Home Makala Mwisho wa uzee Chalinze; wapi mwisho wa ujamaa?

Mwisho wa uzee Chalinze; wapi mwisho wa ujamaa?

2466
0
SHARE

Na Joseph Mihangwa

Kuna msemo unaokita miongoni mwa vijana, hasa vijana wa kike Jijini Dar Es Salaam unaodai kwamba, “Mwisho wa uzee ni Chalinze”, kumaanisha kwamba, linapokuja suala la “mahusiano” kwa watanashati wa Jijini, hakuna cha mzee wala kijana; kwamba, tofauti hizo zinaishia Chalinze [Bara] wanakozingatia [heshima] mila na tamaduni.

Enzi za utawala wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume, alipiga marufuku sera wala kusikia hadithi juu ya Azimio la Arusha na “Ujamaa”. Kwa Karume “Mwisho wa Azimio la Arusha ni kisiwa [kidogo] cha Tunguu”, kilichopo mpakani mwa Zanzibar na Tanzania Bara ndani ya Bahari ya Hindi.

Watanzania tuliridhia Sera za “Ujamaa na Kujitegemea” kwa njia ya Azimio la Arusha mwaka 1967, sera ambazo zimeendelea kudumu kwa maneno [bila vitendo] ndani ya Katiba ya Muungano.  Lakini tunatambua pia mwaka 1992, Halmashauri Kuu ya Taifa [NEC] ya Chama tawala cha Mapinduzi [CCM] ilikaa mjini Zanzibar na kutoa kipigo cha kuua Azimio la Arusha na pamoja sera zake kwa Azimio la Zanzibar kuashiria tamati ya Azimio hilo mashuhuri.  Kuanzia hapo hadi sasa tunaimba “Ujamaa” tukicheza mdundiko wa kibepari.

Kwa mantiki hiyo, kama ni kweli kila jambo lina mipaka yake; kwamba “mwisho wa uzee ni Chalinze”; mwisho wa Azimio la Arusha ni Kisiwa cha Tunguu”; leo mwisho wa “Ujamaa” ni wapi?.  Kwa nini neno “Ujamaa” linazua “mzio” miongoni mwa wengi siku hizi, wakati ni sera bora kupindukia, ya “mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”?.

Kuzungumzia “Ujamaa” leo ni sawa na kukubali kuitwa mwendawazimu.  Ni kwa sababu watu wengi wanaamini kwamba Ujamaa na siasa ya Kujitegemea vilikufa kufuatia Azimio la Zanzibar la mwaka 1992 lililofungua milango kwa sera za uchumi wa soko huria na vyama vingi vya siasa. Vivyo hivyo, wengi wanaona kuwa, kwa Katiba yetu [ibara ya 9] kuendelea kudai kwamba “Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata “Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea”, ni kuifananisha Katiba yake na Katiba ya wendawazimu kwa sababu zile zile tulizozitaja hapo juu.

Mitizamo yote miwili ni potofu na pengine inatokana na ufahamu mdogo wa dhana ya “Ujamaa”, na pia kuuchanganya au kuufananisha “Ujamaa” na Usoshalisti au Ukomunisti ambao kufuatia kuvunjika kwa kambi ya Kisoshalisti iliyoongozwa na Urusi, miaka ya 1990, umelegeza hatamu duniani.

Tafsiri ya “Ujamaa” kwa kifupi ni mfumo wa maisha wa kijamii kwa misingi ya utamaduni wa Kiafrika katika mazingira ya Kiafrika na kwa kuzingatia misingi ile ile ya misahafu ya dini ya “Upendo” kwamba, “mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”.  Tena  Ujamaa maana yake ni jumuiya ya “familia” moja ya binadamu.

Kwa tafsiri hii “Ujamaa” unaweza kubeba na kulea mfumo wowote wa siasa, wa Chama kimoja au wa vyama vingi; na sera yoyote ya uchumi, wa Kisoshalisti au wa Kibepari na hata wa kimwinyi.  Tofauti pekee ni jinsi mfumo huo wa siasa au sera za uchumi zinavyojali au kuzingatia haki za msingi za binadamu kisiasa, kiuchumi na kijamii.  Mfano, Usoshalisti wa chama cha NAZI cha dikteta Adolf Hitler wa Ujerumani ulishindwa na usingeweza kuleleka na kukua katika mazingira ya “Ujamaa” kwa sababu ya ubaguzi  na udikteta wa aina yake, lakini NAZI kiliendelea kuitwa cha Kisoshalisti bila sifa ya kuitwa cha “kijamaa”.

Kwetu, Ujamaa utaendelea kuwapo mradi tu tutaendelea kubakia Waafrika.  Na kama dhana hii ingekuwa inaondolewa minofu na kubakia “Panki”, kama baadhi ya Wazungu weusi,  akina “Charles Njonjo” wa enzi zetu wanavyoamini, wasingetetea hoja ya “takrima” wakidai eti ni ukarimu wa “Kiafrika”, japo kwa tafsiri potofu.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alielewa vyema nafasi ya “Ujamaa” katika ujenzi wa uchumi na katika kusukuma kasi  ya maendeleo kwa nchi. Yeye alikuwa muumini wa Usoshalisti kama sera sahihi ya uchumi kwa maendeleo ndani ya mazingira ya “Ujamaa”.  Aliuona Usoshalisti kama matumizi ya msingi wa usawa wa binadamu katika ujenzi wa jamii. Licha ya kwamba jaribio lake la kukuza na kuongoza uchumi kwa sera za Usoshalisti ndani ya “Ujamaa” hazikufanikiwa sana, lakini kile kitendo cha kuliongoza taifa kwa misingi ya “Ujamaa” na kujenga umoja wa kitaifa imara, bado kinamfanya akumbukwe na wengi kama mpigania haki na usawa.

Ndiyo maana kila mara watu, vikundi na jamii kwa  ujumla inapotoneshwa kwa vitendo au matukio yasiyoshabihiana na ujenzi wa demokrasia, uhuru, usawa na haki au kuonewa, wanaomboleza kwa uchungu kwa ule wimbo ambao umetokea kuwa liwazo katika siasa na sera za mparanganyiko:  “Kama si kwa juhudi zako Nyerere……na uhuru tungepata wapi;….. na amani tungeipata wapi”. Kwa kufanya hivyo wanatuambia kwamba, usawa, na kuwajibika katika jamii yetu vinayoyoma na pia kwamba  uhuru wetu uko njia panda.

Hili tunaomba liwekwe sawa; kwamba kilichouawa na Azimio la Zanzibar si “Ujamaa” bali ni Azimio la Arusha kama mfumo na dira ya uzalishaji na umilikaji mali ndani ya jamii ya Kijamaa unaosimamiwa na Serikali.  Hii haina maana kwamba hapakuwa na “Ujamaa”, kabla ya Azimio la Arusha. Tofauti na Azimio la Arusha ndani ya “Ujamaa”, kilichoanzishwa na Azimio la Zanzibar ni demokrasia ya kumiliki mali kwa mtu binafsi [economic democracy], na kwa Serikali kujitoa katika kupanga na  kusimamia uchumi, kutofanya biashara ili kila kitu kiamliwe na nguvu ya soko katika mazingira ya “Kijamaa”.  Na vivyo hivyo kwa uhuru wa kisiasa.

Kilichofanywa na Azimio la Zanzibar ni kuwaondolea wananchi na Serikali yao jukumu la kupanga na kusimamia uchumi kwa manufaa ya wote ilivyokuwa kabla ya hapo, na katika kuchangia kwa kuweka vipaumbele kwenye mchakato wa maendeleo ya kiuchumi ili kazi hiyo ifanywe na nguvu ya soko kwa manufaa ya wenye mitaji pekee.

Ujamaa haumzuii mtu kumiliki mali na utajiri apendavyo; bali kinachogomba ni pale utajiri huo unapotumika kununua au kuteteresha haki katika nyanja za siasa, uchumi na jamii. Hata katika nchi za ubepari uliokomaa, haki za binadamu, demokrasia na utawala wa Sheria hulindwa na kutetewa kama zinavyotafsiriwa na jamii yenyewe kupitia Katiba na Sheria za nchi hizo.  Lengo la kufanya hivyo  ni kuimarisha “Ujamaa” kwa jamii husika.

Vivyo hivyo, Azimio la Arusha halikuzuia kuwapo kwa sekta binafsi. Na katika kutekeleza hilo, Azimio liliweka mipaka ya shughuli kati ya Serikali na sekta binafsi kwa kuainisha shughuli zipi zifanywe na Serikali na zipi zifanywe na sekta binafsi; lakini yote kwa lengo la kuinua uchumi na maisha ya mwananchi katika jamii yenye usawa-Ujamaa.

Ulimbukeni wa kuipa jina baya dhana ya “Ujamaa” una lengo la kuingiza katika jamii nadharia za kigeni zisizoshabihiana na utamaduni wa mazingira yetu.  Na kwa sababu hiyo, tunajaribu kuendeleza nchi kwa kutumia historia ya nchi zingine – Amerika na Uingereza.  Ndiyo maana mipango yetu ya maendeleo inashindwa kwa sababu ya vigezo na tiba isiyotakiwa na mara nyingi mikakati yetu hushindwa kabla ya kuanza. ITAENDELEA WIKI IJAYO.