Home Afrika Mashariki Muungano huu ni wa mkataba

Muungano huu ni wa mkataba

3696
0
SHARE

SUALA la Muungano baina ya iliyokuwa nchi huru ya Tanganyika na nchi ya Zanzibar iliyounda taifa kwa jina jamhuri ya muungano wa Tanzania limekuwa likiibua mijadala ya aina yake kila linapozungumzwa.

Muungano huu ambao huadhimishwa Aprili 26 ya kila mwaka, ulianzia mwaka 1964 ambako hadi sasa tunaona kuwa muungano huu umepitia changamoto nyingi kutokana na mambo kadhaa ikiwemo historia yake na uhusika wa waasisi wake hayati Julius Nyerere, Rais pekee wa jamhuri ya Tanganyika na Rais wa kwanza wa jamhuri ya muungano wa Tanzania hii; na hayati Abeid Karume Rais wa kwanza wa serikali ya mapinduzi Zanzibar na makamu wa kwanza wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Si siri, kuna mambo mengi yanayohitaji ufafanuzi juu ya muungano na mengine yanahitaji mijadala mipana ya wazi itakayoandika historia mpya. Kwa kuanzia ni lazima kuujua ukweli wote kuhusu muungano kutoka kwa wanaoujua vilivyo, watakaoaminika bila kuweka ushabiki wala kuficha mambo yanayoweza kuonwa magumu Kwa mfano, mabadiliko ya mambo ya muungano kutoka yale 11 ya msingi yaliyokubaliwa ndani ya mkataba wa muungano (sawa tu kusema hati za muungano zilizopewa nguvu na sheria za muungano) ni kati ya misuguano inayotokana na kutokubali kuwa muungano huu uliopo ni wa mkataba hivyo mambo yanayofanywa kukiuka masharti yaliyoingiwa awali ndicho chanzo cha hii iitwayo changamoto au kero za muungano siku hizi.

Uamuzi wa kukubali kuwa muungano huu ni wa mkataba itakuwa hatua kubwa kuelekea kuuimarisha muungano kwa kuondoa manung’uniko na malalamiko yasiyokwisha. Kupingana na dhana hii ya muungano huu kuwa wa mkataba ndiko kunasababisha wanasiasa kubishania idadi ya serikali na kuzuka kwa kero zisizokwisha ambazo zinaweza kutumika kuvunja muungano.

Usipotaka kujua chanzo cha tatizo huwezi kulitatua bali utapoteza muda kulificha hadi litakapokuumbua! Tumeona katika mapendekezo ya iliyokuwa Tume ya mabadiliko ya Katiba ikijitokeza dhana ya muungano wa mkataba na kuonwa kama jambo geni. Kwa mujibu wa tume ilithibitika Wazanzibari wengi waliutaka muungano huu wa mkataba utambulike, uendelee; pendekezo ambalo nahisi wajumbe wa tume hawakutaka kujishughulisha nalo kwa undani ili kung’amua mantiki iliyobebwa nalo. Badala yake tume ya Warioba wakapendekeza serikali tatu ndani ya Rasimu iliyojadiliwa katika bunge maalumu la Katiba.

Kuikwepa dhana yenye mantiki ya mkataba, na mvutano wa idadi ya serikali kati ya mbili au tatu ulifanya bunge maalumu la Katiba kuchukua muda mrefu kujadili pasi kufikia muafaka. Hatimaye mpasuko uliozaa umoja wa katiba ya wananchi – UKAWA ukajidhihirisha nje, huku wajumbe waliobaki ndani (bungeni) wakipitisha Katiba Pendekezwa yenye sharti la serikali mbili.

Matokeo yake matarajio ya kupata Katiba mpya kwa sasa ni kama yanahesabu siku katika chumba cha wagonjwa mahututi. Muungano utasimama imara pale tukaporudi kwenye msingi wa uwepo wa muungano wa mkataba unaohusisha hati za muungano, sheria za muungano na Katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya 1977.

Tukiiheshimu awali bila kupindisha mambo, kwa mfano kuna manung’uniko kuwa hata baadhi ya mabadiliko ndani ya Katiba hususani yale yahusuyo mambo ya muungano yalifanywa kinyemela, tutafikia muafaka utakaowaridhisha wengi; na hata wasioridhika hawatakuwa na kinyongo kama mambo yamefanyika kwa uwazi, weledi na uhuru wa kidemokrasia. Jamhuri ya muungano wa Tanzania imetokana na mkataba halali baada ya makubaliano ya waasisi yaliyowezeshwa na nguvu za ndani na nje ya nchi husika kabla ya muungano, yaani Tanganyika na Zanzibar.

Mkataba halali wa muungano unahusisha hati za muungano (Articles of Union) zilizotiwa saini Aprili 22 mwaka 1964 kisha kuthibitishwa na sheria za muungano (Acts of Union) Aprili 26, 1964; yaani Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (The Union of Tanganyika and Zanzibar Act, 1964) iliyopitishwa na bunge la Tanganyika, na Sheria ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika (The Zanzibar and Tanganyika Law, 1964) iliyopitia baraza la mapinduzi Zanzibar; sawa tu na baraza la wawakilishi la sasa. Hili linatuonesha kwamba waasisi walitambua muungano baina yao ni matokeo yaliyoanzia kwenye makubaliano kisha mkataba kupitia hati za muungano zilizopewa nguvu kisheria na sheria za muungano hivyo kupata mashiko ndani ya Tanganyika na Zanzibar.

Muungano huu wa mkataba umepewa masharti yanayothibitika ndani ya hati za muungano zenyewe, nje ya makubaliano, nje ya mkataba na nje ya sheria hazina mashiko. Lakini hati za muungano na sheria za muungano ndizo msingi wa muungano na Katiba zilizofuatia kuanzia ile ya mpito (Interim Constitution 1964) hadi iliyopo ya jamhuri ya muungano wa Tanzania 1977 na ile ya Zanzibar 1984.

Sheria za muungano ndizo muhuri uliofanya makubaliano kupitia hati za muungano kuwa mkataba kamili. Kwa mujibu wa vipengele vya hati za muungano zenye sahihi na majina ya waasisi, nchi huru husika zilikubaliana kuungana kuwa taifa moja kimataifa. Hata uwepo wa serikali ya jamhuri ya muungano na serikali ya Zanzibar kama msimamizi wa mambo yasiyo ya muungano zilitokana na makubaliano (tuseme mkataba).

Aidha, zinazoendelea ni matokeo ya kukataa ukweli kuwa muungano huu ni wa mkataba. Wadau walio nje ya mstari wakirudi na kutambua muungano huu una mkataba uliouasisi hakutakuwa na ubishani usiofikia muafaka. Katika sheria za muungano, muungano unaanzishwa rasmi ukiwa na mambo 11 yaliyokubaliwa awali kupitia hati za muungano yanapata nguvu kisheria hivyo masharti ya kuyabadilisha hayastahili kukiukwa kirahisi tu. Masharti mengine mengi yameelezwa na yanaeleweka.

Kwa mfano, vifungu 6(1) na 6(2) vya sheria za muungano zilizo pumzi ya awali ya uwepo wa muungano wa mkataba vinabainisha rais wa kwanza wa jamhuri ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar (jina ambalo lilibadilishwa kuwa jamhuri ya muungano wa Tanzania Disemba 11, 1964 kupitia kifungu cha 2 cha sheria namba 61/ 1964 (cap. 573) atakuwa Mwalimu Julius Nyerere na makamu wa kwanza wa Rais atakuwa Sheikh Abeid Karume.

Baadaye sheria kadhaa zilipitishwa kuhakikisha muungano huu wa mkataba unadumu, ikiwemo Katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania 1977 iliyo muendelezo wa mkataba wa waasisi. Manung’uniko yalianza mapema kuanzia mwezi Mei 1964 enzi za katiba ya mpito, yakaendelea kuwa malalamiko kisha kero. Hata wakati na baada ya kuwepo Katiba ya 1977 iliyotungwa na wajumbe 207 kwa takriban saa tatu, Aprili 25, 1977 na kuanza kutumika kesho yake (Aprili 26, 1977) kero hazikukoma.

Maandishi mengi yanaonesha uhaba wa kushirikishwa wananchi, ukiukwaji wa taratibu za kufanya mabadiliko ya mkataba kupitia Katiba na kutotoa fursa kwa wananchi kurejea iliko misingi na kufanya maamuzi magumu kuhusu muungano. Viongozi wasiogope kusema kwamba muungano huu haukuzuka tu kutoka kusikojulikana bali una makubaliano, una mkataba, una sheria, una Katiba. Watanzania wanaoujua muungano kabla na wakati hati za muungano zikiidhinishwa jumatano 22 Aprili 1964 na muungano kuwa rasmi jumapili 26 Aprili 1964 wasikae kimya, waseme wanayoyajua ili kuiongezea ‘utamu’ historia iliyopo.