matatani kutokana na mifumo, sheria na hata tabia walizo nazo wana jamii dhidi yao.

Nchi zote wanachama ziulizwe hali yake kisheria na kitabia katika kuendeleza yaliyomo kwenye itifaki hiyo ya jinsia. Waliofanya vizuri wawasaidie hao wanaositasita. Uwepo wa mkutano huu ukuze fursa si za biashara tu na usafi bali na ulinzi wa aina zote ikiwemo ulinzi wa haki na usawa.