Home kitaifa Nani atamrithi Dk. Shein urais Zanzibar?

Nani atamrithi Dk. Shein urais Zanzibar?

2652
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU

-ZANZIBAR

WINGU zito limetanda katika siasa za CCM Visiwani Zanzibar, huku baadhi ya mawaziri wakitajwa kuanza kupita chinichini kutafuta kuungwa mkono kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Hatua hiyo sasa imeibua minyukano huku baadhi ya makundi wakiwamo mawaziri waliopo ndani ya Baraza la Mawaziri la sasa la Rais Dk. Ali Mohamed Shein, yakianza mikakati ya kutafuta kuungwaji mkono katika siasa za visiwani Zanzibar pamoja na kwa wana CCM wenye ushawishi upande wa Bara.

Mei mwaka jana katika kile kinachotajwa kuwa huenda kama mkakati wa kutaka kuleta vurugu ndani ya chama hicho tawala, ilimfanya Rais Dk. Shein, kutoka hadharani na kuonya  makada hao walioanza kampeni kabla ya muda.

Dk. Shein aliwataka watambue kwamba yeye bado ni Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa sheria.

Onyo hilo alilitoa kwenye mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Tunguu, Wilaya ya Kati Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk. Shein alisema makada hao wameanza kupanga timu za urais badala ya kushughulika na mambo ya msingi ya ujenzi wa chama.

Alisema makada hao badala ya kufanya shughuli za ujenzi wa chama zitakazofanikisha kuibakiza CCM madarakan,i badala yake wanapanga safu kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.

Dk. Shein alisema nafasi ya urais haipatikani kwa kampeni wala makundi yasiyokuwa halali ila hupatikana kwa utaratibu maalumu na kwa mujibu kanuni na Katiba ya CCM.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, aliwatahadharisha viongozi hao kwa kuwataka kuacha tabia hizo kwa sababu inaweza kuleta migogoro na mgawanyiko usiokuwa wa lazima ndani ya CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Alisema watu hao wanaosaka urais kwa sasa wasipoacha tabia hiyo na kuvumilia mpaka 2020, watachukuliwa hatua kali za nidhamu ikiwamo majina yao kufikishwa katika vikao vya Usalama na Maadili vya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) ili wahojiwe na kuchunguzwa kutokana na mienendo yao isyokuwa na manufaa.

Kamati hiyo ya Maadili na Usalama huongozwa na Mwenyekiti wa CCM ingawa kwa ngazi ya uchunguzi Makamu Mwenyekiti husimamia shughuli zote ikiwamo kufungua majalada ya wanaotajwa kila mkoa na wilaya ili kupata taarifa za wahusika.

Aliwatadharosha viongozi, watendaji na wanachama wa CCM kwa kuwataka kuelekeza nguvu zao katika kutekeleza mipango mbalimbali ya kukisaidia chama kushinda na siyo kuhangaika kumrithi yeye kwenye urais.

“Naheshimu Katiba ya nchi, muda wangu ukifika naondoka madarakani kwa vile huo ndiyo utaratibu wa chama chetu na kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Lakini sifurahishwi hata kidogo kuona baadhi yenu mnaanza kuhangaika na urais badala ya kufanya kazi za kuitafutia ushindi CCM mwaka 2020,” alisema na kuonya Dk. Shein.

Aliwataka mabalozi na viongozi wengine wa ngazi za mashina kukataa kuingizwa katika mitandao hiyo ya kampeni.

Machi 3, mwaka huu baada ya kuonekana kukaidi agizo hilo, ambapo pia awali pia liliwahi kutolewa katika vikao vya NEC hasa kwa wana CCM wanaotamani kumrithi Dk. Shein mwaka 2020 kuacha kampeni za chini kwani kufanya hivyo si utamaduni wa chama hicho tawala.

Hali hiyo ilimfanya Dk. Shein kumtoa kwenye Baraza la Mawaziri aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohamed, ambaye alikuwa akitajwa kwenye mikakati ya chinichini huku akidaiwa kutaka kuvaa viatu vya Dk. Shein mwaka 2020.

Kutokana na hali hiyo Dk. Shein, alitangza kumteua aliyekuwa Mshauri wake wa masuala ya uchumi na diplomasia, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Hata hivyo hatua hiyo inatajwa kuibuka kwa msamiti mpya kwamba ‘sasa ni zamu ya Unguja’ ikimaanisha ni wakati wa Waunguja kuongoza baada ya Dk. Shein ambaye anatoka Kisiwani Pemba kuondoka madarakani.

Pamoja na hayo kwa sasa CCM inaonekana ikiendeleza mikakati ya kurejesha hadhi yake baada ya ushindi uchaguzi wa mwaka 2015.

Licha ya kushinda urais mwaka 2015 ambao ulizua mzozo hadi kwa baadhi ya vyama vya upinzani ikiwamo CUF kususia uchaguzi wa marudio wa Machi 2016, lakini bado chama hicho tawala kinaonena kuendelea kuimarika kuelekea mwaka 2020.

KUIMARIKA KWA CCM

Upinzani unaelekea kudhoofika, wakati CCM ikiimarika na kung’ara miongoni vyama vya ukombozi vilivyoleta uhuru katika nchi zao.

Ingawa haikuwepo wakati wa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 wala mapinduzi ya Zanzibar 1964, CCM inahesabika kama chama cha ukombozi kwa sababu kilizaliwa na vyama viwili vyenye sifa hiyo, TANU ya Tanganyika na ASP ya Zanzibar chini ya waasisi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.

Wakati CCM ikizidi kuimarika, vyama vingi vilivyoanzishwa katika miaka ya 1950 na 60 vilishatimuliwa madarakani, vikiwemo United National Independence Party (UNIP), Malawi Congress Party (MCP) na Kenya African National Union, (KANU).

UNIP ya Kenneth Kaunda ilikuwa ya kwanza kuangushwa mwaka 1991 baada ya miaka 27 madarakani, ikafuatiwa na MCP ya Kamuzu Banda mwaka 1994 (miaka 29 madarakani) na kisha mwaka 2002 ikawa zamu ya KANU (miaka 39 madarakani).

Baadhi ya vyama vya ukombozi kama Parmehutu cha Rwanda, Mouvement National Congolais (MNC) cha Kongo- Kinshasa vilishafutwa miaka mingi.

SIRI YA NGUVU YA CCM?

Siri ya kwanza ya nguvu ya CCM ni Nyerere, Rais wa kwanza ambaye Watanzania wanamkumbuka kwa mapenzi makubwa wakimuita ‘Mwalimu, au ‘Baba wa Taifa.’ 

Anaweza kuwa hakufanikiwa sana katika nyanja ya uchumi, lakini Nyerere alijenga taifa na kuwaunganisha Watanzania.

Pia, Nyerere alijijengea heshima kwa kung’atuka mwenyewe madarakani akiwa bado ana nguvu na kusimamia mchakato wa kumpata mrithi wake, kinyume na wengine waliosubiri watolewe.

Nchi chache zina watu wa hadhi ya Nyerere na Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini.

Hakuna kati ya Jomo Kenyatta wa Kenya, Dkt Hastings Kamuzu Banda wa Malawi wala Kenneth Kaunda, aliyewahi hata kupokonywa uraia wa Zambia, anayeheshimiwa katika nchi zao kama anavyoheshimiwa Nyerere.

Kutokana na mapenzi ya Watanzania kwa Nyerere na CCM yake, haikushangaza kwamba, mwaka 1991, matokeo ya Tume ya Rais iliyopewa jukumu la kukusanya maoni ya Watanzania juu ya mfumo wa vyama yalionesha kuwa asilimia 80 ya Watanzania walitaka chama kimoja kiendelee.

Bahati nzuri, mwenyewe aliunga mkono mfumo wa vyama vingi na sauti yake ikawa kura ya turufu.

Hata hivyo, wananchi wengi hadi sasa wanaiona CCM kama urithi wa Mwalimu hivyo kuasi chama hicho ni usaliti wa kumbukumbu yake.

Hii inaonesha kuwa vyama vingi si mtindo wa maisha ya kisiasa uliochaguliwa na Watanzania, bali ulianzishwa kwa sababu ilikuwa ‘fasheni’ ya wakati ule katika siasa mpya za dunia baada ya kudondoka kambi ya Mashariki ya Wajamaa.

Katika hali hii, uzoefu wa miaka 25 wa siasa za vyama vingi unaonesha kuwa Watanzania wanavitumia vyama vya upinzani kama mahali pa kuonesha hasira zao pale serikali ya CCM inaposhindwa kukidhi matarajio yao katika kusimamia uchumi na kupambana na ufisadi.