Home Makala Mwalimu Nyerere aliweza kwa nini sisi tushindwe?

Mwalimu Nyerere aliweza kwa nini sisi tushindwe?

1626
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

NI dhahiri kuwa sekta ya Elimu hususani Elimu ya Juu nchini ilitakiwa kupiga hatua zaidi kuliko ilivyo sasa. Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa, tangu Tanzania ipate uhuru hadi sasa sekta hii imepitia changamoto nyingi ambazo kamwe hazikupaswa kuturudisha nyuma kiasi hiki.

Nasema hivyo kwa sababu licha ya idadi ya vyuo vikuu kuongeza kwa kasi hapa nchini, tafiti mbalimbali zikiwamo za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa ni Watanzania wachache wanaopata fursa ya kujiunga ya elimu ya Chuo Kikuu.

Hadi sasa Tanzania inavyo vyuo vikuu 46 na kila mwaka wanafunzi zaidi ya 200,000 ndio wanaojiunga na vyuo hivyo. Udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vya elimu ya juu ni hatua ya kwanza muhimu katika kuwatambua wale wanaostahili kupata nafasi ya kujiunga na masomo katika ngazi hiyo. Ili kuandaa nguvu kazi au rasilimali watu inayohitajika katika sekta mbalimbali za Taifa, ni dhahiri kuwa kazi hii ya udahili inatakiwa kufanyika kwa umakini wa hali ya juu.

Kazi ya kudahili wanafunzi inakuwa ngumu zaidi kadri idadi ya vyuo na   idadi ya wanafunzi wanaotaka kudahiliwa inavyoongezeka. Kwa mfano, kumbukumbu zinaonesha kwamba, wakati Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kinaanzishwa kama Chuo Kikuu kishiriki cha Chuo Kikuu cha London, Uingereza mwaka 1961, ni wanafunzi 11 tu ndio walidahiliwa, na  kati ya hao 11, ni wanafunzi saba tu ndio walikuwa wananchi – yaani Watanganyika.

Takwimu zinaonesha pia kwamba, hadi kufikia mwaka 1969/1970, Chuo hicho kilikuwa na jumla ya wanafunzi 1,263 tu. Idadi hiyo iliongezeka taratibu mwaka hadi mwaka na ilipofika mwaka 2001/2002, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kilikuwa na  jumla ya wanafunzi 15,939

Suala la kufurahisha ni kwamba licha ya Taifa kuwa na mapato madogo kulingana na vyanzo vya mapato wakati huo wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, wanafunzi hao walisoma kwa raha isiyo kifani kwa kupatiwa mahitaji yote muhimu stahiki kwa mwanafunzi.

Dai hilo pia linaungwa mkono Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Elimu kutoka Chuo Kikuu Ch Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa kuwa kipindi cha Mwalimu Nyerere Elimu ilikuwa bure na watu wote waliosoma vyuo vikuu walithaminiwa wakasoma kwa amani, wakapewa posho ya kujikimu.

“Hali hiyo ilikuwa pia katika vyuo vya ualimu, sasa hayo yaliwezekana tukiwa tumetoka kutawaliwa na mkoloni, lakini sasa  Tanzania imeweza kuboresha sekta ya utalii,  madini, gesi lakini cha ajabu tunapiga hatua kurudi nyuma, tufike mahali taasisi hizi zinazofanya maamuzi zichukuliwa hatua, pia zitambue kuwa maamuzi wanayoyafanya wayapime na kujua kwamba wana wajibu wa kuwasaidia watanzania na si kuwaumiza watanzania,” anasema.

Tukirudi nyuma kidogo tunaona kuwa historia ya vyuo vikuu katika Afrika Mashariki hadi kufikia mwaka 1949, hakukuwa na Chuo Kikuu chochote katika ukanda huo. Mwaka huo wa 1949 ndipo utawala wa Mwingereza uliamua kukipandisha hadhi Chuo Kikuu cha Makerere na kuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha London cha Uingereza.

Mwaka 1956 ilianzishwa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Makerere mjini Nairobi, Kenya, kabla ya mwaka 1961 kuanzishwa Kampasi ya Dar es Salaam, Tanzania.

Kampasi tatu hizo za Chuo Kikuu cha Makerere, kwa maana ya Makerere yenyewe, Nairobi na Dar es Salaam, mwaka 1963 ziliamua kuunda Shirikisho la Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki.

Hata hivyo, kutokana na Shirikisho hilo kushindwa kukidhi mahitaji kampasi hizo, kila kampasi iliamua kujitenga na kuanzisha Chuo Kikuu, katika ukanda huo wa Afrika Mashariki, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hizo, kukuwa na vyuo vikuu vitatu vyenye hadhi sawa, vya Makerere, Nairobi na Dar es Salaam.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilizunduliwa rasmi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Agosti 29,1970. Hadi kufikia miaka ya 1980 chuo hicho kilikuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi hadi zaidi ya 1000 kwa mwaka wa masomo. Baadaye ilianzisha Kampasi ya chuo hicho Morogoro ambayo ilianzisha Kitivo cha Kilimo.

Mwaka 1984, Kampasi ya Morogoro ambayo ilikuwa sehemu ya chuo kikuu cha Dar es Salaam, ilipandishwa hadhi na kuwa chuo kikuu kamili, kwa jina la Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.

Mwaka 1992 Chuo Kikuu cha OUT kilianzishwa rasmi kwa Sheria ya Bunge Namba 17 ya mwaka 1992. Mwaka 1994 chuo hicho kilimpata mkuu wake wa chuo, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza mstaafu, Dk. John Malecela sambamba na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Tolly Mbwete. Udahili kwanza wa chuo hicho ulifanyika mwaka 1994 na kupata wanafunzi wa kwanza kabisa, kiasi cha 766.

Sasa idadi ya vyuo imeongezeka, idadi ya Watanzania imeongezeka hadi kufikia milioni 50, lakini pia idadi ya vyanzo vya mapato imeongezeka, sasa kinachoturudisha nyuma ni nini?

Ni dhahiri kuwa lipo tatizo katika usimamizi wa sekta hii ya elimu hasa elimu ya juu ambayo inatoa picha halisi ya wasomi wa Tanzania.

Msomi yeyote anayefurahia maisha ya elimu ya juu hapa nchini ni yule aliyesoma katika awamu hizo za Mwalimu Nyerere, katika miaka ya karibuni hali imekua mbaya na hata kusababisha idadi ya watanzania wenye sifa kujiunga na elimu ya juu kushindwa kujiunga kwa sababu mbalimbali.

Kwanza ikiwa ni umasikini; licha ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuanzishwa (HESLB), bado kumekuwa na kigugumizi katika kutatua changamoto zinazoikabili bodi hiyo na kushindwa kutoa mikopo inayowafikia wahusika kwa wakati muafaka.

Dk. Kahangwa anasema hali hiyo inasababishwa na baadhi ya mipango ya serikali katika sekta ya elimu ambayo imeonekana kutoafaa kabisa katika kukuza sekta hiyo nchini.

“Niwashauri watu wa mikopo kwa ujumla kwamba wanawatumikia watanzania, kwa hiyo mipango na sera ingetakiwa kuwajali na kuwapa nafuu ya maisha watanzania. Taifa letu katika historia yake kilichowasaidia si biashara, urithi wa mali, ujanjaujanja au akili zao ni elimu ambayo ilitolewa kwa kupitia mfumo wa Mwalimu Nyerere ambao ulilenga kuwasaidia wanyonge,” anasema.

Anasema suala la mikopo ndio linaumiza watu kwani pamoja na kutakiwa kurejesha wengine wanakatwa hata baada ya kumaliza kulipa mikopo hiyo.

Kutokana na hali hiyo anashauri serikali kuunda Benki ya elimu ya juu ambayo itatoa mikopo kwa wakati muafaka na kukusanya madeni hayo kama nchi ya Nigeria inavyofanya.

“Kuzuia vyuo kuhusu vigezo inaleta shida katika nchi ambayo imefanya ugatuaji wa madaraka, kuna vitu ambavyo vingefanyiwa maamuzi katika vyuo husika kuliko kila kitu kupeleka juu, hii inaonesha kuwa hawa viongozi hawana imani na waliopo chini yao,” anasema.

Baadhi ya wadau wengi wamekuwa wakilalamikia anguko katika sekta ya elimu kuwa imeanguka kutokana na viongozi tunaowachagua kufanya maamuzi yasiyokuwa na tija.

Dk. Kahangwa anasema Mwalimu Nyerere alikuwa anasema kupanga ni kuchagua; “Napata shida kumsikiliza Rais Magufuli kuwa tumepanga wakati ni mipango ambayo haijatushikirisha kuna mtu tu amepanga. Mfano shule bure ni maamuzi ya Shirika la IFM, mikopo elimu ya juu ni maamuzi ya Benki ya Dunia.

“Pia wakaja watu wanaomua kuunganisha masomo bila kufanya utafiti, mfano mimi nimesoma shahada ya kwanza hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka minne. Baadaye walikuja wakapunguza wakasema miaka mitatu, sasa tunaona kuwa aina ya walimu tulio nao leo si wanataaluma waliobobea tena. Hivyo tumecheza na vitu kama hivyo mfano wale walimu wa voda fasta na mambo mengine matokeo yake ndio hayo.

“Ila sasa ili tutoke hapo ni lazima tukae chini sisi watalaamu tuzungumze na kufanya utafiti wa kitaaluma ili kupata mipango thabiti ya kutondoa hapa tulipo,” anasema.