Home Habari Muungano wa upinzani Kenya umeanza kumeguka

Muungano wa upinzani Kenya umeanza kumeguka

2286
0
SHARE

NA ISIJI DOMINIC

DALILI zinaonyesha hali si shwari ndani ya muungano wa vyama vya upinzani, NASA (National Super Alliance), huku zikiwa zimebaki takribani miaka miwili kabla ya Kenya kwenda kwenye uchaguzi mkuu.

Kumeguka kwa NASA wakati chama tawala cha Jubilee nacho kikionekana kutetereka ni ishara kwamba kuelekea mwaka 2022, kutakuwa na miungano mipya. Jubilee imefanya mabadiliko kwa wabunge wanaoshikilia nyadhifa mbalimbali jambo ambalo pia limeshuhudiwa kwa vyama vya upinzani.

Ikumbukwe kuwa Rais Uhuru Kenyatta pindi tu alipochaguliwa tena kwa muhula wake wa pili madarakani, tayari wanasiasa walikuwa wameshaanza kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Imekuwa kama desturi hususan kwa nchi za Afrika kila baada ya uchaguzi kumalizika ndiyo mwanzo wa kampeni kwa uchaguzi unaokuja hivyo wengi hubaki kujiuliza ni lini wanasiasa watatekeleza walichoahidi?

Kwa miaka 40, chama cha KANU kimetawala Kenya huku Hayati Rais Mstaafu Daniel arap Moi akiongoza nchi hiyo kwa miaka 24 kati ya miongo hiyo minne ya utawala wa KANU. Mwaka 1982, Katiba ya Kenya ilibadilishwa na kufanya nchi hiyo kuwa ya chama kimoja tu.

Vuguvugu la siasa kutaka vyama vingi iliibuka mwaka 1990 na hatimaye sheria kubadilishwa na uchaguzi wa kwanza kufanyika mwaka 1992 ikihusisha vyama nane. KANU ikiongozwa na Rais Moi, kilishinda kwa asilimia 36.6.

Miaka mitano baadaye, yaani 1997, jumla ya vyama 15 vya siasa vilipitishwa kusimamisha wagombea urais na Rais Moi alifanikiwa kutetea kiti chake kwa Chama cha KANU baada ya kupata asilimia 40.4.

Swali likawa, je, nani atakuwa rais wa Kenya wa awamu ya tatu baada ya Moi kumaliza muda wake wa miaka 10 madarakani? Pendekezo la Moi katika Uchaguzi Mkuu wa 2002 ilikua Uhuru Kenyatta kupitia Chama cha KANU.

Uhuru alipambana na wagombea wengine wanne wa urais lakini kwa mara ya kwanza ilishuhudiwa vyama vya siasa vikiungana. Mwai Kibaki alichaguliwa kwa asilimia 61.3 na kuwa Rais wa awamu ya tatu wa Kenya kupitia NARC, ambacho kilikuwa muunganiko wa vyama vinne vikuu ambavyo ni Liberal Democratic Party (LDP), Democratic Party (DP), FORD-Kenya na National Party of Kenya (NPK).

Haishangazi kuona baada ya mwaka 2002 na hususan baada ya chama cha KANU kuondolewa madarakani, tumekuwa tukishuhudia vyama vikiungana kwa lengo moja tu; kuchukua madaraka. Ukweli unabaki hata kama vyama viungane vipi na kuunda muungano, kama dhamira hazishabihiani, muungano huo hauwezi kudumu. Ndiyo kwa maana Rais mstaafu Kibaki aliachana na NARC na kuungana na takribani vyama saba kuunda muungano mwingine uliotambulika kama Party of National Unity (PNU) kilichomsaidia kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Katika uchaguzi mkuu wa 2013, vyama viwili vikubwa, TNA ya Rais Uhuru na URP ya Naibu Rais William Ruto ziliunda muungano wa Jubilee Alliance na kupambana na muungano wa CORD iliyoundwa na ODM chini ya kinara Raila Odinga, Wiper ya Kalonzo Musyoka, ANC chini ya Musalia Mudavadi na FORD-Kenya ambaye mwenyekiti wake ni Moses Wetangula.

Kwa mara nyingine tena, tulishuhudia vyama vikiungana katika uchaguzi wa mwaka 2017 ambayo Rais Uhuru alifanikiwa kutetea nafasi yake baada ya chama chake cha Jubilee kuishinda muungano wa NASA ambayo ilibadilisha jina lake kutoka CORD.

Ni dhahiri uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 utashuhudia miungano mipya ama ya vyama vya siasa au wanasiasa. Wakati Rais Uhuru akipambana kutimiza agenda nne kuu alizojiwekea, wanasiasa nao wanajipanga kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Hali si shwari ndani ya Jubilee na NASA na yote haya ni baada ya tukio la Machi 9 mwaka 2018 pale Rais Uhuru na kinara wa upinzani Raila kwa pamoja waliibuka hadharani na kisha kuhutubia taifa wakisisitiza lengo lao ni kuwaunganisha Wakenya.

Ni kitendo ambacho moja wa vinara wa NASA ambaye pia ni kiongozi wa chama cha FORD-Kenya, Moses Wetang’ula, alikipinga na matokeo yake NASA ikamvua nafasi yake ya kiongozi wa waliyo wachache kwenye Bunge la Seneti.

Ndani ya Jubilee nako, Aden Duale na Kipchumba Murkomen ambao wamekua katika mstari wa mbele kumpigia debe Naibu Rais Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 huku wakionyesha wazi kutoridhishwa na tukio la Machi 9 lililotokea nje ya Ofisi ya Rais jijini Nairobi, walijikuta wakipoteza nafasi zao.

Duale aliondolewa kwenye nafasi ya kiongozi wa waliyo wengi Bunge la Taifa ili kumpisha Amos Kimunya wakati Murkomen alitimuliwa kwenye nafasi ya kiongozi wa waliyo wengi Bunge la Seneti na badala yake akachaguliwa Seneta Samuel Poghisho.

Wanasiasa wa Jubilee kutoka Mkoa wa Magharibi anapotoka Wetang’ula wamekuwa wakimshawishi mwanasiasa huyo kuunguna na Ruto na haitashangaza endapo wakifikiana makubaliano tukashuhudia muungano mpya wa siasa ukiundwa.

Wetang’ula amekuwa katika wakati mgumu sio tu ndani ya chama chake cha Ford-Kenya, mbali hata pia muungano wa NASA na aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema muungano huo umekufa huku mara kadhaa akimshambulia kwa maneno Raila.

Katika mahojiano aliyowahi kufanya na kituo kimoja cha televisheni nchini Kenya, Wetang’ula alisema Raila ni mtu anayevuruga vyama na kuvipotezea dira kuanzia enzi za KANU, NARC na CORD.

Aidha aliongeza Raila sio mchezaji wa timu na hawezi kuaminika huku akikumbuka namna alivyojitolea mara mbili kuacha azma yake ya kugombea urais ili amuunge mkono kiongozi huyo wa ODM.

Ni mahojiano ambayo hayakupokelewa vyema na wanachama wa ODM, ambao walidai Wetang’ula alitaka Raila akamatwe na kushtakiwa kwa uhaini baada ya kujiapisha kama rais wa wananchi Januari 30 mwaka 2018.

“Kenya ilikuwa inavuja damu, hakuna kitu kinaendelea, shilingi ya Kenya ilishuka thamani vibaya na shule nyingi zilikuwa zimefungwa. Yeye (Raila) aliiokoa Kenya,” ilisema taarifa ya chama iliyosomwa na Mwenyekiti wa ODM, John Mbadi. “Wetang’ula alitaka Raila akamatwe, ashtakiwe na kupelekwa jela ili yeye ashereheke. Yeye sio aina ya rafiki mtu atamhutaji.”

Huku kukiwa na ushawishi wa Wetang’ula ambaye sasa anaonekana ni yatima kisiasa kuungana na Ruto kuelekea uchaguzi mkuu ujao, Wakenya wameshuhudia Mwenyekiti wa KANU, Gideon Moi, akikutana na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho na kwa pamoja wakaahidi kufanya kazi. Tafsiri ya wachambuzi wa siasa ni labda wawili hawa wanapanga mikakati ya kisiasa ya moja kugombea urais na mwingine kuwa mgombea mwenza.