Home Latest News Mgogoro wa Zanzibar na kisa cha chui na mwanakondoo

Mgogoro wa Zanzibar na kisa cha chui na mwanakondoo

3684
0
SHARE

Dk. Ali Mohamed SheinELIAS MSUYA

TANGU uchaguzi wa Zanzibar ulipofutwa Oktoba 28 mwaka huu, jitihada nyingi zimefanyika kusuluhisha vyama vya CCM na CUF vinavyovutana.

Mapema baada ya uchaguzi huo kufanyika mgombea wa CUF ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alitangaza kuwa ameshinda uchaguzi huo kulingana na fomu alizokusanya kutoka vituoni akisema amepata kura 200,007 dhidi ya kura 178,363 za mgombea wa CCM anayetetea nafasi yake, Dk. Ali Mohammed Shein.

Japo hatua hiyo ililaumiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), lakini Maalim Seif alijiweka salama dhidi ya njama zozote ambazo zingeweza kufanywa na CCM ili kumpora ushindi wake.

Tangu wakati huo, CCM Zanzibar wamekuwa wakisisitiza kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa madai ya kuwepo kwa kasoro kwenye uchaguzi wa awali. Lakini CUF nao wamepinga kurudiwa kwa uchaguzi huo wakidai kuwa wameshinda.

Hivi karibuni wameendelea kusisitiza kudurudiwa kwa uchaguzi huo baada ya mazungumzo ya muda mrefu na CUF yanayoonyesha kutozaa matunda.

Maalim Seif ameshakutana na kwenye vikao vya faragha na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na marais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, Amani Abeid Karume na Ali Hassan Mwinyi.

Alishakutana pia na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Rais John Magufuli. Mazungumzo yote yamefanywa kwa siri, lakini hadi sasa inaonyesha suluhu haijapatikana.

Inawezekana katika mazungumzo hayo wamekuwa wakimshinikiza Maalim Seif akubali kushindwa ili Dk. Shein aendelee kutawala muhula wake wa pili jambo ambalo halikubaliki.

Tangu mwanzo CUF wamesisitiza kushinda uchaguzi huo na hakuna kurudi nyuma. Kama ni kuwavumilia CCM, CUF wameshavumilia vya kutosha.

Tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, CUF walidai kuporwa ushindi wao na madai hayo yalikwenda mbali hadi wawakilishi wake wakasusia vikao vya Baraza la Wawakilishi, hadi ulipoanza mwafaka wa kwanza uliosimamiwa na Jumuiya ya Madola mwaka 1999.

Mwaka 2000 hivyo hivyo, CUF waliendelea kudai ushindi wao dhidi ya CCM. Madai hayo yalisababisha maandamano ya mwaka Januari 2001 yaliyosababisha mauaji na wakimbizi kutoka kisiwa cha Pemba kwenda Mombasa nchini Kenya.

Mwaka 2005 ikawa hivyo hivyo, lakini angalau mwaka 2010 Rais Amani Karume akabadilisha Katiba na kuruhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Maalim Seif akakubali kuwa Makamu wa kwanza wa Rais chini ya Dk. Shein.

Sasa mwaka huu tena uchaguzi umefanyika, taratibu zote zimefanyika vizuri, waangalizi wa kitaifa na kimataifa wakatoa taarifa ya awali iliyoonyesha uchaguzi ulikwenda vizuri. Lakini ZEC iliponusa ushindi wa CUF ikafuta matokeo!

Kila siku ni mazungumzo tu. Mazungumzo ya nini wakati mmeshindwa uchaguzi? Ifike mahali nyeupe iwe nyeupe na nyeusi iwe nyeusi, CCM ikubali kushindwa maana huo ndiyo ushindani.

Madai ya CUF kushinda yanaungwa mkono na matokeo ya wawakilishi kila unapofanyika uchaguzi. CCM hawana mwakilishi yoyote kisiwani Pemba, wanategemea tu Unguja ambako pia CUF hupata wawakilishi.

Vilevile kumekuwa na malalamiko kuwa CCM wamekuwa wakitumia majeshi ya Muungano na ya Zanzibar kuibeba kwenye uchaguzi kwa kupiga kura na mbinu nyingine chafu.

Baada ya mazungumzo yaliyokuwa ya siri kufanyika kwa muda mrefu, inaonekana mambo yamegoma ndiyo maana CCM inajipanga kurudiwa kwa uchaguzi ili ikiwezekana mbinu chafu zifanyike.

Hii inanikumbusha kisa Chui na Mwanakondoo. Chui alikuwa akinywa maji upande wa juu wa mto na mwanakondoo akinywa maji upande wa chini wa mto huo.

Chui akamuuliza mwanakondoo, ‘mbona unachafua maji ninayokunywa?’ mwanakondoo akajibu, ‘wewe ndiye unayenichafulia maji maana uko juu na mimi niko chini’.

Chui alipoona amekosa hoja katika hilo, akaibua swali lingine; ‘Mbona bibi yako alinitukana?’ Mwanakondoo akajibu, ‘wakati bibi anakutukana, mimi sikuwepo’. Chui alipoona amekosa hoja, akaamua kutumia nguvu kwa kumrukia mwanakondoo na kumrarua.

Hivyo ndivyo CCM wanavyotaka kufanya. Wamejaribu kila mbinu ya kupindua matokeo lakini wameshindwa. Wamefanya mazungumzo ya faragha, imeshindikana, wamefanya vitisho imeshindikana. Sasa wanataka kutumia nguvu kurudia uchaguzi ili wajihalalishie ushindi hata kama wapiga kura wataamua vinginevyo.

Huo ni ubabe uliozoeleka na umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu. Serikali ya CCM imeshazoea kutumia mabavu kushinda uchaguzi.

Bahati nzuri safari hii, jumuiya ya kimataifa imeshanyoosha kidole chake na kuionya Serikali kuhusu mgogoro huo.

Tayari Marekani imeshasitisha msaada wa akaunti ya Changamoto za Milenia (MCC) kwa sababu ya mgogoro huo. Nchi ya Uingereza na Jumuiya ya Ulaya nayo inaangalia kwa karibu kitakachotokea.

Ni kwa vitisho hivyo walau CCM inaona aibu, lakini ingeshapora ushindi siku nyingi tu. Sasa kinachofanyika ni kujaribu mbinu ya kurudia uchaguzi ili kama kuna ujanja ufanyike humo humo.

Ifike mahali CCM ikubali kushindwa Zanzibar, tufungue ukurasa mpya wa utawala Zanzibar.