Home Maoni Mwisho wa uzee Chalinze, wapi mwisho wa ujamaa?

Mwisho wa uzee Chalinze, wapi mwisho wa ujamaa?

2782
0
SHARE

Na Joseph Mihangwa

Wiki iliyopita tulidadavu kuhusu msemo unaokita miongoni mwa vijana, hasa vijana wa kike Jijini Dar Es Salaam unaodai kwamba, “Mwisho wa uzee ni Chalinze”, kumaanisha kwamba, linapokuja suala la “mahusiano” kwa watanashati wa Jijini, hakuna cha mzee wala kijana; kwamba, tofauti hizo zinaishia Chalinze [Bara] wanakozingatia [heshima] mila na tamaduni.

Makala hiyo iliangazia Sera za “Ujamaa na Kujitegemea” na jinsi utawala wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume, alivyopiga marufuku Azimio la Arusha na “Ujamaa” Endelea…

“Ujamaa” hauwezi kujengwa juu ya sera za uchumi, bali kinyume chake ndiyo kweli.  Hii ni tofauti na dhana ya mfumo/sera za uchumi kama vile Usoshalisti ambao inadaiwa, unaweza kumea baada ya kupitia hatua ya uchumi wa kibepari. Pamoja na hayo, dhana hii nayo sasa inapoteza nguvu kutegemea umakini wa taifa na watu wake.  Ni muungano makini na wenye nguvu kati ya tabaka la wakulima na wafanyakazi pekee utakaoweza kuanzisha harakati za kisiasa na za kiuchumi bila kusubiri kupevuka kwa ubepari.

Ili hili lifanikiwe, kuna mambo makuu matano yanayopaswa kuzingatiwa na kutekelezwa.  La kwanza ni kupiga vita na kukomesha kabisa uchumi wenye kuhodhiwa na wageni.  Pili, kubuni na kutekeleza programu ya mageuzi katika kilimo [Agrarian reform] ili kuondoa aina zote za unyonyaji vijijini.  Programu hii ni tofauti na Programu ya “Mapinduzi ya Kijani”  [Green Revolution] inayopigiwa upatu na wawekezaji wa kigeni kwa kushirikiana na mawakala wao wa ndani ya nchi. Tofauti iliyopo ni kwamba “Mageuzi katika Kilimo” yanalenga kumwinua mkulima kwa kumwekea mazingira bora ya kuendelea; wakati “Mapinduzi ya Kijani” yanalenga kuongeza uzalishaji katika kilimo kwa kutumia wawekezaji wenye mitaji mikubwa, mara nyingi kwa manufaa ya wenye mitaji, na mtu mdogo hutumika kama ngugu-kazi [manamba] tu katika “Mapinduzi” hayo.

Tatu, kusimamia vizuri matumizi ya mapato ya ndani na ya nje ili yaweze kunufaisha jamii kubwa na pana zaidi.  Hii ni pamoja na kupiga vita rushwa na aina mbali mbali za ufisadi. Nne, kuanzisha asasi makini itakayosimamia na kufuatilia majukumu na ujenzi wa msingi imara wa kitaifa; ujenzi wa Viwanda na maendeleo ya kilimo, tofauti na ilivyo sasa ambapo Wawekezaji wamejikita katika sekta ya madini na uporaji wa ardhi badala ya Viwanda kwa mlaji mzalendo na huduma za jamii.

Tano, kudemokrasisha nyanja zote za maisha ya jamii na kupiga vita udikteta wa Serikali ili watu waishi kama familia moja – Ujamaa.  Kwa hili, watu lazima wajione kuwa sehemu ya mchakato wa kisiasa badala ya ukiukwaji wa haki za binadamu na unyonyaji ili waweze kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi. Kuna dhana potofu na ya kipropaganda ya maadui wa “Ujamaa”  inayodai kwamba, katika jamii inayoishi kijamaa “demokrasia” ya kisiasa haipewi nafasi.  Dhana hii haitofautishi kati ya “Ujamaa” na “Usoshalisti”, kama tulivyoeleza mwanzo.  Hata kama wanapropaganda hawa wangekuwa wanazungumzia “Usoshalisti”, watakuwa wanasumbuliwa na tafsiri potofu juu ya maelezo ya Karl Marx kuhusu neno “nguvu ya umma”.

Yeyote aliyemsoma vizuri Marx hawezi kushindwa kuelewa kwamba ile “nguvu ya umma” wa wanyonge si kingine bali ni ukuu wa kisosholojia wa tabaka la wakulima na wafanyakazi.  Tafsiri hii haina maana ya kisiasa ya “Serikali katili” au “utawala wa maguvu” kama ilivyotokea kuwa fasheni ya Serikali nyingi zenye kufuata mrengo wa siasa za Kisoshalisti enzi za vita baridi,  kati ya Mashariki na Magharibi. Dhana ya Karl Marx iko wazi juu ya ushabiki wa “Usoshalisti” na demokrasia ya kisiasa.  Jambo hili iliwekwa wazi na Lenin, aliposema, “Asasi za uwakilishi [demokrasia ya uwakilishi] zinabakia…. Bila asasi hizi hatuwezi kuwa na demokrasia”.

Na ni msimamo pia wa Rosa Luxemburg, aliposema, mwaka 1918:  “Uhuru maana yake si upendeleo kwa wanaounga mkono Serikali pekee, au kwa wanachama wa chama fulani cha siasa ndani ya mfumo wa chama kimoja, hata wawe wengi kiasi gani; uhuru na demokrasia ni pamoja na kusikiliza na kuheshimu mawazo ya walio wachache wanaotokea kutokubaliana na Chama tawala  au Serikali”.

Tunachoelezwa hapa ni kwamba, hata katika Usoshalisti na Ukomunisti, uhuru wa mawazo na wa vyama vya upinzani vinapaswa kuwapo.  Na vyote hivi vilipaswa kufanya kazi ndani ya mazingira ya “Ujamaa”. Kwa sababu hii, demokrasia ya kisiasa na uhuru haviwezi kuwa adui wa Usoshalisti.  Kufikiri kinyume na hilo ni kinyume cha U-Karl Marx.

Upokonyaji wa uhuru kwa kisingizio cha kuelekeza kasi ya maendeleo [developmentalist culture] hauna nafasi katika ujenzi wa Usoshalisti au sera yoyote ya kiuchumi ndani ya “Ujamaa”. Kilichoonekana kuwa ndiyo utekelezaji wa sera za kisoshalisti miaka iliyopita na matokeo yake yasiyofurahisha, ni kazi ya wanasiasa uchwara na vichwa maji kwa lengo la kujijenga kama tabaka, tofauti na matakwa ya “Ujamaa” – ubinadamu. Hata katika nchi za Ubepari, inapotokea kwamba tabaka la mabepari linatishiwa na mwamko wa kisiasa miongoni mwa tabaka la wafanyakazi, hawasiti kuvunjilia mbali uhuru na demokrasia ya kisiasa na kuendesha utawala wa kibepari kwa nguvu na kwa vitisho ndani ya “Ujamaa” wao.

Tanzania imeamua kufuata sera gani za uchumi; kati ya Usoshalisti na Ubepari ndani ya “Ujamaa”?.  Je, ni kweli Azimio la Arusha limefutwa na Azimio la Zanzibar au ni udhaifu wetu katika kutoa tafsiri?.  Uko wapi ubaya wa Usoshalisti, achilia mbali ukichwa maji wa wanasiasa uchwara ulioufanya uonekane tunavyouona leo?.

Demokrasia na uhuru ni viambata katika mfumo wa uchumi, siasa, jamii na uhusiano kwa itikadi yoyote.  Msingi wa demokrasia ya kweli ni demokrasia ya kiuchumi kwa maana ya uhuru kutoka katika ukatili [tyranny] wa mitaji [inayotumiwa kuangamiza wengine] na kumilikiwa kwa nguvu kazi [watu] chini ya taratibu za uzalishaji mali usiojali za wenye mitaji.

Ni kutokana na hili kwamba juhudi za usoshalisti zinakuwa ni kuhakikisha haki ya kijamii kwa njia ya usawa [kama binadamu] na haki yao/thamani ya jasho la kila mtu kwa kiwango chake cha uzalishaji mali.  Ujenzi wa Usoshalisti unataka kupanuliwa kwa uhuru katika maeneo makuu matatu yafuatayo: Kwanza, ushiriki wa umma katika utawala, ulinzi na haki; yaani utekelezaji wa demokrasia kwa vitendo kwa kila ngazi ya Serikali. Pili, Haki ya ajira, elimu, afya kwa kila raia, bila kujali itikadi au uanachama wa vyama vya siasa, na umilikaji wa njia kuu za uchumi.

Tatu, kujenga na kuimarisha utamaduni wa kisiasa ambamo kila raia ana uhuru na haki ya kushiriki [kupitia vyama vya siasa au bila vyama], kwa maana kwamba “haki zote za kidemokrasia ni haki za watu” na ni za kudumu; hazitolewi kwa ridhaa ya Serikali na kwa baadhi tu ya watu; wala haziwezi kuondolewa na Serikali kwa sababu tu mtu au watu hawazingatii matakwa ya Serikali hiyo.

Ujamaa wa kweli haudai haki pekee.  Tawala zinazoshindwa kutambua haki za msingi za raia haziwezi kujenga Ujamaa  bali kujijengea utawala wa kibabe na  kwa manufaa ya walio madarakani pekee.  Na hii ni sumu kwa “Ujamaa”.  Katika “Ujamaa” hakuna aliye “mheshimiwa” zaidi ya wananchi ambao ndio waajiri wa wale  wanaojiita “waheshimiwa”.