Home Uchambuzi MISAADA YA CHINA YAWEZA KUWA SHUBIRI

MISAADA YA CHINA YAWEZA KUWA SHUBIRI

4989
0
SHARE

NA ERICK SHIGONGO


Mkutano mkuu wa mwaka wa nchi za Afrika na China umefanyika mapema mwezi huu katika jiji la Beijing nchini China huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kassim akimwakilisha Rais Dk. John Magufuli.

Mkutano huo uliokutanisha pamoja nchi 53 za Afrika huku China ikiwa mwenyeji, umefanyika wakati dunia ikishuhudia msuguano wa kibiashara kati ya mataifa yenye nguvu ya kiuchumi.

Marekani na China kwa sasa ndiyo yanatazamwa kama mataifa yenye nguvu kubwa ya kiuchumi duniani.

Aidha, kufanyika kwa mkutano huo kumetafsiriwa na baadhi ya wataalam wa mambo ya kisiasa kuwa ni moja ya mbinu za China kupanua ushawishi wake duniani kwa lengo la kupambana na Marekani kiuchumi.

Ikumbukwe kuwa tangu kuingia madarakani kwa Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump (Republican), kumekuwa na kulegalega kwa uhusiano wa kibiashara kati yao.

Hivi karibuni Marekani imepiga marufuku uingizaji wa bidhaa kutoka China zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 200, jambo linalodaiwa  kuiathiri  China kibiashara.

Uamuzi huo pia unatafsiriwa kama kujibu mapigo kwani tayari China ilishapiga marufuku bidhaa za Marekani zenye thamani za Dola za Marekani bilioni 60.

Wataalamu wa uchumi, wanaamini kuwa kama msuguano huo utaendelea si tu utakuwa na athari baina yao, bali utaiathiri dunia ambayo uchumi wake umejizungusha kwenye mataifa haya.

Athari yoyote ya kiuchumi ikiyapata mataifa haya, mtikisiko wake husambaa kwenye mataifa mengine pia.

Moja ya mabara ambayo yanatarajiwa kuathirika zaidi kama msuguano huu utaendelea ni Afrika.

Afrika imekuwa ikitupiwa macho ya kimkakati na mataifa yote mawili, huku kila moja likijaribu kujenga ushawishi.

Katika miaka ya hivi karibuni, mataifa haya mawili yamekuwa yakichuana kuiweka mkononi Afrika, kiuchumi na kidiplomasia ili nguvu na ushawishi wake uweze kusambaa sehemu mbalimbali za dunia.

Katika kuhakikisha kwamba China inaifanya Afrika mdau wake mkubwa wa maendeleo, imekuwa ikiweka kila mkakati ili kulikamata Bara hili  na kuzidisha ushawishi wake, miongoni mwa mikakati hiyo ni ule uliobandikwa jina la “Belt and Road Initiative”.

Ndani ya mkakati huu serikali ya nchi hiyo imedhamiria kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha barani Afrika kikiwa katika muundo wa  mikopo yenye masharti nafuu maarufu kama ‘concessionary loans” ili kuzisaidia nchi za Afrika kujikwamua kiuchumi kwa kujenga miundombinu ikiwemo barabara, reli na  bandari kwa imani kuwa huenda mambo hayo yanaweza kuisaidia Afrika kukua kiuchumi kwa kasi.

Mkakati huu umeifanya China kupokelewa vizuri barani Afrika, ikitazamwa kama mkombozi wa bara hili.

Hatua hiyo imesaidia kuongeza ushawishi wake kwa kasi kubwa barani humu, huku ushawishi wa Marekani ukizidi kupungua mwaka hadi mwaka hasa baada ya serikali ya Rais Trump kuingia madarakani mwaka 2017.

Rais Trump anadaiwa kuhamisha jicho lake Afrika na kulirejesha nchini mwake, tofauti na mtangulizi wake, Barack Obama ambaye wakati wa utawala wake alianzisha miradi mingi ya maendeleo Afrika kama njia ya kupanua ushawishi na nguvu za taifa hilo katika nchi za nje.

Rais Obama  alilipa umuhimu mkubwa bara la Afrika, wakati wa utawala wake, alilitembelea mara nne ili kuonyesha umuhimu wake na pia alipeleka kiasi kikubwa cha fedha kusaidia maendeleo ukiwemo mradi wa  Millennium Challenge Corporation (MCC) ambao Tanzania ilikuwa moja ya wanufaika wakubwa, ikiwa imepokea kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 698 katika awamu ya kwanza ya mradi huo uliomalizika mwaka 2013.

Takwimu zinaonesha kuwa baada ya Trump kuingia madarakani, misaada ya nchi hiyo kwa Afrika imeshuka kwa kasi kubwa, ukiwemo uamuzi wa kuondolewa kwa baadhi ya nchi  katika orodha ya zilizokuwa zikinufaika na msaada wa MCC, Tanzania ikiwa ni mojawapo.

Wakati Marekani ikifanya hivyo na kushusha ushawishi wake barani Afrika, China imeongeza misaada kwa bara hili,  akizungumza mbele ya marais wa Afrika katika mkutano huo na nchi za Afrika, Rais wa China Xi Jinping alisema nchi yake sasa  itaongeza misaada kwa Afrika hadi kufikia  Sh trilioni 137 kwenye  miradi ya miundombinu, biashara na huduma za afya.

Kwa mkakati huu wa China, viongozi wengi wa Afrika sasa badala ya kuelekeza macho yao kwa Marekani, wameyaelekeza China, jambo ambalo limezidisha ushawishi wa China katika Bara hili, kuliko ilivyo kwa Marekani ambayo inatafsiriwa kama inaifuata Afrika ikiwa na mikono mitupu ambayo Waswahili husema “hailambwi”.

Lakini wakati China ikizidi kuongeza misaada yake kwa Afrika na kuonekana mkombozi, mataifa ya Magharibi hasa Marekani yamezionya nchi za Afrika kuwa makini na misaada hiyo kwani si ya bure ama rahisi kama inavyoonekana, bali ni mikopo inayoweza kuzitia umaskini zaidi nchi  za Afrika na hata kupoteza baadhi ya miundombinu yake ambayo huwekwa kama dhamana ya mikopo hiyo.

Inadaiwa kuwa mikataba ambayo nchi ya China huingia na nchi za Afrika kwenye mikopo hiyo si ya wazi, imegubikwa na usiri na huwarubuni viongozi wa Afrika na mataifa mbalimbali ya ulimwengu wa tatu kwa rushwa ili isainiwe, kwa juu huonekana kama ina faida lakini kwa ndani ina vipengele vinavyoweza kuifanya nchi kupoteza sehemu ya vitega uchumi vyake.

Nchi ya Sri Lanka ni miongoni mwa nchi zilizokutana na matatizo makubwa ya kiuchumi kutokana na mikopo isiyolipika kutoka China, nchi hiyo iliingia mkataba wa kujenga bandari yake ya Hambantonta kwa mkopo wa Dola za Kimarekani bilioni 1.5, mkopo ambao  taifa hilo lilishindwa kuulipa na kujikuta bandari yake ikiendeshwa na serikali ya China mpaka deni hili litakapomalizika.

Marekani imekuwa ikiilalamikia China kwani imekuwa ikiziingiza nchi maskini za Afrika katika “mikopo ya mitego”  ambayo kwa Kiingereza huitwa “debt trap loan agreements” ili baadaye zikishindwa kulipa mikopo hiyo ichukue miundombinu yake kama bandari, reli na kadhalika na kuzitia katika umaskini zaidi jambo linalotafisiriwa kama kurejesha utumwa wa kiuchumi kupitia mlango wa nyuma.

Miaka michache iliyopita Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akiwa madarakani Tanzania iliingia mkataba na serikali ya China kujenga bandari kubwa ya kisasa eneo la  Bagamoyo mkoani Pwani, mkataba ambao  mpaka leo miaka mitatu tangu John Magufuli aingie madarakani bado haujatekelezwa kwa kile kinachodaiwa kuwa ulikuwa na “usanii” unaotia hofu.

Mfano huu wa taifa la Sri Lanka unatosha  kabisa kuwakumbusha viongozi wa Afrika kwamba “Duniani hakuna kitu cha bure”, China ipo katika biashara na mfanyabiashara yeyote siku zote huwa “ana moja kichwani”  kama kucheza mchezo wa ‘draft’ unaweza kupewa kete ya kwanza ukala,  ya pili pia ukala, ukiwa bado unashangaa kwa nini unapewa mara ghafla mwenzako akala tatu na kuingia kingi na mchezo ukaisha.

Hivyo basi pamoja na kuwa mkono wa China unalambwa na wa Marekani haulambwi, yawapasa viongozi wetu kuwa makini sana na misaada kutoka China na nchi nyingine yoyote ya nje, kuhakikisha kuwa chochote tunachokipokea kina faida kwa taifa letu kwa vizazi vilivyopo leo na vitakavyofuata baada ya sisi.

Zamani sana nikiwa mtoto mdogo, nilisoma historia ya Mtemi Kimweri  wa kabila la Wasambaa  huko Tanga ambaye alidanganywa na  wakoloni na kujikuta akitoa sehemu ya ardhi yake kwa kubadilishana na nguo, siamini kama Afrika bado ina viongozi wa aina ya kimweri katika ulimwengu wa leo, yawapasa viongozi wetu kuwa macho na misaada tunayopewa isiwe tu na faida kwa watoa misaada wakati inadidimiza maisha  yetu wenyewe.

Ni bora kwenda kidogokidogo, taratibu na tukijiimarisha katika kilimo, viwanda, kujenga miundombinu, elimu, huduma za afya kwa kutumia mapato yetu ya ndani hata kama ni madogo, kuliko kukimbilia mikopo ambayo kwa juu imepakwa sukari lakini ndani ina shubiri, itakuwa ni mateso makubwa sana kwa Watanzania ambao wamedhamiria kujenga Tanzania mpya na wamehamasika.  Uzalendo ukijengwa, Tukakusanya kodi vizuri  kisha kudhibiti upotevu wa mapato yetu, hakika tunaweza kuibadili nchi yetu bila kutegemea misaada ya “kijanjajanja” kutoka kwa mataifa ya Magharibi.